Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wakristo na Mfumo wa Tabaka
    Amkeni!—1998 | Machi 8
    • Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo na Mfumo wa Tabaka

      Wahindu wengi waligeuzwa imani na wamishonari Wareno, Wafaransa, na Waingereza, ambao walikuwa Wakatoliki na Waprotestanti, wakati wa ukoloni. Watu kutoka matabaka yote wakawa Wakristo kwa jina tu, wahubiri fulani wakiwavutia Wabrahman, wengine wakiwavutia Wasioguswa. Mafundisho na mwenendo wa wamishonari yaliathirije itikadi katika mfumo wa tabaka iliyokuwa imepenya kwa kina kirefu?

      Kuhusu Waingereza walio India, mwandishi Nirad Chaudhuri asema kwamba makanisani “kutaniko la Wahindi halingeketi pamoja na Wazungu. Utambuzi wa ubora wa kijamii ambao ulitegemeza utawala wa Uingereza juu ya India haukufichwa na Ukristo.” Akionyesha mtazamo kama huo, katika 1894 mmishonari mmoja aliripoti kwenye Kamati ya Misheni za Kigeni ya Marekani kwamba kugeuza imani watu wa tabaka la chini kulikuwa ni “kukusanya takataka Kanisani.”

      Kwa wazi, ile hisia ya ubora wa kijamii kwa upande wa wamishonari wa mapema na mchanganyiko wa mafundisho ya Kibrahman na mafundisho ya kanisa yamechangia sana mfumo wa tabaka ambao unaungwa mkono waziwazi na wengi wanaojiita eti Wakristo katika India.

      Tabaka Katika Makanisa Leo

      Askofu Mkuu Mkatoliki George Zur, alipokuwa akihutubia Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa India katika 1991, alisema: “Wageuzwa-imani wa Scheduled caste hawaonwi kuwa wa tabaka la chini na Wahindu wa tabaka la juu peke yao bali pia na Wakristo wa tabaka la juu. . . . Mahali palipotengwa huwekwa kando kwa ajili yao katika makanisa ya parokia na katika makaburi. Ndoa za mseto kati ya tabaka huchukiwa . . . Itikadi ya tabaka imeenea sana miongoni mwa makasisi.”

      Askofu M. Azariah, wa Kanisa la Church of South India, ambalo ni la United Protestant Church, alisema katika kitabu chake The Un-Christian Side of the Indian Church: “Kwa hiyo Wakristo wa Scheduled Caste (Dalit) hubaguliwa na kuonewa na Wakristo wenzao walio katika makanisa yao kadhaa na si kutokana na kosa lao bali kwa sababu ya kuzaliwa katika matabaka ya chini, hata wanapokuwa ni Wakristo wa kizazi cha 2, 3 au 4. Wakristo wa tabaka la juu ambao ni wachache Makanisani huendeleza ubaguzi wao wa tabaka hata baada ya vizazi kadhaa, bila kuathiriwa na imani na mazoea ya Kikristo.”

      Uchunguzi wa serikali juu ya matatizo ya jamii za hali ya chini katika India, unaojulikana kuwa Tume ya Mandal, ulipata kwamba wanaojidai kuwa Wakristo katika Kerala waligawanyika katika “vikundi mbalimbali vya kikabila kwa kutegemea matabaka yao. . . . Hata baada ya kugeuzwa, wageuzwa-imani wa tabaka la chini walizidi kuonwa kuwa Harijanb . . . Wasiria na Wapulaya ambao ni washiriki wa Kanisa lilelile walifanya desturi za kidini wakiwa wamejitenga katika majengo mbalimbali.”

      Ripoti ya habari katika Indian Express katika Agosti 1996 ilisema hivi kuhusu Wakristo wa Dalit: “Katika Tamil Nadu, maeneo yao ya makazi hutengwa na matabaka ya juu. Katika Kerala, wao ni vibarua wasio na mashamba, na wao hufanyia kazi Wakristo wa Siria na wengine wa matabaka ya juu walio na mashamba. Hakuna kula pamoja au ndoa za mseto kamwe kati ya Dalit na Wakristo wa Siria. Katika visa vingi, Dalit huabudu katika makanisa yao, yanayoitwa ‘kanisa la Pulaya’ au ‘kanisa la Paraya.’” Haya ni majina ya matabaka madogo-madogo.

      Maitikio ya Kutoridhika

      Vikundi vya watu wa kawaida wenye kuteta, kama vile FACE (Baraza Linalopinga Kutumiwa Vibaya kwa Wakristo), vinataka serikali iwasaidie Wakristo wa Dalit. Hangaiko kubwa ni msaada wa kiuchumi kwa Wakristo wageuzwa-imani. Hata hivyo, wengine wanahangaikia jinsi mambo yanavyotendeka kanisani. Katika barua waliyoandikia Papa John Paul wa Pili, karibu waweka-sahihi 120 walitaarifu kwamba walikuwa “wameukubali Ukristo ili wakombolewe kutoka kwenye mfumo wa tabaka” lakini sasa hawaruhusiwi kuingia katika kanisa la kijijini au kushiriki ibada. Walilazimishwa kujenga nyumba kandokando ya mtaa mmoja ambao hakuna Mkristo yeyote wa tabaka la juu—wala kasisi wa parokia—ambaye aliwahi kwenda! Vivyo hivyo mwanamke mmoja Mkatoliki mwenye kutaabishwa alisema: “Bila shaka ni jambo la maana kwangu kwa mwana wangu kusoma katika chuo cha elimu kilicho bora. Lakini ni jambo la maana hata zaidi aonwe kuwa sawa na waumini wenzake [Wakatoliki].”

      Ingawa wengine wanajaribu kuboresha hali ya Wakristo wa Dalit, wengi wanakosa subira. Mashirika kama vile Vishwa Hindu Parishad (Shirika la Wahindu Ulimwenguni) vinajaribu kuwarudisha tena wageuzwa-imani Wakristo ndani ya kundi la Wahindu. Sherehe iliyohudhuriwa na watu 10,000, iliripotiwa na gazeti Indian Express, ambayo zaidi ya familia 600 za aina hiyo za “Kikristo” zilikubali tena Dini ya Hindu.

      Njia ya Kweli ya Kikristo

      Ikiwa wamishonari wa mashirika ya makanisa wangefundisha mafundisho ya Kristo yenye kutegemea upendo, hakungekuwa na “Wakristo wa Brahma,” wala “Wakristo wa Dalit,” wala “Wakristo wa Paraya.” (Mathayo 22:37-40) Hakungekuwa na makanisa yaliyotengwa kwa ajili ya Dalit na hakungekuwa na kubaguliwa wakati wa milo. Ni jipi fundisho la Biblia ambalo hushinda tofauti za kitabaka?

      “Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu . . . . asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.”—Kumbukumbu la Torati 10:17.

      “Sasa nawahimiza nyinyi kwa bidii, akina ndugu, kupitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kwamba nyote mseme kwa upatano, na kwamba kusiwe na migawanyiko miongoni mwenu, bali kwamba mpate kuunganishwa kwa kufaa katika akili ileile na katika mstari uleule wa fikira.”—1 Wakorintho 1:10.

      “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”—Yohana 13:35.

      Biblia hufundisha kwamba Mungu alifanya wanadamu wote kutoka kwa mtu mmoja. Pia husema kwamba wazao wote wa mtu huyo mmoja wanapaswa ‘wamtafute Mungu na wampate, ijapokuwa, kweli, yeye hayuko mbali sana na kila mmoja wetu.’—Matendo 17:26, 27.

      Wakati tofauti za kitabaka zilipoanza kuingia katika kutaniko la Kikristo la mapema, mwandikaji Yakobo, chini ya upulizio, alizishutumu waziwazi. Alisema: “Nyinyi mna tofauti za kitabaka miongoni mwenu wenyewe nanyi mmekuwa mahakimu mkitoa maamuzi maovu, je, sivyo ilivyo?” (Yakobo 2:1-4) Mafundisho ya kweli ya Kikristo hayaruhusu kuwe na mfumo wa tabaka wa aina yoyote.

  • Wakristo na Mfumo wa Tabaka
    Amkeni!—1998 | Machi 8
    • Mtu Huhisi Namna Gani?

      Ndiyo, mtu huhisi namna gani anapotendewa kama wa tabaka la chini na watu wanaodai kuwa Wakristo? Mkristo mmoja, ambaye wazazi wake waliokufa walikuwa wamegeuzwa imani kutoka kwa tabaka la Dini ya Hindu inayojulikana kuwa Cheramar au Pulaya asimulia kisa kilichotukia katika jimbo la nyumbani kwao la Kerala miaka kadhaa iliyopita:

      Nilialikwa kwenye arusi ambapo idadi kubwa ya wageni walikuwa washiriki wa kanisa. Waliponiona kwenye sehemu ya makaribisho, vurugu fulani ilitokea, na wale waliokuwa wa Kanisa la Othodoksi la Siria walisema kwamba hawangebaki katika sehemu hiyo ya makaribisho ila tu nikiondoka, kwa kuwa hawangekula pamoja na mtu wa tabaka la pulaya. Wakati baba ya bibi-arusi alipokataa sharti lao, waligomea mlo huo kwa pamoja. Walipoondoka, mlo uliandaliwa. Lakini wale waliokuwa wakihudumu walikataa kuondoa jani la mgomba nililotumia kama sahani na kusafisha meza yangu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki