-
Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni PoteAmkeni!—2003 | Agosti 22
-
-
Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni Pote
“Ukija shuleni kesho, tutakuua.” —Mwanafunzi anayeitwa Kristen huko Kanada alipokea tisho hilo alipopigiwa simu na msichana ambaye hakutaja jina lake.a
“Kwa kawaida siathiriwi sana kihisia, lakini mambo yalizidi kiasi cha kwamba sikutaka kwenda shuleni. Niliumwa na tumbo, na kila asubuhi baada ya kula nilitapika.”—Hiromi, mwanafunzi huko Japan, anaeleza jinsi alivyodhulumiwa.
JE, UMEWAHI kudhulumiwa? Wengi wetu tumedhulumiwa, angalau wakati fulani. Huenda ni shuleni au kazini au hata nyumbani, ambapo dhuluma imezidi sana siku hizi. Kwa mfano, chanzo kimoja cha habari huko Uingereza kinakadiria kwamba asilimia 53 ya watu wazima huambiwa maneno yanayoumiza na wapenzi wao au wenzi wao wa ndoa. Wadhalimu na watu wanaodhulumiwa wanaweza kuwa wa kike au wa kiume, au watu wa tabaka lolote lile.
Ni nini maana ya kudhulumiwa? Mara nyingi dhuluma huhusisha matukio mengi madogo-madogo ambayo hufanywa kwa muda fulani bali si tukio moja au matukio machache tu. Dan Olweus, ambaye ni mtaalamu wa akili na mwanzilishi wa uchunguzi kuhusu dhuluma, anasema kwamba kwa kawaida dhuluma inahusisha kufanya ujeuri kimakusudi na kuwadhulumu watu wanyonge waziwazi.
Huenda ufafanuzi wa neno dhuluma hauhusishi aina zote za dhuluma, lakini limefafanuliwa kuwa “kutaka kumuumiza mtu mwingine kimakusudi na kumfadhaisha.” Yule anayedhulumiwa hufadhaika anapotendewa vibaya au hata kwa sababu anaogopa yale atakayotendewa. Matendo hayo ni kama vile kumdhihaki, kumchambua kila wakati, kumtusi, kumsengenya, na kumshurutisha afanye mambo asiyoweza kufanya.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 4.
Kristen, msichana aliyetajwa mwanzoni, alidhulumiwa na wanafunzi wenzake kwa miaka mingi. Alipokuwa katika shule ya msingi, wanafunzi waliomdhulumu walikuwa wakitia chingamu kwenye nywele zake, walikuwa wakimfanyia mzaha kuhusu sura yake, na kumtisha kwamba wangempiga. Alipokuwa katika shule ya sekondari, mambo yalizidi kiasi cha kwamba alipokea vitisho kupitia simu. Sasa akiwa na umri wa miaka 18, anasema hivi kwa masikitiko: “Mtu huenda shuleni kusoma, bali si kuteswa au kutishwa kwamba atauawa.”
Mtaalamu mmoja wa akili anasema hivi: ‘Watu fulani hujisikia vizuri wanapomwaibisha mtu mwingine. Hilo ni jambo la kuhuzunisha lakini la kawaida katika mahusiano ya wanadamu.’ Tabia hiyo inapozidi, huenda ikamfanya yule anayetendewa hivyo kulipiza kisasi kwa jeuri na hata kusababisha msiba. Kwa mfano, mfanyakazi mmoja wa kusafirisha abiria aliyekuwa na tatizo la usemi, alidhihakiwa na kudhulumiwa sana hivi kwamba hatimaye aliwaua wafanyakazi wenzake wanne halafu akajipiga risasi.
Dhuluma Iko Ulimwenguni Kote
Ulimwenguni kote watoto wenye umri wa kwenda shule hukabili dhuluma. Uchunguzi uliofanywa na kuchapishwa katika gazeti la Pediatrics in Review ulionyesha kwamba asilimia 14 ya watoto huko Norway huwadhulumu wengine au hudhulumiwa. Nchini Japan, asilimia 15 ya wanafunzi wa shule za msingi wanasema kwamba wao hudhulumiwa, na asilimia 17 hudhulumiwa huko Australia na Hispania. Mtaalamu mmoja anakadiria kwamba watoto milioni 1.3 hudhulumiwa au kuwadhulumu wengine nchini Uingereza.
Profesa Amos Rolider wa Chuo cha Emek Yizre’el aliwahoji wanafunzi 2,972 wa shule 21. Kulingana na gazeti The Jerusalem Post, profesa huyo aligundua kuwa “asilimia 65 walilalamika kwamba walipigwa makofi au mateke, walisukumwa, na kunyanyaswa na wanafunzi wenzao.”
Kuna mbinu mpya ya dhuluma yenye kudhuru ambayo inahusisha kutuma vitisho kwa simu za mkononi na kompyuta. Pia, vijana wanaochochewa na chuki huwadhulumu wengine kwa kuandika habari mbaya zinazotia ndani habari za kibinafsi na kuziweka kwenye Internet. Kulingana na Dakt. Wendy Craig wa Chuo Kikuu cha Queen’s huko Kanada, mbinu hiyo ya dhuluma “humdhuru sana mtoto anayedhulumiwa.”
Kazini
Wafanyakazi wengi zaidi wanalalamika kuhusu dhuluma kazini. Katika nchi fulani, inasemekana kwamba dhuluma inatukia mara nyingi zaidi kuliko ubaguzi wa rangi au kusumbuliwa kingono. Kila mwaka, asilimia 20 hivi ya wafanyakazi nchini Marekani hudhulumiwa.
Huko Uingereza, ripoti moja iliyotolewa katika mwaka wa 2000 na Chuo Kikuu cha Manchester cha Sayansi na Tekinolojia ilisema kwamba kati ya wafanyakazi 5,300 wa mashirika 70, asilimia 47 waliripoti kwamba walikuwa wameshuhudia dhuluma katika miaka mitano iliyopita. Katika mwaka wa 1996, Muungano wa Ulaya ulifanya uchunguzi katika nchi 15 ambazo ni wanachama wa muungano huo na kuwahoji wafanyakazi 15,800. Asilimia 8 ya waliohojiwa, yaani, wafanyakazi milioni 12 hivi, walisema kwamba walitishwa au kudhulumiwa.
Inaonekana aina zote za dhuluma hufanana kwa njia moja, hata iwe zinatukia shuleni au kazini—nguvu hutumiwa kumuumiza au kumwaibisha mtu mwingine. Lakini, kwa nini watu fulani huwadhulumu wengine? Matokeo ni nini? Na suluhisho ni nini?
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina yamebadilishwa.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Wadhalimu wa Aina Mbalimbali
◼ Wanaotumia Jeuri: Hawa ndio rahisi kutambua. Wanapokasirika wao humpiga mtu wanayemdhulumu, humsukuma, humpiga mateke, au kuharibu mali yake.
◼ Wanaotumia Matusi: Hawa hutumia maneno ili kuwaumiza au kuwaaibisha wengine kwa kuwabandika majina, kuwatukana, au kuwadhihaki tena na tena.
◼ Wanaoharibu Mahusiano: Hawa hueneza uvumi mbaya kuwahusu wengine. Wanawake wanaodhulumu wengine hupenda kutumia mbinu hii.
◼ Wanaolipiza Kisasi: Hawa ni watu ambao wamegeuka kuwa wadhalimu baada ya kudhulumiwa. Kudhulumiwa si udhuru wa kuwadhulumu wengine, bali kunatusaidia kuelewa kwa nini watu hao wamekuwa wadhalimu.
[Hisani]
Source: Take Action Against Bullying, by Gesele Lajoie, Alyson McLellan, and Cindi Seddon
-
-
Dhuluma Baadhi ya Visababishi na MatokeoAmkeni!—2003 | Agosti 22
-
-
Dhuluma Baadhi ya Visababishi na Matokeo
KWA NINI mtoto huanza kuwadhulumu wengine? Ikiwa umewahi kudhulumiwa, huenda ukasema kwamba, “Hata sababu iwe nini hakuna udhuru wa kumdhulumu mwingine.” Na huenda maoni yako ni sawa. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya udhuru na sababu. Sababu zinazomfanya mtoto awadhulumu wengine hazifanyi tabia yake mbaya ikubalike, lakini zinaweza kutusaidia kuielewa. Na ni muhimu sana kuelewa kwa nini anatenda hivyo. Kwa nini?
Methali moja ya kale inasema hivi: “Ufahamu wa mtu hakika hupunguza hasira yake.” (Mithali 19:11, NW) Tukikasirishwa na tabia ya mdhalimu tunaweza kukata kauli kimakosa, na hivyo kufadhaika sana na hata kumchukia. Lakini tukiielewa tabia yake tunaweza kupunguza hasira yetu. Hilo linaweza kutusaidia kuwa na maoni yanayofaa tunapotafuta masuluhisho. Kwa hiyo, hebu tuchunguze visababishi kadhaa vya tabia hiyo mbaya.
Kwa Nini Watu Huwadhulumu Wengine?
Wadhalimu wengi huiga mfano mbaya wa wazazi wao au walipuuzwa kabisa na wazazi wao walipokuwa watoto. Wengi wana wazazi ambao si wachangamfu, wasiojali, au ambao wamewawekea watoto wao mfano mbaya kwa kushughulikia matatizo kwa hasira na jeuri. Huenda watoto ambao wamelelewa kwa njia hiyo wasione kwamba wanawadhulumu wengine kwa maneno na matendo yao ya jeuri. Huenda hata wakafikiri kwamba tabia yao ni sawa kabisa.
Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 16 ambaye alidhulumiwa na baba yake wa kambo na vilevile na wanafunzi wenzake shuleni, alibadilika kuwa mdhalimu alipofika darasa la saba. Anasema hivi: “Nilikuwa na hasira nyingi; nilimdhulumu mtu yeyote tu. Kuhisi uchungu si jambo dogo. Mtu anapoumizwa, yeye hutaka kuwaumiza wengine pia.” Ijapokuwa kwa kawaida wasichana wanaowadhulumu wengine hawatumii jeuri, wao huwadhulumu wengine kwa sababu wamekasirika.a
Shule nyingi huwa na wanafunzi wengi ambao wamelelewa kwa njia zinazotofautiana sana. Kwa kusikitisha, watoto fulani huwa wajeuri kwa sababu wamefundishwa nyumbani kwamba kuwatisha wengine na kuwatusi ndizo njia bora za kupata wanachotaka.
Inasikitisha kwamba mara nyingi njia hizo hufaulu. Shelley Hymel, ambaye ni mshauri msaidizi kwenye Chuo Kikuu cha British Columbia, Kanada, amechunguza tabia za watoto kwa miaka ishirini. Anasema hivi: “Kuna watoto ambao wanajua jinsi ya kupata wanachotaka, na inasikitisha kwamba wao hufanikiwa wanapowadhulumu wengine. Wao hufaulu kupata wanachotaka, yaani, wanapata mamlaka, hadhi na umashuhuri.”
Ukosefu wa mwongozo ni jambo jingine linalofanya dhuluma iongezeke. Watu wengi wanapodhulumiwa huhisi kwamba hakuna mtu anayeweza kuwasaidia na inasikitisha kwamba hali huwa hivyo mara nyingi. Debra Pepler, mkurugenzi wa Kituo cha LaMarsh cha Utafiti Kuhusu Jeuri na Masuluhisho ya Ugomvi kwenye Chuo Kikuu cha York huko Toronto, alifanya uchunguzi kuhusu wanafunzi wa shule na akagundua kwamba walimu hutambua na kukomesha karibu asilimia 4 tu ya visa vya dhuluma.
Hata hivyo, Dakt. Pepler anaamini kwamba ni muhimu kukomesha hali hiyo. Anasema hivi: “Watoto hawawezi kutatua tatizo hilo kwa sababu linahusu nguvu, na mdhalimu hupata nguvu zaidi kila mara anapomdhulumu mtu.”
Kwa hiyo, kwa nini visa vingi vya dhuluma haviripotiwi? Ni kwa sababu wale wanaodhulumiwa huamini kwamba wakiripoti jambo hilo, huenda mambo yakawa mabaya zaidi. Hivyo, vijana wengi huwa na wasiwasi kwa kadiri fulani na hukosa usalama katika miaka yao ya shule. Ni nini matokeo ya hali hiyo?
Athari za Kimwili na Kihisia
Ripoti ya shirika moja la wataalamu wa akili huko Marekani inasema kwamba kila siku zaidi ya watoto 160,000 hukosa kwenda shule kwa sababu wanaogopa kudhulumiwa. Huenda wale wanaodhulumiwa wakaacha kuzungumza juu ya shule au juu ya somo fulani au shughuli fulani hususa ya shuleni. Huenda wakajaribu kuchelewa kwenda shuleni kila siku au kuhepa masomo fulani au hata kutoa udhuru ili wasiende shuleni.
Watoto wanaodhulumiwa wanaweza kutambuliwaje? Huenda wakanuna, wakakasirika haraka, wakavunjika moyo, wakaonekana wachovu, au wakajitenga. Wanaweza kuwadhulumu watoto wenzao nyumbani au marafiki zao. Watoto wanaoshuhudia wengine wakidhulumiwa huathiriwa pia. Hali hiyo huwaogopesha sana na hudhoofisha uwezo wao wa kujifunza.
Hata hivyo, gazeti Pediatrics in Review lasema hivi: “Tokeo baya zaidi la dhuluma miongoni mwa wale waliodhulumiwa na katika jamii ni jeuri, na hiyo inatia ndani kujiua na kuwaua wengine. Watoto wanaodhulumiwa huhisi kwamba hawana nguvu kabisa hivi kwamba wengine wao huamua kujiua au kuwaua wengine.”
Dakt. Ed Adlaf, mtafiti na profesa wa afya ya umma kwenye Chuo Kikuu cha Toronto, anasema kuwa “kuna uwezekano mkubwa kwamba wadhalimu au wanaodhulumiwa wataumia kihisia sasa na baadaye.” Katika mwaka wa shule wa 2001, zaidi ya wanafunzi 225,000 huko Ontario walihojiwa, na kati ya robo na thuluthi ya wanafunzi hao walidhulumiwa au kuwadhulumu wengine. Mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa amefikiria sana kujiua.
Mtu anapodhulumiwa sana anaweza kuacha kujiamini, kupatwa na magonjwa hatari, na hata kushindwa kuendelea na kazi. Huenda watu wanaodhulumiwa wakaumwa na kichwa, wakakosa usingizi, wakawa na wasiwasi, na hata kushuka moyo. Wengine hupata ugonjwa fulani unaosababishwa na mfadhaiko. Ijapokuwa mtu anapoumizwa kimwili anaweza kuhurumiwa sana, mambo huwa tofauti anapoumizwa kihisia. Watu hawawezi kujua kwa urahisi kwamba anaumia. Kwa hiyo badala ya kumhurumia, huenda marafiki na watu wa familia wakachoshwa na malalamiko yake.
Wadhalimu pia huathiriwa na dhuluma. Wasipokomeshwa wanapokuwa wadogo, huenda wakawadhulumu wafanyakazi wenzao wanapokuwa watu wazima. Miradi fulani ya uchunguzi inaonyesha kwamba watu waliokuwa wadhalimu walipokuwa watoto walikuwa na tabia hiyohiyo hata walipokuwa watu wazima. Pia, kuna uwezekano mkubwa kwamba watakuwa wahalifu.
Jinsi Familia Inavyoathiriwa
Dhuluma inayotukia kazini huathiri muungano na amani katika familia. Mtu anayedhulumiwa kazini anaweza kuchochewa kuwaumiza watu wa familia yake na wasielewe kwa nini anafanya hivyo. Isitoshe, hilo linaweza kumfanya mwenzi wake wa ndoa au mtu mwingine katika familia hiyo amuunge mkono na kujaribu kulipiza kisasi isivyofaa. Kwa upande mwingine, mwenzi wake wa ndoa anaweza kumlaumu kwamba amesababisha tatizo hilo. Visa hivyo vya dhuluma vinapoendelea, hata wenzi ambao hapo awali walijitahidi kusaidia hushindwa kuvumilia hali hiyo. Kadiri miaka inavyopita, familia hizo hukabili uwezekano mkubwa wa kuvunjika.
Nyakati nyingine, dhuluma inaweza kusababisha mtu apoteze kazi na kukosa riziki, kutengana, talaka, au hata kujiua. Kati ya nusu na thuluthi mbili ya Waaustralia waliodhulumiwa wakiwa kazini walisema kwamba jambo hilo liliathiri mahusiano yao pamoja na watu walio karibu sana nao kama vile wapenzi wao, wenzi wao wa ndoa, au familia zao.
Hasara za Dhuluma
Dhuluma inayotukia kazini huwasababishia waajiri hasara. Mtu anayewadhulumu wengine kazini anaweza kuwa mwajiri anayesema mambo ya kuumiza au mfanyakazi anayepanga njama, na anaweza kuwa mwanamume au mwanamke. Watu wa aina hiyo huwadhibiti wengine kupita kiasi, huzingatia mambo madogo-madogo, na kuwadharau wengine kwa kusema mambo ya kuwavunja moyo au kwa kuwachambua kila wakati, na mara nyingi huwaaibisha mbele ya watu. Mara nyingi wadhalimu hawatambui ujeuri wao wala kuomba radhi kwa ajili ya tabia yao. Mara nyingi wao huwadhulumu wafanyakazi wenye bidii, waaminifu, na wanaopendwa sana na wafanyakazi wengine.
Kwa kawaida wafanyakazi wanaodhulumiwa hawafanyi kazi vizuri. Wafanyakazi wengine wanaoshuhudia dhuluma hiyo huathiriwa pia na hushindwa kufanya kazi vizuri. Dhuluma inaweza kuwafanya wafanyakazi wasiwe waaminifu kwa mwajiri wao na wasifanye kazi kwa bidii. Ripoti moja inasema kwamba dhuluma husababisha hasara ya dola bilioni tatu kila mwaka katika Muungano wa Uingereza. Na inasemekana kwamba tabia hiyo husababisha zaidi ya asilimia 30 ya magonjwa yanayotokana na mfadhaiko.
Ama kweli, dhuluma huathiri watu ulimwenguni pote. Lakini, je, kuna jambo linaloweza kufanywa ili kudhibiti na kukomesha tatizo hilo?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kawaida, wasichana huwadhulumu wenzao kwa kujitenga nao na kueneza uvumi. Hata hivyo, inaonekana sasa wasichana wengi wanatumia jeuri pia.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Inasikitisha kwamba dhuluma ni jambo la kawaida kazini
[Picha katika ukurasa wa 7]
Watu wanaodhulumiwa kila wakati wanaweza kufadhaika na kuhisi upweke
-
-
Kuacha UdhalimuAmkeni!—2003 | Agosti 22
-
-
Kuacha Udhalimu
‘Mdhalimu anaweza kubadili tabia yake.’—Dakt. C. Sally Murphy.
MDHALIMU na yule anayedhulumiwa wanahitaji msaada. Mdhalimu anahitaji kujifunza jinsi ya kushirikiana na wengine bila kuwadhulumu. Na yule anayedhulumiwa anahitaji kujua jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mara nyingi, mdhalimu hajui jinsi ya kushirikiana na wengine wala haelewi jinsi wale ambao anawadhulumu wanavyohisi. Anahitaji kuongozwa na kufundishwa jinsi ya kueleza maoni yake vizuri. Kitabu Take Action Against Bullying kinasema hivi: “Wadhalimu wasipobadili tabia yao, wao huendelea daima kuwadhulumu wengine. Wao huwadhulumu wenzi wao, watoto wao, na hata labda wafanyakazi walio chini yao kazini.”
Msaada wa Kuacha Kuwadhulumu Wengine
Kuwazoeza watoto kuwa na huruma toka utotoni kwaweza kuwasaidia wasiwe wadhalimu. Walimu katika nchi fulani wameanza kuwafundisha watoto kuelewa hisia za wengine. Wao huwafundisha hata watoto walio na umri wa miaka mitano kuelewa hisia za wengine na kuwatendea watu kwa fadhili. Ijapokuwa hakuna habari nyingi kuhusu faida za kudumu za elimu hiyo, matokeo yaliyopatikana kufikia sasa yanaonyesha kwamba wale ambao wamefundishwa kuwahurumia wengine si wajeuri kama wale ambao hawajafundishwa.
Wewe mzazi unapaswa pia kuwafundisha watoto wako jinsi ya kuwahurumia wengine badala ya kutarajia tu wafundishwe jambo hilo shuleni. Ikiwa hutaki mtoto wako awe mdhalimu, unapaswa kumfundisha kwa maneno na kwa matendo jinsi ya kuwatendea wengine kwa heshima na adhama. Ni nini kinachoweza kukusaidia? Huenda tayari una kitu bora kinachoweza kukusaidia kufundisha lakini kinachopuuzwa sana, yaani, Neno la Mungu, Biblia. Kinaweza kukusaidiaje?
Kwa mfano, kinaeleza waziwazi maoni ya Mungu kuhusu dhuluma. Anaichukia kabisa! Biblia inasema hivi kumhusu Mungu: “Nafsi yake humchukia . . . mwenye kupenda udhalimu.” (Zaburi 11:5) Isitoshe, Mungu anajua mambo yanayoendelea. Biblia inaeleza jinsi alivyohuzunika wakati Waisraeli walipoteseka “kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.” (Waamuzi 2:18) Katika pindi nyingi, Mungu aliwaadhibu wale waliotumia nguvu zao kuwadhulumu wanyonge na wasioweza kujitetea.—Kutoka 22:22-24.
Biblia pia ina ushauri unaojulikana sana kuhusu kuelewa hisia za wengine. Yesu alisema hivi: “Mambo yote mtakayo watu wawafanyie nyinyi, lazima mwafanyie wao pia hivyohivyo.” (Mathayo 7:12) Si rahisi kuwafundisha watoto kuipenda na kuitumia hiyo Kanuni Bora maishani mwao. Ni lazima uwawekee mfano bora, ukazie jambo hilo mara nyingi, na ujitahidi sana, hasa kwa sababu watoto wachanga hujipenda. Lakini jitihada hizo zote zina faida kubwa. Watoto wako wakijifunza kuwa wenye fadhili na kuelewa hisia za wengine, wataepuka kabisa kuwadhulumu wengine.
Msaada kwa Wanaodhulumiwa
Watu wanaodhulumiwa, hasa vijana, wanakabili ugumu fulani, yaani, kutulia na kutenda kwa busara wanaposhambuliwa. Mtu anapokudhulumu, huenda anataka uumie kihisia. Anataka ukasirike sana au uogope. Ukipandwa na hasira au ukilia na kuonyesha kwamba umeumia au unaogopa, basi mdhalimu amefaulu. Kwa hiyo, huenda akajaribu kukuumiza tena na tena.
Unaweza kufanya nini? Zingatia madokezo yafuatayo. Yameandikwa hasa kwa ajili ya vijana, lakini kanuni zilizomo zinahusu pia watu wazima wanaodhulumiwa.
◼ Tulia. Usipandwe na hasira. Biblia inatoa shauri hili la hekima: “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu.” (Zaburi 37:8) Ukipanda mori, unamfanya mdhalimu akudhibiti, na huenda ukafanya mambo ambayo utayajutia baadaye.—Mithali 25:28.
◼ Jitahidi kuepuka kufikiria kulipiza kisasi. Mara nyingi mtu anayelipiza kisasi ndiye anayeumia zaidi. Kulipiza kisasi hakuridhishi hata kidogo. Msichana mmoja ambaye alipigwa na vijana watano alipokuwa mwenye umri wa miaka 16, anasema hivi: “Niliazimia kulipiza kisasi. Kwa hiyo, niliwaomba marafiki zangu wanisaidie kuwashambulia vijana wawili kati ya wale walionipiga.” Matokeo yakawa nini? Anasema hivi: “Nilihisi vibaya sana.” Baada ya hapo tabia yake ikaharibika hata zaidi. Kumbuka maneno haya yenye hekima ya Biblia: “Msirudishe ovu kwa ovu kwa yeyote.”—Waroma 12:17.
◼ Ukiona kwamba mambo yanachacha, ondoka haraka. Biblia inasema hivi: “Acheni ugomvi kabla haujafurika.” (Mithali 17:14) Yaani, jaribu kuwaepuka wadhalimu. Mithali 22:3 inasema hivi: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia.”
◼ Udhalimu ukiendelea, huenda ikakubidi useme waziwazi. Chagua wakati ambapo umetulia, umtazame mdhalimu ana kwa ana, na uzungumze kwa sauti thabiti bila wasiwasi. Mweleze kwamba hupendi yale anayofanya, kwamba hayafurahishi na yanaumiza. Usimtusi wala kumtisha.—Mithali 15:1.
◼ Zungumza na mtu mzima anayetegemeka na anayejali kuhusu jinsi unavyodhulumiwa. Mweleze tatizo lako waziwazi, na umwombe msaada wa kukabiliana nalo. Pia, unaposali mwambie Mungu jambo hilo kwani yeye ndiye chanzo bora zaidi cha msaada na faraja.—1 Wathesalonike 5:17.
◼ Kumbuka kwamba una thamani. Mdhalimu anaweza kukufanya uhisi kwamba wewe ni bure, kwamba unastahili kudhulumiwa. Lakini yeye hastahili kuamua lolote kukuhusu. Mungu ndiye hakimu, naye huona sifa nzuri za kila mmoja wetu. Mdhalimu ndiye anayejivunjia heshima kwa kuwadhulumu wengine.
Enyi Wazazi, Walindeni Watoto Wenu
Wazazi pia wanaweza kuanza mapema kuwafundisha watoto wao kutenda kwa busara wanapokabiliana na wadhalimu. Kwa mfano, wanaweza kucheza michezo ya kuigiza pamoja nao ili kuwafundisha jinsi wanavyoweza kuonyesha kwamba wanajiamini.
Hata kusimama wima kwaweza kuonyesha kwamba unajiamini na kuwafanya wadhalimu waogope kukudhulumu. Pia ni muhimu kumtazama mdhalimu uso kwa uso, kutuliza mikono, na kuzungumza kwa sauti imara. Wazazi wanatiwa moyo wamfundishe mtoto kuwaondokea na kuwaepuka wadhalimu, na kuomba msaada wa mtu mzima anayeaminika, kama vile mwalimu.
Kuielimisha familia ndiyo hatua ya kwanza ya kukomesha dhuluma. Wazazi wanaotumia wakati pamoja na watoto wao na kusikiliza matatizo yao kwa subira na huruma, huwafanya wahisi wanathaminiwa, wanaungwa mkono, na kwamba wanapendwa. Wataalamu wengi wanaotoa mashauri kuhusu kulea watoto na kushughulika na matatizo ya vijana huwatia moyo wazazi kuwasaidia watoto wao kuwa na maoni mazuri kujihusu. Wakiwa na maoni hayo mazuri, uwezekano wa kushambuliwa utapungua.
Lakini kuzungumza hakutoshi. Kila mtu katika familia anahitaji kujifunza kuwatendea wengine kwa heshima na kwa adhama na kuelewa hisia za wengine. Kwa hiyo, usikubali dhuluma yoyote katika familia yako. Fanya nyumba yako iwe mahali salama, mahali penye heshima na upendo.
Mwisho wa Dhuluma
“Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.” (Mhubiri 8:9, chapa ya 1989) Hivyo ndivyo Biblia inavyoeleza kwa ufupi historia ya wanadamu. Naam, wanadamu wamedhulumiwa kwa maelfu ya miaka. Mwandikaji mmoja wa Biblia alisema: “Nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”—Mhubiri 4:1.
Hata hivyo, hapana shaka kwamba Mungu anaona dhuluma yote inayotukia ulimwenguni, na anawahurumia wale wanaodhulumiwa. Lakini je, ataleta suluhisho? Bila shaka! Ona ahadi yake kwenye Mika 4:4: “Wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”
Hebu wazia jinsi ulimwengu utakavyokuwa ahadi hiyo itakapotimia. Hakuna mtu atakayewatia wengine hofu—la, hakutakuwa na wadhalimu! Je, unavutiwa na wazo hilo? Lakini zaidi ya kutoa ahadi hiyo, Mungu amefanya mengi zaidi. Sasa hivi kuna programu ya kuwafundisha watu Biblia ambayo inaendelea ulimwenguni pote, nayo ina matokeo mazuri sana. Wale wanaofaidika kutokana nayo wanafundishwa kubadili sifa zao mbaya za jeuri, kudumisha amani kati yao, na kuwatendea wengine kwa heshima na kwa adhama. (Waefeso 4:22-24) Hivi punde, matokeo ya mafundisho hayo bora yataonekana duniani pote, na dhuluma haitakuwapo tena. Ahadi za Mungu zilizomo katika Biblia zitatimia. Kila mtu atakayekuwapo wakati huo atafurahia kuishi katika ulimwengu usio na wadhalimu!
[Picha katika ukurasa wa 8]
Kumwondokea mdhalimu si jambo la kuaibikia
[Picha katika ukurasa wa 9]
Kukiwa na hali nzuri katika familia, watoto hufundishwa kukabiliana na aina zote za dhuluma
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wafundishe watoto wako kusema waziwazi na kwa uthabiti, lakini kwa busara
-