-
Je, Wajua?Mnara wa Mlinzi—2008 | Machi 1
-
-
Sarafu mbili za yule mjane zilikuwa na thamani gani?
Katika karne ya kwanza W.K., Wayahudi walilipa kodi ya hekalu ya kila mwaka ya “drakma mbili,” ambayo ililingana na mshahara wa kazi ya siku mbili. (Mathayo 17:24) Tofauti na hilo, Yesu alisema kwamba shomoro wawili waliuzwa kwa “sarafu ya thamani ndogo,” ambayo inalingana na mshahara wa kazi ya dakika 45. Pia, shomoro watano wangeweza kununuliwa kwa bei iliyokuwa mara mbili ya hiyo, au iliyolingana na mshahara wa kazi ya dakika 90.—Mathayo 10:29; Luka 12:6.
Mchango wa hekalu uliotolewa na yule mjane ambaye Yesu aliona ulikuwa wenye thamani ndogo kuliko bei ya shomoro watano. Sarafu hizo mbili, au lepta mbili, ndizo zilizokuwa sarafu ndogo zaidi za shaba ambazo zilitumiwa wakati huo katika Israeli. Thamani yake ilikuwa sawa na sehemu moja ya 64 tu ya mshahara wa siku moja, au tukipiga hesabu kwa siku moja ya kazi ambayo kwa wastani ilikuwa na saa 12, basi thamani yake ilikuwa sawa na mshahara wa kazi iliyofanywa kwa muda usiozidi dakika 12.
Yesu Kristo alisema kwamba zawadi ya mjane huyo ilikuwa na thamani kubwa zaidi kuliko zile za wote waliotoa zaidi “kutokana na ziada yao.” Kwa nini? Simulizi hilo linasema kwamba mjane huyo alikuwa na “sarafu ndogo mbili,” kwa hiyo angeweza kutoa moja na kubaki na moja. Hata hivyo, alitoa “vyote alivyokuwa navyo, riziki yake yote.”—Marko 12:41-44; Luka 21:2-4.
-
-
Je, Wajua?Mnara wa Mlinzi—2008 | Machi 1
-
-
[Picha katika ukurasa wa 12]
Lepta, ukubwa halisi
-