Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Seville Lango la Kuelekea Amerika
    Amkeni!—2003 | Julai 22
    • Mshale wa Kuonyesha Mwelekeo wa Upepo na Bustani ya Michungwa

      Hata hivyo, Seville, lilikuwa na enzi nyingine ya ufanisi muda mrefu kabla ya kuvumbuliwa kwa Amerika, na mengi ya majengo yake yenye fahari yalijengwa wakati huo wa mapema. Kwa karne nyingi Wamoori, ambao wengi wao walitoka Morocco, walitawala maeneo makubwa ya Hispania. Katika karne ya 12, watawala wa ukoo wa Almohad walilifanya Seville kuwa jiji lao kuu, na wakati huo walijenga msikiti ambao mnara wake ungali unaelekeana na jiji la kisasa.

      Wamoori walipofukuzwa Seville, wananchi waliubomoa msikiti huo wa jiji hilo ili kujenga kanisa la Seville, ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Ulaya (picha Na. 1). Hata hivyo, hawakutaka kuubomoa mnara wa msikiti huo uliokuwa maridadi sana, kwa hiyo, wakaufanya uwe mnara wa kengele wa kanisa, lililojengwa kando yake. Vipimo, matofali, na madirisha maridadi ya mnara huo huvutia sana kwenye kanisa hilo kubwa.

      Miaka 500 hivi iliyopita, uharibifu uliosababishwa na tetemeko la nchi ulilazimu sehemu ya juu ya mnara huo irekebishwe, na mshale wa shaba wa kuonyesha mwelekeo wa upepo uliwekwa mahali palipokuwa na kuba ya awali. Mnara huo ukapata jina lake la Kihispania La Giralda kutokana na mshale huo (picha Na. 2), nao umekuwa jengo maarufu la Seville. Wageni wenye nguvu za kupanda Giralda hiyo mpaka juu wanaweza kuliona vizuri jiji lote.

      Sehemu ya chini ya mnara wa kanisa hilo, kuna ua mdogo wa Wamoori uliokuwa sehemu ya msikiti wa awali, unaoitwa Patio de los Naranjos (Ua wa Michungwa). Nyua nyingi huko Andalusia zimetengenezwa kama ua huo uliopambwa kwa safu ya michungwa.b Na kwa kuwa barabara na bustani nyingi jijini Seville zina michungwa, wakati wa masika harufu ya michungwa inayochanua huenea katika jiji lote. Michungwa mingi ambayo ililetwa kwa mara ya kwanza na Wamoori bado imejaa jijini, na matunda yake hutumiwa kutengenezea jemu ya machungwa.

      Wafanyabiashara wa Seville huutegemea sana Mto Guadalquivir, unaopitia katikati ya jiji. Mto huo uliliwezesha jiji hilo kuwa bandari kuu ya Hispania kuelekea Amerika na bado meli hutumia bandari hiyo. Kuna bustani nyingi kwenye kingo za mto huo karibu katikati ya jiji. Na katika ukingo mmoja kuna kumbukumbu nyingine ya enzi za Wamoori huko Seville, La Torre del Oro, ule Mnara wa Dhahabu.—Picha Na. 3.

      Jina la mnara huo linatokana na wakati ambapo mnara huo ulikuwa umefunikwa kwa vigae vya rangi ya dhahabu. Hata hivyo, kusudi lake kuu lilikuwa ulinzi wala si mapambo. Wakati mmoja kulikuwa na mnyororo mzito kutoka katika Mnara wa Dhahabu hadi mnara-pacha mwingine uliokuwa ng’ambo ya pili ya mto, ambao uliwasaidia walinzi kudhibiti mashua zilizokuwa zikipita. Hapo ndipo meli kutoka Amerika zilikuwa zikipakua shehena zake za dhahabu na fedha. Siku hizi, badala ya yale majahazi yaliyokuwa yakipakua shehena yake mahali hapo, mashua za watalii ndizo hushusha abiria hapo kando ya Mnara wa Dhahabu.

      Bustani, Nyua, na Vigae

      Wamoori walijenga kasri na misikiti, na wakapanda bustani ili kuzipamba kasri zao. Kwa hiyo, Seville hujivunia kuwa na mojawapo ya kasri maridadi sana yenye bustani huko Hispania, inayoitwa Reales Alcázares, Kasri ya Kifalme (picha Na. 4). Kasri hiyo ilijengwa karne ya 12, lakini marekebisho makubwa yalifanywa katika karne ya 14. Hata hivyo, mtindo wa Kimoori umehifadhiwa na kwa kawaida wageni huvutiwa na jinsi vyumba na nyua zilivyopambwa kwa njia yenye kupendeza pamoja na matao, vigae vya rangi mbalimbali, na kuta zilizopigwa plasta kwa ustadi.

      Kasri hiyo imezungukwa na bustani yenye kupendeza yenye mabubujiko na mitende. Mtawala Mmoori hata alichimba mfereji wa maji wenye urefu wa kilometa 16 ili kuhakikisha kwamba bustani yake imetiliwa maji vizuri. Kasri hiyo na bustani zake inavutia kwelikweli hivi kwamba familia ya kifalme ya Hispania imeitumia kuwa moja ya makao yake rasmi kwa miaka 700.

      Kama tu vile michungwa hutokeza kivuli na harufu yenye kupendeza kwenye barabara za Seville, vigae vya rangi mbalimbali hufanya nyumba za jiji hilo ziwe za kipekee. Mtindo huo pia ulianzishwa nchini Hispania na Wamoori. Ilikuwa desturi yao kufunika kuta za ndani za vyumba vyao kwa vigae vilivyopambwa kwa michoro. Leo hii, vigae vya kupamba vya kila aina hurembesha upande wa nje wa nyumba, maduka, na nyumba za kifahari.

  • Seville Lango la Kuelekea Amerika
    Amkeni!—2003 | Julai 22
    • b Andalusia ni sehemu ya kusini kabisa ya Hispania, ambapo uvutano wa Kimoori uliodumu kwa karne nane hivi huonekana waziwazi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki