Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kujenga Pamoja Duniani Pote
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
    • Ofisi, Matbaa, na Makao ya Betheli Ulimwenguni Pote

      Ulimwenguni pote katika 1992, kulikuwa ofisi za tawi 99 za Watch Tower Society, kila moja yazo ilitumika katika kuratibu utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika sehemu yalo ya shamba la ulimwengu. Zaidi ya nusu ya matawi hayo hufanya uchapaji wa aina tofauti-tofauti ili kusogeza mbele kazi ya elimu ya Biblia. Wengi wa wale wanaofanya kazi katika matawi, huishi wakiwa familia kubwa katika makao yaitwayo Betheli, kumaanisha “Nyumba ya Mungu.” Kwa sababu ya mpanuko wa idadi ya Mashahidi wa Yehova na utendaji wao wa kuhubiri, imekuwa lazima kuongeza ukubwa wa makao hayo na kujenga mapya.

      Ukuzi wa tengenezo umekuwa wa kasi sana hivi kwamba mara nyingi kumekuwa programu za upanuzi wa tawi 20 hadi 40 zikiendelea kwa wakati mmoja. Hiyo imetaka programu kubwa mno ya ujenzi wa kimataifa.

      Kwa sababu ya kazi kubwa mno ya ujenzi inayofanywa ulimwenguni pote, Watch Tower Society ina Idara ya Uhandisi na Uchoraji-ramani yayo yenyewe kwenye makao makuu yayo ya New York. Wahandisi wenye miaka mingi ya ujuzi wameacha kazi zao za kimwili wakajitolea ili kusaidia kwa wakati wote kwenye miradi ya ujenzi inayohusiana moja kwa moja na utendaji wa Ufalme. Kwa kuongezea, wale ambao wana ujuzi wamefundisha wanaume na wanawake wengine katika kazi ya uhandisi, ubuni, na uchoraji-ramani. Kwa kuratibu kazi kupitia idara hii, ujuzi unaopatikana katika ujenzi wa tawi katika sehemu yoyote ya ulimwengu unaweza kunufaisha wale wanaofanya kazi kwenye miradi katika nchi nyinginezo.

      Baada ya wakati, kiasi kikubwa cha kazi inayofanywa kilitokeza uhitaji wa kufungua Ofisi ya Uhandisi ya Kimkoa katika Japani ili kusaidia kufanya uchoraji-ramani kwa ajili ya miradi katika nchi za Mashariki. Ofisi za Uhandisi za Kimkoa nyingine huendesha kazi katika Ulaya na Australia, wafanyakazi wakiwa wametoka katika nchi mbalimbali. Ofisi hizo hufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na ofisi ya makao makuu, na utumishi wazo, pamoja na utumizi wa tekinolojia ya kompyuta, hupunguza idadi ya wafanyakazi wa uchoraji-ramani wenye kuhitajiwa kwenye mahali popote pale pa ujenzi.

      Baadhi ya miradi, kidogo ni ya ukubwa wa kiasi. Ndivyo ilivyokuwa kuhusu ofisi ya tawi iliyojengwa katika Tahiti katika 1983. Ilitia ndani nafasi ya ofisi, ghala kadhaa, na makao kwa ajili ya wafanyakazi wanane wa kujitolea. Na ndivyo ilivyokuwa pia kuhusu lile jengo la tawi lenye orofa nne lililojengwa kwenye kisiwa cha Karibea cha Martinique wakati wa miaka ya 1982 hadi 1984. Majengo hayo huenda yasionekane kuwa yenye kutokeza kwa wakazi wa majiji makubwa katika nchi nyinginezo, lakini yalivuta uangalifu wa umma. Gazeti France-Antilles lilijulisha kwamba jengo la tawi katika Martinique lilikuwa “ujenzi wa ustadi mkubwa” ulioonyesha “upendo mkubwa wa kazi iliyofanywa vizuri.”

      Kwa kutofautisha, kuhusu ukubwa, majengo yaliyokamilishwa katika Kanada katika 1981 yalitia ndani matbaa, au kiwanda, kikiwa na nafasi ya meta za mraba zaidi ya 9,300 na jengo la makazi kwa ajili ya wenye kujitolea 250. Katika Cesario Lange, katika Brazili, majengo mengi ya Watch Tower yaliyokamilishwa mwaka uo huo yalitia ndani majengo manane, yenye nafasi ya sakafu ya meta za mraba 46,000. Yalihitaji malori 10,000 yaliyojaa saruji, mawe, na mchanga, pamoja na vizingiti vyenye mkorogo wa saruji na kokoto vinavyofika mara mbili ya urefu wa Mlima Everest! Katika 1991, matbaa kubwa mpya ilipokamilishwa katika Filipino, ilihitajiwa pia kuandaa jengo la makazi la orofa 11.

      Ili kutimiza mahitaji ya idadi yenye kukua ya wapiga-mbiu wa Ufalme katika Nigeria, mradi mkubwa wa ujenzi ulianzishwa katika Igieduma katika 1984. Ungetia ndani kiwanda, jengo la ofisi lenye nafasi kubwa, majengo manne yaliyounganishwa ya makazi, na vifaa vingine. Mipango ilifanywa kwamba kuta za kiwanda zitangulie kufanyizwa kabisa na kusafirishwa kutoka Marekani. Lakini ndugu walikabiliwa na masharti magumu ya kuingiza vitu nchini yaliyoonekana kuwa hayawezekani. Wakati masharti hayo yalipotimizwa na kila kitu kikawasili salama kwenye mahali pa ujenzi, Mashahidi hawakujipa sifa wenyewe bali walimshukuru Yehova kwa baraka yake.

      Upanuzi wa Kasi Duniani Pote

      Hata hivyo, ukuzi wa kazi ya kupiga mbiu ya Ufalme umekuwa wa kasi sana hivi kwamba, hata baada ya upanuzi mkubwa wa vifaa vya tawi katika nchi, mara nyingi imekuwa lazima kuanza kujenga tena kwa muda mfupi. Fikiria vielelezo vichache.

      Katika Peru tawi jipya zuri—lenye nafasi ya ofisi, vyumba 22 vya kulala pamoja na vifaa vingine vya msingi kwa ajili ya washiriki wa familia ya Betheli, na Jumba la Ufalme moja—vilikamilishwa mwishoni mwa 1984. Lakini itikio kwa ujumbe wa Ufalme katika nchi hiyo ya Amerika Kusini lilikuwa kubwa zaidi ya ilivyotarajiwa. Miaka minne baadaye ilikuwa lazima kurudufisha majengo yaliyokuwako, wakati huu kwa kutumia ubuni unaohimili tetemeko la dunia.

      Majengo mapya ya tawi yenye nafasi kubwa yalikamilishwa katika Kolombia katika 1979. Ilionekana kwamba yangeandaa nafasi ya kutosha kwa miaka mingi ijayo. Hata hivyo, katika muda wa miaka saba idadi ya Mashahidi katika Kolombia ilikuwa karibu imerudufika, na sasa tawi lilikuwa likichapa magazeti La Atalaya (Mnara wa Mlinzi) na ¡Despertad! (Amkeni!) si kwa ajili ya Kolombia tu bali pia kwa ajili ya nchi nne jirani. Walilazimika kuanza kujenga tena katika 1987—wakati huu mahali ambapo palikuwa na nafasi zaidi kwa ajili ya upanuzi.

      Wakati wa 1980, Mashahidi wa Yehova katika Brazili walitumia saa 14,000,000 hivi kwa kazi ya kuhubiri hadharani ujumbe wa Ufalme. Tarakimu hiyo ilipanda kufikia karibu 50,000,000 katika 1989. Watu wengi zaidi walikuwa wakionyesha tamaa ya kutaka njaa yao ya kiroho itoshelezwe. Yale majengo ya tawi yaliyokuwa yamewekwa wakfu katika 1981 hayakutosha tena. Tayari kufikia Septemba 1988, uchimbuzi kwa ajili ya kiwanda kipya ulikuwa ukiendelea. Hicho kingeandaa asilimia 80 ya nafasi zaidi ya sakafu kuliko iliyokuwako katika kiwanda kilichoko, na bila shaka, makazi ya kutunza familia ya Betheli iliyoongezeka yangehitajiwa pia.

      Katika Selters/Taunus, Ujerumani, jengo kubwa la kuchapia la pili kwa ukubwa kati ya viwanda vya kuchapia vya Watch Tower Society liliwekwa wakfu katika 1984. Miaka mitano baadaye, kwa sababu ya maongezeko katika Ujerumani na pia fursa za kupanua kazi ya kutoa ushahidi katika nchi ambazo tawi hilo huchapia fasihi, mipango ilikuwa ikiendelea kuongeza ukubwa wa kiwanda kufikia zaidi ya asilimia 85 na kuongeza vifaa vingine vya utegemezo.

      Tawi la Japani lilikuwa limehamia Numazu kutoka Tokyo kwenye makao makubwa mapya katika 1972. Upanuzi zaidi uliokuwa mkubwa ulifanywa katika 1975. Kufikia 1978 mahali pengine palikuwa pamenunuliwa, katika Ebina; na kazi ya kujenga kiwanda kilichozidi ukubwa wa kile kilicho Numazu kwa mara tatu ilianza haraka. Hicho kilikamilishwa katika 1982. Bado hakikutosha; majengo zaidi yaliongezwa kufikia 1989. Je, haingewezekana kujenga mara moja tu na kukifanya kiwe kikubwa vya kutosha? La. Idadi ya wapiga-mbiu wa Ufalme katika Japani imerudufika tena na tena kwa njia ambayo hakuna mtu angeweza kutazamia. Kuanzia 14,199 katika 1972, idadi yao imepanda hadi 137,941 katika 1989, na walio wengi wao walikuwa katika huduma ya wakati wote.

      Kiolezo icho hicho kinaonwa katika sehemu nyingine za dunia. Katika muda wa mwongo mmoja—na nyakati nyingine miaka michache—baada ya kujenga matawi makubwa yenye vifaa vya kuchapia, ilikuwa lazima kuanza upanuzi mkubwa. Ilikuwa hivyo katika Mexico, Kanada, Afrika Kusini, na Jamhuri ya Korea, miongoni mwa mengine.

      Ni nani ambao hasa hufanya kazi ya ujenzi? Hiyo hutimizwaje?

      Maelfu Mengi Wana Hamu ya Kusaidia

      Katika Sweden, kati ya Mashahidi 17,000 katika nchi wakati ule wa ujenzi wa tawi lao katika Arboga, 5,000 hivi walijitolea kusaidia kazi. Wengi walikuwa tu wasaidizi wenye moyo wa kupenda, lakini kulikuwa pia wafanyakazi wenye ustadi wa hali ya juu wa kutosha kuhakikisha kwamba kazi ilifanywa sawasawa. Msukumo wao ni nini? Kumpenda Yehova.

      Wakati mkuu kwenye ofisi ya upimaji-ardhi katika Denmark aliposikia kwamba kazi kwenye tawi jipya katika Holbæk ingefanywa na Mashahidi wa Yehova, alionyesha kutia shaka. Hata hivyo, miongoni mwa Mashahidi waliojitolea kusaidia, wote wenye ujuzi uliohitajiwa walipatikana. Hata hivyo, je, ingekuwa afadhali kama wafanyakazi wa mkataba wa kibiashara wangalilipwa wafanye kazi hiyo? Baada ya ujenzi huo kukamilishwa, wastadi kutoka idara ya ujenzi ya mji walizuru makao hayo na kueleza juu ya kazi yenye ustadi iliyofanywa—jambo ambalo wao huliona mara chache sana kwenye kazi zilizofanywa na watu wa kulipwa siku hizi. Kwa habari ya yule mkuu aliyetia shaka mapema kidogo, yeye alitabasamu na kusema: “Angalia, wakati ule sikujua nyinyi watu mna tengenezo la aina gani.”

      Miji na majiji katika Australia yametawanyika sehemu zilizo mbali; hivyo, wengi kati ya wale 3,000 waliojitolea kufanya kazi kwenye ofisi ya tawi katika Ingleburn kati ya 1978 na 1983 walilazimika kusafiri angalau kilometa 1,600. Hata hivyo, safari za basi za vikundi vya wenye kujitolea ziliratibiwa, na makutaniko njiani yalijitolea kutoa milo na ushirika kwa ukaribishaji-wageni kwa ajili ya akina ndugu kwenye vituo vya kupumzikia. Baadhi ya ndugu waliuza makao yao, wakafunga biashara zao, wakachukua likizo, na kutoa dhabihu nyingine ili kushiriki katika ujenzi. Vikundi vya mafundi stadi vilikuja—baadhi yavyo zaidi ya mara moja—kumwaga kokoto, kuangika dari, na kujenga ua. Wengine walitoa upaji wa vifaa vya ujenzi.

      Walio wengi kati ya wenye kujitolea kwenye miradi hiyo walikuwa bila ustadi, lakini kwa kuzoezwa kidogo, baadhi yao walitwaa madaraka makubwa wakafanya kazi bora sana. Walijifunza jinsi ya kutengeneza madirisha, kuendesha matrekta, kuchanganya kokoto, na kujenga matufali. Walifurahia mambo yasiyofurahiwa na wasio-Mashahidi wafanyao aina ileile ya kazi ili kulipwa. Kwa njia gani? Wenye ujuzi walikuwa tayari kushiriki maarifa yao. Hapana yeyote aliyehisi kwamba mtu mwingine angechukua kazi yake; kulikuwa kazi nyingi kwa kila mtu kufanya. Na kulikuwa na msukumo wenye nguvu wa kufanya kazi ya hali ya juu, kwa sababu ilifanywa ikiwa wonyesho wa kumpenda Mungu.

      Kwenye mahali pa ujenzi, baadhi ya Mashahidi hufanyiza kiini cha “familia” ya ujenzi. Wakati wa kazi katika Selters/Taunus, Ujerumani, tokea 1979 hadi 1984, mamia kadhaa kwa kawaida walifanyiza kiini hicho cha wafanyakazi. Maelfu wengine walijiunga nao kwa vipindi tofauti-tofauti vya wakati, wengi katika miisho-juma. Kulikuwa mpango wa uangalifu hivi kwamba wenye kujitolea walipowasili, walikuwa na kazi tele ya kufanya.

      Maadamu watu si wakamilifu, kutakuwako matatizo, lakini wale ambao hufanya kazi kwenye ujenzi huo hujaribu kutatua matatizo kwa msingi wa kanuni za Biblia. Wanajua kwamba kufanya mambo katika njia ya Kikristo ni jambo la maana zaidi ya kuwa na matokeo. Kikiwa kikumbusho, kwenye mahali pa ujenzi katika Ebina, Japani, kulikuwa ishara kubwa zenye picha za wafanyakazi wenye kuvalia kofia ngumu, na juu ya kila kofia ngumu liliandikwa kwa herufi za Kijapani moja la matunda ya roho ya Mungu: upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujidhibiti. (Gal. 5:22, 23, NW) Wale ambao hutembelea mahali pa kazi wanaweza kuona na kusikia ile tofauti. Akieleza maoni yake mwenyewe, mwandishi mmoja wa habari aliyetembelea mahali pa ujenzi wa tawi katika Brazili alisema hivi: “Hapana machafuko au ukosefu wa ushirikiano . . . Mazingira haya ya Kikristo huifanya iwe tofauti hapa na yale ambayo huonwa kwa kawaida katika ujenzi wa kulipwa katika Brazili.”

      Ukuzi Wenye Kuendelea Kwenye Makao Makuu ya Ulimwengu

      Wakati matawi ya Watch Tower Society yamekuwa yakikua, imehitajiwa pia kupanua vifaa vya makao makuu ya ulimwengu. Kumekuwa maongezeko makubwa kwenye makao ya kiwanda na ofisi zayo katika Brooklyn na katika mahali pengine katika Jimbo la New York zaidi ya mara kumi tangu Vita ya Ulimwengu 2. Ili kuwapa makao wafanyakazi, imekuwa lazima kujenga au kununua na kurekebisha majengo mengi, makubwa na madogo pia. Upanuzi mwingine mkubwa katika Brooklyn ulitangazwa katika Agosti 1990 na katika Januari 1991—hata ingawa kaskazini mwa New York City ujenzi mkubwa ulioanza katika 1989 ulikuwa ukiendelea kwenye Kitovu cha Elimu cha Watchtower, ambacho kilikusudiwa kuwapa makao watu 1,200, kutia na wafanyakazi na wanafunzi.

      Tangu 1972, kazi ya ujenzi haijaacha kufanywa kwenye makao makuu ya ulimwengu katika Brooklyn na vifaa vyayo vinavyohusiana karibukaribu katika sehemu nyingine za New York na katika New Jersey. Baada ya muda, ilipata kuwa wazi kwamba hata ingawa idadi yao ilifikia mamia, wafanyakazi wa ujenzi wa kawaida walishindwa kuiweza kazi. Kwa hiyo, katika 1984 programu yenye kuendelea ya wafanyakazi wa muda ilianzishwa. Barua zilipelekwa kwa yale ambayo wakati huo yalikuwa makutaniko 8,000 katika Marekani kualika ndugu wenye kustahili waje wasaidie kwa juma moja au zaidi. (Programu kama hiyo ilikuwa tayari imefanya kazi vizuri katika baadhi ya yale matawi, kutia na Australia, ambako wale walioweza kukaa majuma mawili walialikwa wajitolee.) Wafanyakazi wangepewa makao na chakula lakini wangelipia gharama zao za usafiri na hawangepokea mishahara. Ni nani wangeitikia?

      Kufikia 1992, maombi zaidi ya 24,000 yalikuwa yameshughulikiwa! Angalau 3,900 kati ya hawa walikuwa watu waliokuwa wakirudi kwa mara ya 2, ya 3, hata ya 10 au ya 20. Walio wengi wao walikuwa wazee, watumishi wa huduma, au mapainia—watu binafsi wenye sifa nzuri za kiroho. Wote walikuwa wakijitolea kufanya lolote lililohitajiwa, iwe hiyo iliwataka watumie ufundi wao au la. Mara nyingi kazi ilikuwa nzito na chafu. Lakini walilihesabu kuwa pendeleo kuchanga katika njia hiyo kusogeza mbele masilahi ya Ufalme. Baadhi yao walihisi hiyo iliwasaidia kuthamini vizuri zaidi ile roho ya kujidhabihu inayoonyesha aina ya kazi ifanywayo kwenye makao makuu ya ulimwengu. Wote walihisi kuwa walithawabishwa sana kwa sababu ya kuwapo kwa ajili ya programu ya familia ya Betheli ya ibada ya asubuhi na funzo la Mnara wa Mlinzi la familia lifanywalo kila juma.

      Wenye Kujitolea wa Kimataifa

      Kadiri uhitaji wa upanuzi wa kasi ulivyokua, mpango wa wenye kujitolea wa kimataifa ulianzishwa katika 1985. Hiyo kwa vyovyote haikuwa ndiyo mara ya kwanza kuwa na ushirikiano wa kimataifa katika ujenzi, lakini sasa mpango huo uliratibiwa kwa uangalifu kutoka makao makuu. Wote ambao hushiriki ni Mashahidi ambao hujitolea kusaidia kazi ya ujenzi nje ya nchi zao wenyewe. Wao ni wafanyakazi stadi, pamoja na wenzi wa ndoa ambao huenda pamoja na waume zao kusaidia kwa njia yoyote wawezayo. Walio wengi wao hulipia nauli zao wenyewe; hakuna wanaopewa mshahara kwa ajili ya kile wafanyacho. Baadhi yao huenda kwa muda mfupi, kwa kawaida wakikaa kuanzia majuma mawili hadi miezi mitatu. Wengine ni wenye kujitolea wa muda mrefu, wakikaa kwa mwaka au zaidi, labda mpaka ujenzi unapokamilika. Mashahidi wa Yehova zaidi ya 3,000 kutoka nchi mbalimbali 30 walishiriki sehemu katika kazi hiyo wakati wa miaka mitano ya kwanza, na wengi zaidi walikuwa na hamu ya kushiriki kadiri stadi zao zilivyohitajiwa. Wao hulihesabu kuwa pendeleo kujitoa wenyewe na mali zao ili kusogeza mbele masilahi ya Ufalme wa Mungu kwa njia hiyo.

      Wafanyakazi wa kujitolea wa kimataifa huandaliwa makao na milo. Mara nyingi starehe ni ndogo kabisa. Mashahidi wenyeji huthamini sana yale yanayofanywa na ndugu zao wenye kuzuru, na inapowezekana, wao huwakaribisha nyumbani mwao, hata iwe sahili namna gani. Mara nyingi sana milo huliwa kwenye mahali pa kazi.

      Ndugu wa kutoka ng’ambo hawawi hapo ili kufanya kazi yote. Lengo lao ni kufanya kazi pamoja na kikundi cha ujenzi cha wenyeji. Na mamia, hata maelfu, ya wengine katika nchi huenda pia wakaja kusaidia wakati wa miisho-juma au kwa juma moja au zaidi kwa wakati mmoja. Katika Argentina, wenye kujitolea 259 kutoka nchi nyingine walifanya kazi pamoja na maelfu kadhaa ya ndugu wenyeji, baadhi yao walikuwapo kwa ajili ya kazi kila siku, wengine kwa majuma machache, na wengine zaidi wakati wa miisho-juma. Katika Kolombia, wenye kujitolea wa kimataifa zaidi ya 830 walisaidia kwa vipindi mbalimbali vya wakati. Kulikuwa pia wenye kujitolea wenyeji zaidi ya 200 walioshiriki katika mradi huo kwa wakati wote, na wasaidizi wengine 250 au zaidi kila mwisho-juma. Jumla ya zaidi ya watu mmoja-mmoja tofauti 3,600 walishiriki.

      Tofauti ya lugha yaweza kutokeza matatizo, lakini haizuii vikundi vya kimataifa visifanye kazi pamoja. Lugha ya ishara, ishara za uso, ucheshi, na tamaa ya kuona kazi itakayomheshimu Yehova ikikamilishwa husaidia kazi ifanywe.

      Ukuzi wa tengenezo wenye kutokeza—ukitokeza uhitaji wa makao makubwa ya tawi—nyakati nyingine hutokea katika nchi ambako idadi ya watu wenye stadi katika ufundi wa ujenzi ni ndogo. Lakini hicho si kizuizi miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, ambao husaidiana kwa furaha. Wao hufanya kazi pamoja wakiwa sehemu ya familia ya duniani pote ambayo haigawanywi na taifa, rangi ya ngozi, au lugha.

      Katika Papua New Guinea, wenye kujitolea waliotoka Australia na New Zealand kila mmoja alizoeza raia wa Papua New Guinea kazi yake ya kiufundi, kupatana na ombi la Idara ya Wafanyakazi ya Serikali. Katika njia hiyo, huku wakijitoa wenyewe, Mashahidi wenyeji walijifunza kazi za ufundi ambazo zingeweza kuwasaidia kutosheleza mahitaji yao wenyewe na ya familia zao.

      Wakati tawi jipya lilipohitajiwa katika El Salvador, wenye kujitolea 326 kutoka ng’ambo walijiunga na ndugu wenyeji. Kwa ajili ya mradi wa ujenzi katika Ekuado, Mashahidi 270 kutoka nchi 14 walifanya kazi pamoja na ndugu na dada Waekuado. Baadhi ya wenye kujitolea wa kimataifa walisaidia katika miradi kadhaa ya ujenzi iliyokuwa ikiendelea wakati uleule mmoja. Walifanya kazi kwa zamu katika mahali pa ujenzi katika Ulaya na Afrika, kulingana na uhitaji wa stadi zao za kiufundi.

      Kufikia 1992, wenye kujitolea wa kimataifa walikuwa wamepelekwa sehemu 49 za matawi ili kusaidia vikundi vya ujenzi vya wenyeji. Katika visa fulani wale waliopokea msaada kutokana na programu hii waliweza pia kuandaa usaidizi kwa wengine. Hivyo, wakiwa wamenufaika na kazi za bidii za watumishi wa muda mrefu wa kimataifa kama 60 waliosaidia na ujenzi wa mradi wa tawi katika Filipino, pamoja na wenye kujitolea zaidi ya 230 kutoka ng’ambo waliosaidia kwa vipindi vifupi zaidi, baadhi ya Wafilipino walijitoa wenyewe ili kusaidia kujenga vifaa katika sehemu nyingine za Kusini-Mashariki mwa Asia.

  • Kujenga Pamoja Duniani Pote
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
    • [Picha katika ukurasa wa 337]

      Wafanyakazi wa muda wa ujenzi waliotoka tu kuwasili kwenye makao makuu katika New York

      Kila kikundi hukumbushwa kwamba kuwa mtu wa kiroho na kufanya kazi bora hutangulizwa juu ya kufanya kazi haraka

  • Kujenga Pamoja Duniani Pote
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
    • [Picha katika ukurasa wa 338]

      Programu ya Ujenzi wa Kimataifa Hutimiza Mahitaji ya Haraka

      Ukuzi wa kasi wa tengenezo umetaka upanuzi wenye kuendelea wa ofisi, viwanda, na makao ya Betheli duniani pote

      Wenye kujitolea wa kimataifa hutoa usaidizi kwa Mashahidi wenyeji

      Hispania

      Njia za ujenzi zitumiwazo hufanya wenye kujitolea wengi wasiokuwa na ujuzi waweze kufanya kazi yenye thamani

      Puerto Riko

      Wafanyakazi stadi hutoa huduma zao kwa furaha

      New Zealand

      Ugiriki

      Brazili

      Matumizi ya vifaa vyenye kudumu husaidia kupunguza gharama za muda mrefu za udumishaji

      Uingereza

      Kazi bora sana hutokana na kupendezwa kwa binafsi kwa upande wa wenye kuifanya; hiyo ni wonyesho wa upendo wao kwa Yehova

      Kanada

      Ujenzi huo mbalimbali ni pindi za shangwe; urafiki mwingi wenye kudumu hufanyizwa

      Kolombia

      Ishara katika Japani zilikumbusha wafanyakazi juu ya hatua za usalama, pia juu ya uhitaji wa kuonyesha matunda ya roho ya Mungu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki