-
Kujifunza Kutokana na Ubuni wa AsiliAmkeni!—2000 | Januari 22
-
-
Maajabu ya Misombo
Misombo ni vitu vigumu vinavyotokana na mchanganyiko wa dutu moja au mbili ili kufanyiza dutu mpya yenye sifa bora kuliko dutu za awali. Mfano mmoja ni kioo-nyuzi chenye msombo sanisia, kinachotumiwa kwa kawaida katika ujenzi wa mashua, fito za kuvua, pinde, mishale, na vifaa vingine vya michezo.a Kioo-nyuzi hutengenezwa kwa kutia nyuzi laini za glasi katika umajimaji au mseto wa plastiki unaofanana na jeli (unaoitwa polima). Polima hiyo inapokuwa ngumu, au kutulia, hutokeza msombo mwepesi, mgumu, na unaonyumbulika. Bidhaa nyingi mbalimbali zaweza kutengenezwa endapo nyuzi na mseto tofauti-tofauti vinatumiwa. Bila shaka, misombo inayotengenezwa na watu ingali duni ikilinganishwa na ile ya asili iliyo ndani ya wanadamu, wanyama, na mimea.
Wanadamu na wanyama, badala ya kuwa na nyuzi za glasi au kaboni, huwa na protini yenye nyuzinyuzi inayoitwa kolajeni ambayo hufanyiza misombo inayoimarisha ngozi, matumbo, tishu, kano, mifupa, na meno (isipokuwa gamba la jino).b Kitabu kimoja cha marejezo kinaeleza misombo ya kolajeni kuwa “miongoni mwa vifaa bora zaidi vya muundo wa msombo vinavyojulikana.”
Kwa mfano, fikiria kano zinazounganisha misuli na mifupa. Kano ni zenye kutokeza sana, si kwa sababu tu ya nyuzi zake zenye nguvu zinazotokana na kolajeni bali pia kwa sababu ya jinsi ambavyo zimeunganishwa kwa njia bora. Katika kitabu chake Biomimicry, Janine Benyus aandika kwamba kano isiyofumbuliwa “ina utaratibu bora ajabu isivyoaminika. Kano iliyo katika kigasha chako ni tita lililojipinda la nyuzi, kama kamba zinazotumiwa katika daraja linaloning’inia. Kila kamba ni tita lililojipinda la kamba nyembamba. Na kila kamba nyembamba ni tita lililojipinda la molekuli, ambazo, bila shaka ni matita yaliyosokotwa ya atomi. Uzuri wenye utaratibu wafumbuka tena na tena.” Huo ni, yeye asema, “uhandisi bora.” Si ajabu kwamba wanasayansi husema juu ya kuchochewa na ubuni wa asili?—Linganisha Ayubu 40:15, 17.
Kama ilivyotajwa, misombo iliyotengenezwa na watu haiwezi kulinganishwa na ile ya asili. Hata hivyo, sanisia ni bidhaa bora sana. Kwa hakika, ni miongoni mwa vitu kumi bora vya uhandisi vilivyotokezwa katika miaka 25 iliyopita. Kwa mfano, misombo inayotegemea grafati au nyuzi za kaboni imetokeza aina mpya za ndege na sehemu za vyombo vya anga, vifaa vya michezo, magari ya mbio, yoti, na viungo bandia vyepesi—vichache tu kati ya vitu vingi vinavyobuniwa.
-
-
Kujifunza Kutokana na Ubuni wa AsiliAmkeni!—2000 | Januari 22
-
-
b Misombo ya mboga hutokana na selulosi badala ya kolajeni. Selulosi huifanya miti ifae kwa ujenzi na kwa kazi nyinginezo. Selulosi imetajwa kuwa “kitu chenye kutanuka kisicho na kifani.”
-