-
Biashara Iliyoanza KaleAmkeni!—2001 | Februari 22
-
-
Biashara Iliyoanza Kale
Karakana ya John ya useremala ilikuwa karakana iliyojengwa vyema na yenye vifaa vingi zaidi katika eneo lao. Aliionea fahari na shangwe. Lakini moto ulizuka usiku mmoja. Baada ya muda wa saa chache, karakana yake nzuri iliteketea kabisa.
HAPO awali, John alifikiria kukata bima ya moto kwa kutumia kiasi fulani cha fedha za ujenzi wa karakana yake. Hata hivyo, akasababu hivi: ‘Mimi ni mwangalifu sana. Na moto usipozuka kamwe, basi nitakuwa nimepoteza fedha kwa kukata bima.’ Lakini moto ulizuka. Endapo John angekuwa ameikatia bima karakana yake, yamkini angeweza kuijenga upya. Lakini hangeweza kuijenga bila bima.
Bima Ni Nini?
Si lazima bima iwe biashara ambayo mtu anatarajia kurudishiwa fedha zake. Wala si kamari. Mcheza-kamari hujasiria hatari, ilhali bima huandaa ulinzi dhidi ya hatari zilizopo. Bima ni njia ya kushiriki hatari na wengine.
Tangu nyakati za kale, jamii zimekuwa zikichanga baadhi ya rasilimali zake ili kuwasaidia watu wanaopata hasara. Miaka 3,500 hivi iliyopita, Musa aliagiza taifa la Israeli litoe fungu la mazao yake pindi kwa pindi kwa ajili ya “mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe.”—Kumbukumbu la Torati 14:28, 29.
Mwanzo wa Bima
Bima imekuwapo kwa maelfu ya miaka. Sheria za Hammurabi zilitaja bima fulani ya malipo, sheria hizo zilitia ndani sheria za Babiloni ambazo yadhaniwa zilitangulia Sheria ya Musa. Ili kugharimia safari zao za kibiashara nyakati za kale, wamiliki wa meli waliomba mikopo kutoka kwa wawekezaji. Iwapo meli ingezama, wamiliki hawakuwa na wajibu wa kulipa mikopo hiyo. Kwa kuwa meli nyingi zilirejea salama salimini, faida iliyolipwa na wamiliki wengi wa meli hizo ilitosha kuwapa faida wakopeshaji.
Mojawapo ya kampuni mashuhuri zaidi za bima ulimwenguni, Lloyd’s of London, iliibuka baadaye kutokana na shughuli hizohizo za baharini. Kufikia mwaka wa 1688, Edward Lloyd alikuwa akiendesha mkahawa ambamo wafanyabiashara wa London na wafanyakazi wa benki walikutana ili kufanya biashara za ziada. Humo wadhamini waliowapa mabaharia kandarasi za bima waliandika majina yao chini ya kiasi fulani hususa cha fidia ambacho walikuwa tayari kutoa baada ya kupokea malipo fulani ya bima. Hao watoaji-bima wakaanza kuitwa watoaji wa hati za bima (underwriters). Hatimaye, kampuni ya Lloyd’s ikawa shirika rasmi la bima mnamo mwaka wa 1769, na muda si muda ikasitawi na kuwa kampuni kubwa zaidi ya bima ya hatari za baharini.
Shughuli za Bima Leo
Watu wanapokata bima leo, wangali wanashiriki hatari yao na wengine. Makampuni ya kisasa ya bima huchunguza takwimu zinazoonyesha hasara zilizotokea awali—kwa mfano, hasara za mioto kuteketeza karakana—ili kujaribu kukisia hasara ambayo wateja wao watakabili wakati ujao. Kampuni ya bima hutumia fedha zinazolipwa na wateja wengi ili kulipa fidia kwa wateja wanaopata hasara.
Je, wahitaji bima? Ikiwa ndivyo, ni bima ipi inayofaa hali zako? Uwe na bima au la, ni tahadhari zipi zinazoweza kukusaidia kukabiliana kwa mafanikio na hatari maishani?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Mojawapo ya kampuni mashuhuri zaidi za bima ulimwenguni ilianzia kwenye mkahawa
[Hisani]
Courtesy of Lloyd’s of London
-
-
Je, Wahitaji Bima?Amkeni!—2001 | Februari 22
-
-
Je, Wahitaji Bima?
BIMA fulani ni za lazima katika nchi fulani. Katika nchi nyingine, bima nyingi hata hazijulikani. Isitoshe, gharama ya bima na fidia inayotolewa hutofautiana sana nchi hadi nchi. Lakini kanuni ya msingi ya bima—kushiriki hatari—haibadiliki.
Kwa kawaida, mtu anayemiliki mali nyingi huwa katika hatari ya kupata hasara kubwa. Vivyo hivyo, athari zinakuwa kubwa zaidi wakati mtu aliye na wajibu mkubwa zaidi wa kifamilia anapokufa au kulemaa. Kuwa na bima kwaweza kuondoa mahangaiko kuhusu hatari ya kupoteza mali au kulemazwa na aksidenti.
Lakini, je, ni hekima kukata bima ingawa huenda mtu asidai kamwe malipo? Je, kubeba gurudumu la ziada garini ni kupoteza fedha kwa kuwa huenda gurudumu hilo lisitumiwe? Dereva aweza kuchochewa kununua gurudumu la ziada kwa sababu linamfanya ajihisi akiwa salama. Ijapokuwa malipo ya kifedha hayawezi kugharimia hasara fulani, huenda yakagharimia hasara nyinginezo.
Bima hugharimia hasara zipi?
Aina za Bima
Bima nyingi zinazokatwa na watu huainishwa chini ya bima za mali, wajibu, afya, ulemavu, na bima ya maisha.
Bima ya mali: Kukata bima kwa uharibifu wa mali—nyumba, biashara, gari, au mali nyinginezo—ni miongoni mwa mipango maarufu sana ya kudhibiti hasara. Hiyo ndiyo bima ambayo John, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, aliamua kutokata kwa ajili ya karakana na vifaa vyake vya useremala.
Bima fulani za nyumbani hutia ndani bima ya vifaa fulani vilivyo nyumbani. Endapo unakata bima hii, ni hekima kwako kuorodhesha vifaa vyako vya nyumbani vyenye bima, na uvipige picha au kuvirekodi kwenye video ikiwezekana. Orodha hiyo pamoja na makadirio yoyote au risiti za ununuzi wa vifaa hivyo yapasa kuhifadhiwa mahali salama wala si nyumbani mwako. Madai ya bima yaweza kushughulikiwa haraka zaidi ukiwa na rekodi hizo.
Bima ya wajibu: Mtu yeyote anayeendesha gari, anayemiliki nyumba au mali nyingine isiyohamishika, anayeendesha biashara, au kuajiri wengine ana wajibu wa kulipia hasara ya aksidenti. Aksidenti hiyo yaweza kusababisha uharibifu wa mali, majeraha au kifo cha mtu mwingine. Dereva wa gari au mmiliki wa mali au biashara aweza kuwajibika kulipa gharama ya urekebishaji wa mali au ya matibabu au hata kwa ajili ya maumivu na mateso yanayompata mwingine. Katika nchi nyingi waajiri na madereva wanatakiwa na sheria kuwa na bima ya wajibu ili kulipia gharama hizo. Hata mahali ambapo bima si takwa la kisheria, dereva, mmiliki wa mali, au mwajiri aweza kuwa na wajibu wa kisheria au wa kiadili wa kuwasaidia wahasiriwa wa aksidenti au familia zao.
Bima ya afya: Nchi nyingi zina bima fulani inayogharimiwa na serikali ambayo inaandaa malipo kama vile malipo ya uzeeni na kulipia matibabu ya wazeewazee. Lakini, hata katika nchi zenye mpango huo, bima hiyo yaweza kulipia tu sehemu ya gharama za matibabu au yaweza kulipia tu matibabu fulani. Kwa hiyo, baadhi ya watu hukata pia bima binafsi ili kuwasaidia kulipia gharama zinazosalia. Katika sehemu nyingi wafanyakazi wanaweza kukatiwa bima ya afya wanapoajiriwa.
Mipango fulani ya huduma ya afya, kutia ndani mipango ya utunzaji wa afya na mashirika ya huduma ya afya (HMO), huandaa utunzaji muafaka wa kitiba kwa ada fulani ya kila mwezi au mwaka. Mashirika hayo hujitahidi kupunguza gharama kwa kuandaa huduma za kitiba za gharama ya chini na kwa kuzuia magonjwa. Hata hivyo, katika shirika la HMO, mgonjwa huweza tu kuhudumiwa na madaktari fulani tu au kupokea tiba fulanifulani tofauti na bima ya kawaida ya afya.
Bima ya ulemavu na bima ya maisha: Bima ya ulemavu humpa marupurupu fulani mtu aliyejeruhiwa kiasi cha kutoweza kufanya kazi. Bima ya maisha huwasaidia kifedha wale wanaomtegemea mtu fulani endapo anakufa. Bima hizo zimesaidia familia nyingi kulipa madeni na kujiruzuku maishani baada ya mkimu wa familia kujeruhiwa au kufa.
Kupata Watoa-Bima Wenye Kutegemeka
Bima hutegemea mpango wa kulipa fedha sasa ili kupata ulinzi wa kifedha wakati ujao, kwa sababu hiyo biashara ya bima huvutia walaghai wengi sana. Ndivyo ilivyo katika nchi zinazositawi na zile zilizositawi kiuchumi. Kwa hiyo, ni hekima kujihadhari na zile zinazoitwa eti bima za malipo nafuu na mipango mingine ya bima yenye kutiliwa shaka. Wateja wengi sana wenye matumaini wameambulia patupu wakati makampuni hayo yanaposhindwa kulipa madai yao—au yanapotokomea ghafula!
Kama ilivyo na ununuzi mwingineo muhimu, ni hekima kulinganisha malipo ya makampuni mbalimbali ya bima, na mara nyingi kufanya hivyo huokoa fedha. Mathalani, makampuni fulani hutoza malipo ya chini ya bima ya afya kwa wale wasiovuta sigareti na ya bima ya gari kwa wale waliofaulu mtihani wa udereva. Mteja anayetafuta bima anaweza kupataje kampuni ya bima inayotegemeka?
Hatua ya kwanza yaweza kuwa kujua maoni ya watu wengine kuhusiana na makampuni na mawakala mbalimbali wa bima. Huenda marafiki na majirani wakajua ubora wa huduma zinazotolewa na kampuni fulani au unyoofu na upendezi binafsi kuelekea wateja wa wakala fulani. Ni vizuri kuwa chonjo kusikia habari zinazotaja makampuni ya bima yenye matatizo.
Isitoshe, rekodi ya kampuni na hali yake ya kifedha yaweza kuchunguzwa kwa kusoma miongozo ya kutathmini makampuni ya bima inayopatikana katika maktaba au maduka ya vitabu au kwenye Internet. Miongozo hiyo yaweza kujibu maswali kama vile: Je, kampuni hiyo ni salama kifedha? Je, imekuwa ikitoa bima kwa mafanikio kwa miaka mingi? Je, yajulikana kwa kushughulikia madai himahima na kwa njia ya kirafiki?
Hata hivyo, miongozo ya kutathmini makampuni ya bima haipasi kuonwa kuwa haiwezi kukosea. Kampuni moja ya bima yenye rasilimali za mabilioni ya dola na iliyodumu kwa muda mrefu, ilichukuliwa na serikali juma moja tu baada ya kusifiwa kuwa bora zaidi na kitabu kimoja maarufu!
Kazi ya Mawakala wa Bima
Kwa kawaida wakala wa bima huwakilisha kampuni mahususi ya bima. Dalali, au wakala aliyejiajiri, aweza kuwasiliana na makampuni mbalimbali ya bima ili kujua bima bora iliyopo kwa malipo fulani hususa. Wote wanahitaji kudumisha uhusiano mzuri na wateja ili biashara yao ifaulu. Wakala wa bima anaweza kuwasaidia sana wateja wake akiwa mwenye kutumainika na akipendezwa nao kibinafsi.
Kwanza, wakala au dalali mzuri anaweza kumsaidia mteja kuchagua bima inayofaa kati ya orodha ndefu ya bima zilizopo. Atamweleza pia mteja wake kinaganaga kuhusu bima hiyo. Kama wengi wajuavyo, hati za bima huwa na mambo mengi sana. Msimamizi wa kampuni moja ya bima alikiri kwamba hakufahamu masuala mengine ya bima ya nyumba yake!
