-
Sydney—Jiji la Bandari Lenye PilikapilikaAmkeni!—1999 | Julai 8
-
-
Daraja la Bandari ya Sydney—Uhandisi Bora
Kule nyuma mwaka wa 1815, uhitaji wa kujenga daraja la kuvuka bandari hiyo kutoka kaskazini kuelekea kusini ulifikiriwa kwa uzito, lakini rekodi ya kwanza ya mchoro wa daraja hilo ilitokea baadaye mwaka wa 1857. Leo, daraja hilo laanzia Dawes Point kwenye upande wa kusini wa bandari na kufikia Milsons Point kwenye ufuo wa kaskazini—mahali hususa ambapo palidokezwa kwa mara ya kwanza! Daraja hilo ambalo ni mojawapo ya madaraja yasiyo na nguzo yaliyo marefu zaidi ulimwenguni lilijengwa kwa miaka tisa na kugharimu takriban dola milioni 20 za Australia—kiasi kikubwa sana wakati wa mshuko wa uchumi mapema katika miaka ya 1930. Lilifunguliwa rasmi Machi 19, 1932.
Utao mkubwa wa katikati una urefu wa meta 503, na kimo cha meta 134 juu ya maji. Kuna meta 50 hivi katikati ya daraja na maji, jambo linalowezesha meli kubwa-kubwa kupitia chini ya daraja kwa usalama. Daraja lenyewe lina upana wa meta 49 na awali lilikuwa na reli mbili, njia mbili za tramu, barabara yenye nafasi sita za magari, na njia mbili za miguu. Mwaka wa 1959, Sydney lilianza kutumia mabasi badala ya tramu, na hivyo basi njia za tramu zilibadilishwa kuwa barabara. Sasa kuna barabara yenye nafasi nane za magari, mabasi, na malori. Urefu wote wa daraja hilo, kutia ndani mahali linapoanzia ni meta 1,149.
Kufikia miaka ya 1980, magari yalikuwa yakisongamana sana kwenye daraja hilo hivi kwamba kukawa na wazo la kujenga kivuko kingine cha bandari. Wakati huu ilikuwa bora kwenda chini ya maji. Basi, mnamo Agosti 1992, handaki la bandari lenye barabara yenye nafasi nne za magari lilifunguliwa.
Ukitembea kwenye daraja hilo unaona mandhari nzuri sana ya Sydney. Kwenye upande wa kaskazini wa bandari, ambao una miteremko yenye miti, kuna Makao ya Wanyama katika Hifadhi ya Taronga. Kwenye upande mwingine wa bandari na karibu chini ya daraja, kwenye Bennelong Point, kuna lile jumba kuu la opera la Sydney.
-
-
Sydney—Jiji la Bandari Lenye PilikapilikaAmkeni!—1999 | Julai 8
-
-
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Jumba la Opera la Sydney pamoja na daraja la bandari
[Picha zimeandiliwa na]
By courtesy of Sydney Opera House Trust (photograph by Tracy Schramm)
-