Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Elekeza Moyo Wako Kwenye Ufahamu
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Machi 15
    • Elekeza Moyo Wako Kwenye Ufahamu

      “BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa [“ujuzi,” “NW”] na ufahamu.”—MITHALI 2:6.

      1. Twaweza kuelekezaje moyo wetu kwenye ufahamu?

      YEHOVA ndiye Mfunzi wetu Mtukufu. (Isaya 30:20, 21) Lakini ni lazima tufanye nini ili tunufaike kutokana na “ujuzi wenyewe juu ya Mungu” (NW) uliofunuliwa katika Neno lake? Kwa sehemu, ni lazima ‘tuelekeze moyo wetu kwenye ufahamu’—tuwe na tamaa ya kuhisiwa moyoni ya kujipatia na kuonyesha sifa hiyo. Ili hilo liwezekane, ni lazima tumtegemee Mungu, kwani yule mtu mwenye hekima alisema hivi: “BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa [“ujuzi,” NW] na ufahamu.” (Mithali 2:1-6) Ujuzi, hekima, na ufahamu ni nini?

      2. (a) Ujuzi ni nini? (b) Ungefafanuaje hekima? (c) Ufahamu ni nini?

      2 Ujuzi ni kujua sana mambo ya hakika kunakopatikana kupitia uzoefu, kujionea mambo, au kujifunza. Hekima ni uwezo wa kutumia ujuzi. (Mathayo 11:19) Mfalme Solomoni alionyesha hekima wanawake wawili walipomtaka mtoto yuleyule na alitumia ujuzi wake juu ya ujitoaji wa mama kwa mzao wake ili kusuluhisha kushindana huko. (1 Wafalme 3:16-28) Ufahamu ni “ustadi wa kuamua mambo.” Ni “nguvu au uwezo wa akili ambao kwao hiyo [akili] hutofautisha kati ya jambo moja na jingine.” (Webster’s Universal Dictionary) Tukielekeza moyo wetu kwenye ufahamu, Yehova atatupatia sifa hiyo kupitia Mwana wake. (2 Timotheo 2:1, 7) Lakini ufahamu waweza kuathirije sehemu mbalimbali za maisha?

      Ufahamu na Usemi Wetu

      3. Ungeelezaje Mithali 11:12, 13 na maana ya ‘kupungukiwa na moyo’?

      3 Ufahamu hutusaidia kung’amua kwamba kuna “wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena.” (Mhubiri 3:7) Sifa hiyo hutusaidia pia kuwa waangalifu juu ya yale tunayosema. Mithali 11:12, 13 yataarifu hivi: “Asiye na akili [“yule aliyepungukiwa na moyo,” NW] humdharau mwenziwe; bali mtu aliye na ufahamu [“ufahamu mpana,” NW] hunyamaza. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.” Ndiyo, mwanamume au mwanamke anayemdharau mtu mwingine ni mtu “aliyepungukiwa na moyo.” Kulingana na mtunga-kamusi Wilhelm Gesenius, mtu wa aina hiyo “anakosa uelewevu.” Anakosa hali ya kuamua vizuri, na utumizi wa neno “moyo” waonyesha kwamba sifa chanya za mtu wa ndani zinakosekana. Mtu anayedai kuwa Mkristo akiendeleza porojo zake kufikia hatua ya uchongezi au kutukana, wazee waliowekwa rasmi lazima wachukue hatua ili wakomeshe hali hiyo isiyo yenye kujenga kutanikoni.—Mambo ya Walawi 19:16; Zaburi 101:5; 1 Wakorintho 5:11.

      4. Wakristo wenye ufahamu na waaminifu hufanya nini juu ya habari ya siri?

      4 Tofauti na wale ‘waliopungukiwa na moyo,’ watu mmoja-mmoja wenye “ufahamu mpana” hunyamaza inapofaa kufanya hivyo. Hawafunui siri. (Mithali 20:19) Wakijua kwamba usemi usioangaliwa waweza kusababisha madhara, wale wenye ufahamu ni ‘wenye roho ya uaminifu.’ Wao ni waaminifu kwa waamini wenzao na hawafunui mambo ya siri yawezayo kuwahatarisha waamini hao. Wakristo wenye ufahamu wakipokea habari za siri za aina yoyote ile zinazohusu kutaniko, hawazifunui kwa yeyote hadi wakati tengenezo la Yehova lionapo kwamba yafaa kutoa habari hizo kwa njia yalo ifaayo ya uchapishaji.

      Ufahamu na Mwenendo Wetu

      5. ‘Wapumbavu’ huonaje mwenendo mlegevu, na kwa nini?

      5 Mithali za Biblia hutusaidia kutumia ufahamu na kuepuka mwenendo usiofaa. Kwa kielelezo, Mithali 10:23 husema hivi: “Kwa mpumbavu kutenda maovu [“mwenendo mlegevu,” NW] ni kama mchezo; bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.” Wale waonao mwenendo mlegevu kuwa “kama mchezo” hawaoni ubaya wa mwendo wao nao hawamhesabu Mungu kuwa yule ambaye ni lazima wote wamtolee hesabu. (Waroma 14:12) ‘Wapumbavu’ hao wanapotoka katika kusababu kwao kufikia hatua ya kudhania kwamba Mungu haoni kosa lao. Kwa matendo yao, wao kwa kweli husema: “Hakuna Mungu.” (Zaburi 14:1-3; Isaya 29:15, 16) Kwa sababu ya kutoongozwa na kanuni za kimungu, wanakosa ufahamu na hawawezi kuamua mambo kwa usahihi.—Mithali 28:5.

