Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Watoto Mashakani
    Amkeni!—1999 | Aprili 8
    • Watoto Mashakani

      “Wakati, nishati, na uangalifu usipotolewa kwa ajili ya watoto, matatizo yote ya kibinadamu ambayo mengi ni ya muda mrefu yatabaki kuwa matatizo ya msingi ya muda mrefu”—Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa.

      WATOTO wako mashakani ulimwenguni pote. Uthibitisho wenye kusadikisha unaokazia ukubwa wa msiba huu ulitolewa kwenye Mkutano wa Kimataifa Dhidi ya Biashara ya Ngono Inayoharibu Watoto uliofanywa Stockholm, Sweden, mwaka wa 1996 na kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi 130. Kwa kielelezo, ilisemwa kwamba katika sehemu nyingi za ulimwengu, kuna mamilioni mengi ya wasichana wachanga, wengine wana umri wa miaka kumi, wanaolazimishwa wafanye kazi wakiwa makahaba.

      Gazeti la Australia Melbourne University Law Review lilisema kwamba ukahaba huo wa kulazimishwa umetajwa kuwa “mojawapo ya utumwa wa siku hizi ulio mbaya zaidi.” Baada ya miaka mingi ya kuumizwa kimwili, kiakili, na kihisia-moyo, wasichana hawa wanapata madhara mabaya sana katika maisha yao yote. Katika visa vingi wasichana hawa hukubali kutendwa ukatili huu kwa sababu tu wanataka kupata chakula ili waishi. Wasipofanya hivyo watakufa kwa sababu ya kukosa chakula. Kwa kusikitisha, wengi wa watoto hawa wasiokuwa na makao walilazimishwa kuwa makahaba na wazazi wao wenyewe walio maskini, waliowauza ili wapate pesa.

      Jambo linaloongezea msiba huu wa watoto ulio dhahiri ni suala ambalo mara nyingi hujadiliwa kwa ukali sana kuhusu kufanyiza watoto kazi. Katika Asia, Amerika Kusini, na kwingineko na katika sehemu nyingine za wahamaji huko Marekani, watoto kama vile wenye umri wa miaka mitano wanalazimishwa kuingia katika ile inayoweza kuitwa “kazi ya utumwa.” Hufanya kazi kama roboti ndogo chini ya hali zenye kufadhaisha zinazoharibu kabisa miili na akili zao changa. Wengi wao hawana elimu, hawapati upendo wa wazazi, hawana makao salama, hawana vitu vya kuchezea vya watoto, hawana bustani za kuchezea. Wengi hutumiwa kwa faida kwa njia isiyo na hisia na wazazi wao wenyewe.

      Askari-Jeshi Watoto na Makao ya Mayatima

      Jambo linalofanya msiba huu uwe mbaya hata zaidi ni kwamba, watoto wanazidi kutumiwa kama askari-jeshi katika majeshi ya msituni. Watoto waweza kutekwa nyara au kununuliwa katika masoko ya watumwa na kisha kufanywa wawe wakatili hatua kwa hatua, nyakati nyingine wakifanywa watazame uuaji. Wengine hata wameamriwa wawaue wazazi wao au watumie dawa za kulevya kusudi wazidi kuua bila kufikiri.

      Kielelezo kifuatacho chaonyesha madhara ya kutiwa kasumba ambayo yamewapata maelfu ya watoto walio askari-jeshi katika Afrika. Mazungumzo haya yenye kuvunja moyo yalikuwa baina ya mfanyakazi wa huduma za jamii na mvulana ambaye ni askari-jeshi ambaye yaelekea alikuwa akijaribu kudumisha hisia kidogo sana ya hatia aliyokuwa nayo:

      “Je, uliua? ‘La.’

      Je, ulikuwa na bunduki? ‘Ndiyo.’

      Je, ulilenga shabaha? ‘Ndiyo.’

      Je, ulifyatua risasi? ‘Ndiyo.’

      Ni nini kilichotukia? ‘Walianguka tu.’”