Maelezo ya wakala yanaweza kumsaidia mteja aepuke kutamauka. Kwa mfano, bima nyingi za mali na afya zinatozwa ada fulani. Hicho ni kiasi fulani hususa ambacho lazima mteja wa bima alipe—tuseme, kwa ajili ya urekebishaji wa gari au gharama za matibabu—kabla kampuni ya bima haijalipa fungu lake la madai. Wakala anaweza pia kumtetea mteja wake endapo mteja huyo anakosa kulipwa na kampuni ya bima.
Bima na Wakristo
Je, Mkristo anayetumaini kupata msaada wa Mungu na ambaye anatarajia mwisho wa mfumo wa mambo anahitaji bima? Huko nyuma katika mwaka wa 1910, watu fulani walimwuliza swali hilo Charles Taze Russell, mhariri wa gazeti ambalo leo linajulikana kama Mnara wa Mlinzi, na gazeti-jenzi lake la Amkeni! Russell alikiri kwamba Biblia hutabiri mwisho wa mfumo wa sasa wa kiuchumi, lakini akaongezea kwamba yeye binafsi hakuwa na bima ya maisha.
“Lakini hali za watu zinatofautiana,” akasema Russell. “Baba anayetegemewa na mke na watoto—ikiwa watoto hao ni wachanga mno kujiruzuku—ana wajibu kuwaelekea.” (1 Timotheo 5:8) Mwanamume anaweza kutenga fedha kwa ajili ya familia yake, akasema Russell. “Na kama hawezi kufanya hivyo, anaweza kutimiza wajibu wake kuwaelekea kwa kuwawekea bima ya maisha.”
Yule mwenye wajibu wa familia anaweza pia kuwaandalia washiriki wake bima ya afya, ulemavu, na bima nyinginezo. Waseja wengi hukata bima ili kuweza kupokea huduma muhimu vilevile kuepuka kuwa na deni kwa sababu ya aksidenti au ugonjwa.
Unyoofu ni muhimu sana kwa habari ya bima. Mkristo wa kweli hatadanganya kamwe kampuni ya bima, ama anapojaza ombi la bima au anapodai malipo. (Waebrania 13:18) Atakumbuka kwamba kusudi la bima ni kugharimia hasara. Si tiketi ya bahati nasibu—fursa ya kuishi raha mustarehe.—1 Wakorintho 6:10.
Wakristo hutii sheria zote zinazohusiana na matakwa kama vile kukata bima. Wao hutii wakati ambapo sheria husema kwamba lazima wawe na bima inayofaa ili kuendesha biashara au kuendesha gari. (Waroma 13:5-7) Mtu mnyoofu na mwenye hekima inayotumika hulipa pia malipo yote ya bima. Kampuni yaweza kufutilia mbali bima na kukataa kulipa madai ikiwa bima hailipiwi. Ni jambo la busara kuhakikisha mara kwa mara kwamba bima inalipiwa kwa kuwasiliana moja kwa moja na kampuni hiyo na kuhifadhi hati ya malipo, kama vile nakala ya hundi ulizolipa.
Iwe bima yapatikana unakoishi au la, kuna tahadhari za msingi zinazoweza kukusaidia uepuke hasara na hivyo kujilinda na kuwalinda wapendwa wako kutokana na maumivu ambayo hayawezi kuponywa na madai yoyote ya bima. Sasa tutachunguza baadhi ya tahadhari hizo.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wakala anayetumainika anaweza kukusaidia kufanya maamuzi kuhusu bima
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wengi wana bima, iwe ni takwa la kisheria au la
-
-
Bima Ambayo Kila Mtu AnahitajiAmkeni!—2001 | Februari 22
-
-
Bima Ambayo Kila Mtu Anahitaji
UWE waishi mahali ambapo bima ni kawaida au mahali ambapo haipatikani, kuna bima moja ambayo kila mtu anaweza na anapaswa kuwa nayo. Kwa kuwa “bima” yaweza kurejezea “mpango wa kupata ulinzi au usalama,” unaweza kupataje bima ya aina hiyo?
Unaweza kuipata kwa kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hatari unazokabili. Biblia yasema kwamba “wakati na tukio lisilotazamiwa” huathiri kila mtu. (Mhubiri 9:11, NW) Lakini, ukiepuka kujihatarisha isivyo lazima, uwezekano wa kujeruhiwa au kupata hasara hupungua.
Fikiria Wakati Ujao
Kuwa na hekima inayotumika ni ulinzi. Unapokuwa na ufanisi fulani wa kiuchumi, unaweza kuweka akiba fulani kwa ajili ya wakati wa hari—wakati wa uhitaji. Katika nyakati za kale mwanamume mcha-Mungu aitwaye Yosefu alijipatia sifa ya kuwa “mtu wa akili na hekima” kwa kuweka akiba ya nafaka kwa ajili ya nchi yote ya Misri kulipokuwa na shibe. Nchi ilipokumbwa na njaa hatimaye, hatua ya Yosefu iliandalia chakula si Wamisri tu bali pia jamaa yake mwenyewe.—Mwanzo 41:33-36.
Tunaweza kujilinda pia kwa kuwa wenye kiasi katika matumizi. Tunaweza kuweka akiba ya fedha na kupunguza mkazo kwa kutokimbilia daima vifaa vipya, mitindo, au vitumbuizo—zoea ambalo halituletei usalama halisi. Kwa kweli, kama ilivyotajwa awali, kuna uwezekano mkubwa wa kuibiwa au kupata hasara unapomiliki vitu vingi vya kimwili.—Luka 12:15.
Jali Usalama Wako
Tunaweza kupunguza sana hatari maishani kwa kujali tu usalama. Ni aksidenti ngapi mbaya sana zingeweza kuepukwa endapo kila mtu angeendesha gari kwa uangalifu na kwa mwendo salama? Fikiria pia, uhai ambao ungeokolewa ikiwa kila mtu angeepuka kuendesha gari akiwa mchovu au baada ya kunywa kileo. Pia kuna hatari nyingine za uendeshaji-gari tunazoweza kudhibiti.
Kwa mfano, sheria za nchi nyingi zimepiga marufuku kutumia simu ya mkononi unapoendesha gari. Uchunguzi mmoja ulifikia mkataa wa kwamba kutumia simu hiyo huzidisha mara nne hatari ya aksidenti kutukia. Hatari hiyo ni sawa na hatari ya kupata aksidenti unapoendesha gari huku kipimo cha kileo katika damu yako kikiwa cha asilimia 0.1, sheria za sehemu mbalimbali huwaona watu wenye kipimo hicho kuwa walevi mno kuendesha gari.
Kujifunga mkanda wa usalama kwa ukawaida hupunguza pia hatari ya madereva na abiria kufa. Lakini usidhani kamwe kwamba kuwa na vifaa vya usalama kama vile mikanda ya usalama na mifuko ya kinga au kuwa na bima hukuruhusu kujihatarisha. Utafiti waonyesha kwamba maoni hayo husababisha aksidenti zaidi.
Kujali usalama ni bima nzuri nyumbani na kazini pia. Je, makazi na mahali pako pa kazi ni nadhifu bila hatari yoyote? Kagua kila mahali. Je, kuna kitu chochote njiani kinachoweza kuwakwaa watu? Je, vifaa vyenye makali au vilivyo moto—meko, vipasha-joto, pasi—vimewekwa mahali ambapo vinaweza kuwakata au kuwaunguza watu? Je, kuna rundo la karatasi au vifaa vingine vinavyoweza kushika moto? Uwe mwangalifu sana kuhusu hatari kwa watoto. Kwa mfano, je, vileo na bidhaa nyingine za kusafishia zenye sumu zimewekwa mahali pasipofikiwa na watoto wadogo?
Tunza Afya Yako
Kwa kutunza afya yako ifaavyo, unaweza kupunguza hatari ya magonjwa. Kuhusu hilo, kuwa na ujuzi kwaweza kuwa kama bima. Jihadhari na hatari kwa afya yako, na uchukue hatua mara moja matatizo ya afya yanapozuka. Jambo la muhimu zaidi, jifunze jinsi ya kutunza afya yako na ya familia yako. Kumbuka msemo wa jadi: “Kukinga ni bora kuliko kutibu.”
Kwa muda mrefu gazeti la Amkeni! limeandaa habari ambayo huwatia watu moyo kuishi kulingana na kanuni za Biblia na hivyo kuepuka mazoea na mitindo ya maisha inayodhuru afya. Mathalani, miongoni mwa habari nyingi zinazozungumziwa katika Amkeni! zimekazia umuhimu wa usafi, mlo unaofaa, kupata usingizi wa kutosha, na kufanya mazoezi kwa ukawaida na vilevile uhitaji wa kudhibiti mkazo na hekaheka za maisha.
Bima Muhimu Sana
Katika ulimwengu huu usio mkamilifu, bima yaweza kuwa mpango unaofaa sana, lakini hakuna bima iwayo yote inayoweza kutulinda kikamili au kulipia kikamili hasara zetu. Lakini, wawe na bima au la, kuna watu walio na uhakika wa kwamba hawataachwa peke yao. Kwa nini? Kwa sababu misiba inapozuka, wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo—wale wanaomtumikia Baba yake, Yehova Mungu—hujitahidi sana kusaidiana.—Zaburi 83:18; Yakobo 2:15-17; 1 Yohana 3:16-18.
Isitoshe, Yehova mwenyewe anaahidi kutowaacha kamwe watumishi wake waaminifu. Mtunga-zaburi wa Biblia aliandika hivi: ‘Baba yangu na mama yangu wakiniacha, BWANA atanikaribisha kwake.’ (Zaburi 27:10) Akiwa Chanzo cha uhai, Yehova anaweza kuwafufua wafu, na Biblia yasema kwamba amempa Mwanawe, Yesu Kristo, uwezo wa kufufua wafu. (Zaburi 36:9; Yohana 6:40, 44) Lakini, Neno la Mungu laonyesha kwamba si wote watakaofufuliwa. (Yohana 17:12) Hivyo basi, twaweza kufanyaje ili tukumbukwe na Mungu wakati wa ufufuo?
Kwa wazi, Yesu alizungumzia bima yenye kutegemeka zaidi katika Mahubiri yake maarufu ya Mlimani. Alisema: “Komeni kujiwekea akiba ya hazina duniani, ambako nondo na kutu hula kabisa, na ambako wezi huvunja na kuiba. Badala ya hivyo, jiwekeeni akiba ya hazina mbinguni, ambako wala nondo wala kutu haili kabisa, na ambako wezi hawavunji na kuiba. Kwa maana ilipo hazina yako, ndipo moyo wako utakapokuwa pia.”—Mathayo 6:19-21.
Mara nyingi watu hufikiria kujiwekea akiba ya fedha wakitumaini kwamba itawawezesha kuishi raha mustarehe wanapozeeka. Hata hivyo, Yesu alitaja bima iliyo salama zaidi. Thamani yake haina kifani, haitashindwa kamwe! Alieleza hivi: ‘Hii yamaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.’—Yohana 17:3.
Kwa kutwaa ujuzi sahihi juu ya Mungu na Mwanawe na kutumia yale tunayojifunza maishani mwetu, tutajijengea jina zuri na Mungu. (Waebrania 6:10) Mtume Petro na mtume Yohana, wakitegemeza itikadi zao kwa mafundisho ya Bwana wao, Yesu Kristo, walikazia kwamba mfumo uliopo wa utawala wa wanadamu utakoma. Lakini, Yohana akaeleza: “Yeye ambaye hufanya mapenzi ya Mungu hudumu milele.”—1 Yohana 2:17; Mathayo 24:3, 14; 2 Petro 3:7, 13.
Tunaweza kuwa na hakika kwamba ikiwa tutamtumikia Mungu kisha tufe, atatufufua au ikiwa tutakuwa hai anapoleta mwisho wa mfumo huu wa mambo, atatuhifadhi tukiwa hai hadi kwenye ulimwengu wake mpya wa uadilifu. Kwa kweli, Mungu anaahidi ‘kufuta kabisa kila chozi kutoka katika macho [yetu]’ na kufanya “vitu vyote kuwa vipya.” (Ufunuo 21:4, 5) Kumtumikia Mungu na kutumaini kabisa ahadi zake kwa kweli ni bima bora kupita zote. Kila mtu anaweza kuipata.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Kujali usalama na kutunza afya ni kama bima
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kujifunza kumhusu Mungu na kufanya mapenzi yake ndiyo bima bora zaidi ya wakati ujao
-