-
Jiji la Kale la Yerusalemu Liliharibiwa Mwaka Gani?—Sehemu ya PiliMnara wa Mlinzi—2011 | Novemba 1
-
-
● Mabamba ya wataalamu wa nyota.
Mabamba hayo ni nini? Hayo ni mabamba ya kikabari yenye maelezo ya mpangilio wa jua, mwezi, sayari, na nyota, pamoja na habari za kihistoria kama vile mwaka wa utawala wa mfalme hususa. Kwa mfano, maandishi ya wataalamu wa nyota yaliyo hapa chini yanaonyesha kupatwa kwa mwezi kulikotokea mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Mukin-zeri.11
Wataalamu wamesema nini? Wanakubali kwamba Wababiloni walikuwa na chati na orodha nyingi sana waliyotumia kufanya hesabu ili kubashiri wakati ambapo yaelekea mwezi ungepatwa.12
Lakini je, Wababiloni wangeweza kuhesabu kwa kurudi nyuma ili kujua wakati ambapo kupatwa kwa mwezi kulitokea wakati uliopita? Profesa John Steele anasema: “Inawezekana kwamba baadhi ya ubashiri wa kwanza kabisa ulitolewa kwa kuhesabu kurudi nyuma wakati maandishi hayo yalipokuwa yakiandikwa.” (Italiki ni zetu.)13 Profesa David Brown, anayeamini kwamba chati hizo kuhusu mpangilio wa mwezi, sayari, na nyota zilikuwa na ubashiri uliokuwa umetolewa muda mfupi kabla ya matukio yaliyotajwa kutokea, anasema inawezekana kwamba baadhi ya “hesabu hizo zilifanywa kwa kurudi nyuma na waandishi katika karne ya nne Kabla ya Kristo na karne za baadaye.”14 Ikiwa hesabu hizo zilifanywa kwa kurudi nyuma, je, zinaweza kutegemeka kabisa bila kuungwa mkono na uthibitisho mwingine?
Hata kama kupatwa kwa mwezi kulitokea tarehe fulani, je, hilo linamaanisha kwamba habari za kihistoria ambazo mwandishi anahusianisha na tarehe hiyo ni sahihi? Si lazima iwe hivyo. Msomi R. J. van der Spek anaeleza: “Walioandika habari hizo walikuwa wataalamu wa nyota bali si wanahistoria.” Anaeleza kwamba habari za kihistoria kwenye sehemu fulani za mabamba hayo ni “za kijuujuu tu,” na kuonya kwamba ni lazima “zitumiwe kwa tahadhari.”15
Maandishi hayo yanaonyesha nini? Kwa mfano, fikiria bamba la VAT 4956. Mstari wa kwanza katika bamba hilo unasema: “Mwaka wa 37 wa Nebukadneza, mfalme wa Babiloni.”16 Kisha, linaeleza kwa undani mahali ambapo mwezi na sayari zilikuwa angani kwa kulinganishwa na nyota na makundi ya nyota. Pia, lina habari kuhusu tukio moja la kupatwa kwa mwezi. Wasomi wanasema kwamba mipangilio hiyo ya mwezi, sayari, na nyota ilitukia mwaka wa 568/567 K.W.K., kumaanisha kwamba mwaka wa 18 wa utawala wa Nebukadneza wa Pili ulikuwa 587 K.W.K., wakati alipoharibu jiji la Yerusalemu. Lakini je, marejeo hayo yanayotegemea uchunguzi wa mpangilio wa mwezi, sayari, na nyota yanaonyesha tu mwaka wa 568/567 K.W.K.?
Bamba hilo linataja tukio la kupatwa kwa mwezi ambalo hesabu za wataalamu wa nyota zinaonyesha lilitokea siku ya 15 ya mwezi wa tatu, au Simanu, katika kalenda ya Babiloni. Hapana shaka kwamba tukio hilo la kupatwa kwa mwezi lilitokea mwezi huo wa Simanu, tarehe inayolingana na Julai 4 (katika kalenda ya Yulio), mwaka wa 568 K.W.K. Hata hivyo, kulikuwa na tukio lingine la kupatwa kwa mwezi miaka 20 mapema, mnamo Julai 15, mwaka wa 588 K.W.K.17
Ikiwa mwaka 588 K.W.K. ndio mwaka wa 37 wa Nebukadneza wa Pili, basi mwaka wa 18 wa utawala wake ulikuwa 607 K.W.K.—mwaka ambao jiji la Yerusalemu liliharibiwa kulingana na mfuatano wa matukio ya Biblia! (Ona mfuatano wa matukio ulio hapa chini.) Lakini je, bamba la VAT 4956 lina habari zaidi zinazounga mkono mwaka wa 607 K.W.K.?
Mbali na tukio la kupatwa kwa mwezi ambalo limetajwa, bamba hilo lina rekodi 13 za uchunguzi wa mwezi, na rekodi 15 za uchunguzi wa sayari. Rekodi hizo zinaonyesha mahali ambapo mwezi au sayari zilikuwa angani kwa kulinganishwa na nyota au makundi ya nyota.18 Pia, kuna vipindi vinane vya wakati, kati ya kuchomoza na kutua kwa jua au mwezi.18a
Kwa sababu habari kuhusu mahali ambapo mwezi ulikuwa angani kwa kulinganishwa na nyota nyingine zinategemeka sana, watafiti wamechunguza kwa makini rekodi hizo 13 kwenye bamba la VAT 4956. Walichunguza rekodi hizo kwa kutumia programu fulani ya kompyuta inayoweza kuonyesha mipangilio ya mwezi, sayari, na nyota katika tarehe fulani wakati uliopita.19 Uchunguzi wao ulifunua nini? Ingawa si rekodi zote kuhusu mipangilio hiyo zinazolingana na mwaka wa 568/567 K.W.K., zile rekodi 13 zinapatana na mahali ambapo mwezi ulikuwa angani miaka 20 mapema, yaani, mwaka wa 588/587 K.W.K.
Kuna sehemu moja ya bamba la 4956 ambayo imeonyeshwa kwenye kurasa hizi inayoonyesha kwamba mpangilio wa mwezi na nyota nyingine ulilingana na mwaka wa 588 K.W.K. vizuri zaidi kuliko mwaka wa 568 K.W.K. Mstari wa 3 wa bamba hilo unasema kwamba mwezi ulikuwa mahali fulani angani mnamo “usiku wa tarehe 9 [mwezi wa Nisanu].” Hata hivyo, wasomi walioonyesha mara ya kwanza kuwa mpangilio huo ulitokea mwaka wa 568 K.W.K. walisema kwamba katika mwaka huo wa 568 K.W.K., mwezi ulikuwa mahali hapo “tarehe 8 ya mwezi wa Nisanu, bali si tarehe 9.” Ili waunge mkono mwaka huo wa 568 K.W.K., walisema kwamba mwandishi aliandika kimakosa nambari “9” badala ya “8.”20 Lakini mahali ambapo mwezi ulikuwa kulingana na mstari wa 3 panalingana kabisa na Nisanu 9, mwaka wa 588 K.W.K.21
Kwa wazi, habari za wataalamu wa nyota katika bamba la VAT 4956 zinaonyesha kuwa mwaka wa 588 K.W.K. ndio mwaka wa 37 wa Nebukadneza wa Pili. Kwa hiyo, jambo hilo linaunga mkono mwaka wa 607 K.W.K. kuwa mwaka ambao jiji la Yerusalemu liliharibiwa—kama Biblia inavyoonyesha.
-
-
Jiji la Kale la Yerusalemu Liliharibiwa Mwaka Gani?—Sehemu ya PiliMnara wa Mlinzi—2011 | Novemba 1
-
-
11. Kitabu Astronomical Diaries and Related Texts From Babylonia, Buku la 5, kilichosahihishwa na Hermann Hunger na kuchapishwa mwaka wa 2001, ukurasa wa 2-3.
12. Kitabu Journal of Cuneiform Studies, Buku la 2, Na. 4, 1948, “A Classification of the Babylonian Astronomical Tablets of the Seleucid Period,” cha A. Sachs, ukurasa wa 282-283.
13. Kitabu Astronomical Diaries and Related Texts From Babylonia, Buku la Tano, ukurasa wa 391.
14. Kitabu Mesopotamian Planetary Astronomy-Astrology, cha David Brown, kilichochapishwa mwaka wa 2000, ukurasa wa 164, 201-202.
15. Kitabu Bibliotheca Orientalis, L N° 1/2, Januari-Maart, 1993, “The Astronomical Diaries as a Source for Achaemenid and Seleucid History,” cha R. J. van der Spek, ukurasa wa 94, 102.
16. Kitabu Astronomical Diaries and Related Texts From Babylonia, Buku la Kwanza, cha Abraham J. Sachs, kilichokamilishwa na kusahihishwa na Hermann Hunger, kilichapishwa mwaka wa 1988, ukurasa wa 47.
17. Kitabu Babylonian Eclipse Observations From 750 BC to 1 BC, cha Peter J. Huber na Salvo De Meis, kilichochapishwa mwaka wa 2004, ukurasa wa 186. Kulingana na bamba la VAT 4956, tukio hili la kupatwa kwa mwezi lilitokea siku ya 15 ya mwezi wa tatu katika kalenda ya Babiloni, jambo linalodokeza kwamba mwezi wa Simanu ulianza siku 15 mapema. Ikiwa tukio hilo la kupatwa kwa mwezi lilitokea Julai 15, 588 K.W.K. kulingana na kalenda ya Yulio, basi siku ya kwanza ya mwezi wa Simanu ingekuwa Juni 30/Julai 1, 588 K.W.K. Kwa hiyo, mwezi wa (Nisanu) katika kalenda ya Babiloni ndio ungekuwa mwezi wa kwanza wa mwaka mpya ambao ungeanza miezi miwili mapema, mnamo Mei 2/3. Ingawa kwa kawaida mwaka wa tukio hilo la kupatwa kwa mwezi ungeanza Aprili 3/4, bamba la VAT 4956 linasema kwenye mstari wa 6 kwamba mwezi wa ziada uliongezwa baada ya mwezi wa (mwisho) wa 12 (Addaru) wa mwaka uliotangulia. (Bamba hilo linasema: “Siku ya 8 ya mwezi wa XII2 [mwezi 13].”) Kwa hiyo, mwaka mpya haungeanza mpaka Mei 2/3. Hivyo, tarehe hiyo ya kupatwa kwa mwezi katika mwaka wa 588 K.W.K. inalingana kabisa na maandishi ya bamba hilo.
18. Kulingana na Berichte über die Verhandlungen der Königl. Sächsischen Gesellschaft der Wissenschaften zu Leipzig (Ripoti Kuhusu Mazungumzo ya Taasisi ya Royal Saxonian Society of Sciences huko Leipzig); Buku la 67; Mei 1, 1915; katika makala “Ein astronomischer Beobachtungstext aus dem 37. Jahre Nebukadnezars II” (Maandishi ya Mtaalamu wa Nyota Kuhusu Mwaka wa 37 wa Nebukadneza wa Pili), cha Paul V. Neugebauer na Ernst F. Weidner, ukurasa wa 67-76, kuna rekodi 13 za uchunguzi wa mwezi ambazo zinaeleza mahali ambapo mwezi ulikuwa angani kwa kulinganishwa na nyota fulani au kundi la nyota. Pia, wameorodhesha rekodi 15 za uchunguzi wa sayari. (Ukurasa wa 72-76) Ingawa alama ya kikabari ya mwezi inaonekana waziwazi kabisa, alama nyingine za majina ya sayari na mahali zilipokuwa hazionekani vizuri. (Kitabu Mesopotamian Planetary Astronomy—Astrology, cha David Brown, kilichochapishwa mwaka wa 2000, ukurasa wa 53-57) Kwa sababu hiyo, mipangilio hiyo ya sayari inaweza kusababisha udadisi na kufasiriwa kwa njia tofauti-tofauti. Kwa kuwa mzunguko wa mwezi wakati uliopita unaweza kutambuliwa kwa urahisi na wataalamu wa nyota, sayari na nyota nyingine ambazo zimetajwa kwenye bamba la VAT 4956 na kuhusianishwa na mwezi zinaweza kutambuliwa. Pia, inawezekana kukadiria kwa usahihi wa kadiri fulani tarehe ambapo mipangilio hiyo ilitokea.
18a. Vipindi hivyo ni kipimo cha wakati, kwa mfano, kuanzia kuchomoza na kutua kwa mwezi katika siku ya kwanza ya mwezi na nyakati nyingine mbili baadaye katika mwezi. Wasomi wamelinganisha vipimo hivyo na tarehe kwenye kalenda. (Makala “The Earliest Datable Observation of the Aurora Borealis” iliyoandikwa na F. R. Stephenson na David M. Willis, katika kitabu Under One Sky—Astronomy and Mathematics in the Ancient Near East, kilichosahihishwa na John M. Steele na Annette Imhausen, kilichochapishwa mwaka wa 2002, ukurasa wa 420-428) Wataalamu wa kale wa nyota walihitaji saa ya aina fulani ili waweze kupima kipindi hicho cha wakati. Vipimo hivyo havikutegemeka. (Kitabu Archimedes, Volume 4, New Studies in the History and Philosophy of Science and Technology, “Observations and Predictions of Eclipse Times by Early Astronomers,” cha John M. Steele, kilichochapishwa mwaka wa 2000, ukurasa wa 65-66) Kwa upande mwingine, hesabu ya kuchunguza mahali ambapo mwezi ulikuwa angani kwa kulinganishwa na sayari na nyota nyingine, ilifanywa kwa uhakika zaidi.
19. Uchunguzi huu ulifanywa kwa kutumia programu fulani ya kompyuta iliyoitwa TheSky6™. Zaidi ya hayo, uchunguzi huu ulifanywa kwa makini zaidi kwa kutumia programu nyingine ya kompyuta inayoitwa Cartes du Ciel/Sky Charts (CDC), na pia programu ya kugeuza tarehe iliyotolewa na kituo cha kuchunguza anga cha jeshi la wanamaji la Marekani. Kwa kuwa alama za kikabari zinazoonyesha mipangilio ya sayari zinaweza kusababisha udadisi na kufasiriwa kwa njia tofauti-tofauti, mipangilio hiyo haikutumiwa katika uchunguzi huu ili kuonyesha mwaka hususa uliokusudiwa katika maandishi hayo ya wataalamu wa nyota.
20. Kitabu Berichte über die Verhandlungen der Königl. Sächsischen Gesellschaft der Wissenschaften zu Leipzig (Ripoti Kuhusu Mazungumzo ya Taasisi ya Royal Saxonian Society of Sciences huko Leipzig); Buku la 67; Mei 1, 1915; Kitabu“Ein astronomischer Beobachtungstext aus dem 37. Jahre Nebukadnezars II, (-567/66)” (Maandishi ya Uchunguzi wa Mtaalamu wa Nyota Kuhusu Mwaka wa 37 wa Utawala wa Nebukadneza wa Pili), cha Paul V. Neugebauer na Ernst F. Weidner, ukurasa wa 41.
21. Bamba la VAT 4956 linasema hivi kwenye mstari wa tatu: “Mwezi ulisimama umbali wa mkono mmoja [au digrii 2] mbele ya nyota ya ß Virginis.” Uchunguzi huu ambao ulikuwa umetajwa awali ulionyesha kwamba siku ya Nisanu 9, mwezi ulikuwa digrii 2 na nyuzi 04 mbele ya nyota ß Virginis na digrii 0 chini yake. Ilionekana kuwa vipimo hivyo vinalingana kabisa.
-