      “Baadhi ya vijana hawa ni wadogo tu kama watoto unapofikiria kwamba askari-jeshi fulani wana umri wa miaka sita na zaidi.” Imeripotiwa kwamba mapema mwaka wa 1988, kulikuwa na watoto askari-jeshi 200,000 ulimwenguni pote.

      Inasemekana kwamba kati ya mwaka wa 1988 na 1992, katika makao ya mayatima katika nchi moja ya Asia, watoto 550, wengi wao wakiwa ni wasichana, walinyimwa chakula kimakusudi ili wafe njaa. Daktari mmoja anaripoti kwamba: “Mayatima hao hawakuwa na tembe za kumaliza maumivu yao. Hata walipokuwa wamelala wakiwa wamekufa, walifungiwa kwenye vitanda vyao.”

      Vipi juu ya Ulaya? Nchi moja huko ilifadhaishwa na ugunduzi wa kikundi cha kimataifa kinachohusika na ponografia ya watoto ambacho kiliwateka nyara wasichana ili kuwatumia vibaya kingono. Kwa kusikitisha wasichana fulani waliuawa au wakanyimwa chakula hadi wakafa.

      Kwa wazi ripoti hizi zinaonyesha kwamba nchi nyingi zina tatizo kubwa kuhusu kutenda watoto vibaya na kuwatumia ili kujifaidi. Lakini je, ni kutilia chumvi kusema kwamba tatizo hili limeenea ulimwenguni pote? Makala ifuatayo itajibu swali hilo.

  • Mashaka Yako Ulimwenguni Kote
    Amkeni!—1999 | Aprili 8
    • Mashaka Yako Ulimwenguni Kote

      MAUJI ya kinyama ya watoto wanaoishi barabarani katika Brazili bado ni mfano mwingine unaoonyesha ukosefu wa usalama wa watoto wasiotakikana. Ripoti kutoka nchi hiyo zilisema kwamba mamia kadhaa ya watoto walikuwa wakiuawa kila mwaka.

      Watoto wameshambuliwa kikatili katika Dunblane, Scotland, na Wolverhampton, Uingereza, na sehemu nyinginezo. Kwa kielelezo, wazia kuteseka kwa Maria mwenye umri wa miaka 12, ambaye ni yatima kutoka Angola aliyebakwa na kupata mimba. Baadaye alilazimishwa kutembea kilometa 320 hivi, ambapo baadaye alijifungua mtoto kabla ya wakati wake aliyeishi majuma mawili tu. Maria alikufa baada ya juma moja, akiwa mgonjwa na aliyekosa kulishwa chakula cha kutosha.

      Mwaka wa 1992 ripoti moja ya Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) ilisema kwamba “‘vita dhidi ya watoto’ ni jambo lililobuniwa katika karne ya 20.” Kulingana na ripoti moja ya 1996 ya shirika la UNICEF, maoni ya watu fulani ni kwamba ‘vizazi vijavyo vya adui, yaani, watoto wa adui, lazima pia viondolewe.’ Mwelezaji wa kisiasa alifafanua jambo hili kwa njia hii: “Ili kuua panya wakubwa, ni lazima uue panya wadogo.”

      Hivi karibuni watoto milioni mbili wameuawa kijeuri katika kipindi cha miaka kumi. Wengine milioni nne wamelemazwa, wakapofushwa, au wakaharibiwa akili na mabomu yanayotegwa chini ya ardhi, wakijitahidi kupambana na maisha kadiri wawezavyo pamoja na mamilioni wengi waliopoteza makao yao wakati wa vita. Haishangazi kwamba ripoti moja ilikuwa na kichwa hiki cha habari: “Majinamizi Yenye Kuogofya ya Ukatili wa Vita kwa Watoto.”

      Ukatili huu ambao umefanywa dhidi ya watoto ni tatizo kwa jamii ya kibinadamu, ithibati hakika kwamba watoto wana matatizo, si katika nchi chache tu bali ulimwenguni pote. Na watoto wengi ambao wametendwa vibaya wamevunjiwa tumaini pia.

      Tumaini Lao Lavunjwa na Wale Waliowaitibari

      Mtoto anapovunjiwa tumaini makovu mabaya sana ya kihisia-moyo yaweza kutokea. Huwa hivyo hasa mtu anayevunja tumaini la mtoto anapokuwa ni mzazi, rafiki, au mshauri. Mweneo wa tatizo hili la wazazi kuwatenda watoto vibaya unaonyeshwa na simu nyingi zilizopokewa kwenye laini ya simu ya moja kwa moja baada ya kutangazwa kwa kipindi cha mazungumzo kilichoitwa “Kutishwa Kimyakimya: Kufichua na Kukomesha Kutenda Watoto Vibaya,” kilicholetwa na Oprah Winfrey katika Marekani. “Simu zenye kuogofya zaidi zilitoka kwa watoto wachanga, waliosema kwa hofu, wanataka kutoroka wasipatwe na maumivu ya kimwili au kutendwa vibaya kingono,” akasema msimamizi wa kipindi hicho Arnold Shapiro, kama alivyonukuliwa katika jarida Children Today.

      Tukio hili lilichangia sehemu kubwa ya kukanusha wazo la kwamba watu wanaowatenda watoto vibaya ni wageni wakubwa wenye kutisha. Uhakika ni kwamba “wengi wanaowatenda watoto vibaya ni wazazi na jamaa wengine wa karibu,” amalizia Shapiro. Uchunguzi mwingine unathibitisha jambo hili na pia unaonyesha kwamba nyakati nyingine rafiki za familia wanaotumainiwa walimtayarisha mtoto na familia kwa kisa cha kumtenda mtoto huyo vibaya baadaye. Ngono ya maharimu ni uvunjaji wa tumaini wenye kushtua zaidi.

      Kutendwa vibaya kingono na watu wanaovutiwa kingono na watoto ni tisho jingine linalowakabili watoto ulimwenguni pote. Kijarida Trends & Issues in Crime and Criminal Justice chatoa fasiri hii: “Kuvutiwa kingono na watoto kwarejezea uvutio wa kingono kuelekea mtoto aliye mchanga sana. . . . Sikuzote kuvutiwa kingono na watoto huhusisha kutenda uhalifu kama vile kushambulia kingono, mambo ya aibu na makosa yanayohusisha ponografia ya watoto.”

      Ripoti zenye kusikitisha za vikundi vya watu wenye kuvutiwa kingono na watoto, ambao huwatumia watoto vibaya kwa pupa, zinazidi kupokewa kutoka sehemu zote za ulimwengu. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.) Wenye kutendwa vibaya ni wavulana na wasichana wachanga. Wakishawishwa na wanaume wasio na adili, wanatendwa vibaya kingono na kisha wanatishwa au kudekezwa kupita kiasi ili kuwachochea wabaki katika “kikundi” hiki. Wanaume ambao hupanga na kufanya matendo haya maovu mara nyingi huwa ni viongozi mashuhuri wa jumuiya na nyakati nyingine hufanya hivyo huku polisi na idara ya mahakama wakiwa na habari za kutosha na kuwalinda.

      Jambo lenye kufedhehesha pia linasababishwa na makasisi wanaowatenda watoto vibaya kingono. Habari kutoka ulimwenguni pote zafunua kiwango kikubwa cha watoto wanaotendwa vibaya kingono na makasisi, nyakati nyingine hata kwa jina la Mungu. Kwa kielelezo, kasisi Mwanglikana aliyethibitishwa kuwa na hatia alimwambia mvulana mwenye umri wa miaka kumi kwamba “Mungu alikuwa akinena kupitia kwake [kasisi huyo], na kitu chochote alichofanya au kitu chochote [mvulana huyo] alichofanya kilimpendeza Mungu na kwa hiyo kilifaa.”

