-
Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanasherehekea Krismasi?Amkeni!—2010 | Desemba
-
-
Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanasherehekea Krismasi?
JE, WEWE hutazamia Krismasi kwa hamu? Au wewe hujawa na wasiwasi wakati huo unapokaribia? Mamilioni ya watu hujiuliza: ‘Nitamnunulia nani zawadi? Ninunue zawadi gani? Je, nina pesa za kutosha kuinunua? Nikikopa, itanichukua muda gani kulipa deni langu?’
Hata ingawa watu huwa na mahangaiko hayo, bado Krismasi ni sherehe inayopendwa sana. Kwa kweli, sherehe hiyo imeenea kufikia nchi ambazo si za Kikristo. Huko Japani, familia nyingi husherehekea Krismasi, si kwa sababu za kidini, lakini kwa sababu ni pindi ya sherehe. Huko China “madirisha ya maduka mengi katika majiji makubwa huwa na picha ya Baba Krismasi,” linasema jarida The Wall Street Journal, na linaongezea hivi: “Roho ya Krismasi imeanza kuwanasa watu wanaoishi katika miji ya China nao wanaona hiyo kuwa nafasi ya kununua vitu, kula na kuwa na karamu.”
Kusherehekea Krismasi kumeinua sana uchumi wa nchi nyingi ulimwenguni. Imekuwa hivyo hasa kwa China, ambayo sasa “inasafirisha kwa wingi sana miti ya plastiki, mapambo, taa zinazomweka-mweka, na mapambo mengine ya Krismasi,” linasema jarida The Wall Street Journal.
Pia nchi za Kiislamu zinaendeleza sherehe zinazofanana na zile za Krismasi, ingawa huenda zisifanywe Desemba (Mwezi wa 12) 25. Huko Ankara, Uturuki, na Beirut, Lebanoni, si ajabu kuona madirisha ya maduka yakiwa na miti iliyofunikwa mapambo na zawadi zilizopakiwa katika karatasi za pekee. Nchini Indonesia, hoteli na maduka makubwa huandaa sherehe ambapo watoto wanaweza kula pamoja na Baba Krismasi au wapigwe picha pamoja naye.
Katika nchi nyingi za Kikristo, Krismasi ni wakati hasa wa biashara, na matangazo mengi ya kibiashara “yamekusudiwa hasa ili kuwanasa watoto,” linasema jarida Royal Bank Letter la Kanada. Kwa kweli, bado watu fulani huenda kanisani ili kuadhimisha Krismasi. Lakini nyimbo za Krismasi husikika hasa katika maduka makubwa, kwani siku hizi hayo ndiyo yamekuwa mahekalu. Kwa nini kumekuwa na badiliko hilo? Je, huenda ikawa ni kwa sababu ya chanzo cha Krismasi? Krismasi ilianzia wapi?
Kabla ya kuzungumzia maswali hayo, ingefaa tusome masimulizi ya Biblia ambayo hutumiwa kuigiza Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
WAANDIKAJI WA INJILI WANASEMA NINI?
Mtume Mathayo: “Baada ya Yesu kuzaliwa katika Bethlehemu ya Yudea siku za Mfalme Herode, tazama! wanajimu kutoka sehemu za mashariki walikuja Yerusalemu, wakisema: ‘Yuko wapi yule mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa? Kwa maana tuliiona nyota yake wakati tulipokuwa mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.’ Aliposikia hilo Mfalme Herode akafadhaika.” Kwa hiyo, Herode akawauliza “wakuu wa makuhani . . . ni wapi Kristo alipaswa kuzaliwa.” Alipoambiwa kwamba angezaliwa “katika Bethlehemu,” Herode akawaambia hivi wale wanajimu: “Nendeni mkamtafute kwa uangalifu yule mtoto mchanga, na mkiisha kumpata nileteeni habari.”
“Waliondoka wakaenda; na, tazama! nyota waliyokuwa wameona wakati walipokuwa mashariki ikaenda mbele yao, mpaka ikaja kutua juu ya mahali alipokuwa yule mtoto mchanga. . . . Walipoingia ndani ya ile nyumba wakamwona huyo mtoto mchanga pamoja na Maria mama yake.” Baada ya kumpa Yesu zawadi hizo, “walipewa onyo la kimungu katika ndoto wasirudi kwa Herode, [kwa hiyo] wakaondoka kwenda nchi yao kwa njia nyingine.”
“Walipokuwa wamekwisha kuondoka, tazama! malaika wa Yehova akamtokea Yosefu katika ndoto, akisema: ‘Simama, mchukue huyo mtoto mchanga na mama yake mkimbie kuingia Misri . . .’ Kwa hiyo akasimama na kuchukua pamoja naye mtoto huyo mchanga na mama yake wakati wa usiku, akaondoka . . . Ndipo Herode, alipoona ameshindwa akili na wale wanajimu, akaingiwa na ghadhabu kubwa, akatuma watu na kuagiza wavulana wote katika Bethlehemu na katika wilaya zake zote wauawe, kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini.”—Mathayo 2:1-16.
Mwanafunzi Luka: Yosefu “akapanda kutoka Galilaya, kutoka jiji la Nazareti, akaingia Yudea, kwenye jiji la Daudi, linaloitwa Bethlehemu, . . . ili apate kuandikishwa pamoja na Maria . . . Walipokuwa huko, . . . akamzaa mwana wake, mzaliwa wa kwanza, akamfunga vitambaa na kumlaza katika hori, kwa sababu hapakuwa na mahali kwa ajili yao katika chumba cha kukaa.”
“Katika nchi hiyo kulikuwako pia wachungaji wakiishi nje, wakichunga makundi yao usiku. Na kwa ghafula malaika wa Yehova akasimama kando yao, . . . nao wakaogopa sana. Lakini malaika akawaambia: ‘Msiogope, kwa maana, tazama! ninawatangazia ninyi habari njema ya shangwe kubwa ambayo watu wote watakuwa nayo, kwa sababu leo katika jiji la Daudi, Mwokozi ambaye ni Kristo Bwana, amezaliwa kwenu.’” Wachungaji hao “wakaenda haraka wakamkuta Maria na vilevile Yosefu, na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori.”—Luka 2:4-16.
-
-
Ukweli Kuhusu KrismasiAmkeni!—2010 | Desemba
-
-
Ukweli Kuhusu Krismasi
JE, UNAFIKIRI ni muhimu kujua ukweli kuhusu mafundisho na sherehe za kidini? Ikiwa ndivyo, basi huenda umewahi kujiuliza maswali haya: (1) Je, kweli Yesu alizaliwa Desemba 25? (2) “Mamajusi” walikuwa nani, na je, kweli walikuwa watatu? (3) Ni “nyota” ya aina gani iliyowaongoza kwa Yesu? (4) Baba Krismasi ana uhusiano gani na Yesu na kuzaliwa kwake? (5) Mungu ana maoni gani kuhusu desturi ya Krismasi ya kubadilishana zawadi?
Acheni tufikirie maswali hayo kwa kupatana na mambo hakika ya Biblia na ya kihistoria.
(1) Je, Yesu Alizaliwa Desemba 25?
Desturi: Kulingana na mapokeo, Yesu alizaliwa Desemba 25 na sherehe inafanywa siku hiyo. “Krismasi,” kinasema kitabu Encyclopedia of Religion, inamaanisha “‘Misa ya Kristo,’ yaani, misa ya kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo.”
Chanzo: “Desemba 25 haikutokana na chanzo chochote cha kibiblia,” kinasema kitabu The Christmas Encyclopedia, “lakini ilitokana na sherehe za kipagani za Kiroma zinazofanywa mwishoni mwa mwaka,” karibu na wakati jua lilipochomoza tena wakati wa majira ya baridi kali katika Kizio cha Kaskazini. Sherehe hizo zinatia ndani Saturnalia, sherehe ya Saturn, mungu wa kilimo, “na sherehe mbili zilizofanywa pamoja za miungu wawili wa jua, Sol wa Waroma na Mithra wa Waajemi,” kinasema kitabu hicho. Sherehe zote mbili zilifanywa Desemba 25, jua lilipochomoza tena wakati wa majira ya baridi kali kulingana na kalenda ya Yulio.
Sherehe hizo za kipagani zilianza kuingizwa katika ibada inayodaiwa kuwa ya Kikristo katika mwaka wa 350, wakati ambapo Papa Julius wa Kwanza alitangaza Desemba 25 kuwa siku ya kuzaliwa kwa Kristo. “Pole kwa pole, maigizo ya kuzaliwa kwa Yesu yalimeza au kuchukua mahali pa desturi nyingine za kuchomoza kwa jua,” kinasema kitabu Encyclopedia of Religion. “Picha za jua zikaanza kutumiwa sana kumwakilisha Kristo aliyefufuka (ambaye pia aliitwa Sol Invictus), na duara la jua . . . likaja kuwakilisha nuru ya mviringo juu ya watakatifu Wakristo.”
Biblia inasema nini: Biblia haitaji tarehe ambayo Yesu alizaliwa. Lakini tunaweza kusema kwamba hakuzaliwa Desemba 25. Kwa nini? Biblia inatuambia kwamba Yesu alipozaliwa, wachungaji walikuwa “wakiishi nje” wakichunga makundi yao usiku karibu na Bethlehemu. (Luka 2:8) Kwa kawaida, majira ya baridi na mvua yalianza Oktoba (Mwezi wa 10), na mwezi wa Desemba ndio uliokuwa na baridi kali zaidi ambayo nyakati nyingine iliandamana na theluji. Wachungaji—hasa wale waliokuwa katika nyanda za juu zenye baridi, kama zile karibu na Bethlehemu—waliingiza kondoo wao katika vibanda usiku.a
Inafaa kuzingatia kwamba Wakristo wa mapema, ambao wengi wao walikuwa wameshirikiana na Yesu katika huduma yake, hawakuwahi kusherehekea kuzaliwa kwake katika tarehe yoyote. Badala yake, kupatana na amri yake, waliadhimisha tu kifo chake. (Luka 22:17-20; 1 Wakorintho 11:23-26) Lakini, bado huenda wengine wakasema, ‘Je, kuna ubaya wowote kwa Wakristo kuanza kufuata desturi za kipagani?’ Jibu? Kwa Mungu kuna ubaya. “Waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli,” akasema Yesu Kristo.—Yohana 4:23.
(2) Wale Mamajusi Walikuwa Wangapi? Walikuwa Nani?
Desturi: Wakiongozwa na “nyota” kutoka mashariki, mamajusi huonyeshwa wakimpa Yesu zawadi akiwa katika hori ndani ya zizi. Nyakati nyingine wachungaji huonyeshwa wakiwapo pia.
Chanzo: Mbali na simulizi fupi lililo katika Biblia, “kila kitu kilichoandikwa kuwahusu Mamajusi kinatokana na hekaya,” kinasema kitabu The Christmas Encyclopedia.
Biblia inasema nini: Biblia haisemi ni mamajusi wangapi waliomtembelea Yesu. Huenda walikuwa wawili, au huenda walikuwa watatu, wanne, au zaidi. Ingawa katika Biblia fulani wanaitwa “wanaume wenye hekima,” neno lililotumiwa katika lugha ya awali ni magoi, linalomaanisha wanajimu au walozi—kazi ambazo Biblia inasema ni “chukizo kwa Yehova.” (Kumbukumbu la Torati 18:10-12) Kwa kuwa walisafiri mbali sana kutoka Mashariki, wanajimu hao hawakuwasili kwa wakati kumtembelea Yesu akiwa katika zizi. Badala yake, baada ya kusafiri kwa miezi mingi, walienda kwenye “nyumba” ambako Yesu alikuwa akiishi. Huko walimwona “mtoto mchanga pamoja na Maria mama yake.”—Mathayo 2:11.
(3) Ni Nyota ya Aina Gani Iliyowaongoza Wanajimu?
Tunaweza kuelewa nyota hiyo ilikuwa ya aina gani tunapochunguza mambo iliyofanya. Jambo moja ni kwamba haikuwaongoza moja kwa moja hadi Bethlehemu, lakini iliwapeleka Yerusalemu, ambako Mfalme Herode alisikia kuwa walikuwa wakiuliza kumhusu Yesu. Kisha Herode “akawaita wale wanajimu kwa siri,” nao wakamwambia kuhusu “mfalme wa Wayahudi” aliyekuwa amezaliwa. Kisha Herode akasema: “Mkamtafute kwa uangalifu yule mtoto mchanga, na mkiisha kumpata nileteeni habari.” Hata hivyo, Herode hakuwa na nia nzuri. Badala yake, mtawala huyo mwenye kiburi na mkatili alikuwa ameazimia kumwua Yesu!—Mathayo 2:1-8, 16.
Kwa kushangaza, “nyota” hiyo ikawaongoza upande wa kusini hadi Bethlehemu. Ilipofika “ikaja kutua” juu ya nyumba ambamo Yesu alikuwa.—Mathayo 2:9, 10.
Kwa wazi, hiyo haikuwa nyota ya kawaida! Kwa nini Mungu, ambaye alikuwa ametumia malaika kuwajulisha wachungaji wa hali ya chini kuhusu kuzaliwa kwa Yesu, atumie nyota kuongoza wanajimu wapagani—kwanza kwa adui ya Yesu kisha kwa mtoto mwenyewe? Inapatana na akili kusema kwamba nyota hiyo ilikuwa mbinu ya Shetani, anayeweza kujitokeza katika njia kama hizo. (2 Wathesalonike 2:9, 10) Jambo la kushangaza ni kwamba nyota inayoitwa ya Bethlehemu huwekwa juu kabisa ya mti wa Krismasi.
(4) Baba Krismasi ana Uhusiano Gani na Yesu na Kuzaliwa Kwake?
Desturi: Katika nchi nyingi, Baba Krismasi anasemwa kuwa ndiye mtu anayewaletea watoto zawadi.b Mara nyingi, watoto humwandikia Baba Krismasi barua wakimwomba zawadi, ambazo inasemekana kwamba anasaidiwa kuzitengeneza na watu fulani wadogo wa kuwaziwa katika makao yake makuu kwenye Ncha ya Kaskazini.
Chanzo: Kulingana na maoni ya watu wengi, hekaya kumhusu Baba Krismasi zinatokana na Mtakatifu Nicholas, Askofu Mkuu wa Myra huko Asia Ndogo, ambayo sasa ni Uturuki. “Mambo yote yaliyoandikwa kumhusu Mt. Nicholas ni hekaya,” kinasema kitabu The Christmas Encyclopedia. Huenda jina la Baba Krismasi la Kiingereza “Santa Claus” linatokana na neno Sinterklaas, mchanganyiko wa maneno mawili ya Kiholanzi ya jina “Saint Nicholas.” Kulingana na historia na Biblia, Baba Krismasi hana uhusiano wowote na Yesu Kristo.
Biblia inasema nini: “Sasa kwa kuwa mmeuondolea mbali uwongo, semeni kweli kila mmoja wenu na jirani yake.” ‘Majirani’ wetu wa karibu zaidi ni watu wa familia yetu. (Waefeso 4:25) Pia Biblia inasema kwamba tunapaswa ‘kupenda kweli,’ “kusema kweli katika moyo [wetu].” (Zekaria 8:19; Zaburi 15:2) Ni kweli kwamba huenda ikaonekana kuwa hakuna madhara kuwaambia watoto kuwa Baba Krismasi (au Kristo mtoto) ndiye huwaletea zawadi wakati wa Krismasi, lakini je, ni jambo linalofaa kuwadanganya watoto wadogo, hata usipokuwa na nia mbaya? Je, si jambo la ajabu kwamba siku inayopaswa kumtukuza Yesu imekuwa siku ya kuwadanganya watoto?
(5) Mungu ana Maoni Gani Kuhusu Zawadi na Karamu za Krismasi?
Desturi: Zawadi zinazotolewa wakati wa Krismasi si za kawaida kwani zinahusisha kubadilishana zawadi, na kipindi cha Krismasi kinahusiana na karamu, kula, na kunywa.
Chanzo: Sherehe ya Saturnalia ya Roma ya kale ilianza Desemba 17 na kwisha tarehe 24, wakati ambapo watu walipeana zawadi. Nyumba na barabara zilikuwa na kelele za watu wakifanya karamu, wakinywa sana, na wakitenda bila kujizuia. Saturnalia ilifuatwa na kusherehekea siku ya kwanza ya Januari. Siku hiyo pia iliadhimishwa kwa sherehe ambayo kwa kawaida iliendelea kwa siku tatu hivi. Kuna uwezekano kwamba Saturnalia na siku ya kwanza ya Januari zilifanyiza sherehe moja.
Biblia inasema nini: Shangwe na ukarimu ni sehemu muhimu ya ibada ya kweli. Biblia inasema: ‘Iweni na shangwe, enyi waadilifu; na mpige vigelegele vya shangwe.’ (Zaburi 32:11) Mara nyingi, shangwe ya aina hiyo inahusianishwa na ukarimu. (Methali 11:25) Yesu Kristo alisema: “Kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko ilivyo katika kupokea.” (Matendo 20:35) Pia alisema hivi: “Muwe na mazoea ya kuwapa watu,” yaani, tunapaswa kuhakikisha kwamba hilo ni jambo la kawaida katika maisha yetu.—Luka 6:38.
Kutoa kwa njia hiyo hakuna uhusiano na kutoa kidesturi au kutoa kwa kulazimishwa, kwa sababu tu ni zoea katika jamii. Biblia inasema hivi ikifafanua roho ya kweli ya kutoa: “Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha.” (2 Wakorintho 9:7, Biblia Habari Njema) Wale wanaotii kanuni hizo nzuri za Biblia hutoa kwa sababu moyo wao wenye ukarimu unawachochea kufanya hivyo, na wanatoa wakati wowote katika mwaka. Kwa kweli, Mungu hubariki kutoa kwa njia hiyo, na kufanya hivyo si mzigo mzito.
Sherehe Bandia!
Inapochunguzwa kwa kutumia Biblia, ni kana kwamba kila kitu kuhusu Krismasi kimetokana na mambo ya kipagani au kupotoshwa kwa masimulizi ya Biblia. Kwa hiyo, desturi za Krismasi zinaitwa tu za Kikristo. Basi zilianza jinsi gani kuitwa hivyo? Karne kadhaa baada ya kifo cha Kristo, walimu wengi wa uwongo walitokea, kama Biblia ilivyokuwa imetabiri. (2 Timotheo 4:3, 4) Watu hao wasioongozwa na kanuni walipendezwa zaidi na kufanya Ukristo upendwe na wapagani kuliko walivyopendezwa na kufundisha kweli. Kwa sababu hiyo, walianza kujiingiza hatua kwa hatua katika sherehe za dini za kipagani zilizopendwa sana na wakaziita eti ni za Kikristo.
Biblia ilionya kwamba ‘walimu hao wa uwongo watawatumia watu vibaya kwa maneno yasiyo ya kweli. Lakini kuwahusu wao, hukumu ya tangu zamani za kale haisongi polepole, na maangamizi yao hayalali.’ (2 Petro 2:1-3) Mashahidi wa Yehova huchukua maneno hayo kwa uzito—kama tu wanavyochukua kwa uzito maneno ya Biblia nzima, ambayo wanaiona kuwa Neno la Mungu lililoandikwa. (2 Timotheo 3:16) Kwa sababu hiyo, wanakataa desturi au sherehe za dini za uwongo. Je, uamuzi huo umewafanya wasiwe na furaha? Tofauti na hilo, kama tutakavyoona, wanajua kutokana na mambo ambayo wamejionea kwamba kweli ya Biblia inawaweka watu huru!
[Maelezo ya Chini]
a Inaonekana ni kama Yesu alizaliwa katika mwezi wa kale wa Wayahudi unaoitwa Ethanimu (Septemba—Oktoba).—Ona kitabu Insight on the Scriptures, Buku la 2, ukurasa wa 56, au Étude perspicace des Écritures, Buku la 2, ukurasa wa 20, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
b Katika nchi fulani za Ulaya, kama vile Austria, “Baba Krismasi haonwi kuwa mtu wa Kristo,” au mtoto wa Kristo, inasema ripoti ya habari ya shirika la BBC. Hata hivyo, bado ziara yake inahusu kuleta zawadi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
PANDA MAGUGU, VUNA MAGUGU
Wakati fulani, viongozi wa kanisa walipigana “kufa na kupona kuondoa mambo yoyote ya kipagani,” kinasema kitabu Christmas Customs and Traditions—Their History and Significance. Lakini baada ya muda, viongozi wa kanisa wakawa na hamu zaidi ya kujaza makanisa kuliko kufundisha kweli. Kwa sababu hiyo, wakaanza kupuuza mazoea hayo ya kidini. Baadaye, waliyakubali.
‘Lolote lile unalopanda, utavuna hilo,’ inasema Biblia. (Wagalatia 6:7) Baada ya kupanda mbegu za upagani katika mashamba yao, makanisa hayapaswi kushangaa kwamba kuna “magugu” mengi sana. Sherehe ambayo ilipaswa kutukuza kuzaliwa kwa Yesu inakuwa kisingizio cha kulewa na karamu zenye fujo, watu wanapenda zaidi kwenda kwenye maduka makubwa kuliko kwenda kanisani, familia zinajiingiza sana katika madeni kwa sababu ya kununua zawadi, na watoto hawajui tofauti kati ya mambo halisi na ya kuwaziwa, hawajui tofauti kati ya Baba Krismasi na Yesu Kristo. Naam, akiwa na sababu nzuri Mungu alisema hivi: “Mwache kugusa kitu kilicho najisi.”—2 Wakorintho 6:17.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kipindi cha Krismasi, kama sherehe ya zamani ya Saturnalia, huwa ni wakati wa karamu, kula, na kunywa
[Hisani]
© Mary Evans Picture Library
-
-
“Kweli Itawaweka Ninyi Huru”!Amkeni!—2010 | Desemba
-
-
“Kweli Itawaweka Ninyi Huru”!
MANENO hayo ya Yesu Kristo, yanayopatikana katika Biblia kwenye Yohana 8:32, siku zote yamethibitika kuwa kweli kabisa. Kweli hiyo inatuweka huru kutokana na mambo ya ushirikina na desturi zinazomchukiza Mungu na kutudhuru. Masimulizi yafuatayo yanaonyesha jinsi ambavyo kweli ya Biblia imewaweka watu huru katika nchi mbalimbali kutokana na desturi zenye kulemea zinazohusiana na Krismasi.
Kweli ya Biblia Iliwaweka Huru!
Argentina “Familia yetu imewekwa huru kutokana na matatizo yanayohusiana na kula na kunywa kupita kiasi na gharama ya zawadi ambazo hatungeweza kununua,” anasema Oscar.
Mario alijihisi akiwa na uhuru mwingi wakati ule anaouita “uwongo wa Krismasi” ulipofunuliwa kwake. “Sasa mimi hupata shangwe ya kuwapa wengine zawadi wakati wowote katika mwaka ninapokuwa na pesa za kufanya hivyo.”
Kanada “Mimi ninapenda kutoa na kupokea zawadi,” anaandika Elfie. “Lakini sipendi wakati mtu anaponipa zawadi kwa sababu anahisi ana wajibu wa kufanya hivyo. Familia yetu ilipoacha kusherehekea Krismasi, nilihisi ni kama nimepumzishwa mzigo mzito sana!”
Ulli, binti mmoja wa Elfie, anakumbuka hivi: “Baada ya wazazi wetu kuacha kusherehekea Krismasi, walikuwa wakitufanyia mambo yenye kufurahisha na kutupa zawadi wakati wowote katika mwaka, nasi tulifurahia hilo sana. Wanafunzi wenzetu walipotuuliza kwa nini walifanya hivyo, tuliwaambia, ‘Ni kwa sababu tu walitaka!’ Lakini haikuwa rahisi kwa wazazi wetu kubadili maisha yao yapatane na mambo waliyojifunza katika Biblia, kwa sababu walipingwa na kushinikizwa sana na watu wa familia. Lakini walisimama imara. Kuona jinsi walivyoazimia kumwabudu Yehova Mungu kwa njia inayofaa kulikuwa na uvutano mkubwa sana kwangu.”
Silvia anasema kwamba kuacha kusherehekea Krismasi “kulikuwa jambo lenye kutuliza sana. Baadaye nilijihisi vizuri sana. Nilijua kwamba ninampendeza Yehova Mungu, na hilo lilinifanya nijihisi vizuri sana kuliko vile ambavyo ningehisi ikiwa ningesherehekea Krismasi zaidi ya elfu moja.”
Kenya Peter anaandika hivi: “Nilipokuwa nikisherehekea Krismasi, nilikopa pesa nyingi sana ili ninunue zawadi na kulipia milo yenye madoido mengi. Bila shaka, hilo lilimaanisha kwamba lazima nifanye kazi ya ziada, na hilo lilinifanya nisiwe na wakati wa kuwa na familia yangu. Nilifurahi kama nini kuwekwa huru kutokana na mambo yote hayo!”
“Mimi hutoa—na kupokea—zawadi kutoka kwa watu wa familia na marafiki wakati wowote,” anasema Carolyne. “Ninaamini kwamba zawadi kama hizo zisizotarajiwa, ambazo zimetolewa kwa moyo mnyoofu, ndizo bora zaidi.”
Japani “Watoto wetu,” wanaandika Hiroshi na Rie, “hawana tatizo la kutazamia zawadi kisha kuzipuuza. Tukiwa wazazi tunafurahi kuona wanaelewa kwamba mtu anapaswa kuchochewa kutoka moyoni kuwapa wengine zawadi.”
Keiko anakumbuka hivi: “Familia yetu ilikuwa ikisherehekea Krismasi. Baada ya kuhakikisha kwamba mwana wetu alikuwa amelala, mimi na mume wangu tulimwekea zawadi kando ya kitanda chake. Asubuhi iliyofuata tungemwambia: ‘Kwa sababu umekuwa mtoto mzuri, Baba Krismasi amekuletea zawadi.’ Nilipojifunza ukweli kuhusu Krismasi na nikamweleza mwanangu mambo niliyojifunza, alishtuka na akalia sana. Hapo ndipo nilipotambua kwamba Krismasi si kitu kizuri kama inavyoonyeshwa kuwa. Badala yake, ni uwongo, na kwa kuendeleza uwongo huo, nilihisi kwamba nilikuwa nimemsaliti mwanangu.”
Filipino Dave anasema hivi: “Ni vigumu kueleza kuhusu shangwe ambayo Yehova ananipa kupitia kweli zake safi zinazopatikana katika Biblia. Watu wa familia yetu wanapotoa zawadi, hawatazamii chochote kutoka kwa yule anayewapa. Nasi hutoa kutoka moyoni.”
Watu walionukuliwa hapo juu ni baadhi tu ya mamilioni ambao wamejionea kwamba kweli ya Biblia inawaweka watu huru. Jambo muhimu hata zaidi ni kwamba tunapoishi kupatana na kweli hiyo, tunamletea Mungu shangwe. (Methali 27:11) Yesu Kristo alisema: “Waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli, kwa maana, kwa kweli, Baba anawatafuta watu wa namna hiyo wamwabudu.” (Yohana 4:23) Mungu anapochunguza moyo wako, je, anaona mtu anayetaka kujua kweli? Tunatumaini kwamba bila shaka jibu lako ni ndiyo!
[Picha katika ukurasa wa 9]
Wakristo hutoa zawadi wakichochewa na upendo wakati wowote wa mwaka
-