-
Krismasi—Sikukuu ya Kilimwengu Au Siku Takatifu ya Kidini?Mnara wa Mlinzi—1997 | Desemba 15
-
-
Krismasi—Sikukuu ya Kilimwengu Au Siku Takatifu ya Kidini?
HUKO China aitwa Mzee-Krismasi. Katika Uingereza, ajulikana kuwa Baba Krismasi. Urusi watu humwita Babu Jalidi, na huko Marekani, amepewa jina la utani Santa Klaus.
Watu wengi humwona mzee huyu mwenye furaha ambaye ana tumbo kubwa na ndevu nyeupe kama theluji kuwa ndiye wonyesho wenyewe wa Krismasi. Pia ni jambo lijulikanalo sana kwamba Santa Klaus ni ngano, hekaya itegemeayo mapokeo ambayo yashirikishwa na askofu wa Myra wa karne ya nne (katika Uturuki ya siku ya kisasa).
Sikuzote desturi na mapokeo yamekuwa na uvutano wenye nguvu juu ya sherehe mbalimbali, na ndivyo ilivyo Krismasi. Ngano ya Santa ni kimojawapo cha vielelezo vya sanaa-jadiiya yenye kuhusianishwa na sikukuu ipendwayo sana. Ingawa watu fulani hudai kwamba desturi za Krismasi zategemea matukio ambayo yamerekodiwa katika Biblia, kwa uhalisi nyingi za desturi hizi zina vyanzo vya kipagani.
Ule mti wa Krismasi ni kielelezo kingine. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema hivi: “Baada ya kugeuzwa imani kwa Wazungu wapagani kuwa Wakristo, ibada ya mti, iliyo ya kawaida miongoni mwao, ilibaki katika desturi za Kiskandinavia za kurembesha nyumba na ghala kwa majani ya kijani kibichi katika Mwaka Mpya ili kufukuza ibilisi na katika desturi ya kusimamisha mti kwa ajili ya ndege wakati wa Krismasi, baada ya kugeuzwa imani kwao.
Kutengeneza shada za maua ya mholi au miti mingine isiyokauka ni pokeo jingine la Krismasi lipendwalo sana. Jambo hili pia, limetia mizizi kabisa katika ibada ya kipagani. Waroma wa kale walitumia matawi ya mholi kuremba mahekalu wakati wa Saratenalia, msherehekeo wa siku saba wa katikati ya majira ya baridi ambao ulikuwa umetolewa Sarateni, mungu wa kilimo. Msherehekeo huo wa kipagani ulijulikana hasa kwa sababu ya kelele za ulevi na ngono zisizozuiliwa.
Ile desturi ya Krismasi ya kubusu chini ya kitawi cha mlimbo (kionyeshwacho hapa) huenda ikaonekana kwa watu fulani kuwa ya kimahaba, lakini hiyo ni desturi iturejezayo kwenye Enzi za Kati. Makasisi wa Uingereza ya kale waliamini kwamba mlimbo ulikuwa na nguvu za mizungu; kwa sababu hiyo, ulitumiwa kuwa kinga dhidi ya roho waovu, mafumbo ya uchawi, na dhidi ya aina nyingine za uovu. Baada ya muda, ushirikina ulitokea kwamba kubusu chini ya mlimbo kungeongoza kwenye ndoa. Zoea hili bado ni lenye kupendwa sana miongoni mwa watu fulani karibu na wakati wa Krismasi.
Hizo ni chache kati ya desturi za Krismasi ya kisasa ambazo zimeathiriwa na mafundisho ya kipagani au ambazo zimetokana moja kwa moja nayo. Ingawa hivyo, huenda ukajiuliza jinsi mambo hayo yote yalivyotukia. Ni jinsi gani sikukuu ambayo yadai kuheshimu kuzaliwa kwa Kristo ilivyopata kutatanishwa hivyo na desturi zisizo za Kikristo? La maana hata zaidi, Mungu huonaje hilo jambo?
-
-
Mizizi ya Krismasi ya KisasaMnara wa Mlinzi—1997 | Desemba 15
-
-
Mizizi ya Krismasi ya Kisasa
KWA mamilioni ya watu ulimwenguni pote, majira ya Krismasi ni wakati wa mwaka wenye shangwe sana. Ni wakati wa milo ya bei ya juu, mapokeo yenye kuheshimiwa kwa sababu ya ukale wake, na wa kuwa pamoja kifamilia. Sikukuu ya Krismasi pia ni wakati ambapo marafiki na jamaa huonea shangwe kubadilishana kadi na zawadi.
Hata hivyo, miaka 150 iliyopita, Krismasi ilikuwa sikukuu tofauti sana. Katika kitabu chake The Battle for Christmas, profesa wa historia Stephen Nissenbaum aandika hivi: “Krismasi . . . ilikuwa wakati wa unywaji wa kupindukia wakati ambapo kanuni zilizoongoza tabia ya watu hadharani ziliachwa kwa muda kwa kupendelea ‘kanivali’ isiyo na vizuizi, aina fulani ya sherehe ya Desemba iliyo kama sherehe ya kabla ya Kwaresima.”
Kwa wale ambao huitazama Krismasi kwa kicho chenye staha, ufafanuzi huo huenda ukawashtusha sana. Kwa nini yeyote angechafua sikukuu ambayo yadai kuadhimisha kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu? Huenda jibu likakushangaza.
Msingi Wenye Kasoro
Tangu ilipoanzishwa karne ya nne, Krismasi imezingirwa na ubishi. Kwa mfano, kulikuwa na lile swali juu ya siku ya kuzaliwa kwa Yesu. Kwa kuwa Biblia haitaji siku wala mwezi wa kuzaliwa kwa Kristo, tarehe mbalimbali zimedokezwa. Katika karne ya tatu, kikundi kimoja cha wanatheolojia Wamisri kiliweka siku hiyo kuwa Mei 20, huku wengine wakipendelea tarehe za mapema zaidi kama vile Machi 28, Aprili 2, au Aprili 19. Kufikia karne ya 18, kuzaliwa kwa Yesu kulikuwa kumeshirikishwa na kila mwezi wa mwaka! Basi, Desemba 25 ilichaguliwaje mwishowe?
Wasomi walio wengi hukubali kwamba Desemba 25 iliagizwa na Kanisa Katoliki kuwa siku ya kuzaliwa kwa Yesu. Kwa nini? “Yaelekea sana sababu,” chasema kichapo The New Encyclopædia Britannica, “ni kwamba Wakristo wa mapema walitaka hiyo tarehe isadifiane na msherehekeo wa kipagani wa Roma uliotia alama ‘siku ya kuzaliwa kwa jua lisiloshindwa.’” Lakini kwa nini Wakristo ambao walikuwa wamenyanyaswa na wapagani kwa zaidi ya karne mbili na nusu kwa ghafula waliwaachia nafasi wanyanyasaji wao?
Ufisadi Waingizwa
Katika karne ya kwanza, mtume Paulo alionya Timotheo kwamba “watu waovu na walaghai” wangepenya ndani ya kutaniko la Kikristo na kuwaongoza vibaya watu wengi. (2 Timotheo 3:13) Uasi-imani huu mkubwa ulianza baada ya kifo cha mitume. (Matendo 20:29, 30) Baada ya ule uitwao kwa kawaida mgeuzo wa imani wa Konstantino katika karne ya nne, idadi kubwa ya wapagani ilijiunga kwa wingi na namna ya Ukristo ulioenea wakati huo. Kukiwa na matokeo gani? Kitabu Early Christianity and Paganism chataarifu hivi: “Kile kikundi cha waamini wenye bidii kwa kweli ambacho kwa kulinganishwa ni kidogo kilipotea katika umati mkubwa wa wenye kudai kuwa Wakristo.”
Maneno ya Paulo yalithibitika kuwa kweli kama nini! Ilikuwa ni kana kwamba Ukristo wa kweli ulikuwa ukimezwa na ufisadi wa kipagani. Na hakuna mahali popote ambapo uchafuzi huo ulikuwa dhahiri kuliko katika kusherehekea sikukuu mbalimbali.
Kwa kweli, sherehe tu ambayo Wakristo wameamriwa waadhimishe ni ile ya Mlo wa Jioni wa Bwana. (1 Wakorintho 11:23-26) Kwa sababu ya mazoea ya ibada ya sanamu yaliyoshirikishwa na misherehekeo ya Roma, Wakristo wa mapema hawakuishiriki. Kwa sababu hiyo wapagani wa karne ya tatu waliwashutumu Wakristo, wakisema hivi: “Hamzuru maonyesho; hamjihusishi na maonyesho ya hadharani; mwakataa karamu za watu wote, na kukirihi mashindano matakatifu.” Kwa upande mwingine, wapagani walijigamba hivi: “Twaabudu miungu kwa uchangamfu, kwa karamu, nyimbo na michezo.”
Kufikia katikati ya karne ya nne, kuguna kwa wapagani kulitulia. Jinsi gani? Wakristo bandia zaidi na zaidi walipopenya ndani ya kundi, mawazo ya uasi-imani yalizidi. Jambo hilo liliongoza kwenye kuridhiana na ulimwengu wa Roma. Kikieleza juu ya hilo, kitabu The Paganism in Our Christianity chataarifu hivi: “Ilikuwa ni sera hususa ya Kikristo kuidhibiti na kuipa umaana wa Kikristo misherehekeo ya kipagani ambayo pokeo lilifanya ipendwe na watu.” Ndiyo, uasi-imani mkubwa ulikuwa ukitokeza madhara yake. Utayari wa wale waitwao Wakristo isivyofaa wa kukubali rasmi sherehe za kipagani sasa ulileta kiasi fulani cha ukubalifu ndani ya jumuiya. Punde si punde, Wakristo walipata kuwa na misherehekeo mingi ya kila mwaka kama vile wapagani wenyewe. Haishangazi kwamba Krismasi ilikuwa ya kwanza kabisa miongoni mwa hiyo misherehekeo.
Sikukuu ya Kimataifa
Namna ya Ukristo wenye nguvu ilipoenea kotekote Ulaya, watu wengi zaidi na zaidi walianza kusherehekea Krismasi. Kanisa Katoliki lilikubali maoni ya kwamba lilikuwa jambo lifaalo kuendeleza msherehekeo wenye shangwe katika kuiheshimu siku ya kuzaliwa kwa Yesu. Basi, mwaka wa 567 W.K., Baraza la Tours “likatangaza siku zile 12 kuanzia Krismasi hadi Epifania kuwa majira yenye utakatifu na ya kusherehekea.”—The Catholic Encyclopedia for School and Home.
Upesi Krismasi ilitwaa sehemu nyingi kutoka misherehekeo ya mavuno ya kilimwengu ya Kaskazini mwa Ulaya. Kusherehekea kuliendelea kuwa kwa kawaida zaidi ya uchaji kwa maana washerehekeaji walijitia mno katika ulafi na ulevi. Badala ya kuteta dhidi ya mwenendo mlegevu, kanisa liliukubali. (Linganisha Waroma 13:13; 1 Petro 4:3.) Mwaka wa 601 W.K., Papa Gregory wa Kwanza alimwandikia Mellitus, mmishonari wake huko Uingereza, akimwambia “[asi]komeshe shughuli hizo za sherehe za kipagani, lakini kuzirekebisha zifae sherehe ya ibada ya Kanisa, kubadili tu sababu ya sherehe hizo kuwa msukumo wa Kikristo bali si wa kipagani.” Hivyo ndivyo aripotivyo Arthur Weigall, aliyekuwa wakati mmoja mkaguzi mkuu wa mambo ya kale wa serikali ya Misri.
Katika Enzi za Kati, waliotaka marekebisho walihisi uhitaji wa kuteta dhidi ya mazidio hayo. Walipeleka maagizo mengi sana dhidi ya “kutumiwa vibaya kwa sherehe ya Krismasi.” Katika kitabu chake Christmas in America—A History, Dakt. Penne Restad asema hivi: “Makasisi fulani walikazia kwamba jamii ya kibinadamu isiyokamilika ilihitaji majira ya kutojizuia kabisa na ya kuzidi mno katika tamaa za asili, maadamu hayo majira ya kuzidi mno yaliendelezwa chini ya uangalizi wa Kikristo.” Wazo hilo liliongeza tu hali ya mvurugo. Ingawa hivyo, hilo halikubadili hali ya mambo sana, kwa maana desturi za kipagani zilikuwa tayari zimeunganishwa kwa ukaribu sana na Krismasi hivi kwamba watu walio wengi hawakupenda kuziacha. Mwandikaji Tristram Coffin, alisema hivi: “Kwa ujumla watu [walikuwa] wakifanya tu lile walilokuwa wa[me]fanya sikuzote na kuikazia uangalifu mdogo mijadala ya waadilishi.”
Kufikia wakati Wazungu walipoanza kufanya Amerika iwe koloni, Krismasi ilikuwa sikukuu yenye kujulikana sana. Na bado, Krismasi haikukubaliwa katika hizo koloni. Warekebishaji Wapiuriti waliiona hiyo sherehe kuwa ya kipagani na kuipiga marufuku huko Massachusetts kati ya mwaka wa 1659 na wa 1681.
Baada ya hayo marufuku kuondolewa, kusherehekea Krismasi kuliongezeka kotekote katika hizo koloni, hasa kusini mwa New England. Hata hivyo, kwa kufikiria wakati uliopita wa sikukuu hiyo, si jambo la kushangaza kwamba watu fulani walihangaikia kujitumbuiza zaidi ya kumheshimu Mwana wa Mungu. Desturi moja ya Krismasi iliyokuwa hasa yenye kuvuruga ni ile ya ulevi. Vikosi vya vijana wenye ghasia vilikuwa vikiingia katika nyumba za majirani wenye mali na kudai chakula na kinywaji cha bure kwa kutisha kuwakenga wakikataa. Ikiwa mwenye nyumba alikataa, kwa kawaida alilaaniwa, na nyumba yake kuharibiwa pindi kwa pindi.
Hali katika miaka ya 1820 ziliharibika kiasi cha kwamba “michafuko wakati wa sherehe ya Krismasi” ilipata kuwa “tisho kali la kijamii,” asema Profesa Nissenbaum. Katika majiji kama New York na Philadelphia, wamiliki-ardhi wenye mali walianza kuajiri walinzi ili kulinda mashamba yao. Hata yasemwa kwamba Jiji la New York liliunda kikosi chake cha kwanza cha polisi wa kulipwa kufuatia fujo zenye jeuri katika majira ya Krismasi ya mwaka wa 1827/1828!
-