Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu
    Amkeni!—1996 | Oktoba 8
    • Serikali Zinajaribu Kudhibiti Uhalifu

      Uchunguzi mmoja wa 1990 uliofanywa na Umoja wa Mataifa ulifunua kwamba nchi zenye maendeleo zaidi zinatumia wastani wa asilimia 2 hadi 3 wa bajeti zao za kila mwaka kudhibiti uhalifu, huku nchi zenye kuendelea zikitumia hata zaidi, wastani wa asilimia 9 hadi 14. Kuongeza idadi ya polisi na kuwaandalia vifaa bora ni mambo ya kutangulizwa katika nchi fulani. Lakini matokeo ni tofauti-tofauti. Wananchi fulani wa Hungaria wanalalamika hivi: “Hakuna kamwe polisi wa kutosha kushika wahalifu lakini sikuzote kuna polisi wengi zaidi wa kushika wavunjaji wa sheria za barabarani.”

      Hivi majuzi serikali nyingi zimepata ikiwa jambo la lazima kuweka sheria kali zaidi za uhalifu. Kwa kielelezo, kwa kuwa “utekaji-nyara unaongezeka katika Amerika ya Latini,” lasema gazeti Time, serikali za huko zimeitikia kwa kutunga sheria ambazo “ni kali na hazitumiki. . . . Ni rahisi kupitisha sheria,” hilo lakiri, “lakini ni vigumu zaidi kuzitekeleza.”

      Inakadiriwa kwamba katika Uingereza zaidi ya programu 100,000 za majirani kuchungiana nyumba, ambazo zinachunga angalau nyumba milioni nne, zilikuwapo katika 1992. Programu kama hizo zilitekelezwa katika Australia katika miaka ya katikati ya 1980. Lengo lao, yasema Taasisi ya Australia ya Uhalifu, ni kupunguza uhalifu “kwa kuboresha ufahamu wa umma kuhusu usalama wa peupe, kwa kuboresha mtazamo na mwenendo wa wakazi katika kuripoti uhalifu na visa vyenye kutilika shaka katika ujirani na kwa kupunguza urahisi wa kupatwa na uhalifu kwa kuwekea alama mali zao na kuweka vifaa vya usalama vinavyotumika vizuri.”

      Televisheni za ulinzi hutumiwa katika sehemu fulani kuunganisha vituo vya polisi pamoja na maeneo ya biashara. Kamera za vidio hutumiwa pia na polisi, benki, na maduka ili kuzuia uhalifu au kuwa vyombo vya kutambulisha wavunja-sheria.

      Katika Nigeria polisi wana vizuizi vya barabarani katika jitihada za kushika wanyang’anyi na wezi wa magari. Serikali imeanzisha kikosi cha kupambana na uhalifu wa kibiashara na upunjaji. Kamati za uhusiano kati ya polisi na jumuiya ambayo imefanyizwa kwa viongozi wa jumuiya huarifu polisi juu ya utendaji wa uhalifu na watu wenye kutilika shaka.

      Wageni ambao huenda Filipino huona kwamba nyumba nyingi mara nyingi haziachwi bila mtu wa kulinda na kwamba watu wengi wana mbwa. Wafanyabiashara hutumia walinzi wa kibinafsi kulinda biashara zao. Vifaa vya kuzuia gari lisiibwe huuzwa sana. Watu wawezao kufanya hivyo huingia katika maeneo au makao yao yenye ulinzi mkali.

      Gazeti la Uingereza The Independent lilisema: “Watu wakosapo uhakika katika sheria, wananchi wengi huzidi kujiundia kinga za jumuiya zao zenyewe.” Na watu wengi zaidi na zaidi wanajihami. Kwa kielelezo, katika Marekani, inakadiriwa kwamba nusu za nyumba zote zina angalau bunduki moja.

      Daima serikali zinasitawisha njia mpya za kupambana na uhalifu. Lakini V. Vsevolodov, wa Chuo cha Mambo ya Kitaifa katika Ukrainia, asema kwamba kulingana na ripoti za UM, watu wengi wenye vipawa hupata “njia za kipekee sana za kutenda uhalifu” hivi kwamba “mazoezi ya watekelezaji sheria” hayawezi kuwafikia. Wahalifu wenye akili hurudisha pesa nyingi sana katika biashara na mambo ya kijamii, wakijitambulisha na jamii na “kujipa wenyewe vyeo vya juu katika jamii.”

      Kupoteza Uhakika

      Idadi yenye kuongezeka ya watu katika baadhi ya nchi hata imeanza kuamini kwamba serikali yenyewe ni sehemu ya tatizo hilo. Gazeti Asiaweek lilinukuu mkuu wa kikundi fulani cha kupambana na uhalifu akisema: “Karibu asilimia 90 ya washukiwa wote tunaowakamata ama ni polisi ama ni wanajeshi.” Ziwe ni za kweli au sivyo, ripoti hizo zilimfanya mtungaji-sheria mmoja kueleza hivi: “Ikiwa wale wanaoapishwa kutegemeza sheria wenyewe ndio wavunjaji wa sheria, jamii yetu imo matatani.”

      Kashfa za ufisadi zinazohusu maofisa wa ngazi za juu zimekumba serikali nyingi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, jambo lenye kudhoofisha hata zaidi uhakika wa wananchi. Mbali na kupoteza imani katika uwezo wa serikali kudhibiti uhalifu, watu sasa wanatilia shaka azimio lao la kufanya hivyo. Mwelimishaji mmoja aliuliza: “Hawa wenye mamlaka wanawezaje kupambana na uhalifu ikiwa wao wenyewe wamejiingiza sana katika uhalifu?”

      Serikali huja na kwenda, lakini uhalifu unadumu. Lakini kuna wakati unaokuja karibuni ambapo uhalifu hautakuwapo tena!

  • Hatimaye—Serikali Itakayomaliza Uhalifu
    Amkeni!—1996 | Oktoba 8
    • BIBLIA ilitabiri kwamba katika siku zetu watu wangekuwa “wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema.” (2 Timotheo 3:2, 3) Watu wa namna hiyo hutenda uhalifu.

      Kwa kuwa watu hutenda uhalifu, kwa kadiri wabadilikavyo na kuwa watu wema, ndivyo uhalifu unavyopunguka. Lakini haijapata kuwa rahisi kwa watu kubadilika na kuwa watu wazuri. Ni vigumu zaidi leo kuliko wakati mwingine wowote, kwa kuwa tangu 1914, tarehe iliyotajwa katika kronolojia ya Biblia, tumekuwa tukiishi katika “siku za mwisho” za mfumo huu wa mambo. Kama Biblia ilivyotabiri, kipindi hiki ni “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” Hizi nyakati za hatari zimesababishwa na Shetani Ibilisi, mhalifu mkubwa kuliko wote, ambaye ana “ghadhabu nyingi, akijua ya kwamba ana wakati mchache tu.”—2 Timotheo 3:1, NW; Ufunuo 12:12.

      Hilo laonyesha sababu ya ongezeko la uhalifu leo. Shetani ajua kwamba yeye na mfumo wake wataangamizwa karibuni. Katika huo muda mfupi unaobaki, yeye anatafuta kila njia iwezekanayo kuingiza katika wanadamu vitabia vibaya vinavyotajwa katika 2 Timotheo sura ya 3. Hivyo, ili serikali yoyote imalize uhalifu, ni lazima iondoe uvutano wa Shetani na pia isaidie kubadili watu ili wasitende kamwe kwa njia inayofafanuliwa hapo juu. Lakini je, kuna serikali iwezayo kutimiza jambo hili lililo gumu kupita uwezo wa wanadamu?

      Hakuna serikali ya kibinadamu iwezayo kufaulu. J. Vaskovich, mwalimu wa sheria katika Ukrainia, adokeza uhitaji wa kuwa na “shirika moja lenye uwezo, ambalo laweza kuunganisha na kuratibu jitihada za mashirika yote ya serikali na ya umma.” Na Rais Fidel Ramos wa Filipino alisema hivi katika mkutano mmoja kuhusu uhalifu: “Kwa sababu maendeleo yamefanya ulimwengu wetu uonekane kuwa mdogo, uhalifu umeweza kuvuka mipaka ya mataifa nao umekuwa tatizo la kimataifa. Na hivyo masuluhisho yapaswa kuwa pia ya kimataifa.”

      “Msiba wa Ulimwenguni Pote”

      Umoja wa Mataifa ni shirika la kimataifa. Tangu lianzishwe, limejaribu kupambana na uhalifu. Lakini halina masuluhisho kuliko serikali za mataifa. Kitabu The United Nations and Crime Prevention chasema: “Uhalifu unaofanywa nchini umeshinda udhibiti wa mataifa moja-moja na uhalifu wa kimataifa umeongezeka sana kuliko uwezo wa jumuiya ya kimataifa. . . . Uhalifu uliofanywa na vikundi vya magenge ya uhalifu umeongezeka kwa kiasi cha kushangaza sana, ukiwa na matokeo mabaya sana kwa habari ya jeuri ya kimwili, matisho na ufisadi wa maofisa wa umma. Uharamia umeua makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia. Ulanguzi wa dawa za kulevya wenye kudhuru umekuwa msiba wa ulimwenguni pote.”

      Pindi moja, James Madison, rais wa nne wa Marekani, alisema hivi: “Katika kuanzisha serikali itakayoongozwa na watu wanaotawala watu, kuna tatizo hili kubwa: ni lazima kwanza uiwezeshe serikali idhibiti wenye kutawalwa; kisha uilazimishe ijidhibiti yenyewe.” (Linganisha Mhubiri 8:9.) Hivyo suluhisho lifaalo lingekuwa kubadili serikali ‘inayoongozwa na watu wanaotawala watu’ kwa mfumo ambao Mungu angetawala. Lakini, je, suluhisho hilo lawezekana?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki