-
Je, Misiba ya Asili Inaongezeka?Amkeni!—2005 | Julai 22
-
-
Je, Misiba ya Asili Inaongezeka?
“Inatazamiwa kwamba matukio yasiyo ya kawaida yanayosababishwa na kubadilika kwa hali ya hewa yatatokeza madhara makubwa zaidi wakati ujao. Kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari kukabiliana na hatari mpya zinazosababishwa na hali ya hewa na uwezekano wa kupata hasara kubwa zaidi. . . . Kupatana na kanuni ya kujikinga mapema, ni muhimu kujitayarisha mapema kwa ajili ya mabadiliko makubwa.”—“Topics Geo—annual Review: Natural Catastrophes 2003.”
KATIKA kiangazi cha 2003, sehemu fulani za Ulaya zilikumbwa na joto jingi sana. Joto hilo jingi lilisababisha vifo vya watu wapatao 30,000 huko Hispania, Italia, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ureno. Joto kali la kabla ya mvua za msimu huko Bangladesh, India, na Pakistan lilisababisha vifo 1,500, na ukame na joto jingi sana huko Australia zikasababisha mioto ya msituni ambayo iliteketeza zaidi ya ekari milioni saba.
Kulingana na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni, “msimu wa tufani wa Atlantiki wa 2003 ulitokeza dhoruba 16 zilizopewa majina. Idadi hiyo ilizidi wastani wa dhoruba 9.8 zilizotokea kila mwaka kuanzia 1944 hadi 1996, lakini zinapatana na ongezeko la kila mwaka linaloonekana wazi la dhoruba na tufani zinazotokea katika maeneo ya tropiki tangu miaka ya katikati ya 1990.” Ongezeko hilo liliendelea mnamo 2004, kulipotokea tufani zilizosababisha madhara makubwa huko Karibea na Ghuba ya Mexico, ambako watu 2,000 hivi walikufa na uharibifu mkubwa ukatokea.
Mnamo 2003, Sri Lanka ilikumbwa na kimbunga kilichosababisha mafuriko makubwa yaliyowaua watu 250 hivi. Mnamo 2004, angalau tufani 23 zilitokea magharibi mwa Pasifiki. Kumi kati yake zilikumba Japani, ambako zilisababisha madhara makubwa na vifo zaidi ya 170. Mafuriko yaliyosababishwa na mvua nyingi za msimu yaliathiri watu wapatao milioni 30 huko Asia Kusini, hasa Bangladesh. Mamilioni waliachwa bila makao, karibu watu milioni tatu wakalazimika kutoroka makwao na zaidi ya 1,300 wakafa.
Matetemeko makubwa kadhaa ya nchi yalitokea mwaka wa 2003. Katika Mei 21, tetemeko la nchi lilijeruhi watu 10,000 na kuacha 200,000 bila makao huko Algiers, Algeria. Desemba 26, saa 11:26 alfajiri, tetemeko kubwa la nchi lilitokea kilometa nane kusini ya jiji la Bam huko Iran. Tetemeko hilo la kipimo cha 6.5 liliharibu asilimia 70 ya jiji hilo, likaua watu 40,000, na kuacha watu zaidi ya 100,000 bila makao. Huo ndio msiba mbaya zaidi wa asili uliotukia mwaka huo. Pia liliharibu sehemu kubwa ya ngome ya Arg-e-Bam iliyokuwa imedumu kwa miaka 2,000, na kufanya jiji la Bam lipoteze pesa zinazoletwa na watalii ambao huja kuiona.
Mwaka mmoja kamili baadaye, tetemeko lenye kipimo cha 9.0 lilitokea karibu na pwani ya magharibi ya kaskazini mwa Sumatra, Indonesia, na kutokeza mojawapo ya tsunami mbaya zaidi katika historia. Mawimbi hayo yalisababisha vifo zaidi ya 200,000, yakajeruhi na kuacha watu wengi zaidi bila makao. Madhara ya tetemeko hilo yalifika pwani ya mashariki mwa Afrika, iliyoko umbali wa kilometa 4,500 au zaidi magharibi ya mahali tetemeko hilo lilipotokea.
Je, Tutazamie Misiba Mingi Zaidi?
Je, matukio hayo yanaonyesha mambo yatakayotukia wakati ujao? Kuhusiana na misiba inayotokana na hali ya hewa, wanasayansi wengi wanaamini kuwa mabadiliko ya hewa yanayosababishwa na wanadamu yanabadili hali ya hewa ulimwenguni na kufanya iwe mbaya zaidi. Ikiwa hilo ni kweli, hali itakuwa mbaya zaidi wakati ujao. Kuongezea hatari hiyo, watu wengi zaidi huishi katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na misiba kwa sababu ya hali au kwa kutaka.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya misiba yote inayosababisha vifo hutukia katika nchi zinazositawi. Kwa upande mwingine, watu wachache zaidi hufa katika nchi tajiri lakini hizo hupata asilimia 75 ya hasara ya kiuchumi. Mashirika fulani ya bima hujiuliza ikiwa yataweza kulipia hasara zinazozidi kuongezeka.
Katika makala inayofuata, tutachunguza baadhi ya mambo ya asili yanayosababisha misiba na njia ambazo huenda wanadamu wanachangia na kuifanya iwe mibaya zaidi. Tutachunguza pia iwapo mwanadamu ana uwezo na nia ya kufanya mabadiliko yanayohitajiwa ili dunia iwe salama zaidi kwa vizazi vijavyo.
[Picha katika ukurasa wa 3]
UFARANSA 2003, Joto jingi wakati wa kiangazi huko Ulaya lawaua watu 30,000; Hispania yafikisha nyuzi 44.8 Selsiasi
[Hisani]
Alfred/EPA/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
IRAN 2003, Tetemeko la nchi huko Bam lawaua watu 40,000; wanawake waombolezea jamaa zao katika kaburi la jumla
[Hisani]
Background and women: © Tim Dirven/Panos Pictures
-
-
Misiba ya Asili—Jinsi Wanadamu Wanavyochangia Kuongezeka KwakeAmkeni!—2005 | Julai 22
-
-
Misiba ya Asili—Jinsi Wanadamu Wanavyochangia Kuongezeka Kwake
GARI linapotunzwa vizuri, linaweza kusafirisha watu kwa usalama. Lakini gari hilo likitumiwa vibaya na kutotunzwa linaweza kuwa hatari. Kwa njia fulani, tunaweza kusema hivyo kuhusu dunia.
Wanasayansi kadhaa wanaona kwamba mabadiliko yanayosababishwa na wanadamu katika angahewa na bahari yamechangia kuongezeka kwa misiba ya asili iliyo mibaya zaidi na kufanya dunia iwe mahali hatari. Na huenda mambo yakawa mabaya wakati ujao. Tahariri katika gazeti Science ilisema hivi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa: “Hatujui mambo tunayofanya katika sayari pekee ambayo wanadamu wanaweza kuishi yatakuwa na matokeo gani.”
Ili tuelewe vizuri zaidi jinsi utendaji wa wanadamu unavyoweza kuchangia kuongezeka kwa misiba mibaya zaidi ya asili, tunahitaji kuelewa kidogo mambo ya asili ambayo hutokeza misiba hiyo. Kwa mfano, ni nini husababisha dhoruba kubwa kama vile tufani?
Vihamisha-Joto vya Asili
Mfumo wa hali ya hewa wa dunia umelinganishwa na mashini ambayo hubadili na kusambaza nguvu za jua. Kwa kuwa maeneo ya Tropiki hupata joto jingi la jua, halijoto inayotokea hufanya hewa isonge.a Mzunguko wa kawaida wa dunia hufanya hewa hiyo nyingi yenye unyevu inayosonga itokeze mikondo inayozunguka-zunguka, na baadhi yake huwa maeneo yenye shinikizo ndogo la hewa. Huenda maeneo hayo yakatokeza dhoruba.
Ukichunguza njia ya kawaida ya dhoruba za kitropiki, utaona kwamba hizo huelekea mbali na ikweta, iwe ni kaskazini au kusini, kuelekea maeneo baridi zaidi. Kwa kufanya hivyo, dhoruba pia huwa kama vihamisha-joto vikubwa ambavyo husaidia kusawazisha hali ya hewa. Lakini hali ya joto katika bahari za maeneo ya tropiki inapozidi nyuzi 27 Selsiasi hivi, dhoruba za kitropiki zinaweza kupata nguvu za kutosha na kuwa vimbunga na tufani.
Msiba mbaya zaidi wa asili nchini Marekani uliowaua watu wengi zaidi ni tufani iliyokumba jiji la kisiwani la Galveston, Texas, Septemba 8, 1900. Mawimbi ya dhoruba yaliua kati ya watu 6,000 na 8,000 katika jiji hilo, kuongezea watu 4,000 hivi katika maeneo ya karibu na kuharibu nyumba 3,600 hivi. Kwa kweli, hakuna hata jengo moja huko Galveston ambalo halikuathiriwa.
Kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, kumekuwa na dhoruba nyingi kubwa katika miaka ya karibuni. Wanasayansi wanachunguza ikiwa dhoruba hizo zinahusiana na ongezeko la joto duniani, ambalo huenda likawa linafanya dhoruba ziwe na nguvu nyingi zaidi. Hata hivyo, huenda mabadiliko ya hali ya hewa yakawa dalili moja tu ya kuongezeka kwa joto duniani. Huenda matokeo mengine yenye kudhuru yakawa yanaonekana.
Kuongezeka kwa Maji Baharini na Ukataji-Miti
Kulingana na tahariri katika jarida Science, “maji baharini yamepanda kwa sentimeta 10 hadi 20 [inchi nne hadi nane] katika karne iliyopita, na huenda yakapanda zaidi.” Jambo hilo linaweza kuhusianaje na kuongezeka kwa joto duniani? Watafiti wanasema huenda kukawa na njia mbili. Njia moja ni uwezekano wa barafu kuyeyuka na kuongeza maji baharini. Njia nyingine ni kuongezeka kwa joto baharini ambalo hufanya maji yaongezeke.
Huenda tayari visiwa vidogo vya Tuvalu katika Bahari ya Pasifiki vinapatwa na athari za kupanda kwa maji baharini. Gazeti Smithsonian linasema kuwa vipimo vilivyokusanywa kwenye kisiwa cha matumbawe cha Funafuti vinaonyesha kwamba maji baharini yamepanda “kwa wastani wa milimeta 5.6 kila mwaka katika miaka kumi iliyopita.”
Katika sehemu nyingi za ulimwengu, kuongezeka kwa idadi ya watu kumefanya miji ipanuliwe, mitaa ya mabanda iongezeke, na kuharibiwa kwa mazingira. Huenda mambo hayo yakafanya misiba ya asili iwe mibaya zaidi. Fikiria mifano kadhaa.
Haiti, ni kisiwa chenye watu wengi na misitu yake imekatwa kwa muda mrefu. Ripoti moja ya habari ya karibuni ilisema kwamba hata ingawa matatizo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii nchini Haiti ni mabaya, ukataji-miti ndio unaohatarisha maisha ya watu zaidi nchini humo. Hatari hiyo ilionekana wazi mnamo 2004, mvua za mafuriko ziliposababisha maporomoko ya matope na kuua maelfu ya watu.
Gazeti Time la Asia linataja “ongezeko la joto duniani, mabwawa, ukataji-miti na kilimo cha kufyeka na kuchoma miti na mimea” kuwa sababu zinazozidisha misiba ya asili ambayo imekumba Asia Kusini. Pia ukataji-miti unaweza kufanya ukame uwe mbaya zaidi kwa kufanya udongo ukauke haraka zaidi. Katika miaka ya karibuni, ukame nchini Indonesia na Brazili umetokeza mioto mikubwa katika misitu yenye miti mibichi ambayo kwa kawaida ni vigumu kuteketea. Hata hivyo, si hali mbaya tu ya hewa ambayo husababisha misiba ya asili. Nchi nyingi hupatwa na misiba inayotokea kwa sababu ya utendaji ulio chini ya ardhi.
Ardhi Inapotikisika Sana
Tabaka la juu la dunia limefanyizwa na miamba yenye ukubwa mbalimbali ambayo husonga kwa upatano. Kwa kweli, miamba hiyo husonga sana hivi kwamba matetemeko mengi ya nchi hutokea kila mwaka. Bila shaka, mengi kati yao hayagunduliwi.
Inasemekana kwamba karibu asilimia 90 ya matetemeko yote ya nchi hutukia kwenye nyufa zilizo kwenye kingo za miamba hiyo. Matetemeko hutukia pia katikati ya miamba hiyo, ingawa hilo hutukia mara chache na husababisha uharibifu mkubwa nyakati nyingine. Kulingana na makadirio, tetemeko baya zaidi katika historia ni lile lililokumba majimbo matatu nchini China mnamo 1556. Huenda liliua watu wapatao 830,000!
Pia matetemeko yanaweza kutokeza madhara baadaye. Kwa mfano, katika Novemba 1, 1775, tetemeko lilibomoa jiji la Lisbon, huko Ureno, lililokuwa na watu 275,000. Lakini kulikuwa na madhara mengine. Tetemeko hilo lilitokeza mioto na pia tsunami zilizokadiriwa kuwa na kimo cha meta 15, ambazo zilipiga nchi kavu kwa kasi kutoka Bahari ya Atlantiki iliyoko karibu. Kwa ujumla, watu zaidi ya 60,000 walikufa.
Hata hivyo, wanadamu pia walichangia kwa kiasi fulani madhara yaliyosababishwa na msiba huo. Kisababishi kimoja ni idadi kubwa ya watu wanaoishi katika maeneo hatari. Mwandishi Andrew Robinson anasema: “Karibu nusu ya majiji makubwa ulimwenguni yako katika sehemu ambazo matetemeko yanaweza kutokea.” Kisababishi kingine ni majengo, yaani, vifaa vya ujenzi vilivyotumiwa na ubora wa jengo. Msemo, “Matetemeko ya nchi hayaui watu; watu huuawa na majengo,” umethibitika kuwa kweli mara nyingi. Lakini watu wanaweza kufanya nini ikiwa wao ni maskini sana wasiweze kujenga nyumba zinazoweza kuhimili matetemeko ya nchi?
Volkano Hujenga na Kubomoa
Ripoti moja ya Taasisi ya Smithsonian ya Marekani inasema kwamba “huenda angalau volkano 20 zinalipuka unaposoma maneno haya.” Kwa ujumla, nadharia ya miamba ya dunia huonyesha kwamba matetemeko ya nchi na volkano hutokea sehemu zilezile, yaani kwenye nyufa, hasa nyufa zilizo kwenye sakafu ya bahari; katika tabaka la juu la dunia, ambako miamba iliyoyeyuka hutokea kwenye mianya iliyo katika tabaka la katikati la dunia; na mahali ambapo miamba hukutana kisha mmoja kwenda chini ya mwingine.
Volkano zinazotokea mahali ambapo miamba miwili hukutana ndiyo hatari zaidi kwa wanadamu kwa sababu hizo hulipuka mara nyingi na hutokea mahali penye watu wengi. Ukingo wa Pasifiki unaoitwa Eneo la Pasifiki Lenye Volkano una volkano nyingi kama hizo. Volkano chache pia hutokea katika tabaka la katikati la dunia ambapo miamba huyeyuka mbali na mipaka ya miamba. Yaonekana visiwa vya Hawaii, Azores, Galápagos, na Society vilitokana na utendaji wa aina hiyo wa volkano.
Kwa kweli, kwa muda mrefu, volkano zimechangia ujenzi wa dunia. Kulingana na kituo cha Intaneti cha chuo kikuu kimoja, karibu “asilimia 90 ya mabara na mabonde kwenye sakafu za bahari zimetokana na utendaji wa volkano.” Lakini ni nini hufanya milipuko fulani iwe hatari sana?
Milipuko huanza miamba iliyoyeyuka inapotokea kwenye sehemu za chini ya ardhi zenye moto. Volkano fulani hutoa lava inayotiririka polepole hivi kwamba ni mara chache sana huwapata watu ghafula. Lakini nyingine hulipuka kwa nguvu kuliko bomu la nyuklia! Milipuko hutegemea jinsi miamba iliyoyeyuka ilivyo na kiasi cha gesi na maji moto katika mchanganyiko huo. Myeyuko huo unapokaribia kutokea juu ya ardhi, maji na gesi huongezeka upesi. Vitu hivyo vinapochanganyika kikamili, hulipuka kama soda kutoka kwenye chupa.
Kwa kupendeza, mara nyingi volkano hutoa dalili mapema kabla ya kulipuka. Ndivyo Mlima Pelée, kwenye kisiwa cha Karibea cha Martinique, ulivyofanya mwaka wa 1902. Hata hivyo, uchaguzi ulikuwa ukikaribia katika jiji la St. Pierre lililokuwa karibu na mlima huo, nao wanasiasa waliwatia watu moyo wasihame licha ya majivu, ugonjwa na woga uliotanda jijini humo. Hata maduka mengi yalikuwa yamefungwa kwa siku nyingi!
Mei 8 ilikuwa siku ya kusherehekea kupaa kwa Yesu Kristo mbinguni, na watu wengi walienda kwenye kanisa Katoliki ili kuomba wakombolewe kutokana na volkano hiyo. Asubuhi hiyo, dakika chache kabla ya saa mbili, Mlima Pelée ulilipuka na kutupa angani majivu, vipande vya lava na glasi, mawe mepesi ya volkano, na gesi moto sana iliyokuwa na joto la kati ya nyuzi 200 hadi 500 Selsiasi. Mchanganyiko huo hatari ulipotiririka chini ulifunika jiji hilo na kuwaua watu karibu 30,000, ukayeyusha kengele ya kanisa na kuteketeza meli zilizokuwa bandarini. Mlipuko huo ndio uliokuwa mbaya zaidi katika karne ya 20. Lakini haungekuwa mbaya hivyo ikiwa watu wangetii maonyo.
Je, Misiba ya Asili Itaongezeka?
Katika ripoti yao ya World Disasters Report 2004, Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu, linasema kwamba katika miaka kumi iliyopita, misiba inayosababishwa na vitu vya asili na hali ya hewa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60. Ripoti hiyo iliyochapishwa kabla ya msiba wa tsunami uliotokea Desemba 26 katika Bahari ya Hindi, inasema: “Hilo linaonyesha jinsi mambo yatakavyokuwa kwa muda mrefu.” Bila shaka, idadi ya watu katika maeneo hatari ikiendelea kuongezeka na misitu iendelee kukatwa, hakuna matumaini.
Isitoshe, nchi nyingi zilizoendelea kiviwanda zinazidi kutokeza gesi zinazoongeza joto katika angahewa la dunia. Kulingana na tahariri katika jarida Science, kusitasita kupunguza gesi zinazochafua hewa “ni sawa na kutotibu ambukizo linapoanza: Kufanya hivyo kutatokeza gharama kubwa baadaye.” Ikitaja gharama hizo, ripoti moja ya Kanada ya kupunguza misiba ilisema: “Mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kusemwa kuwa suala kubwa zaidi la kimazingira ambalo limewahi kushughulikiwa na jumuiya ya kimataifa.”
Hata hivyo, sasa hivi jumuiya ya kimataifa haiwezi kukubaliana kuwa utendaji wa wanadamu unachangia kuongezeka kwa joto duniani, na hata haiwezi kukubaliana na jinsi ya kusuluhisha jambo hilo. Hali hiyo inatukumbusha ukweli huu wa Biblia: “Mwanadamu . . . hana uwezo wa kuongoza hatua yake.” (Yeremia 10:23) Lakini kama tutakavyoona katika makala inayofuata, bado kuna tumaini. Kwa kweli, misiba ya sasa kutia ndani misukosuko katika jamii ya wanadamu, inakazia uhakika wa kwamba kitulizo kiko karibu.
[Maelezo ya Chini]
a Pia viwango tofauti-tofauti vya joto hufanyiza mikondo ya bahari na kuhamisha nishati hadi maeneo baridi zaidi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
VOLKANO ILIPOKUA KWENYE SHAMBA LA MAHINDI
MNAMO 1943, mkulima wa mahindi huko Mexico aliona kitu tofauti na mahindi kikikua shambani mwake. Alipokuwa shambani aliona mianya au nyufa ardhini. Siku iliyofuata, nyufa hizo zilikuwa volkano ndogo. Juma lililofuata, volkano hiyo ilikua kufikia meta 150, na mwaka mmoja baadaye ikafikia kimo cha meta 360. Hatimaye, volkano hiyo iliyo meta 2,775 juu ya usawa wa bahari, ilifikia kimo chake cha meta 430. Volkano hiyo iliyoitwa Paricutín, iliacha kulipuka kwa ghafula mnamo 1952 na tangu hapo haijalipuka tena.
[Picha katika ukurasa wa]
U. S. Geological Survey/Photo by R. E. Wilcox
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
MUNGU ALIPOOKOA MATAIFA KUTOKANA NA MSIBA
NJAA ni mojawapo ya misiba ya asili. Mojawapo ya njaa zilizotukia zamani ni ile ya Misri wakati wa Yosefu, mwana wa Yakobo, au Israeli. Njaa hiyo ilidumu miaka saba na kuathiri Misri, Kanaani, na maeneo mengine. Lakini watu wengi sana hawakufa kutokana nayo kwa sababu Yehova aliitabiri miaka saba mapema. Pia alisema kungekuwa na chakula kingi huko Misri miaka saba ambayo ingetangulia. Chini ya usimamizi wa Yosefu aliyemwogopa Mungu, ambaye kwa mwongozo wa Mungu aliwekwa kuwa waziri mkuu na msimamizi wa chakula, Wamisri walihifadhi nafaka nyingi sana hivi kwamba “wakaacha kuihesabu.” Hivyo, Misri iliweza kuwalisha raia zake na pia “watu wa dunia yote,” kutia ndani familia ya Yosefu.—Mwanzo 41:49, 57; 47:11, 12.
[Picha katika ukurasa wa 7]
HAITI 2004, Wavulana wanabeba maji ya kunywa katika barabara zilizofurika. Kukatwa kwa miti mingi kumesababisha maporomoko makubwa ya matope
[Hisani]
Background: Sophia Pris/EPA/Sipa Press; inset: Carl Juste/Miami Herald/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 9]
Mataifa mengi yanazidi kutokeza gesi zinazoongeza joto katika angahewa la dunia
[Hisani]
© Mark Henley/Panos Pictures
-
-
Misiba Yote Itakoma Hivi KaribuniAmkeni!—2005 | Julai 22
-
-
Misiba Yote Itakoma Hivi Karibuni
“Watoto na wajukuu. Sikilizeni! . . . Muda si muda, mlima huu utawaka moto. Lakini kabla ya hilo kutukia, kutakuwa na mingurumo, kelele, na matetemeko. Moshi, miale na radi itatemwa, na hewa itatetema na kunguruma. Kimbia wakati uwezapo . . . Ukiupuuza, ukiona vitu na mali kuwa vyenye thamani zaidi kuliko uhai wako, mlima utakuadhibu kwa sababu ya kutojali na pupa. Usijishughulishe na nyumba yako, kimbia bila kusitasita.”
ONYO hilo lililonukuliwa katika kitabu Earth Shock, cha Andrew Robinson, lilikuwa limeandikwa kwenye jiwe la ukumbusho huko Portici, mji ulio chini ya Mlima Vesuvius huko Italia, baada ya volkano hiyo kulipuka mwaka wa 1631 W.K. Mlipuko huo uliua watu zaidi ya 4,000. Robinson anasema, “bila kutazamiwa, mlipuko huo wa mwaka wa 1631 ndio uliofanya Mlima Vesuvius ujulikane sana.” Jinsi gani? Kujengwa upya kwa Portici ndiko kulifanya majiji ya Herculaneum na Pompeii yavumbuliwe. Majiji hayo yaliharibiwa kabisa Mlima Vesuvius ulipolipuka mnamo 79 W.K.
Plini Mchanga, Mroma aliyeokoka msiba huo na ambaye baadaye akawa gavana, aliandika kuhusu matetemeko yasiyo ya kawaida ambayo yalitoa onyo. Yeye, mama yake, na wengine walitii onyo hilo na kuokoka.
Ishara ya Kuonya ya Wakati Wetu
Leo tunakaribia sana mwisho wa mifumo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa ya ulimwengu huu. Tunajuaje? Kwa sababu Yesu Kristo alitabiri mfululizo wa matukio ya ulimwengu ambayo yangekuwa ishara ya kwamba siku ya hukumu ya Mungu imekaribia. Kama volkano inayonguruma, kutoa moshi, na vipande vya lava, ishara hiyo yenye mambo mengi inatia ndani vita vikubwa, matetemeko ya nchi, njaa, na tauni, mambo hayo yote yameukumba ulimwengu kwa kiwango kisicho na kifani tangu 1914.—Mathayo 24:3-8; Luka 21:10, 11; Ufunuo 6:1-8.
Lakini ishara ya kuonya ya Yesu pia inatia ndani ujumbe wa tumaini. Alisema: “Hii habari njema ya ufalme itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa ili kuwa ushahidi kwa mataifa yote; na ndipo ule mwisho utakapokuja.” (Mathayo 24:14) Ona kwamba Yesu aliuita ujumbe wa Ufalme “habari njema.” Kwa kweli, ni habari njema kwa sababu Ufalme wa Mungu, ambao ni serikali ya kimbingu ambayo mfalme wake ni Kristo Yesu, itaondoa madhara yote ambayo wanadamu wamesababisha. Isitoshe, itakomesha misiba ya asili.—Luka 4:43; Ufunuo 21:3, 4.
Kwa kweli, Yesu alipokuwa mwanadamu duniani, alionyesha nguvu zake za kudhibiti hali ya hewa kwa kutuliza dhoruba iliyohatarisha uhai. Wanafunzi wake wenye woga walisema hivi kwa mshangao: “Kwa kweli huyu ni nani, kwa maana anaagiza hata pepo na maji, nazo zinamtii?” (Luka 8:22-25) Leo, Yesu si mwanadamu duni, bali ni kiumbe wa roho mwenye nguvu. Kwa hiyo, hatakuwa na tatizo lolote la kudhibiti nguvu za asili ili zisiwadhuru raia zake!—Zaburi 2:6-9; Ufunuo 11:15.
Huenda wengine wakaona kuwa jambo hilo ni ndoto tu. Lakini kumbuka kwamba tofauti na ahadi na utabiri wa wanadamu, unabii wa Biblia, kutia ndani unabii mbalimbali ambao tumeona ukitimizwa tangu 1914, umetimia kikamili. (Isaya 46:10; 55:10, 11) Naam, wakati ujao wenye amani duniani ni jambo hakika. Tunahakikishiwa wakati wetu ujao utakuwa hivyo iwapo tutatii Neno la Mungu na onyo lake lenye upendo kuhusu matukio yenye kutetemesha dunia yatakayotukia hivi karibuni.—Mathayo 24:42, 44; Yohana 17:3.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]
KUNA TUMAINI GANI KWA WAPENDWA WETU WALIOKUFA?
TUNAWEZA kulemewa na huzuni mpendwa wetu anapokufa. Biblia inatuambia kuwa Yesu alilia rafiki yake mpendwa Lazaro alipokufa. Hata hivyo, dakika chache baadaye Yesu alifanya muujiza wenye kushangaza, kwa kumfufua Lazaro! (Yohana 11:32-44) Kwa kufanya hivyo, aliwapa wanadamu wote msingi thabiti wa kuamini ahadi nzuri aliyokuwa ametoa mapema katika huduma yake aliposema: “Saa inakuja ambayo wale wote waliomo ndani ya makaburi ya ukumbusho wataisikia sauti [ya Yesu] na kutoka.” (Yohana 5:28, 29) Tumaini zuri la kufufuliwa na kuishi kwenye dunia paradiso na liwafariji wote ambao wamefiwa na wapendwa wao.—Matendo 24:15.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Je, unatambua onyo la kwamba hizi ndizo siku za mwisho za ulimwengu huu?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
USGS, David A. Johnston, Cascades Volcano Observatory
-