      6. Kwa nini mwenendo mlegevu ni upumbavu, nasi tutauonaje ikiwa tuna ufahamu?

      6 “Mtu mwenye ufahamu” anang’amua kwamba mwenendo mlegevu si “mchezo.” Anajua kwamba huo haumpendezi Mungu na waweza kuharibu uhusiano wetu pamoja naye. Mwenendo huo ni wa kipumbavu kwa sababu unawanyang’anya watu hali ya kujistahi, huharibu ndoa, hudhuru akili na pia mwili, na huongoza kwenye ukosefu wa hali ya kiroho. Kwa hiyo acheni tuelekeze moyo wetu kwenye ufahamu na kuepuka mwenendo mlegevu au ukosefu wa adili wa aina yoyote ile.—Mithali 5:1-23.

      Ufahamu na Mtazamo Wetu

      7. Ni yapi baadhi ya matokeo ya kimwili ya hasira?

      7 Kuelekeza moyo wetu kwenye ufahamu hutusaidia pia kudhibiti mtazamo wetu. “Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi,” yasema Mithali 14:29, “bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.” Sababu moja inayomfanya mtu mwenye ufahamu ajitahidi kuepuka hasira isiyodhibitiwa ni kwamba hasira hutuathiri vibaya kimwili. Yaweza kuongeza msongo wa damu na kusababisha maradhi ya upumuaji. Madaktari wametaja hasira na ghadhabu kuwa hisia-moyo zinazozidisha au zinazosababisha maradhi kama vile ugonjwa wa pumu, magonjwa ya ngozi, matatizo ya umeng’enyaji, na vidonda vya tumboni.

      8. Kutokuwa na subira kwaweza kuongoza kwenye nini, lakini ufahamu waweza kutusaidiaje kwa habari hiyo?

      8 Sababu yetu ya kutumia ufahamu na kutokuwa ‘wepesi wa hasira’ haipaswi kuwa ili tu kuepuka kudhuru afya yetu. Kutokuwa wenye subira kwaweza kuongoza kwenye matendo ya kipumbavu ambayo tutajuta. Ufahamu hutufanya tufikirie matokeo ya usemi usiozuiwa au wa mwenendo wa kutokufikiri na hivyo hutuzuia ‘tusitukuze upumbavu’ kwa kufanya jambo lisilo lenye hekima. Ufahamu hutusaidia hasa kung’amua kwamba ghadhabu yaweza kuvuruga kufikiri kwetu, hivi kwamba hatuwezi kuamua mambo vizuri. Hilo lingedhoofisha uwezo wetu wa kufanya mapenzi ya kimungu na kuishi kulingana na kanuni za Mungu zenye uadilifu. Ndiyo, kujiruhusu kuwa na hasira isiyodhibitiwa kunadhuru kiroho. Kwa kweli, “hasira za ghafula” zinaainishwa miongoni mwa zile “kazi za mwili” zenye kuchukiza ambazo zingetuzuia tusiurithi Ufalme wa Mungu. (Wagalatia 5:19-21) Basi, tukiwa Wakristo wenye ufahamu, acheni tuwe ‘wepesi sana juu ya kusikia, wa polepole juu ya kusema, wa polepole juu ya hasira ya kisasi.’—Yakobo 1:19.

      9. Ufahamu na upendo wa kidugu zaweza kutusaidiaje kusuluhisha tofauti mbalimbali?

      9 Tukikasirika, ufahamu waweza kuonyesha kwamba twapaswa kunyamaza ili kuepuka pambano. Mithali 17:27 yasema hivi: “Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; na mwenye roho ya utulivu ana busara [“ufahamu,” NW].” Ufahamu na upendo wa kidugu zitatusaidia kuona uhitaji wa kudhibiti msukumo wa kusema upesi jambo lenye kudhuru. Ikiwa hasira tayari imetokea ghafula, upendo na unyenyekevu utatusukuma kuomba radhi na kusuluhisha mambo. Lakini tuseme mtu fulani ametuudhi. Basi acheni tuseme naye peke yake kwa njia ya upole na yenye unyenyekevu na kwa kusudi la kuendeleza amani hasa.—Mathayo 5:23, 24; 18:15-17.

      Ufahamu na Familia Yetu

      10. Hekima na ufahamu zina fungu jipi katika maisha ya familia?

      10 Washiriki wa familia wanahitaji kuonyesha hekima na ufahamu, kwa maana sifa hizo zitaijenga nyumba. Mithali 24:3, 4 yasema hivi: “Nyumba hujengwa kwa hekima, na kwa ufahamu huthibitika, na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.” Hekima na ufahamu ni kama matufali mazuri ya kutumiwa kwa ujenzi wa maisha ya familia yenye mafanikio. Ufahamu husaidia wazazi Wakristo wapate kujua hisia na mahangaiko ya watoto wao. Mtu mwenye ufahamu anaweza kuwasiliana, kusikiliza na kupata ufahamu wenye kina juu ya hisia na mawazo ya mwenzi wake wa ndoa.—Mithali 20:5.

      11. Mwanamke mwenye ufahamu aliyeolewa aweza ‘kuijengaje nyumba yake’?

      11 Hekima na ufahamu ni muhimu bila shaka ili kuwa na maisha ya familia yenye furaha. Mathalani, Mithali 14:1 yasema: “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake, bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.” Mwanamke aliyeolewa ambaye ni mwenye hekima na ufahamu anayejitiisha ifaavyo chini ya mumeye atafanya kazi kwa bidii kwa faida ya nyumba yake na hivyo atasaidia kuijenga familia yake. Jambo moja ‘litakaloijenga nyumba yake’ ni kwamba sikuzote yeye husema mema juu ya mumeye na hivyo huongeza staha ya wengine kwa mumeye. Na mke mwenye uwezo na ufahamu, anayemhofu Yehova kwa staha hujishindia sifa.—Mithali 12:4; 31:28, 30.

