-
Kuhangaikia Urembo Kupita KiasiAmkeni!—2004 | Desemba 22
-
-
Kuhangaikia Urembo Kupita Kiasi
MARIAa ni msichana ambaye amefanikiwa maishani na ametoka katika familia nzuri. Lakini hana furaha. Kwa nini? Hapendi sura yake. Ingawa washiriki wa familia yao humtia moyo, Maria hufikiri kwamba yeye si mrembo, na hilo humvunja moyo sana.
José ametoka katika familia yenye kuheshimika, hivyo anapaswa kuwa mwenye furaha. Hata hivyo, anafikiri hatapata mwenzi. Kwa nini? José anafikiri ana sura mbaya. Anaamini hawezi kumvutia mwanamke mzuri.
Luis ni mtoto mwenye urafiki aliye na umri wa miaka minane, naye hupenda kwenda shule. Ijapokuwa Luis hufurahia kucheza na wanafunzi wenzake, yeye hulia mara nyingi kwa sababu wao hufanya mzaha kuhusu sura yake. Wao husema yeye ni mnene.
Kuna visa vingi kama hivyo. Tatizo la Maria, José, na Luis halisababishwi na kutojiheshimu. Kusema kweli, hakuna anayefurahia kukataliwa na wengine kwa sababu ya sura yake.
Hata hivyo, katika jamii sura huonwa kuwa muhimu kupita kiasi. Mara nyingi, ni kana kwamba mafanikio hutegemea sura ya mtu. Kwa mfano, watu wenye sura nzuri zaidi hufanikiwa kupata kazi haraka zaidi. Pilar Muriedas, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa Mashirika ya Afya ya Wanawake ya Amerika ya Latini na Karibea, anasema kwamba kwa wanawake “urembo ni mojawapo ya matakwa muhimu ya mafanikio.” Kulingana na Dakt. Laura Martínez, wanawake wanafahamu kwamba “kupata au kukosa kazi hutegemea sana sura yao.”
Hata wanaume wengi hujishughulisha kupita kiasi kupata umbo zuri. Ama kweli, wanaume na wanawake wengi hujitahidi juu chini kuwa na sura ya kuvutia. Hata wengine hukubali kupata matibabu yanayoumiza na kukataa kula ili wawe na sura nzuri au umbo zuri. Je, kuna faida zozote za kufanya hivyo? Je, kuna hatari zozote?
[Maelezo ya Chini]
a Majina yamebadilishwa.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Sura ya mtu inaweza kuathiri uwezekano wake wa kupata kazi
-
-
Hatari za Kuhangaikia UremboAmkeni!—2004 | Desemba 22
-
-
Hatari za Kuhangaikia Urembo
UREMBO wa kweli hutegemea nini? Watu fulani husema urembo hutegemea maoni ya mtazamaji. Isitoshe, maoni ya watu wengi kuhusu urembo yametofautiana sana katika utamaduni na enzi mbalimbali.
Jeffery Sobal, mtaalamu wa sayansi ya lishe katika Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, anasema hivi: “Katika karne ya kumi na tisa, jamii nyingi ziliwaona watu wanene kuwa watu wanaoheshimika. Watu wanene walionwa kuwa watu wenye afya na ufanisi, huku watu wembamba wakionwa kuwa maskini hohehahe ambao hawawezi kununua chakula cha kutosha.” Sanaa nyingi za kipindi hicho zinaonyesha maoni hayo. Mara nyingi sanaa hizo zilionyesha wanawake wenye mikono mikubwa, miguu minene, mgongo mpana, na mapaja manene. Baadhi ya sanaa hizo zilikuwa picha za watu halisi walioonwa kuwa warembo zaidi.
Ingawa urembo unahusisha mengi zaidi ya kuwa mnene au mwembamba, watu fulani wangali na maoni hayo. Jamii fulani zinazoishi kwenye visiwa vya Pasifiki Kusini hupenda sana unene. Katika maeneo fulani ya Afrika, wasichana wanaotarajia kuolewa hupelekwa kwenye makao ya pekee ambako wanalishwa vyakula vingi vyenye mafuta mengi ili wanenepe na kuvutia zaidi. Mtu mmoja anayemiliki klabu cha usiku huko Nigeria anasema hivi: “Kwa kawaida, wanawake Waafrika ni wanene . . . Huo ndio urembo wao. Huo ndio utamaduni wetu.” Katika jamii nyingi za Hispania, unene huonwa kuwa ishara ya utajiri na ya mafanikio.
Lakini katika maeneo mengine mengi, watu wanene hawaonwi kuwa warembo. Kwa nini? Watu fulani husema kwamba biashara zilipoongezeka na viwanda kuenea, chakula kilizalishwa kwa wingi na kusambazwa katika maeneo mengi, hivyo kuwawezesha watu maskini kupata vyakula ambavyo hapo awali vililiwa na matajiri tu. Hivyo, pole kwa pole watu wanene wakaacha kuonwa kuwa warembo. Kwa upande mwingine, dini fulani huwaona watu walionenepa kupita kiasi kuwa walafi, na hilo limewafanya watu wawe na maoni mabaya kuhusu unene. Pia, mavumbuzi ya kisayansi kuhusu magonjwa yanayosababishwa na kunenepa kupita kiasi yameathiri maoni ya watu. Mambo hayo na mengineyo yamewafanya watu wabadili maoni yao kuhusu urembo. Kwa miaka mingi sasa, watu wengi ulimwenguni wamesema kwamba watu wembamba ndio warembo.
Vyombo vya habari vimechangia sana maoni hayo. Watu wanaoonyeshwa katika matangazo ya biashara kwenye mabango na televisheni huwa wembamba na wenye misuli. Watu wenye maumbo hayo hutumiwa katika matangazo hayo ili kuonyesha kwamba mtu atakayetumia bidhaa zinazotangazwa atakuwa mwenye uhakika na atafanikiwa. Pia, waigizaji maarufu wa sinema na vipindi vya televisheni huwa na maumbo kama hayo.
Maoni hayo huwaathirije watu wa kawaida, kutia ndani vijana? Makala moja ya hivi karibuni iliyozungumzia maoni ya watu kuhusu umbo lao ilionyesha kwamba “kufikia wakati msichana Mmarekani anapomaliza shule ya sekondari, yeye huwa ametazama televisheni kwa zaidi ya saa 22,000.” Wakati mwingi, wasichana hao huwatazama wanawake warembo wanaoonwa kuwa wenye maumbo bora. Makala hiyo inaongeza hivi: “Wanawake wanapotazama maumbo hayo tena na tena, wao huyahusianisha na umashuhuri, furaha, upendo, na mafanikio.” Basi si ajabu kwamba baada ya kutazama picha za wanamitindo katika gazeti fulani, asilimia 47 ya wasichana waliohusishwa katika uchunguzi mmoja walitamani sana kupunguza uzito, ingawa ni asilimia 29 tu kati yao waliokuwa wanene sana.
Vilevile, maoni ya watu kuhusu urembo huathiriwa sana na biashara ya mitindo. Jennifer, mwanamitindo anayetoka Venezuela, ambaye hufanya kazi huko Mexico City, anasema: “Ni lazima mwanamitindo awe mrembo, na siku hizi ni lazima uwe mwembamba ili uwe mrembo.” Mwanamitindo mmoja Mfaransa, anayeitwa Vanessa, anasema: “Hakuna anayekulazimisha kuwa mwembamba, bali ni wewe unayejilazimisha mwenyewe. Hilo ni zoea lililoenea ulimwenguni pote.” Wasichana fulani walipochunguzwa, asilimia 69 kati yao walikubali kwamba wanamitindo wanaoonyeshwa katika magazeti wameathiri maoni yao kuhusu umbo lenye kupendeza.
Lakini sio wanawake tu ambao huathiriwa na maoni yanayotolewa kuhusu umbo bora. Gazeti El Universal la Mexico linasema: “Bidhaa zinazokusudiwa kuboresha umbo la wanaume zinapatikana kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote.”
Je, Jitihada za Kupata Umbo Bora Zimefanikiwa?
Watu wengi huamua kufanyiwa upasuaji wa kubadili maumbile ili wawe na umbo bora au wapendeze zaidi. Kuna matibabu mbalimbali ya aina hiyo na gharama zake zinazidi kupungua. Matibabu hayo yalianzaje?
Kulingana na kitabu Encyclopædia Britannica, mbinu za kisasa za upasuaji wa kubadili maumbile zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, wakati ambapo watu waliojeruhiwa vitani walitibiwa majeraha yao. Tangu wakati huo, mbinu hizo zimetumiwa sana kutibu majeraha makubwa yanayosababishwa na moto au misiba na kurekebisha kasoro za kuzaliwa. Hata hivyo, kama vile kitabu Britannica kinavyosema, mara nyingi upasuaji wa kubadili maumbile “hufanywa hasa ili kuboresha sura za watu wenye afya.” Kwa mfano, umbo la pua linaweza kubadilishwa, ngozi inaweza kupunguzwa usoni na shingoni, ukubwa wa masikio unaweza kupunguzwa, mafuta yanaweza kuondolewa kiunoni na mapajani, sehemu fulani za mwili zinaweza kuongezwa ukubwa, na kitovu pia kinaweza kurekebishwa kupatana na mapendezi ya mtu.
Lakini, vipi watu wenye afya ambao huhatarisha afya yao ili kuboresha umbo lao? Wao hukabili hatari gani? Angel Papadopulos, katibu wa Chama cha Upasuaji wa Kubadili na Kuboresha Maumbile cha Mexico, anasema kwamba nyakati nyingine watu ambao hawajazoezwa ifaavyo hufanya upasuaji huo na kusababisha madhara makubwa. Kliniki nyingine hutumia vitu fulani hatari ili kuboresha umbo la mtu. Mapema katika mwaka wa 2003, gazeti moja liliripoti kwamba hali zisizofaa katika saluni fulani zilisababisha kashfa kwenye Visiwa vya Canary, ambako mamia ya wanawake walikuwa wamefanyiwa upasuaji hatari.a
Hata wanaume hujitahidi kupata umbo bora. Baadhi yao hutumia saa nyingi wakifanya mazoezi ili kuboresha umbo lao na kuongeza misuli yao. Gazeti Milenio linasema: “Hatimaye wao hupoteza marafiki, na mahusiano yao na watu wengine huharibika kwa sababu ya kujishughulisha sana na mazoezi ya mwili.” Kwa sababu ya kutamani sana kuwa na misuli, wengi wao hutumia vitu vinavyoweza kudhuru mwili, kama vile dawa za steroidi.
Wasichana fulani hujinyima chakula au hula sana na kujitapisha kwa sababu ya kuhangaikia sana umbo lao. Baadhi yao hutumia dawa za kupunguza uzito haraka ambazo hazijaidhinishwa na taasisi za afya zenye kuheshimika. Dawa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa.
Zaidi ya madhara ya kimwili, kuna hatari nyingine zinazosababishwa na kuhangaikia sura kupita kiasi. Dakt. Katherine Phillips wa Chuo Kikuu cha Brown, Marekani, anasema kwamba watu wanaohangaikia umbo lao kupita kiasi hupata ugonjwa fulani unaowafanya wadhanie kwamba wana kasoro za mwili, ijapokuwa hazipo. Inakadiriwa kwamba mtu 1 kati ya kila watu 50 ana ugonjwa huo. Pia anasema kwamba watu wenye ugonjwa huo “huamini kuwa wana sura mbovu sana hivi kwamba wao hujitenga na marafiki na wapendwa wao. Wanaweza kushuka moyo na kutaka kujiua.” Phillips anataja kisa cha msichana mmoja mrembo aliyedhania kwamba uso wake umejaa makovu, ijapokuwa alikuwa na vipele vidogo tu usoni. Msichana huyo aliacha shule alipokuwa katika darasa la nane kwa sababu hakutaka kuonekana na watu.
Je, sura ya mtu ni muhimu sana hivi kwamba ahatarishe afya yake ya kiakili na ya kimwili ili kupata umbo bora? Je, kuna urembo ulio bora zaidi ambao mtu anapaswa kuuhangaikia?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa Wakristo, upasuaji wa kubadili maumbile ni uamuzi wa kibinafsi. Hata hivyo, kuna mambo fulani muhimu ya kufikiria. Kwa habari zaidi, soma gazeti la Amkeni! la Agosti 22, 2002, ukurasa wa 18-20.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Maoni ya asilimia 69 ya wasichana kuhusu urembo hutegemea wanamitindo wanaoonyeshwa kwenye magazeti
[Picha katika ukurasa wa 4]
Matangazo ya biashara huathiri sana maoni ya watu kuhusu urembo
[Picha katika ukurasa wa 6]
Wengine wamejiumiza kwa kuamua kufanyiwa upasuaji wa kubadili maumbile
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wengine hujitahidi juu chini ili wapate umbo wanalotaka
-
-
Urembo Ulio Bora ZaidiAmkeni!—2004 | Desemba 22
-
-
Urembo Ulio Bora Zaidi
WATU hupendezwa na watu wanaovutia. Lakini ni nini humfanya mtu avutie? Ni kweli kwamba huwezi kubadili kabisa maumbile uliyorithi bila kujiumiza. Isitoshe, urembo ni wa muda tu, kwa kuwa hakuna mtu asiyeweza kuathiriwa na uzee na ugonjwa. Je, kuna urembo ulio muhimu zaidi, unaodumu, na unaoweza kupatikana?
Umuhimu wa Urembo wa Ndani
Biblia hutuhakikishia kwamba Muumba wetu, Yehova Mungu, huthamini sana urembo wa ndani. Hebu ona mifano kadhaa.
Yehova alipomwambia nabii Samweli achague mfalme kwa ajili ya Israeli miongoni mwa wana wa Yese, nabii huyo alivutiwa na Eliabu ambaye alikuwa na sura nzuri. Samweli alisema: “Hakika huyu ndiye aliyechaguliwa na Bwana.” Lakini Yehova akamwambia Samweli: “Usifikiri ni Eliabu kwa sababu tu yeye ni mrefu na mwenye sura nzuri. Sijamchagua yeye. Watu huwahukumu wengine kulingana na sura yao, lakini mimi huwahukumu watu kulingana na yale yaliyo katika mioyo yao.”—1 Samweli 16:6, 7, Contemporary English Version.
Daudi, mwana wa mwisho, ndiye aliyechaguliwa kuwa mfalme. Ingawa inasemekana Daudi alikuwa na “macho yenye kupendeza” na “mwenye sura nzuri,” huenda hakuvutia sana kama ndugu zake wakubwa. Lakini “roho ya Yehova ikaanza kutenda kazi juu ya Daudi kuanzia siku hiyo na kuendelea.” Ingawa Daudi hakuwa mkamilifu na alitenda dhambi nzito, alijulikana kuwa mtu mwenye moyo mzuri na alikuwa mtumishi mwaminifu wa Mungu hadi alipokufa. (1 Samweli 16:12, 13) Bila shaka, Mungu alivutiwa naye hasa kwa sababu ya urembo wake wa ndani.
Kwa upande mwingine, mfikirie Absalomu, mwana wa Daudi. Japo alikuwa na sura nzuri sana, alikuwa mtu mwenye kuchukiza. Biblia inasema hivi kumhusu: “Basi, kwa kulinganisha na Absalomu, hakuna mwanamume aliyekuwa na sura nzuri sana katika Israeli yote kuweza kusifiwa sana hivyo. Hakuwa na kasoro yoyote, kuanzia wayo wa mguu wake mpaka kipaji cha kichwa chake.” (2 Samweli 14:25) Hata hivyo, tamaa ya makuu ya Absalomu ilimchochea kumwasi baba yake na kunyakua ufalme. Hata alilala na masuria wa baba yake. Hivyo, Mungu akamkasirikia, naye akafa kwa maumivu mengi.—2 Samweli 15:10-14; 16:13-22; 17:14; 18:9, 15.
Je, wewe huvutiwa na Absalomu? Bila shaka huvutiwi naye. Kwa ujumla, alikuwa mtu mwenye kuchukiza. Sura yake nzuri haikufunika kiburi na ukosefu wake wa uaminifu, wala haikumzuia asiangamie. Kwa upande mwingine, Biblia inataja mifano mingi ya watu wenye hekima na wenye kuvutia bila kufafanua lolote kuhusu sura yao. Ni wazi kwamba urembo wao wa ndani ndio uliokuwa muhimu zaidi.
Urembo wa Ndani Huvutia
Je, urembo wa ndani unaweza kuwavutia watu? Georgina, ambaye ameolewa kwa karibu miaka kumi sasa, anasema hivi: “Muda wote huo, nimevutiwa na mume wangu kwa sababu yeye ni mnyoofu na mwaminifu kwangu. Kumpendeza Mungu ndilo jambo la maana maishani mwake. Hilo limemfanya awe mwenye kujali na mwenye upendo. Yeye hunifikiria anapofanya maamuzi, naye huonyesha kwamba ananithamini. Ninajua ananipenda sana.”
Daniel, ambaye alioa katika mwaka wa 1987, anasema: “Mimi humwona mke wangu kuwa mrembo. Ijapokuwa ninavutiwa na sura yake, mimi humpenda hasa kwa sababu ya utu wake. Yeye huwafikiria watu wengine na hujitahidi kuwafurahisha. Ana sifa nzuri sana za Kikristo. Hilo hunifanya nifurahie kuwa pamoja naye.”
Katika ulimwengu huu unaokazia sana urembo wa nje, tunapaswa kujitahidi kuona urembo wa ndani. Inafaa tutambue kwamba ni vigumu sana kupata umbo bora na kwamba hilo si muhimu. Hata hivyo, tunaweza kusitawisha sifa nzuri ambazo hutuwezesha kuwa warembo kwa ndani. Biblia inasema hivi: “Uvutio unaweza kudanganya, nayo sura yenye kupendeza inaweza kuwa ubatili; lakini mwanamke anayemwogopa Yehova ndiye anayejiletea sifa.” Kwa upande mwingine, Biblia huonya hivi: “Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, ndivyo alivyo mwanamke mwenye umbo la kupendeza lakini anayegeuka na kuacha kuwa na akili.”—Methali 11:22; 31:30.
Neno la Mungu hutusaidia kuthamini “yule mtu wa siri wa moyoni katika vazi lisiloharibika la roho ya utulivu na ya upole, ambayo ni ya thamani kubwa machoni pa Mungu.” (1 Petro 3:4) Bila shaka, urembo huo wa ndani ni bora zaidi ya urembo wa nje. Naam, sote tunaweza kuwa warembo kwa ndani.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Sifa nzuri zinaweza kukurembesha kuliko matibabu yoyote ya kuboresha umbo
-