Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Magumu ya Vita Yalinitayarisha kwa Ajili ya Maisha
    Amkeni!—2004 | Juni 22
    • Nilihamia Jamhuri ya Afrika ya Kati

      Nilitumwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na mishonari wengine. Kifaransa kilikuwa lugha rasmi ya nchi hiyo, lakini tulilazimika kujifunza Kisango ili tuweze kuwahubiria watu wengi. Tulitumwa tuanzishe makao ya mishonari katika mji wa Bambari, karibu kilometa 300 kutoka Bangui, jiji kuu la nchi hiyo. Ingawa mji wa Bambari haukuwa na stima wala maji ya mabomba, makutaniko mawili ya huko yalihitaji msaada wetu. Mambo niliyojionea wakati wa vita huko Ulaya yalinisaidia sana kuvumilia hali za maisha huko Bambari na vilevile sehemu nyingine tulizoishi baadaye.

      Baada ya kutumikia kwa miaka miwili huko Bambari, nilipewa mgawo wa kutembelea makutaniko nikiwa mwangalizi asafiriye. Kulikuwa na makutaniko 40 hivi nchini humo, nami nilikaa kwa juma moja na kila kutaniko nililogawiwa. Nilikuwa na gari dogo, lakini barabara za vumbi zilipokuwa mbovu, nilitumia usafiri wa umma.

      Bangui ndipo palipokuwa mahali pekee pa kurekebishia magari nchini humo. Kwa kuwa nilihitaji kusafiri sana katika huduma yangu, nilinunua vifaa fulani pamoja na vitabu vyenye mwongozo wa kurekebisha magari, hivyo mara nyingi nilikuwa nikijirekebishia gari langu. Wakati mmoja mwanzi wa beringi ya mtaimbo-endeshi ulivunjika na gari likakwama. Nyumba iliyokuwa karibu ilikuwa umbali wa kilometa 60 hivi kutoka nilipokuwa. Nilikata mti kutoka kwenye msitu na kutengeneza mwanzi wa beringi. Nikitumia mafuta mengi, niliuunganisha kwa waya kwenye mtaimbo-endeshi na kufaulu kuendelea na safari yangu.

      Ilikuwa vigumu kutumikia katika maeneo ya mashambani kwa sababu ni wachache tu waliojua kusoma au kuandika. Katika kutaniko moja, ni mtu mmoja tu aliyejua kusoma na alikuwa na kigugumizi. Funzo la Mnara wa Mlinzi lilikuwa gumu sana, lakini imani yangu iliimarishwa nilipoona kutaniko hilo likijitahidi sana kuelewa habari zilizozungumziwa.

      Baadaye niliwauliza jinsi walivyofaidika ikiwa hawakuzielewa habari hizo vizuri. Jibu walilotoa lilitia moyo sana: “Sisi hutiana moyo.”—Waebrania 10:23-25.

      Ingawa wengi wa ndugu zangu Wakristo hawakujua kusoma na kuandika, walinifunza mengi juu ya maisha na jinsi ya kuishi. Nilianza kuthamini umuhimu wa shauri la Maandiko la ‘kuwaona wengine kuwa bora.’ (Wafilipi 2:3) Ndugu zangu Waafrika walinifundisha mengi kuhusu upendo, fadhili, na ukarimu na jinsi ya kuishi mashambani. Sasa nilielewa kwa ukamili maneno ambayo Ndugu Nathan Knorr, ambaye wakati huo alikuwa msimamizi wa Shule ya Gileadi, alisema katika hotuba yake ya kutuaga wakati wa kufuzu kutoka shule hiyo. Alisema: “Tuwe wanyenyekevu, tusifikiri tunajua kila kitu. Hatujui mambo yote. Tuna mengi sana ya kujifunza.”

      Kuishi Katika Maeneo ya Mashambani ya Afrika

      Niliishi na ndugu wenyeji nilipotembelea makutaniko mbalimbali. Kwa kawaida, juma la ziara yangu lilikuwa kipindi cha sherehe, hasa kwa watoto. Hiyo ni kwa sababu washiriki wa kutaniko nililotembelea walikuwa wakienda kuwinda au kuvua samaki ili kuhakikisha kuna chakula cha kumtosha kila mtu.

      Nilipokuwa nikiishi na akina ndugu katika vibanda vyao, nilikula vyakula vingi kutia ndani mchwa na nyama ya tembo. Nyani waliliwa mara nyingi. Nguruwe wa mwituni na nungunungu hasa walikuwa watamu sana. Hata hivyo, kuna siku ambazo chakula hakikuwa kingi. Ilichukua muda kuzoea chakula hicho kipya, lakini hatimaye tumbo langu liliweza kumeng’enya karibu kila aina ya chakula. Nilijifunza kwamba kula papai pamoja na mbegu zake kunafaidi tumbo.

      Mambo mengi yasiyotazamiwa yanaweza kutokea katika maeneo ya mashambani. Wakati mmoja nilidhaniwa kuwa mzuka unaoishi ndani ya maji. Watu wengine wanaamini kwamba mzuka unaweza kumvuta mtu na kumtumbukiza majini. Pindi moja nilipotoka kuoga mtoni, msichana mmoja aliyekuwa amekuja kuteka maji aliniona, akapiga mayowe na kutoroka. Shahidi mwenzangu alipojaribu kuwaeleza kwamba mimi ni mhubiri anayetembelea eneo hilo wala si mzuka, watu hawakuamini. Walisema, “Mzungu hawezi kamwe kuja hapa msituni.”

      Mara nyingi nililala nje kwa kuwa kulikuwa na hewa safi. Nyakati zote nilibeba neti kwa sababu ilinilinda kutokana na nyoka, nge, panya, na vinginevyo. Neti ilinilinda mara kadhaa nilipovamiwa na siafu. Usiku mmoja nilimulika neti kwa tochi nikaona siafu wengi. Nilitoroka kwa sababu ingawa siafu ni wadogo, wanaweza hata kuwaua simba.

      Nilipokuwa katika eneo la kusini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, karibu na Mto Kongo, niliwahubiria Mbilikimo ambao ni wawindaji hodari na wanajua vyakula vinavyoweza kuliwa na visivyoweza kuliwa. Baadhi yao huzungumza Kisango, na walifurahi kusikiliza. Walikubali tuwarudie, lakini tuliporudi hatukuwapata kwani walikuwa wamehamia eneo lingine. Wakati huo hakuna Mbilikimo aliyepata kuwa Shahidi, lakini baadaye nilipata kujua kwamba baadhi yao wamekuwa Mashahidi katika Jamhuri ya Kongo.

      Nilitumikia nikiwa mwangalizi wa mzunguko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa miaka mitano. Nilisafiri kotekote nchini, mara nyingi nikitembelea makutaniko yaliyo mashambani.

  • Magumu ya Vita Yalinitayarisha kwa Ajili ya Maisha
    Amkeni!—2004 | Juni 22
    • [Picha katika ukurasa wa 20]

      Nikiwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, niliishi katika vijiji kama hiki

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki