Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • “Utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa . . . huhusika sana katika kuchanganua kabisa mawazo, akili, kichocheo, na utu. Sehemu hiyo hushirikisha mambo yanayoonwa maishani ambayo ni muhimu katika kufikiria mambo, kufanya uamuzi, kuwa mwenye udumifu, kupangia mambo, kuwahangaikia wengine, na dhamiri. . . . Uchanganuzi wa habari katika sehemu hii ndio huwafanya wanadamu wawe tofauti na wanyama wengine.” (Human Anatomy and Physiology cha Marieb) Kwa kweli twaona uthibitisho wa tofauti hii kati ya wanadamu na wanyama kwa kutazama matimizo ya mwanadamu katika mambo kama hesabu, falsafa, na haki, mambo ambayo kwa msingi hutegemea utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa.

      Kwa nini wanadamu wana utando mkubwa wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa, ambao ni wenye kubadilikana, na ambao huchangia sana kufikiri kwa hali ya juu, ilhali katika wanyama sehemu hiyo ni ndogo sana au hata haipo kabisa? Tofauti hiyo ni kubwa sana hivi kwamba wanabiolojia wanaosema kwamba sisi tumetokea kupitia mageuzi husema juu ya “ukuzi mkubwa sana wa ghafula wa ubongo wa binadamu.” Profesa wa Biolojia Richard F. Thompson, akisema juu ya ukubwa usio wa kawaida wa utando wa bongo kubwa wa binadamu, akiri hivi: “Kufikia sasa hatuelewi kabisa ni kwa nini jambo hili lilitukia.” Je, inawezekana sababu ni kwamba mwanadamu aliumbwa akiwa na ubongo wenye uwezo mkubwa usio na kifani?

  • Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • Ubongo Hauna Kifani kwa Stadi za Kuwasiliana

      Sehemu nyinginezo za ubongo pia huchangia kuwa kwetu viumbe vya kipekee. Nyuma ya utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa kuna ukanda unaovuka juu ya ubongo—ule utando unaoongoza miendo ya misuli. Huo una mabilioni ya chembe za neva ambazo zimeunganishwa kwa misuli yetu. Pia una sehemu mbalimbali zinazofanya tuwe tofauti kabisa na nyani au wanyama wengine. Utando mkuu wa kuongoza miendo ya misuli hutupatia “(1) uwezo bora sana wa kutumia mikono, vidole, na kidole gumba ili kutimiza mambo yanayohitaji ustadi sana, na (2) matumizi ya kinywa, midomo, ulimi, na misuli ya uso ili kuweza kuzungumza.”—Textbook of Medical Physiology cha Guyton.

      Ebu fikiria kifupi jinsi utando huo wa kudhibiti miendo ya misuli unavyohusiana na uwezo wako wa kuzungumza. Zaidi ya nusu ya sehemu hiyo hudhibiti viungo vya mawasiliano pekee. Jambo hili lasaidia kuelewa sababu inayofanya wanadamu wawe na stadi zisizo na kifani za kuwasiliana. Ingawa mikono yetu inatimiza fungu kubwa katika kuwasiliana (katika maandishi, ishara za kawaida, au lugha ya ishara), mara nyingi mdomo huchangia sehemu kubwa sana. Usemi wa mwanadamu—tokea neno la kwanza la mtoto mchanga hadi sauti ya mtu aliye mzee kwa umri—ni ajabu sana isiyotilika shaka. Misuli ipatayo 100 iliyo katika ulimi, midomo, utaya, koo, na kifua hushirikiana ili kutokeza sauti mbalimbali. Ebu tazama tofauti hii: Chembe moja ya ubongo inaweza kuongoza nyuzi 2,000 zilizo katika msuli mmoja wa shavu la mguu la mwanariadha lakini chembe za ubongo zenye kuongoza zoloto zaweza kuongoza nyuzi 2 tu au 3 za msuli. Je, hilo halidokezi kwamba ubongo wetu umeandaliwa kwa njia ya kipekee kwa ajili ya mawasiliano?

      Kila fungu la maneno mafupi ambayo wewe hutamka huhitaji mwendo fulani hususa wa misuli. Maana ya neno moja yaweza kubadilika kwa kutegemea kadiri ya mwendo na kuingiliana barabara kabisa kwa misuli mingine mingi. “Kwa kawaida,” aeleza mtaalamu wa usemi Dakt. William H. Perkins, “sisi hutamka karibu sauti 14 kwa sekunde moja. Hiyo inashinda kwa mara mbili uwezo wetu wa kudhibiti ulimi, midomo, utaya au sehemu yoyote ya usemi tunapozisogeza zikiwa tofauti-tofauti. Lakini ukitumia sehemu hizo zote pamoja ili zitokeze usemi, hizo hutenda kama vidole vya mstadi wa kuchapa taipu na jinsi ambavyo vidole vya wacheza-piano hucheza. Miendo yao hutokeza mchanganyiko uliopimwa barabara.”

      Ile habari hasa inayohitajika ili kuuliza tu swali rahisi, “Hujambo leo?” imehifadhiwa katika eneo fulani la sehemu ya mbele ya bongo kubwa liitwalo eneo la Broca, ambalo wengine huliona kuwa kitovu cha usemi. Mshindi wa tuzo la Nobeli aliye mwanasayansi wa ubongo, Sir John Eccles aliandika: “Hakuna eneo lolote linalolingana . . . na eneo la usemi la Broca ambalo limetambuliwa katika nyani.” Hata kama sehemu nyinginezo zinazofanana na hizo zinapatikana katika wanyama, ukweli ni kwamba wanasayansi hawawezi kuwafundisha nyani watokeze usemi ila tu sauti chache tu rahisi. Lakini, wewe unaweza kutokeza lugha yenye mambo mengi sana. Ili kufanya hivyo, unapanga maneno yako kulingana na sarufi ya lugha yako. Eneo la Broca hukusaidia kufanya hivyo, katika usemi na katika maandishi.

      Bila shaka, huwezi kudhihirisha muujiza huu wa usemi ila tu uwe unafahamu angalau lugha moja na kuelewa maana ya maneno yake. Hilo lahusisha sehemu nyingine ya pekee ya ubongo wako, ambayo huitwa eneo la Wernicke. Hapa, mabilioni ya chembe za neva hutambua maana na maneno yanayozungumzwa au kuandikwa. Eneo la Wernicke hukusaidia kuelewa maneno na kufahamu yale unayoyasikia au kusoma; likikusaidia kuweza kujifunza habari na kutenda ifaavyo.

      Kuna mambo mengi hata zaidi yanayohusu usemi wenye ufasaha. Kwa mfano: Kusema “Hujambo” kwaweza kutokeza maana tofauti-tofauti. Sauti yako yaonyesha ikiwa umefurahi, umesisimuka, umechoshwa, una shughuli nyingi, umekasirika, una huzuni, au unaogopa, na pia inaweza kufunua kiwango cha kihisia-moyo cha hisia hizo. Eneo jingine la ubongo wako huandaa habari za hali yako ya kihisia-moyo katika usemi wako. Kwa hiyo sehemu mbalimbali za ubongo wako huhusika unapowasiliana.

      Sokwe wengine wamefunzwa kutoa ishara chache, lakini ishara hizo ni za kuomba chakula au mambo mengine ya msingi pekee. Baada ya kufundisha sokwe mawasiliano rahisi ya ishara, Dakt. David Premack alikata kauli hivi: “Lugha ya wanadamu inafedhehesha sana nadharia ya mageuzi kwa sababu hiyo [lugha] ina uwezo sana kuliko inavyoweza kufafanuliwa.”

      Huenda tukajiuliza: ‘Kwa nini wanadamu wana ustadi huu wa ajabu wa kuwasilisha mawazo na hisia, wa kuulizia na kuitikia?’ Kitabu The Encyclopedia of Language and Linguistics chasema kwamba “usemi wa [wanadamu] ni wa kipekee” nacho chakiri kwamba “utafutaji wa usemi wa awali katika mawasiliano ya wanyama hausaidii kuziba lile pengo kubwa lililopo kati ya lugha [ya wanadamu] na sauti za wanyama.” Profesa Ludwig Koehler alitaja kifupi tofauti iliyopo: “Usemi wa binadamu ni siri; ni zawadi ya Mungu, na muujiza.”

      Kuna tofauti kubwa kama nini kati ya jinsi nyani atumiavyo ishara na uwezo mkubwa wa lugha ya watoto! Sir John Eccles alirejezea kile ambacho wengi wetu tumeona, uwezo “udhihirishwao na hata watoto wenye umri wa miaka 3 waulizapo maswali mengi wakitaka kuelewa mambo mengi wanayoyaona.” Yeye aliongezea: “Kwa kutofautisha, nyani hawaulizi maswali.” Ndiyo, ni wanadamu pekee waulizao maswali, kutia ndani maswali kuhusu maana ya maisha.

      Kumbukumbu na Mengi Zaidi!

      Utazamapo kioo, huenda ukafikiria jinsi ulivyofanana ulipokuwa mchanga, na hata kulinganisha hali hiyo na jinsi utakavyofanana miaka ijayo au jinsi ambavyo ungalifanana kwa kutumia vipodozi. Mawazo hayo yanaweza kutokea tu bila wewe kufahamu, lakini kuna kitu cha kipekee kinachotukia, kitu ambacho hakuna mnyama awezaye kuwa nacho.

      Tofauti na wanyama, ambao hasa huishi na kutegemea mahitaji ya sasa, wanadamu wanaweza kutafakari yaliyopita na kupangia wakati ujao. Jambo linalokuwezesha kufanya hivyo ni uwezo mkubwa sana wa ubongo wako wa kukumbuka. Ni kweli kwamba wanyama wana kadiri fulani ya kumbukumbu, na hivyo wao waweza kukumbuka njia ya kurudi nyumbani au kukumbuka mahali pa kupata chakula. Kumbukumbu ya mwanadamu ni kubwa sana. Mwanasayansi mmoja alikadiria kwamba ubongo wetu unaweza kubeba habari ambazo “zinaweza kujaza mabuku yapatayo milioni ishirini, yaani yanayotoshana na vitabu vyote vilivyo katika maktaba kubwa zaidi za ulimwengu.” Wanasayansi fulani wa ubongo wakadiria kwamba katika maisha ya wastani, mtu hutumia sehemu 1 tu kati ya 10,000 (.0001) ya uwezo wa ubongo wake. Huenda ukajiuliza, ‘Kwa nini tuna ubongo wenye uwezo mkubwa hivyo ambao hatutumii hata sehemu kidogo sana yake katika muda wote wa maisha?’

      Wala ubongo wetu si kama ghala kubwa tu ya habari, kama ilivyo kompyuta kubwa sana. Profesa wa biolojia Robert Ornstein na Richard F. Thompson waliandika: “Uwezo wa akili ya wanadamu wa kujifunza—kuhifadhi na kukumbuka habari—ndilo jambo lenye kutokeza sana katika vitu vyote vilivyo hai ulimwenguni. Kila kitu kitufanyacho kuwa wanadamu—lugha, mawazo, ujuzi, utamaduni—ni tokeo la uwezo huu mkubwa ajabu.”

  • Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • [Sanduku katika ukurasa wa 54]

      “Karibu ubongo wote wa binadamu umefanyizwa na utando [wa bongo kubwa]. Kwa mfano, ubongo wa sokwe una utando pia, lakini ni mdogo sana kwa kulinganishwa. Huo utando hutuwezesha kufikiri, kukumbuka, na kuwazia mambo. Kwa msingi, sisi ni binadamu kwa sababu ya utando wetu.”—Edoardo Boncinelli, mkurugenzi wa utafiti wa biolojia ya molekuli, Milan, Italia.

  • Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
    • ●Utando wa Bongo Kubwa ndio utando wa nje wa bongo unaohusika sana na akili. Utando wa bongo kubwa wa binadamu ukilainishwa unaweza kufunika kurasa nne; wa sokwe unaweza kufunika ukurasa mmoja tu; na wa panya unaweza kufunika stampu ya barua.—Scientific American.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki