-
Kwa Nini Ninahangaikia Sana Uzito Wangu?Amkeni!—1999 | Aprili 22
-
-
Hata hivyo, ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula si tatizo pekee la ulaji, na wala si tatizo pekee lililoenea sana. Kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida ni ugonjwa unaoathiri idadi ya wasichana inayopita kwa mara tatu ile ya ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula. Kisha kuna kula kusikodhibitiwa, kunakohusiana kwa ukaribu na ugonjwa wa kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida. Acheni tuchunguze kwa ukaribu magonjwa haya.
Tatizo la Siri
“Hivi karibuni rafiki yangu aliungama kwamba yeye huleta chakula na kukila kwa siri. Kisha hujilazimisha kutapika. Yeye adai kwamba amekuwa akifanya hivyo kwa miaka miwili.” Kwa maneno haya, kijana mmoja, akiandikia safu moja ya ushauri kwenye gazeti, aeleza dalili zinazofanana na zile za tatizo la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.
Mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hula chakula kingi sana kwa kipindi kifupi cha wakati. Kisha mara nyingi huondoa chakula hicho mwilini kwa kujilazimisha kutapika.c Kwa kweli, wazo la kuondoa chakula tumboni kwa njia hii laweza kuonekana kuwa lenye kuchukiza. Hata hivyo, mfanya-kazi wa huduma za jamii Nancy J. Kolodny aandika hivi: “Kadiri unavyokula kwa wingi na kusafisha tumbo, ndivyo iwavyo rahisi kwako. Hisi zako za mapema za kuchukizwa au hata hofu hubadilishwa mara moja na kichocheo cha kurudia mazoea haya ya kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida.”
Tatizo la kukosa hamu ya chakula na la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida limeonwa kuwa “dalili tofauti za kisababishi kimoja.” Huku yakiwa na dalili zinazotofautiana, matatizo yote mawili huchochewa na tamaa kubwa ya chakula.d Hata hivyo, tofauti na tatizo la kukosa hamu ya chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida huweza kufichwa kwa urahisi. Kwa vyovyote, kula chakula kingi humzuia aliye na tatizo hilo kupunguza uzito, na kusafisha tumbo humzuia kuongeza uzito. Kwa sababu hiyo, yaelekea kwamba mwenye hamu ya chakula isiyo ya kawaida hatakuwa mnene sana wala mwembamba, na huenda mazoea yake ya kula yakaonekana kuwa ya kawaida hadharani. “Kwa miaka tisa,” asema mwanamke aitwaye Lindsey, “nilikula kupita kiasi na kutapika mara nne au tano kila siku. . . . Hakuna yeyote aliyejua tatizo langu la kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, kwa sababu kwa unafiki nilionyesha sura ya uhodari, furaha, na uzito wa mwili wa wastani.”
-
-
Kwa Nini Ninahangaikia Sana Uzito Wangu?Amkeni!—1999 | Aprili 22
-
-
Hatari za Kiafya
Matatizo yote matatu ya ulaji yanaweza kuhatarisha sana afya ya mtu. Kukosa hamu ya chakula kwaweza kusababisha utapiamlo mbaya sana, na katika visa vingi—wengine hukadiria kwamba asilimia 15 ya visa—huweza kusababisha kifo. Kula kupita kiasi, kuwe kunafuatwa na usafishaji wa tumbo au la, ni hatari kwa afya. Baada ya muda, kunenepa sana kwaweza kutokeza maradhi ya mishipa ya moyo yaliyo hatari kwa uhai, kisukari, na hata aina fulani za kansa. Kujilazimisha kutapika kwaweza kuharibu umio, na matumizi ya kupita kiasi ya dawa za kuharisha na kukojoza yaweza katika visa vibaya zaidi kusababisha shtuko la moyo.
Hata hivyo, kuna jambo jingine kuhusu matatizo ya ulaji linalohitaji kufikiriwa. Kwa kawaida wale walio na tatizo la kukosa hamu ya chakula, kuwa na hamu ya chakula isiyo ya kawaida, na kula kusikodhibitiwa hukosa furaha. Wao huelekea kukosa kujistahi, kuwa na mahangaiko na kuwa na mshuko-moyo. Kwa wazi, wanahitaji msaada. Lakini wale walio na tatizo la ulaji wanaweza kusaidiwaje kuepuka kuhangaikia sana uzito? Swali hili litazungumziwa katika makala ya wakati ujao katika mfululizo huu.
-