      Katika Australia pitio la kitabu The Battle and the Backlash: The Child Sexual Abuse War lilisema juu ya kutendwa vibaya kwa watoto na makasisi na watu wengine wenye nyadhifa zenye kuitibariwa. Lilisema kwamba mashirika yaliyohusika yalijali zaidi kulinda jinsi ambavyo yangeonekana na kujikinga yenyewe badala ya kuwalinda watoto wanaoweza kudhurika kwa urahisi.

      Matokeo Mabaya Sana

      Kwa kawaida tumaini la mtoto huwa kamili. Hivyo, tumaini hilo linapovunjwa, kunakuwa na matokeo mabaya sana kwa mtoto mchanga asiyeshuku hatari yoyote. Kichapo Child Abuse & Neglect chasema hivi: “Watu na mahali ambapo awali palikuwa penye kuandaa usalama au tegemezo pamehusianishwa na hatari na hofu. Maisha ya mtoto yanazidi kuwa yasiyotabirika na yasiyoweza kudhibitiwa.”

      Tokeo la kutendwa vibaya namna hiyo, ambapo visa vingi vimeendelea kwa miaka mingi, ni kwamba watoto fulani wamepatwa na matatizo ya kijamii na ya kiakili baadaye maishani, mpaka wanapokuwa watu wazima. Kuvunjwa huku kwa tumaini ni jambo baya sana kwa sababu mtoto ametumiwa kwa kujinufaisha kwa sababu tu ni mtoto. Lakini watoto wengi wanaotendwa vibaya hawasemi habari hizo kamwe—jambo ambalo hutumainiwa na watu wenye kuwatenda watoto vibaya.

      Katika miaka ya karibuni, uthibitisho kutoka ulimwenguni pote wa kuwatenda watoto vibaya unazidi kuongezeka, hivi kwamba leo umekuwa mwingi sana kutoweza kukanushwa au kupuuzwa tena. Lakini wengi wanakubali kwamba kukomeshwa kabisa kwa zoea la kuwatenda watoto vibaya ni kazi yenye kutisha. Hivyo kunatokea maswali haya: Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuwalinda kikweli watoto wetu? Wale ambao ni wazazi miongoni mwetu wanaweza kulindaje urithi kutoka kwa Mungu na kutunza maisha yanayoweza kudhurika kwa urahisi ya watoto wetu wachanga? Wazazi wanaweza kupata wapi msaada?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Utendaji wa Internet Unaofanywa kwa Uangalifu

      Miezi michache iliyopita, katika mojawapo ya jitihada kubwa zaidi iliyopata kufanywa ya utendaji wa siri dhidi ya ponografia ya watoto inayopitishwa kwenye Internet, polisi katika nchi 12 walivamia nyumba za washukiwa zaidi ya 100 wenye kuvutiwa kingono na watoto. Kutoka kikundi kimoja tu cha wanaume wenye kuvutiwa kingono na watoto huko Marekani, walitwaa picha za kiponografia za watoto zaidi ya 100,000.

      Mpelelezi wa Uingereza aliyeratibu uchunguzi huo wa Internet wa miezi mitano alisema hivi: “Mambo yaliyomo yangemfanya mtu yeyote mwenye akili timamu ashikwe na kichefuchefu.” Kulikuwa na watoto wa jinsia zote mbili, wengine wakiwa na umri wa miaka miwili. Polisi wa Ubelgiji walisema kwamba picha za Internet ndizo zilizokuwa “zenye kunyarafisha zaidi kati ya ponografia ya watoto. . . . Zilikuwa mbaya sana hivi kwamba watu walifikia kiwango cha kuwatenda vibaya watoto wao wenyewe ili waweze kutokeza picha zenye kutazamisha zaidi.” Mtu mmoja alipiga picha zake mwenyewe akimbaka mpwa wake wa kike na kuingiza picha hizi ndani ya kompyuta.

      Washukiwa walitia ndani walimu, mwanasayansi, mwanafunzi wa sheria, kiongozi wa maskauti, mhasibu, na profesa wa chuo kikuu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki