-
Mawasiliano Ni Muhimu kwa Viumbe na MimeaAmkeni!—2003 | Septemba 22
-
-
Hata hivyo, si wanadamu peke yao wanaoweza kuwasiliana. Ijapokuwa wanyama huongozwa hasa na silika, wao pia wana njia za kustaajabisha za kuwasiliana. Kwa mfano, kila mwaka pengwini wa emperor wanaochumbiana katika eneo lenye theluji la Antaktika huwasiliana kwa kutoa milio kabla ya majira ya baridi kali. Pengwini hao hawatoi milio hiyo ili kuwafurahisha wenzao, bali wanafanya hivyo kwa sababu maisha ya kifaranga wao wa baadaye yanahusika. Jinsi gani?
Baada ya kutaga yai, pengwini wa kike humwachia pengwini wa kiume yai hilo ili aende baharini kutafuta chakula, naye pengwini wa kiume huliatamia kwa kuliweka katikati ya manyoya yake. Baada ya siku 65 hivi, pengwini wa kike hurudi akitembea na kuteleza kwa tumbo kwenye barafu kwa umbali wa kilometa 150. Yeye hukabili kibarua kigumu anapotafuta kikundi chake cha pengwini. Lakini atamjuaje mwenzi wake na kifaranga wake kati ya makumi ya maelfu ya pengwini wanaotoa milio? Wakati wa uchumba, kila ndege hujitahidi kukumbuka nyimbo za mwenzi wake kabisa hivi kwamba hata baada ya kutengana kwa miezi kadhaa wanaweza kutambuana!
Zaidi ya kuwasiliana kwa milio mbalimbali yenye kustaajabisha, viumbe huwasiliana pia kwa ishara, kwa rangi zenye kuvutia, kwa kumulika-mulika, na kwa harufu.
-
-
Mawasiliano ya Viumbe na MimeaAmkeni!—2003 | Septemba 22
-
-
Mawasiliano ya Viumbe na Mimea
“Bila mawasiliano, kila kiumbe angekuwa kama kisiwa kilichojitenga na visiwa vingine.”—The Language of Animals.
IWE ni msituni, mbugani, au katika bustani yako, huenda wanyama mbalimbali wanawasiliana sasa hivi. Kitabu The Language of Animals kinasema hivi: “Wanyama hutumia hisi zote kuwasiliana. Wao hutoa ishara za mwili, huketi na kusimama kwa njia maalumu; hutoa na kunusa harufu kali kama vile vicheche waliotishwa wanavyofanya, hutoa harufu isiyo kali; hutoa kilio chembamba au cha hofu, huimba; hutoa na kupokea mawimbi ya umeme; humulika-mulika; hubadili rangi; ‘hucheza dansi;’ na hata hupigapiga na kutikisa ardhi wanapotembea.” Lakini hizo ishara zote zina kusudi gani?
Wanasayansi hufahamu maana ya ishara za wanyama kwa kuwachunguza kwa makini. Kwa mfano, wamegundua kwamba kuku anapomwona adui ambaye hawezi kuruka kama vile aina fulani ya kicheche, yeye huwaonya kuku wengine kwa kutoa sauti kali ya kuk, kuk, kuk. Lakini kuku anapomwona mwewe, yeye hutoa mlio mwembamba mrefu. Katika visa vyote viwili, kuku wale wengine huitikia upesi kupatana na aina ya mlio waliosikia. Hilo huonyesha kwamba wameelewana. Ndege wengine pia wameonekana wakitoa milio kama hiyo yenye ujumbe mbalimbali.
Kitabu Songs, Roars, and Rituals kinasema kwamba “njia moja kuu ya kuchunguza mawasiliano ya wanyama ni kurekodi mlio hususa na kuwachezea wanyama mlio huo kuona kama wataitikia kwa njia inayotarajiwa.” Wakati kuku walipojaribiwa kwa milio hiyo, waliitikia kama kawaida. Mbinu hiyo imetumiwa pia kuwachunguza buibui. Watafiti walichunguza kile kinachowavutia buibui wa kike aina ya wolf kwa buibui wa kiume ambao hujaribu kuwafurahisha buibui wa kike kwa kuwapungia miguu yao ya mbele yenye manyoya-manyoya. Watafiti hao walifanya majaribio hayo kwa kupiga picha ya video ya buibui wa kiume kisha wakaondoa manyoya ya miguu katika video hiyo. Walipocheza ukanda huo wa video mbele ya buibui wa kike, buibui huyo hakuvutiwa hata kidogo. Walijifunza nini? Inaonekana buibui wa kike aina ya wolf huvutiwa tu na buibui wa kiume wanaopunga miguu yenye manyoya!
Kuwasiliana kwa Harufu
Wanyama wengi huwasiliana kwa kutokeza kemikali kali zinazoitwa pheromone. Kwa kawaida wao huzitokeza kupitia tezi maalumu, mkojo, au kinyesi chao. Wanyama kama vile mbwa na paka hutia mpaka eneo lao kama tu mwanadamu anavyoweka jina au ua kuonyesha kwamba anamiliki eneo fulani. Ijapokuwa mipaka hiyo haionekani, inawasaidia wanyama wa jamii moja kuishi mbali-mbali.
Lakini zaidi ya kutia alama eneo fulani, kemikali za pheromone hutumiwa pia kwa njia nyingine. Kemikali hizo hutoa habari nyingi ambazo wanyama wengine huchunguza na kupendezwa nazo sana. Kitabu How Animals Communicate kinasema kwamba “huenda harufu za kemikali hizo zinaonyesha umri wa mnyama, jinsia, nguvu na sifa zake nyingine, [na] kama yuko tayari kujamiiana . . . Harufu hizo ni kama kitambulisho cha mnyama.” Wanyama fulani hawapendi alama walizoziweka zichezewe, jambo ambalo watunzaji wa bustani za wanyama wanafahamu. Baada ya kusafisha vizimba au sehemu zilizotengewa wanyama, watunzaji hao wamegundua kwamba wanyama wengi hutia alama tena sehemu zao bila kukawia. Naam, “mnyama anaweza kuvurugika na kutenda kwa njia isiyo ya kawaida na hata anaweza kuwa tasa iwapo hatanusa harufu yake,” chasema kitabu kilichonukuliwa juu.
Kemikali za pheromone ni muhimu hata kwa wadudu. Kwa mfano, aina fulani ya kemikali hizo huwachochea wadudu kuhama kwa wingi na kushambulia. Aina nyingine huwasaidia kutambua mahali chakula kipo au mahali pa kujenga makao. Hizo zinatia ndani kemikali zinazowachochea kujamiiana, na viumbe fulani huchochewa sana nazo. Nondo wa hariri wa kiume wana vipapasio viwili vidogo vyenye manyoya mengi madogo-madogo. Vipapasio hivyo vinaweza kutambua hata molekuli moja ya kemikali ambayo humchochea nondo wa kike kujamiiana! Nondo wa kiume anapotambua molekuli 200 za nondo wa kike, ataanza kumtafuta. Hata hivyo, si viumbe tu wanaowasiliana kwa kutumia kemikali.
-