-
Je, Uhai Unakosa Kuthaminiwa kwa Vyovyote?Amkeni!—2000 | Julai 8
-
-
Je, Uhai Unakosa Kuthaminiwa kwa Vyovyote?
“Ulimwengu hauthamini uhai. Uuaji waweza kutekelezwa kwa mamia machache ya pauni [za Uingereza] na kuna watu chungu nzima walio tayari kukodiwa ili kuua.”—The Scotsman.
Mnamo mwezi wa Aprili 1999, kisa kilichoshtua ulimwengu mzima kilitukia huko Littleton, Colorado, Marekani, wakati vijana wawili waliposhambulia kwa jeuri Shule ya Sekondari ya Columbine na kuwaua watu 15. Uchunguzi ulionyesha kwamba mmojawapo wa washambuliaji hao alikuwa na Web site kwenye Internet ambamo alikuwa ameandika: “WAFU HAWAJADILIANI!” Washambuliaji wote wawili walikufa katika msiba huo.
UUAJI-KIMAKUSUDI umeenea ulimwenguni pote, kila siku idadi isiyohesabika ya watu huuawa kinyama. Mwaka wa 1995, nchi ya Afrika Kusini iliongoza ulimwenguni ikiwa na kiwango cha mauaji cha 75 kwa kila wakazi 100,000. Uhai hauthaminiwi hususan katika nchi moja ya Amerika Kusini, ambako zaidi ya watu 6,000 waliuawa kwa sababu za kisiasa mwaka wa 1997. Mauaji yanayotekelezwa na wauaji wa kukodiwa yamekuwa jambo la kawaida. Ripoti moja juu ya nchi hiyo yasema: “Jambo linalotisha ni kwamba uuaji-kimakusudi wa watoto umeongezeka sana: Mnamo mwaka wa 1996, watoto 4,322 waliuawa, ongezeko la asilimia 40 kwa muda wa miaka miwili tu.” Hata watoto pia wameanza kuwa wauaji—wanaua watoto wengine na wazazi wao wenyewe. Kwa kweli uhai hauthaminiwi kwa vyovyote.
Mbona Kuna “Utamaduni wa Mauaji”?
Mambo hakika na takwimu hizo zaonyesha nini? Ongezeko la kutostahi uhai. Watu wenye tamaa ya uongozi na ya fedha huua bila wasiwasi wowote. Mabwanyenye wa ulanguzi wa dawa za kulevya huagiza mauaji ya familia nzima-nzima. Wao hupunguza uzito wa uuaji wanaotekeleza kwa kutumia misemo kama “kipigo,” “kufutilia mbali,” “kuondosha,” au “kukomesha” wahasiriwa wanaolengwa. Maangamizi ya jamii nzima-nzima na uuaji-kimakusudi wa kikabila yameongeza idadi ya wanaouawa na hivyo kudunisha uhai wa binadamu. Tokeo ni kwamba visa vya mauaji vimekuwa habari za kawaida kwenye televisheni kotekote ulimwenguni.
Zingatia pia jeuri na machafuko yanayotukuzwa kwenye televisheni na sinema, inaonekana kwamba jamii yetu imezingirwa na utamaduni wenye kuchukiza unaokazia mauaji. Kichapo Encyclopædia Britannica chasema hivi kuhusiana na jambo hilo: “Katika nusu ya mwisho ya karne ya 20, habari za mauaji zimekuja kupendwa mno isivyo kawaida. Jambo la kushangaza ni kwamba, hapo awali, habari za mauaji ziliepukwa kabisa katika utafiti wa kina wa kisayansi, na kwa kadiri fulani katika makisio ya kifalsafa.” Josep Fericgla, profesa Mkataloni wa elimu ya utamaduni wa binadamu asema, “mauaji yamekuwa uamuzi wa mwisho katika jamii zetu, na hivyo yamekuwa mojawapo ya vyombo muhimu sana vya kudhibiti mawazo leo.”
Huenda sifa kuu ya “utamaduni [huu] wa mauaji” ikawa dhana inayopendwa sana ya kwamba nguvu, mamlaka, fedha, na raha ni muhimu zaidi kuliko uhai wa binadamu na viwango vya adili.
“Utamaduni [huu] wa mauaji” huenezwaje? Wazazi wanaweza kufanya nini ili kuzuia athari hii yenye kufisidi iliyoenea na ambayo inawaathiri watoto wao? Hayo ni baadhi ya maswali yatakayojibiwa katika makala zifuatazo.
-
-
“Utamaduni wa Mauaji” Huendelezwaje?Amkeni!—2000 | Julai 8
-
-
“Utamaduni wa Mauaji” Huendelezwaje?
“Licha ya kwamba wakimbizi wachanga wa Kosovo wenye wasiwasi wako mbali sana na watoto Wamarekani wanaokabili jeuri na mambo mengine yenye kuumiza, hali yao ya kihisia-moyo inalingana.” —Marc Kaufman, The Washington Post.
Tupende tusipende, sote tunaathiriwa na kifo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hilo ni kweli bila kujali tunakoishi—iwe ni katika nchi inayokumbwa na mapambano ya kikatili au katika ile iliyo na amani ya kadiri.
“UTAMADUNI wa mauaji” wadhihirishwa na visa chungu nzima vya kushuka moyo, maumivu makali ya moyo, uraibu wa dawa za kulevya, utoaji-mimba, mazoea hatari, kujiua, na mauaji ya umati leo. Profesa Michael Kearl, wa Kitengo cha Elimu-jamii na Elimu ya Binadamu katika Chuo Kikuu cha Trinity huko San Antonio, Texas, Marekani, alieleza hivi kuhusu matumizi ya hila ya habari ya kifo: “Tuchunguzapo hali mwishoni mwa karne yetu ya 20 [1999], twaona kwamba . . . kifo kinaonwa kuwa kani muhimu inayotegemeza uhai, afya, na muundo wa utaratibu wa kijamii. Kifo huchochea dini zetu, falsafa, mawazo ya kisiasa, sanaa na tekinolojia ya tiba. Huchochea watu wanunue magazeti na bima, hufanyiza njama zenye kusisimua kwenye vipindi vya televisheni, na . . . hata huimarisha viwanda vyetu.” Acheni tuchunguze mifano kadhaa inayodhihirisha hali hii iitwayo utamaduni wa mauaji katika nyakati zetu.
Uuzaji wa Silaha
“Utamaduni wa mauaji” hudhihirishwa kila siku na uuzaji wa silaha. Silaha hutumiwa kuangamiza askari, lakini hutumiwa hasa kuua raia, kutia ndani wanawake na watoto wasio na hatia. Katika vita, iwe ya wenyewe kwa wenyewe au la, sikuzote uhai hukosa kuthaminiwa. Risasi inayorushwa na mwuaji aliyekodiwa au askari-doria hugharimu fedha ngapi?
Katika nchi fulani uwezo wa umma wa kupata silaha kwa urahisi umesababisha ongezeko kubwa la kuogofya la vifo vya watu mmoja-mmoja na vya vikundi vya watu. Maandamano mengi yalizuka baada ya msiba wa ufyatuaji risasi katika shule ya sekondari huko Littleton, Colorado, kwa sababu ya kuenea kwa uuzaji wa silaha na jinsi ambavyo watoto wanazipata kwa urahisi. Idadi ya vijana wanaouawa kinyama huko Marekani inatisha—gazeti Newsweek, lasema ni wastani wa vijana 40 kila juma. Takriban asilimia 90 kati yao hupigwa risasi. Hiyo ni sawa na visa 150 vya mauaji kila mwaka kama kile kisa cha Littleton!
Ulimwengu wa Vitumbuizo
Sinema hutumia kwa faida habari zinazohusu kifo. Kwa mfano, sinema yaweza kutukuza mno ukosefu wa adili, jeuri, ulanguzi wa dawa za kulevya, au uhalifu uliopangwa na hivyo kupunguza thamani ya uhai na kudunisha kanuni za adili. Hata kuna sinema zinazotilia chumvi kifo—zikikazia hekaya ya uhai baada ya kifo na dhana ya wafu fulani kurudi na kuwatembelea walio hai—hekaya hizo hudunisha kifo.
Ndivyo ilivyo na vipindi fulani vya televisheni na muziki. Kwa mujibu wa ripoti za habari, wale vijana wauaji wa Littleton walikuwa wapenzi shupavu wa mwimbaji mmoja wa roki ambaye amejulikana sana kwa sababu ya “picha zake za wake-dume, na za kishetani,” na nyimbo “zinazokazia uasi na kifo.”
Huko Marekani, njia ya kuainisha vipindi vya televisheni ilirekebishwa ili kuwalinda vijana wasiangalie mambo yanayoweza kuwadhuru. Hata hivyo hali imezidi kuzorota. Jonathan Alter, aeleza kwenye gazeti Newsweek kwamba uainishaji huo wa televisheni “waweza kuwachochea watoto watamani zaidi mambo yasiyo ya adili.” Aliongezea kwamba ili kuwafedhehesha na kuwashurutisha wale wenye wajibu wapunguze jeuri kwenye vyombo vya habari, itambidi Rais Clinton “atangaze hadharani majina ya kampuni zote kubwa (na maofisa wake wakuu)” ambao mbali na kutunga sinema za kudungana visu na kurekodi ‘muziki wa rapu ya magenge,’ pia hubuni programu za michezo ya kompyuta inayowawezesha watoto “waue watu ‘kihalisi’.”
Mauaji Kwenye Michezo ya Kompyuta na Kwenye Internet
Katika kitabu chake The Deathmatch Manifesto, Robert Waring achanganua jinsi ambavyo vijana hupenda ile inayoitwa eti michezo ya misafara ya mauaji.a Bw. Waring anaamini kwamba kikundi kingine cha siri cha wachezaji wa michezo hiyo kimezuka. Kwa kweli michezo hiyo hufunza kuua badala ya kuelimisha. “Mtu huathiriwa sana anapocheza na mpinzani aliye hai kutoka mahali popote ulimwenguni, na kujaribu kuthibitisha kuwa ana uwezo. Ni rahisi mno kutumbukia katika mtego huo,” aeleza Waring. Vijana hunaswa na uvutano wa mandhari kamili zilizobuniwa ili kuremba mapambano yaliyojaa umwagikaji-damu. Wengine hununua programu za michezo ya kompyuta ili wazitumie kwenye televisheni nyumbani wanapokosa Internet. Wengine huzuru kumbi za umma kwa kawaida ambako hukodi mashine za michezo ya kompyuta na kupigana ‘kihalisi’ hadi kifo na wapinzani wengine.
Ijapokuwa michezo ya “misafara ya mauaji” huainishwa kulingana na umri wa mchezaji, ukweli ni kwamba haidhibitiwi vyakutosha. Eddie mwenye umri wa miaka 14 kutoka Marekani alisema hivi: “Kwa kawaida watu hukuambia ungali mtoto, lakini hawakuzuii kununua [mchezo huo].” Yeye hufurahia mchezo wenye mapambano kabambe ya ufyatulianaji risasi. Ingawa wazazi wake wanajua jambo hilo, nao wanalichukia, wao huchunguza mara chache sana kuona kama anaucheza mchezo huo. Kijana mmoja alifikia mkataa huu: “Kizazi chetu tofauti kabisa na kizazi kingine chochote kimekufa ganzi kabisa kuelekea jeuri. Televisheni huwalea watoto leo badala ya wazazi, na televisheni hutosheleza hamu ya watoto ya kuona jeuri.” John Leland, aliandika hivi kwenye gazeti Newsweek: “Huku vijana milioni 11 sasa wakitumia Internet [huko Marekani], wengi hutumia wakati mwingi zaidi katika mazingira wasiyojua wazazi wengi.”
Mitindo ya Maisha Iongozayo Kwenye Kifo
Vipi juu ya utendaji mwingine mbali na ulimwengu wa michezo ya “misafara ya mauaji” na sinema zenye jeuri? Ijapokuwa hatushindani kufa kupona na viumbe wa ajabu maishani, mtindo wa maisha wa watu wengi hutia ndani mazoea hatari. Kwa mfano, licha ya uvutano wa familia, mifumo ya utunzaji wa afya, na watu fulani wenye mamlaka ambao wanaonya juu ya hatari ya kuvuta sigareti na kutumia vibaya dawa za kulevya, mazoea hayo yanazidi kusitawi. Mara nyingi husababisha kifo cha mapema. Ili kuchuma faida zaidi kwa njia haramu, mashirika makubwa ya kibiashara na walanguzi wa dawa za kulevya huendelea kujifaidi kutokana na wasiwasi, kutamauka, na ufukara wa kiroho wa watu.
Ni Nani Chanzo cha Hayo Yote?
Je, Biblia inaeleza mauaji kuwa kitumbuizo? Je, inatetea mitindo ya maisha inayoweza kutufisha? La hasha. Wakristo wa kweli sawa na mtume Paulo huona kifo kuwa “adui” tu. (1 Wakorintho 15:26) Wakristo hawakioni kifo kuwa kitu cha kuvutia na cha kuchezea, badala yake, wanakiona kuwa kitu kinachokiuka asili ya mwanadamu, tokeo la moja kwa moja la dhambi na kumwasi Mungu. (Waroma 5:12; 6:23) Kifo hakikuwa kamwe sehemu ya kusudi la awali la Mungu kwa mwanadamu.
Shetani husemwa kuwa ana “uwezo wa kusababisha kifo.” Anaitwa “muua-binadamu,” si kwa sababu tu anasababisha kifo moja kwa moja, bali kwa sababu anasababisha kifo kwa kutumia udanganyifu, kwa kuwashawishi watu wafanye dhambi, kwa kuendeleza mwenendo unaofisidi na kuleta kifo, na kwa kusitawisha mitazamo ya uuaji-kimakusudi katika akili na mioyo ya wanaume, wanawake, na hata watoto. (Waebrania 2:14, 15; Yohana 8:44; 2 Wakorintho 11:3; Yakobo 4:1, 2) Hata hivyo, kwa nini vijana ndio shabaha yake kuu? Twaweza kuwasaidiaje?
[Maelezo ya Chini]
a Katika michezo ya “Misafara ya Kifo,” ripoti hiyo yasema, “wachezaji huchochewa kuuana katika michezo yenye mandhari kamili kwenye Internet.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
“Kizazi chetu tofauti kabisa na kizazi kingine chochote kimekufa ganzi kabisa kuelekea jeuri”
-
-
Kuwasaidia Vijana Waepuke “Utamaduni wa Mauaji”Amkeni!—2000 | Julai 8
-
-
Kuwasaidia Vijana Waepuke “Utamaduni wa Mauaji”
Ni nini kinachowafanya vijana wavutiwe na mauaji leo? Henry Hyde, Mbunge wa jimbo la Illinois, Marekani, alisema hivi: “Vijana hawa wana utupu wa kiroho ambao hujazwa na utamaduni wa mauaji na jeuri.”
MSOMAJI mmoja wa gazeti Time aliandika: “Utamaduni wa mauaji uliopo miongoni mwa vijana wetu leo husababishwa na wazazi wazembe, vitumbuizo vya jeuri na ukosefu wa msingi maalum wa kiadili na kiroho.”
Tatizo jingine kubwa linalowasumbua vijana ni upweke. Wengine huishi na wazazi ambao hushinda kazini mchana kutwa; wengine wana mzazi mmoja tu. Kichapo kimoja chasema kwamba, wabalehe huko Marekani hubaki peke yao kwa muda wa saa tatu na nusu kila siku nao huwa pamoja na wazazi wao kwa muda unaopungua saa 11 kila juma tofauti na ilivyokuwa kwa vijana walioishi miaka ya 1960. Kwa kweli, vijana fulani, mbali na kutupiliwa mbali na wazazi wao, hawategemezwi kihisia-moyo.
Wanaloweza Kufanya Wazazi
Fungu la wazazi ni muhimu kadiri gani tuzingatiapo “utupu wa kiroho” ambao vijana hukabiliana nao? Wazazi wenye hekima hufahamu kwamba watoto wao wanahitaji vitumbuizo vinavyofaa pamoja na msaada wa kibinafsi wa kawaida. Huku wakichochewa na upendo, wazazi waweza kuzungumza nao kuhusu muziki, vipindi vya televisheni, vidio, riwaya, michezo ya kompyuta, na sinema wanazopenda. Vijana wengi hutamani sana kupata urafiki na mwongozo wenye upendo wa wazazi wao japo huenda wasiseme. Wanahitaji majibu yaliyo wazi kwa sababu wanaishi katika ulimwengu usioaminika kabisa. Watu wazima wapaswa kufahamu kwamba watoto wanakabili ulimwengu mgumu zaidi kuliko ule ambao wao walikabili walipokuwa vijana.
Wazazi wanaotaka kuwalinda watoto wao watawasiliana nao kwa ukawaida, watawasikiliza kwa makini, na kuwaonya kuhusu hatari za utamaduni wa kisasa. Wazazi wanapoweka mipaka imara na isiyobadilika-badilika na wanapokuwa tayari kusababu na kuwaonyesha urafiki watoto wao, kwa kawaida watafanikiwa.—Mathayo 5:37.
Wazazi ambao ni Mashahidi wa Yehova hujitahidi kuzungumza na watoto wao kwa ukawaida wakitumia Biblia na vichapo na vidio zinazotegemea Biblia.a Wao hawatumii pindi hizo kuwaadhibu watoto, bali kuzungumzia mambo yenye kujenga kiroho. Katika vikusanyiko hivyo vya familia, wao husikiliza matatizo au magumu yanayomkumba kila mtoto na hilo hutokeza fursa ya kumpa kila kijana msaada wa kibinafsi.
Vijana wasiopokea mwongozo wa kiroho kutoka kwa wazazi wao wanaweza kuimarishwa na Zaburi 27:10, inayosema hivi: ‘Baba yangu na mama yangu wakiniacha, BWANA atanikaribisha kwake.’ Yehova, Baba wa rehema nyororo, huwasaidiaje vijana? Makutaniko ya Mashahidi wa Yehova yamekuwa kimbilio ambamo wengi wamepata marafiki na wametatua matatizo yao. Josías, kijana aliyeona jambo hilo, asema: “Tengenezo la Yehova hutimiza fungu muhimu. Nilihisi kwamba maisha hayakuwa na maana. Niliishi bila kusudi, bila tumaini. Kujua tu kwamba sikuwa peke yangu kulibadili kabisa maisha yangu. Nilihisi kwamba ndugu katika kutaniko walichukua mahali pa familia yangu iliyopotea. Wazee na familia katika kutaniko ni kama nanga ya kihisia-moyo.”
Kwa kweli, vijana na watu wazima wengi wameboresha afya yao ya kiakili na ya kiroho kwa kuhudhuria mikutano ya kutaniko ya Mashahidi wa Yehova kwa kawaida. Mtaalamu wa Elimu ya Binadamu Patricia Fortuny alieleza kuhusu ushirika huo unaojenga katika insha yake iitwayo Los Testigos de Jehová: una alternativa religiosa para enfrentar el fin del milenio (Mashahidi wa Yehova: Njia Badala ya Kidini ya Kukabili Mwisho wa Milenia): “Mashahidi wa Yehova hueleza utaratibu ulio wazi kabisa wa kufuata katika maisha ya kila siku, sheria na kanuni barabara zinazoongoza mawazo na mwenendo.” “Utaratibu wa kufuata” na “kanuni” zinazotajwa hapa hutegemea Biblia. Kwa hiyo, ingawa Mashahidi wa Yehova hukumbwa na matatizo na mikazo ileile sawa na jirani zao, wanaimarishwa na hekima isiyo na kifani ya kitabu hicho cha kale. Naam, Mashahidi hupata kimbilio katika itikadi zilizo wazi na kanuni zilizo katika Biblia.
Wakati “Kifo Hakitakuwapo Tena”
Mafundisho yanayotolewa kwenye Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova hukazia tena na tena ahadi ya Mungu ya ulimwengu mpya utakaokuwapo karibuni, ambamo “uadilifu utakaa” na ambamo ‘hakuna mtu atakayewatia hofu.’ (2 Petro 3:13; Mika 4:4) Isitoshe, nabii Isaya aandika kwamba wakati huo Mungu ‘atameza mauti hata milele, na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote.’ Kifo kilikumba jamii ya kibinadamu kwa sababu ya ukiukaji-sheria wa mtu wa kwanza, Adamu, lakini Mungu aahidi kwamba karibuni “kifo hakitakuwapo tena.”—Isaya 25:8; Ufunuo 21:3, 4; Waroma 5:12.
Endapo wewe ni kijana anayetafuta msaada, twakualika upate tumaini na kusudi la uhai kwa kusoma Biblia. Mashahidi wa Yehova watakusaidia uwe na tumaini la kwamba kutakuwa na maisha bora kabisa hivi karibuni katika ulimwengu mpya unaoahidiwa na Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a Vidio Young People Ask—How Can I Make Real Friends? inatayarishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc. Kwa sasa iko kwa lugha ya Kiingereza nayo huandaa msaada wenye kutumika kwa vijana.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Wazazi wapaswa kuwasikiliza kwa makini watoto wao na kufahamu matatizo yao
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Mashahidi wa Yehova hueleza utaratibu ulio wazi kabisa wa kufuata katika maisha ya kila siku”
-