Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Danieli
    Mnara wa Mlinzi—2007 | Septemba 1
    • TUNAJIFUNZA NINI KUTOKANA NA MFUATANO WA MATUKIO?

      (Danieli 1:1–6:28)

      Ni mwaka wa 617 K.W.K. Danieli na marafiki wake watatu, Shadraki, Meshaki, na Abednego, wako katika makao ya mfalme wa Babiloni. Wakati wa miaka mitatu ya mazoezi katika makao ya mfalme, vijana hao wanadumisha utimilifu wao kwa Mungu. Miaka minane hivi baadaye, Mfalme Nebukadneza anaota ndoto ambayo inamfadhaisha. Danieli anafunua ndoto hiyo na kisha anatafsiri maana yake. Mfalme anakiri kwamba Yehova ni “Mungu wa miungu na Bwana wa wafalme na Mfunuaji wa siri.” (Danieli 2:47) Hata hivyo, punde si punde, inaonekana Nebukadneza anasahau somo hilo. Marafiki watatu wa Danieli wanapokataa kuabudu sanamu kubwa, mfalme anaamuru watupwe ndani ya tanuru ya moto. Mungu wa kweli anawaokoa wanaume hao watatu, na Nebukadneza analazimika kutambua kwamba “hakuna mungu mwingine yeyote anayeweza kuokoa kama huyu.”—Danieli 3:29.

      Nebukadneza anaota ndoto nyingine ya maana sana. Anaona mti mrefu sana, ambao unakatwa na kufungwa pingu ili usikue. Danieli anatafsiri maana ya ndoto hiyo. Ndoto hiyo inatimia kwa sehemu Nebukadneza anapopatwa na wazimu na kisha kupata nafuu. Miaka mingi baadaye, Mfalme Belshaza anafanya karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake na bila heshima anatumia vyombo ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka katika hekalu la Yehova. Usiku huohuo, Belshaza anauawa na Dario Mmedi anaupokea ufalme. (Danieli 5:30, 31) Katika siku za Dario, Danieli akiwa na umri wa miaka zaidi ya 90, wakuu wa serikali wenye wivu wanapanga njama ya kumuua nabii huyo aliyezeeka. Lakini Yehova anamwokoa “kutoka katika makucha ya simba.”—Danieli 6:27.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Danieli
    Mnara wa Mlinzi—2007 | Septemba 1
    • MAONO YA DANIELI YANAFUNUA NINI?

      (Danieli 7:1–12:13)

      Danieli anapopokea maono ya ndoto yake ya kwanza katika mwaka wa 553 K.W.K., ana umri wa zaidi ya miaka 70. Danieli anaona wanyama mwitu wanne wakubwa ambao wanawakilisha mfuatano wa serikali za ulimwengu kuanzia siku zake mpaka siku zetu. Katika maono ya mambo yanayotendeka mbinguni, anaona “mtu fulani kama mwana wa binadamu” akipewa “utawala unaodumu mpaka wakati usio na kipimo.” (Danieli 7:13, 14) Miaka miwili baadaye, Danieli anaona maono yanayohusu Umedi na Uajemi, Ugiriki, na kikundi ambacho kinakuwa “mfalme mwenye sura kali.”—Danieli 8:23.

      Sasa tuko katika mwaka wa 539 K.W.K. Jiji la Babiloni limeanguka, na Dario Mmedi amekuwa mtawala juu ya ufalme wa Wakaldayo. Danieli anasali kwa Yehova kuhusu kurudishwa kwa nchi yake. Huku akiwa bado anasali, Yehova anamtuma malaika Gabrieli ili kumfanya Danieli ‘apate ufahamu kwa kuelewa’ kuhusu kuja kwa Masihi. (Danieli 9:20-25) Wakati unasonga mpaka mwaka wa 536/535 K.W.K. Mabaki ya Waisraeli wamerudi Yerusalemu. Lakini kuna upinzani kuelekea kazi ya ujenzi wa hekalu. Jambo hilo linamsumbua sana Danieli. Anasali sana kulihusu, na Yehova anamtuma malaika wa cheo cha juu kwa Danieli. Baada ya kumwimarisha na kumtia moyo Danieli, malaika huyo anaeleza unabii unaoonyesha mapambano ya kupata mamlaka kubwa kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini. Mapambano kati ya wafalme hao wawili yanaanza wakati ufalme wa Aleksanda Mkuu unapogawanyika kati ya majemadari wake wanne mpaka wakati ambapo Mikaeli yule Mkuu “atasimama.”—Danieli 12:1.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki