-
Ugumu wa Kulisha MajijiAmkeni!—2005 | Novemba 22
-
-
Tayari majiji fulani katika nchi zinazositawi ni makubwa na yanatarajiwa kuwa makubwa hata zaidi. Kufikia mwaka wa 2015, jiji la Mumbai (ambalo zamani liliitwa Bombay) linatarajiwa kuwa na wakazi milioni 22.6, Delhi milioni 20.9, Mexico City milioni 20.6, na São Paulo milioni 20. Inakadiriwa kwamba jiji lenye watu milioni kumi, kama vile Manila au Rio de Janeiro linahitaji kuleta tani 6,000 za chakula kila siku.
Hiyo si kazi rahisi, na inazidi kuwa ngumu, hasa katika maeneo yaliyo na ongezeko kubwa la watu. Kwa mfano, jiji la Lahore, Pakistan, lina idadi kubwa ya watu wanaozaliwa (asilimia 2.8) na pia watu wengi sana wanahamia huko kutoka mashambani. Katika nchi nyingi zinazositawi, mamilioni ya watu wanahamia majiji ambayo tayari yamesongamana ili kutafuta maisha mazuri, kazi, bidhaa, na huduma bora. Kwa sababu ya watu kuhamia jiji la Dhaka, Bangladesh, idadi ya watu katika jiji hilo inatazamiwa kuongezeka kwa milioni moja au zaidi kila mwaka katika miaka ya karibuni. Kulingana na makadirio, idadi kubwa ya watu nchini China ambao sasa huishi mashambani, watahamia mijini kufikia mwaka wa 2025. Kufikia wakati huohuo, inatarajiwa kwamba watu milioni 600 watakuwa wakiishi katika majiji ya India.
Kwa sababu ya watu kuhamia mijini, mpangilio wa kugawanya chakula katika sehemu nyingi za ulimwengu unabadilika. Kwa mfano, katika Afrika Magharibi, asilimia 14 ya watu waliishi mijini katika mwaka wa 1960. Kufikia mwaka wa 1997, asilimia 40 ya watu waliishi mijini, na inaaminika kwamba kufikia 2020, idadi hiyo itaongezeka kufikia asilimia 63. Katika pembe ya Afrika, idadi ya watu wanaoishi mijini inatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka kumi ijayo. Na inatabiriwa kwamba hivi karibuni, asilimia 90 ya ongezeko la idadi ya watu katika nchi zinazositawi litakuwa katika miji na majiji.
-
-
Ugumu wa Kulisha MajijiAmkeni!—2005 | Novemba 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
MAJIJI YANAKUA
◼ Inatarajiwa kwamba katika miaka 30 ijayo, ongezeko la watu ulimwenguni pote litakuwa hasa katika majiji.
◼ Inatarajiwa kwamba kufikia mwaka wa 2007, zaidi ya nusu ya watu ulimwenguni wataishi katika sehemu za mijini.
◼ Inakadiriwa kwamba idadi ya watu wanaoishi majijini ulimwenguni itaongezeka kwa wastani wa asilimia 1.8 kwa mwaka; ongezeko hilo likiendelea kwa kiwango hicho, idadi ya watu mijini itaongezeka maradufu katika miaka 38.
◼ Idadi ya majiji yenye watu milioni tano au zaidi inatarajiwa kuongezeka kutoka 46 mwaka 2003, hadi 61 mwaka wa 2015.
[Hisani]
Chanzo: World Urbanization Prospects—The 2003 Revision, Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Uchumi na Jamii, Kitengo cha Idadi ya Watu
-