      Ufahamu na Mwendo Wetu Maishani

      12. Wale ‘waliopungukiwa na moyo’ huonaje upumbavu, na kwa nini?

      12 Ufahamu hutusaidia kudumisha mwendo ufaao katika mambo yetu yote. Hilo laonyeshwa kwenye Mithali 15:21, isemayo hivi: “Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili [“moyo,” NW]; bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake [“huenda mbele moja kwa moja,” NW].” Twapaswa kuielewaje mithali hiyo? Mwendo wa kipumbavu, au kiupuzi, ni kisababishi cha shangwe kwa wanaume, wanawake, na vijana wasio na akili. ‘Wanapungukiwa na moyo,’ wakikosa kichocheo kizuri, nao wanakosa hekima sana hivi kwamba wanashangilia katika upumbavu.

      13. Solomoni alifahamu nini juu ya kicheko na kuchezacheza?

      13 Mfalme Solomoni wa Israeli mwenye ufahamu alipata kujua kwamba kuchezacheza kuna maana ndogo sana. Alikiri hivi: “Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu [“kichaa,” NW]; na juu ya furaha, Yafaa nini?” (Mhubiri 2:1, 2) Akiwa mtu mwenye ufahamu, Solomoni alipata kuona kwamba ufurahifu na kicheko peke yazo si zenye kuridhisha, kwa maana hazitokezi furaha halisi na idumuyo. Huenda kicheko kikatusaidia kusahau matatizo yetu kwa muda fulani, lakini baadaye matatizo yetu yanaweza kutokea yakiwa makubwa hata zaidi. Solomoni aliweza kwa kufaa kuita kicheko “kichaa.” Kwa nini? Kwa sababu kicheko cha kipumbavu huzuia uwezo wa kuamua mambo vizuri. Chaweza kutufanya tupuuze mambo yaliyo mazito sana. Kule kushangilia kunakolingana na maneno na matendo ya mfanya vitimbi hakuwezi kurejezewa kuwa hali inayotokeza jambo lifaalo. Kufahamu umaana wa kule kujaribu kwa Solomoni kicheko na ufurahifu kwatusaidia kuepuka kuwa “wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu.”—2 Timotheo 3:1, 4.

      14. Mwenye ufahamu huendaje mbele “moja kwa moja”?

      14 Ni jinsi gani kwamba mtu mwenye ufahamu huenda mbele “moja kwa moja”? Ufahamu wa kiroho na kule kutumia kanuni za kimungu huongoza watu katika mwendo mnyoofu, wa moja kwa moja. Tafsiri ya Byington husema waziwazi hivi: “Upumbavu ni raha mustarehe kwa mtu asiye na ubongo, lakini mtu mwenye akili ataenda moja kwa moja.” “Mwenye ufahamu” hufanyia miguu yake mapito yaliyo manyoofu na aweza kutambua kati ya lililo sawa na lililo kosa kwa sababu ya kutumia Neno la Mungu maishani.—Waebrania 5:14; 12:12, 13.

      Mtegemee Yehova Sikuzote ili Kupata Ufahamu

      15. Twajifunza nini kutokana na Mithali 2:6-9?

      15 Ili kufuata mwendo mnyoofu maishani, sisi sote twahitaji kutambua hali yetu ya kutokukamilika na kumtegemea Yehova ili tupate ufahamu wa kiroho. Mithali 2:6-9 yasema hivi: “BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu; huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu; apate kuyalinda mapito ya hukumu na kuhifadhi njia ya watakatifu wake. Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, na adili, na kila njia njema.”—Linganisha Yakobo 4:6.

      16. Kwa nini hakuna hekima, ufahamu, wala shauri katika upinzani na Yehova?

      16 Huku tukitambua hali yetu ya kumtegemea Yehova, acheni tujaribu kwa unyenyekevu kufahamu mapenzi yake kwa kuchunguza Neno lake kwa kina. Yeye ana hekima kwa ukamili, na shauri lake lina manufaa sikuzote. (Isaya 40:13; Waroma 11:34) Kwa kweli, shauri lolote lile linalompinga halina thamani yoyote. Mithali 21:30 yataarifu hivi: “Hapana hekima, wala ufahamu, wala shauri, juu ya [“kwa ushindani na,” NW] BWANA.” (Linganisha Mithali 19:21.) Ni ufahamu wa kiroho pekee, unaositawishwa kwa kujifunza Neno la Mungu kwa msaada wa vichapo vinavyoandaliwa kupitia “mtumwa mwaminifu na mwenye busara,” utakaotusaidia kufuatia mwendo ufaao maishani. (Mathayo 24:45-47) Kwa hiyo acheni tuelekeze njia yetu ya maisha kwa kupatana na shauri la Yehova, tukijua ya kwamba hata huenda shauri la ushindani likaonekana kuwa lenye kuaminika jinsi gani, haliwezi kulinganishwa na Neno lake.

      17. Tokeo laweza kuwa nini ikiwa shauri lenye kosa latolewa?

      17 Wakristo wenye ufahamu watoao shauri wanang’amua kwamba hilo lapaswa kutegemea Neno la Mungu kwa uthabiti na kwamba kujifunza Biblia na kutafakari kunahitajiwa kabla ya kujibu swali. (Mithali 15:28) Maswali juu ya mambo mazito yakitolewa jibu lisilo sahihi, madhara makubwa yaweza kutokea. Kwa sababu hiyo, wazee Wakristo wahitaji ufahamu wa kiroho na wapaswa kusali ili wapate mwongozo wa Yehova wanapojitahidi kusaidia waamini wenzao kiroho.

      Zidi na Ufahamu wa Kiroho

      18. Tatizo likitokea kutanikoni, ufahamu waweza kutusaidiaje kudumisha usawaziko wetu wa kiroho?

      18 Ili kumpendeza Yehova, twahitaji “ufahamu katika mambo yote.” (2 Timotheo 2:7) Kujifunza Biblia kwa bidii na kutii uelekeo wa roho na tengenezo la Mungu kutatusaidia kufahamu jambo la kufanya tunapokabili hali ambazo zingeweza kutuongoza kwenye mwendo wenye kosa. Kwa kielelezo, tuseme jambo fulani kutanikoni halishughulikiwi kwa njia tuonayo lapasa kushughulikiwa. Ufahamu wa kiroho utatusaidia kuona kwamba hiyo si sababu ya kuacha kushirikiana na watu wa Yehova na kuacha kumtumikia Mungu. Fikiria pendeleo letu la kumtumikia Yehova, ule uhuru wa kiroho tunaofurahia, ile shangwe twaweza kupata kutokana na utumishi wetu tukiwa wapiga-mbiu wa Ufalme. Ufahamu wa kiroho hutuwezesha kuwa na maoni yafaayo na kung’amua kwamba tumejiweka wakfu kwa Mungu na twapaswa kuthamini sana uhusiano wetu pamoja naye, hata liwe ni jambo gani wengine wanafanya. Ikiwa hakuna jambo tuwezalo kufanya kitheokrasi ili kushughulikia tatizo fulani, twahitaji kumngojea Yehova kwa subira asuluhishe hali hiyo. Badala ya kuondoka au kujiruhusu tupatwe na hali ya kukata tamaa, acheni ‘tumngojee Mungu.’—Zaburi 42:5, 11.

      19. (a) Ni nini kilichokuwa kiini cha sala ya Paulo kwa ajili ya Wafilipi? (b) Ufahamu waweza kutusaidiaje tusipoelewa jambo kikamili?

      19 Ufahamu wa kiroho hutusaidia kubaki tukiwa waaminifu-washikamanifu kwa Mungu na kwa watu wake. Paulo aliwaambia Wakristo katika Filipi hivi: “Hili ndilo mimi huendelea kusali, kwamba upendo wenu upate kuzidi bado hata zaidi na zaidi pamoja na ujuzi sahihi na ufahamu kamili; kwamba mpate kuhakikisha mambo yaliyo ya maana zaidi, ili mpate kuwa bila dosari na kutowakwaza wengine hadi siku ya Kristo.” (Wafilipi 1:9, 10) Ili tusababu ifaavyo, twahitaji “ujuzi sahihi na ufahamu kamili.” Neno la Kigiriki ambalo lafasiriwa “ufahamu” hapa huonyesha “kuona kwepesi kiadili.” Tunapojifunza jambo fulani, twataka kuona uhusiano walo pamoja na Mungu na Kristo na kutafakari juu ya jinsi linavyotukuza utu na maandalizi ya Yehova. Hilo lakuza ufahamu wetu na uthamini wetu kwa yale ambayo Yehova Mungu na Yesu Kristo wametufanyia. Ikiwa hatuelewi jambo fulani kikamili, ufahamu utatusaidia kung’amua kwamba hatupaswi kuachia mbali imani yetu katika mambo yote ya maana ambayo tumejifunza juu ya Mungu, Kristo, na kusudi la kimungu.

      20. Twaweza kuzidije na ufahamu wa kiroho?

      20 Tutazidi na ufahamu wa kiroho ikiwa sikuzote twapatanisha mawazo na matendo yetu na Neno la Mungu. (2 Wakorintho 13:5) Kufanya hivyo kwa njia ya kujenga kwatusaidia kuwa wanyenyekevu, si wenye kushika sana maoni yetu wenyewe na si wenye kuchambua wengine. Ufahamu utatusaidia kunufaika kutokana na usahihisho na kuhakikisha mambo yaliyo ya maana zaidi. (Mithali 3:7) Basi, tukiwa na tamaa ya kumpendeza Yehova, acheni tujaribu kujazwa ujuzi sahihi wa Neno lake. Hilo litatuwezesha kufahamu kati ya lililo sawa na lililo kosa, kuamua lililo la maana kikweli, na kushikamana kwa uaminifu-mshikamanifu na uhusiano wetu wenye thamani pamoja na Yehova. Hayo yote yawezekana tukielekeza moyo wetu kwenye ufahamu. Hata hivyo, jambo jingine lahitajiwa. Ni lazima turuhusu ufahamu utulinde salama.

  • Acha Ufahamu Ukulinde Salama
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Machi 15
    • Acha Ufahamu Ukulinde Salama

      “Busara itakulinda; ufahamu utakuhifadhi [“utakulinda salama,” “NW”].”—MITHALI 2:11.

      1. Ufahamu waweza kutulinda salama dhidi ya nini?

      YEHOVA ataka udhihirishe ufahamu. Kwa nini? Kwa sababu ajua kwamba sifa hiyo itakulinda salama dhidi ya hatari mbalimbali. Mithali 2:10-19 yaanza kwa kusema: “Hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yatakupendeza nafsi yako; busara itakulinda; ufahamu utakuhifadhi.” Utakulinda salama dhidi ya nini? Dhidi ya mambo kama ile “njia ya uovu,” wale wanaoacha mapito manyoofu, na watu wenye vipengee katika mwendo wao wa kawaida.

      2. Ufahamu ni nini, na Wakristo watamani upi hasa?

      2 Yamkini utakumbuka kwamba ufahamu ni uwezo wa akili ambao kwao hiyo akili yaweza kutofautisha kati ya jambo moja na jingine. Mtu mwenye ufahamu huona tofauti kati ya mawazo au mambo mbalimbali na aweza kuamua mambo vizuri. Tukiwa Wakristo, twatamani kuwa na ufahamu wa kiroho hasa unaotegemea ujuzi sahihi wa Neno la Mungu. Tunapojifunza Maandiko, ni kana kwamba twachimbua matufali ya kujengea ufahamu wa kiroho. Yale tunayojifunza yaweza kutusaidia kufanya maamuzi yanayompendeza Yehova.

      3. Twaweza kujipatiaje ufahamu wa kiroho?

      3 Mungu alipomwuliza Mfalme Solomoni wa Israeli ni baraka gani aliyotaka, yule mtawala mchanga alisema: “Nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua [“kufahamu kati ya,” NW] mema na mabaya.” Solomoni aliomba apewe ufahamu, naye Yehova akampa sifa hiyo kwa kadiri isiyo ya kawaida. (1 Wafalme 3:9; 4:30) Ili kujipatia ufahamu, twahitaji kusali, na ni lazima tujifunze Neno la Mungu kwa msaada wa vichapo vyenye kuelimisha vinavyoandaliwa kupitia “mtumwa mwaminifu na mwenye busara.” (Mathayo 24:45-47) Hilo litatusaidia kukuza ufahamu wa kiroho kwa kadiri ya kwamba tutakuwa “watu wazima katika nguvu za kuelewa,” wawezao “kupambanua [au, kufahamu kati ya] mema na mabaya.”—1 Wakorintho 14:20; Waebrania 5:14.

      Uhitaji wa Pekee wa Kupata Ufahamu

      4. Kuwa mwenye jicho “sahili” kwamaanisha nini, nalo laweza kutunufaishaje?

      4 Tukiwa na ufahamu ufaao, twaweza kutenda kwa kupatana na maneno haya ya Yesu Kristo: “Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme na uadilifu [wa Mungu], na vitu vingine vyote hivi [vya kimwili] mtaongezewa.” (Mathayo 6:33) Yesu alisema hivi pia: “Taa ya mwili ni jicho lako. Wakati jicho lako ni sahili, mwili wako wote ni mwangavu pia.” (Luka 11:34) Jicho ni taa ya kitamathali. Jicho lililo “sahili,” ni lenye unyoofu, lenye kuelekezwa upande mmoja tu. Tukiwa na jicho kama hilo, twaweza kuonyesha ufahamu na kutembea bila kujikwaa kiroho.

      5. Kwa habari ya shughuli za kibiashara, twapaswa kukumbuka nini juu ya kusudi la kutaniko la Kikristo?

      5 Badala ya kuweka jicho lao sahili, watu fulani wamevuruga maisha zao na maisha za wengine kwa shughuli za kibiashara zenye kushawishi. Lakini twapaswa kukumbuka kwamba kutaniko la Kikristo ni “nguzo na tegemezo la ile kweli.” (1 Timotheo 3:15) Sawa na nguzo za jengo, kutaniko hutegemeza kweli ya Mungu, halitegemezi shughuli za kibiashara za mtu yeyote yule. Makutaniko ya Mashahidi wa Yehova hayakuanzishwa ili yawe mahali mbalimbali pa kuendelezea masilahi, bidhaa, au huduma za kibiashara. Twapaswa kuepuka kufuatia mambo ya biashara ya kibinafsi katika Jumba la Ufalme. Ufahamu watusaidia kuona kwamba Majumba ya Ufalme, Mafunzo ya Kitabu ya Kutaniko, makusanyiko, na mikusanyiko ya Mashahidi wa Yehova ni mahali mbalimbali pa ushirika wa Kikristo na pa mazungumzo ya kiroho. Ikiwa tungetumia mahusiano ya kiroho ili kuendeleza namna yoyote ya ubiashara, je, hilo lisingeonyesha angalau ukosefu fulani wa uthamini kuelekea mambo ya kiroho? Mahusiano ya kikutaniko hayapasi kutumiwa kamwe ili kupata faida ya kifedha.

      6. Kwa nini bidhaa na huduma za kibiashara hazipasi kuuzwa au kuendelezwa kwenye mikutano ya kutaniko?

      6 Watu fulani wametumia mahusiano ya kitheokrasi ili kuuza dawa au vipodozi, bidhaa za vitamini, huduma za uwasiliano wa simu, vifaa vya ujenzi, mipango ya kusafiri, programu na vifaa vya kompyuta, na kadhalika. Hata hivyo, mikutano ya kutaniko si mahali pa kuuzia au pa kuendelezea bidhaa au huduma za kibiashara. Twaweza kufahamu kanuni ya msingi tukikumbuka kwamba Yesu “aliondosha nje ya hekalu wale wote wenye kondoo na ng’ombe, naye akamwaga sarafu za wabadili-fedha na kupindua meza zao. Naye akawaambia wale wenye kuuza njiwa: ‘Ondoleeni mbali vitu hivi kutoka hapa! Komeni kufanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya bidhaa za biashara!’”—Yohana 2:15, 16.

      Namna Gani Kuweka Fedha Katika Biashara ili Kupata Faida?

      7. Kwa nini ufahamu na hadhara zahitajiwa kuhusiana na habari ya mipango ya kuweka fedha katika biashara ili kupata faida?

      7 Ufahamu na hadhari zinahitajiwa wakati mtu anapofikiria kuweka fedha katika biashara ya kujasiria ili kupata faida. Tuseme mtu ataka kukopa fedha na atoa ahadi za namna hii: “Nakuhakikishia kwamba utapata faida.” “Huwezi kukosa faida. Hili ni jambo hakika.” Jihadhari mtu atoapo mahakikishio kama hayo. Ama haoni mambo kihalisi ama yeye si mwenye kufuatia haki, kwa kuwa ni nadra kwamba kuweka fedha katika biashara kunakuwa jambo hakika. Kwa kweli, watu fulani wasio wanyoofu, wenye kusema kwa kurairai wamepunja washiriki wa kutaniko. Hilo latukumbusha wale “watu wasiomwogopa Mungu” waliopenyeza katika kutaniko la karne ya kwanza, ‘wakageuza fadhili isiyostahiliwa ya Mungu kuwa sababu ya kujitetea kwa ajili ya mwenendo mlegevu.’ Walikuwa kama miamba yenye ncha kali iliyofichwa chini ya maji ambayo ingeweza kurarua na kuua waogeleaji. (Yuda 4, 12) Ni kweli, makusudio ya wapunjaji ni tofauti, lakini wao pia huwinda washiriki wa kutaniko.

      8. Ni jambo gani limetendeka kwa kuhusiana na biashara za kujasiria zionekanazo kuwa zenye kuleta faida?

      8 Hata Wakristo wenye nia njema wameshiriki pamoja na Wakristo wengine habari juu ya biashara za kujasiria zionekanazo kuwa zenye kuleta faida, lakini wamepata kugundua tu kwamba wao pamoja na wale wanaofuata kielelezo chao wamepoteza fedha walizoweka katika biashara hizo. Tokeo ni kwamba, Wakristo kadhaa wamepoteza mapendeleo kutanikoni. Biashara za kujasiria za kutajirika-haraka zinapothibitika kuwa miradi ya upunjaji, mtu pekee apataye faida ni yule mpunjaji, ambaye mara nyingi hutoweka upesi. Ufahamu waweza kumsaidiaje mtu kuepuka hali kama hizo?

      9. Kwa nini ufahamu wahitajiwa ili kuchanganua madai juu ya mipango ya kuweka fedha katika biashara ili kupata faida?

      9 Ufahamu humaanisha kuweza kuelewa kile kilichofichika. Uwezo huo wahitajiwa ili kuchanganua madai juu ya mipango ya kuweka fedha katika biashara ili kupata faida. Wakristo huwa na itibari kati yao, na huenda baadhi yao wakasababu kwamba ndugu na dada zao wa kiroho wasingejihusisha katika biashara za kujasiria ambazo zingehatarisha mali za waamini wenzao. Lakini uhakika wa kwamba mfanyabiashara ni Mkristo hautoi uhakikisho kwamba yeye atafaulu kupita wengine katika mambo ya biashara au kwamba shughuli yake ya biashara itafanikiwa.

      10. Kwa nini Wakristo fulani hujaribu kupata mikopo ya biashara kutoka kwa waamini wenzao, na tokeo la mipango hiyo ya kuweka fedha katika biashara ili kupata faida lingeweza kuwa nini?

      10 Wakristo fulani hujaribu kupata mikopo ya biashara kutoka kwa waamini wenzao kwa sababu mashirika makubwa ya kutoa mikopo yasingetolea mikopo biashara zao zenye kujasiria. Wengi wamepumbazwa kuamini kwamba kwa kuweka tu fedha zao katika biashara, wangeweza kuwa na mafanikio ya haraka, bila kufanya kazi nyingi au labda bila kufanya kazi yoyote kabisa. Watu fulani wanavutiwa kuweka fedha katika biashara kwa sababu ya msisimko unaohusianishwa na kufanya hivyo, lakini wanapata tu kupoteza akiba zao za fedha zilizokusanywa kwa muda mrefu! Mkristo mmoja aliweka kiasi kikubwa cha fedha katika biashara, akitarajia kupata faida ya kiwango cha asilimia 25 baada ya majuma mawili tu. Alipoteza fedha hizo zote wakati kampuni hiyo ilipotangazwa kuwa imefilisika! Katika biashara nyingine ya kujasiria, msitawishaji wa mashamba na majengo alikopa fedha nyingi kutoka kwa wengine kutanikoni. Aliahidi kuwapa wakopeshaji hao faida kubwa kupita kiasi lakini alifilisika, akapoteza fedha alizokopa.

      Wakati Ambapo Biashara za Kujasiria Hazifaulu

      11. Paulo alitoa shauri gani kwa habari ya pupa na upendo wa fedha?

      11 Kutokufaulu kwa biashara kumeongoza kwenye hali ya kukata tamaa na hata kwenye kupoteza hali ya kiroho kwa upande wa Wakristo fulani waliojihusisha katika biashara za kujasiria zisizo thabiti. Tokeo la kutoruhusu ufahamu uwalinde salama limekuwa maumivu ya moyoni na uchungu. Pupa imenasa watu wengi. ‘Pupa hata isitajwe miongoni mwenu, kama vile ifaavyo watu watakatifu,’ akaandika Paulo. (Waefeso 5:3) Na alionya hivi: “Wale waazimiao kuwa matajiri huanguka ndani ya kishawishi na mtego na tamaa nyingi zisizo za akili na zenye kuumiza, ambazo hutumbukiza watu ndani ya uharibifu na uangamizo. Kwa maana kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote, na kwa kujitahidi kufikilia kupenda huku wengine wameongozwa wapotee njia kutoka kwenye imani na wamejichoma wenyewe kotekote kwa maumivu mengi.”—1 Timotheo 6:9, 10.

      12. Wakristo wakifanya biashara kati yao, wao wapaswa kukumbuka nini hasa?

      12 Ikiwa Mkristo angekuza upendo wa fedha, yeye angejisababishia madhara mengi ya kiroho. Mafarisayo walikuwa wapenda-fedha, na hicho ni kitabia cha watu wengi katika siku hizi za mwisho. (Luka 16:14; 2 Timotheo 3:1, 2) Kinyume cha hilo, njia ya maisha ya Mkristo yapaswa kuwa “bila upendo wa fedha.” (Waebrania 13:5) Bila shaka, Wakristo waweza kufanya biashara kati yao au kuanzisha biashara pamoja. Hata hivyo, wakifanya hivyo mazungumzo na mapatano yapasa kutenganishwa na mambo ya kikutaniko. Na mkumbuke: Hata miongoni mwa ndugu za kiroho, andikeni mapatano ya kibiashara sikuzote. Yenye kusaidia kwa habari hii ni makala “Andikeni!,” iliyochapishwa katika Amkeni! la Agosti 8, 1984, kurasa 14 hadi 16.

      13. Ungetumiaje Mithali 22:7 kwa habari ya biashara za kujasiria?

      13 Mithali 22:7 yatuambia: “Akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” Mara nyingi ni jambo lisilo la hekima kwetu kujiweka wenyewe au kuweka ndugu yetu katika hali hiyo ya kuwa mtumwa. Yeyote atuombapo tumkopeshe fedha kwa ajili ya biashara ya kujasiria, ingefaa kufikiria uwezo wake wa kurudisha fedha hizo. Je, yeye ajulikana kuwa mwenye kutegemeka na kutumainiwa? Bila shaka, twapaswa kutambua kwamba kutoa mkopo huo kungeweza kumaanisha kupoteza fedha kwa sababu biashara nyingi za kujasiria hazifaulu. Kuwa na mkataba kwenyewe hakuhakikishi mafanikio ya biashara hiyo ya kujasiria. Na kwa hakika si jambo la busara kwa yeyote kujasiria kukopesha fedha nyingi kwa shughuli fulani ya kibiashara kuliko kiasi cha hasara awezacho kustahimili.

      14. Kwa nini twahitaji kuonyesha ufahamu ikiwa tumemkopesha fedha Mkristo mwenzetu ambaye biashara yake haifaulu?

      14 Twahitaji kuonyesha ufahamu ikiwa tumemkopesha Mkristo fedha kwa sababu za kibiashara na hizo fedha zilipotezwa, ingawa mazoea ya kutokufuatia haki hayakuhusika. Ikiwa kutokufaulu kwa biashara hakukuwa kosa la mwamini mwenzetu aliyekopa hizo fedha, je, twaweza kusema kwamba tulikosewa? La, kwa sababu tulimpa mkopo huo kwa hiari, labda tumekuwa tukikusanya riba kutoka kwazo, na hakuna jambo la kutokufuatia haki ambalo limetendeka. Kwa kuwa kutokufuatia haki hakukuhusika, hatuna msingi wowote wa kuchukua hatua ya kisheria dhidi ya mkopaji. Kwa hakika, kungekuwa na manufaa gani kumshtaki kisheria Mkristo mwenzetu mwenye kufuatia haki aliyelazimika kufuata hatua ya kisheria ya kuwa na hali ya kufilisika kwa sababu biashara yake ya kujasiria yenye nia njema haikufaulu?—1 Wakorintho 6:1.

      15. Ni mambo yapi yanayotaka kufikiriwa ikiwa hali ya kufilisika yatangazwa?

      15 Nyakati nyingine wale wasiofaulu kibiashara hutafuta kitulizo kwa kutangaza wana hali ya kufilisika. Kwa kuwa Wakristo hawapuuzi madeni, hata baada ya kuondolewa madeni fulani kisheria, baadhi yao wamehisi wajibu wa kujaribu kulipa madeni yaliyofutwa ikiwa wakopeshaji wangekubali malipo. Lakini, namna gani ikiwa mkopaji alipoteza fedha za ndugu yake kisha akaishi kwa namna ya kufurahia anasa? Au namna gani ikiwa mkopaji alijipatia fedha za kutosha za kurudisha zile alizokopa lakini akapuuza huo wajibu wa kiadili ambao huenda akawa nao kuelekea ndugu yake kifedha? Basi kungekuwa na shaka juu ya sifa za ustahili za mkopaji za kutumikia katika cheo chenye madaraka kutanikoni.—1 Timotheo 3:3, 8; Ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 15, 1994, kurasa 30-31.

      Namna Gani Kukiwa na Upunjaji?

      16. Ni hatua zipi zaweza kuchukuliwa ikiwa twaonekana kuwa wahasiriwa wa upunjaji wa kibiashara?

      16 Ufahamu watusaidia kung’amua kwamba faida hazitokani na kila mpango wa kuweka fedha katika biashara ili kupata faida. Lakini namna gani ikiwa upunjaji unahusika? Upunjaji ni “kule kutumia kimakusudi udanganyifu, hila, au upotoshaji wa kweli kwa kusudi la kushawishi mtu mwingine kutoa kitu fulani chenye thamani kilicho chake au kuacha haki fulani ya kisheria.” Yesu Kristo aliorodhesha hatua ziwezazo kuchukuliwa mtu anapoona amepunjwa na mwabudu mwenzake. Kulingana na Mathayo 18:15-17, Yesu alisema hivi: “Ndugu yako akifanya dhambi, nenda ufunue wazi kosa lake kati yako na yeye peke yake. Akikusikiliza, umempata ndugu yako. Lakini ikiwa yeye hasikilizi, chukua pamoja nawe mmoja au wawili zaidi, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila jambo lipate kuthibitishwa. Ikiwa yeye hawasikilizi wao, liambie kutaniko. Ikiwa hasikilizi hata kutaniko, mwache awe kwako kama vile mtu wa mataifa na kama mkusanya-kodi.” Kielezi ambacho Yesu alitoa baada ya hapo chaonyesha kwamba alikuwa akifikiria dhambi kama zile zinazohusu mambo ya kifedha, kutia ndani upunjaji.—Mathayo 18:23-35.

      17, 18. Mtu anayedai kuwa Mkristo akitupunja, ufahamu waweza kutulindaje salama?

      17 Bila shaka, kusingekuwa na msingi wa Kimaandiko wa kuchukua hatua zilizoorodheshwa kwenye Mathayo 18:15-17 ikiwa hakukuwa na uthibitisho wowote au hata dokezo la upunjaji. Hata hivyo, namna gani ikiwa mtu anayedai kuwa Mkristo alitupunja kwa kweli? Ufahamu waweza kutulinda salama dhidi ya kuchukua hatua iwezayo kuharibu sifa njema ya kutaniko. Paulo alishauri Wakristo wenzake wajiruhusu wakosewe na hata wapunjwe badala ya kumpeleka ndugu mahakamani.—1 Wakorintho 6:7.

      18 Ndugu na dada zetu wa kweli si ‘wenye kujaa kila namna ya upunjaji na ulaghai,’ sawa na yule mchawi Bar-Yesu. (Matendo 13:6-12) Kwa hiyo acheni tutumie ufahamu wakati fedha zinapopotea katika biashara za kujasiria zinazohusisha waamini wenzetu. Ikiwa twafikiria kuchukua hatua ya kisheria, twapaswa kufikiria matokeo yawezayo kutupata sisi binafsi, kumpata yule mtu au watu wengine, kulipata kutaniko, na kuwapata walio nje ya kutaniko. Kufuatilia malipo ya ridhaa kungeweza kutumia wakati wetu mwingi, nishati, na mali nyingine. Tokeo la kufanya hivyo huenda likawa kuwatajirisha tu mawakili na wataalamu wengine. Kwa kuhuzunisha, Wakristo fulani wamedhabihu mapendeleo ya kitheokrasi kwa sababu ya kujihusisha kupita kiasi katika mambo hayo. Kukengeushwa-fikira kwetu kwa namna hiyo ni lazima kuwe kwamfurahisha Shetani, lakini twataka kuufanya moyo wa Yehova ushangilie. (Mithali 27:11) Kwa upande mwingine, kukubali kupatwa na hasara kwaweza kutuzuia tusiwe na maumivu ya moyoni na kwaweza kutuokolea sisi na wazee wakati mwingi. Kutatusaidia tuhifadhi amani ya kutaniko na kutatuwezesha kufuliza kuutafuta Ufalme kwanza.

      Ufahamu na Kufanywa kwa Maamuzi

      19. Ufahamu wa kiroho na sala zaweza kutufanyia nini tunapofanya maamuzi yenye kuleta mkazo?

      19 Kufanya maamuzi kuhusu mambo ya kifedha au ya kibiashara kwaweza kuwa jambo lenye kuleta mkazo. Lakini ufahamu wa kiroho waweza kutusaidia kupima mambo yote na kufanya maamuzi yenye hekima. Isitoshe, kumtegemea Yehova kwa sala kwaweza kutuletea “amani ya Mungu.” (Wafilipi 4:6, 7) Hiyo ni utulivu na ustarehe unaotokana na uhusiano wa kibinafsi wenye ukaribu pamoja na Yehova. Kwa hakika, amani ya jinsi hiyo yaweza kutusaidia tudumishe usawaziko wetu tunapokabiliwa na maamuzi magumu.

      20. Twapaswa kuazimia kufanya nini kwa habari ya mambo ya biashara na kutaniko?

      20 Acheni tuazimie kutoruhusu mabishano juu ya biashara yavuruge amani yetu au ile ya kutaniko. Twahitaji kukumbuka kwamba kutaniko la Kikristo lafanya kazi ili kutusaidia kiroho, si kutumika likiwa kitovu cha ufuatiaji wa kibiashara. Mambo ya biashara yapasa sikuzote kutenganishwa na utendaji mbalimbali wa kutaniko. Twahitaji kutumia ufahamu na hadhari tuanzapo biashara za kujasiria. Na acheni sikuzote tudumishe maoni yenye usawaziko kuhusu mambo hayo, tukitafuta masilahi ya Ufalme kwanza. Iwapo biashara ya kujasiria inayohusisha waabudu wenzetu haifaulu, na tujitahidi kuwafaidi wote wanaohusika.

      21. Twaweza kutumiaje ufahamu na kutenda kwa kupatana na Wafilipi 1:9-11?

      21 Badala ya kuhangaikia kupita kiasi mambo ya kifedha na mambo mengine yasiyo ya maana sana, sisi sote na tuelekeze mioyo yetu kwenye ufahamu, tusali ili tupate mwongozo wa Mungu, na tufulize kutanguliza masilahi ya Ufalme. Kwa kupatana na sala ya Paulo ‘upendo wetu na upate kuzidi pamoja na ujuzi sahihi na ufahamu kamili kwamba tupate kuhakikisha mambo yaliyo ya maana zaidi na tusiwakwaze wengine’ au sisi wenyewe. Sasa kwa kuwa Kristo Mfalme yu kwenye kiti chake cha ufalme cha kimbingu, acheni tuonyeshe ufahamu wa kiroho katika kila sehemu ya maisha. ‘Na tujazwe matunda ya uadilifu kupitia Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu wetu,’ Yehova Bwana Mwenye Enzi Kuu.—Wafilipi 1:9-11.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki