-
Kijiji Kimoja cha Dunia Nzima Lakini Bado KimegawanyikaAmkeni!—1996 | Julai 8
-
-
Kijiji Kimoja cha Dunia Nzima Lakini Bado Kimegawanyika
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
JE, UMEPATA kusikia hadithi za jamii fulani ya watu ambao hawakuwa na vinywa na hivyo hawakuweza kula au kunywa chochote? Ilisemekana kwamba wao waliishi kwa kunusa, hasa kwa kunusa matofaa. Uvundo ungewaua.
Pia kulikuwa na hadithi za watu fulani wa Afrika Magharibi waliokuwa na dhahabu za kufanyia biashara. Nahodha mmoja wa wakati huo wa meli ya Ureno aliripoti hivi: “[Umbali] wa leagues mia mbili ng’ambo ya ufalme wa [Mali], mtu apata nchi yenye wakazi ambao wana vichwa na meno ya mbwa na mikia kama ya mbwa. Hawa ndio Weusi wanaokataa mazungumzo kwa sababu hawataki kuona watu wengine.” Hayo yalikuwa baadhi ya mawazo ya ajabu ambayo yaliaminiwa miaka mingi iliyopita, kabla ya enzi ya usafiri na uvumbuzi.
Watu Watangamana
Hadithi kama hizo zilionwa kuwa za kweli kwa karne nyingi. Lakini wavumbuzi walipovumbua dunia, hawakupata watu wasio na vinywa ambao walinusa matofaa, wala hawakupata watu wenye vichwa vya mbwa. Leo hakuna fumbo lolote kuhusu watu wanaoishi ng’ambo ya mipaka yetu. Ulimwengu umekuwa kijiji kimoja. Televisheni huleta habari kuhusu nchi na watu wa kigeni katika vyumba vyetu. Kusafiri kwa ndege hufanya iwezekane kuzuru nchi hizo za kigeni kwa muda wa saa chache; mamilioni ya watu hufanya hivyo kila mwaka. Wengine huhama kwa sababu za kiuchumi au za kisiasa. Ripoti moja ya Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu yasema hivi: “Kwa kiwango kikubwa zaidi katika historia—na ambacho kwa hakika kitaendelea kuongezeka—watu ulimwenguni pote wanahama na kutafuta maisha bora.” Watu wapatao milioni 100 wanaishi nje ya nchi ambamo walizaliwa.
Kwa kuongezeka kuna utegemeano wa kiuchumi kati ya mataifa. Mfumo wa mawasiliano ya duniani pote, kama mfumo mkuu wa neva, huunganisha kila taifa duniani. Huku mawazo, habari, na tekinolojia zikibadilishanwa, tamaduni huungana na kujipatanisha na nyingine. Ulimwenguni pote watu huvalia kwa karibu njia sawa kuliko wakati mwingine wowote. Majiji ya ulimwengu yana mambo yafananayo—polisi, hoteli za anasa, magari, maduka, benki, uchafuzi. Hivyo, watu wa ulimwengu wajapo pamoja, twaona kile ambacho watu wengine hukiita utamaduni unaojitokeza wa ulimwengu.
Sababu Inayofanya Watu Wabaki Wakiwa Wamegawanyika
Lakini ingawa watu na tamaduni huchangamana, kwa wazi si wote wanaoona wengine kuwa ndugu. “Kila mtu ni mwepesi kumlaumu mgeni,” akaandika mwandikaji mmoja Mgiriki wa tamthilia zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Kwa kusikitisha ndivyo hali ilivyo leo. Uthibitisho waonekana kwa urahisi katika ripoti za magazeti ya habari juu ya ushupavu, chuki kwa wageni, “utakasaji wa kikabila,” mashindano ya kijamii, fujo za kidini, machinjo ya raia, mauaji ya kiholela, kambi za kulala wanawake kinguvu, mateso, au maangamizi ya jamii nzima-nzima.
Bila shaka, wengi wetu hawawezi kufanya lolote ili kubadili mwendo wa mapambano ya kikabila. Hata huenda hatuathiriwi nayo moja kwa moja. Hata hivyo, kwa wengi wetu matatizo hutokea kwa sababu ya kutowasiliana na wageni tunaokutana nao—majirani, wafanyakazi wenzetu, au wanashule wenzetu.
Je, haionekani kuwa ajabu sana kwamba watu wa kabila tofauti-tofauti mara nyingi hupata ugumu wa kuaminiana na kuthaminiana? Dunia ina vitu vyenye kutofautiana sana, vya aina nyingi sana. Wengi wetu huthamini wingi wa aina ya vyakula, muziki na rangi mbalimbali na vilevile aina mbalimbali za mimea, ndege, na wanyama. Lakini kwa njia fulani uthamini wetu kwa vitu tofauti-tofauti mara nyingi hauhusishi watu ambao hawafikiri na kutenda kama sisi.
Badala ya kutazama uzuri wa tofauti zilizoko miongoni mwa watu, watu wengi huelekea kukazia tofauti za watu na kuzifanya msingi wa mabishano. Kwa nini? Kuna manufaa gani katika kujaribu kushirikiana na watu ambao utamaduni wao hutofautiana na wetu? Tunaweza kushindaje vizuizi vya mawasiliano na kuziba pengo la mawasiliano? Makala ifuatayo itajaribu kujibu maswali hayo.
-
-
Vizuizi Vinavyozuia MawasilianoAmkeni!—1996 | Julai 8
-
-
Vizuizi Vinavyozuia Mawasiliano
ROBERT ni mishonari wa Watch Tower aishiye Sierra Leone, Afrika Magharibi. Siku moja muda mfupi baada ya kuwasili nchi hiyo, alipokuwa akitembea barabarani, aliona kwamba watoto wa huko walikuwa wakiimba: “Mzungu!” Mzungu!” Robert, ambaye ni Mmarekani mweusi, alitazama huku na huku aone mzungu, lakini hapakuwa na mtu yeyote hapo. Ndipo akang’amua kwamba watoto walikuwa wakipiga kelele kumhusu!
Hakukuwa na ubaya wowote katika kuimba huko. Hao watoto walikuwa tu wanaonyesha kwamba Robert ni wa utamaduni ulio tofauti na wao. Kumwita Robert mzungu kulikuwa ndiko njia bora zaidi ya kutaja tofauti iliyokuwako kati yao.
Jinsi Utamaduni Huathiri Jinsi Tulivyo
Utamaduni umefafanuliwa kwa mapana kuwa “mawazo yanayoshirikiwa yenye kufanana, . . . desturi, itikadi, na ujuzi unaotambulisha njia fulani ya maisha.” Sisi hujifunza maadili mengi ya kitamaduni kupitia kufundishwa kwa njia ya moja kwa moja, lakini sisi hujifunza mengi bila hata kujua. Mtafiti mmoja alisema hivi: “Tangu wakati wa kuzaliwa kwa [mtoto] desturi zinazofuatwa na wazazi wake hufanyiza maono na tabia yake. Kufikia wakati awezapo kuzungumza, yeye ni tokeo la utamaduni wake, na kufikia wakati ambapo yeye ni mtu mzima na kuweza kushiriki katika utendaji wa utamaduni, tabia za [utamaduni] huwa zake, itikadi za [utamaduni] huwa zake, na mambo yasiyowezekana kwa [utamaduni] hayawezekani kwake.”
Kwa njia nyingi utamaduni hufanya maisha yawe rahisi kwetu. Tukiwa watoto sisi hujifunza upesi jinsi ya kuwapendeza wazazi wetu. Kujua mambo yakubaliwayo na yasiyokubaliwa na jamii yetu hutuongoza katika kufanya maamuzi juu ya jinsi ya kutenda, mavazi, na jinsi ya kushughulika na wengine.
Bila shaka, kile tulicho tukiwa watu mmoja-mmoja hakitegemei malezi yetu ya kitamaduni pekee. Katika kila utamaduni kuna tofauti miongoni mwa watu. Jinsi tulivyo huamuliwa pia na tabia ya urithi, maono yetu maishani, na mambo mengine mengi. Hata hivyo, utamaduni ndio njia ambayo sisi hutumia kuona ulimwengu.
Kwa kielelezo, utamaduni wetu huamua si lugha tusemayo tu bali pia jinsi tuisemavyo. Katika sehemu fulani za Mashariki ya Kati, watu huthamini uwezo wa kujieleza kwa ustadi kwa kutumia maneno mengi, ya kujirudia-rudia pamoja na misemo. Kwa kutofautisha, watu wa nchi fulani za Mashariki ya Mbali huzungumza kidogo sana. Mithali moja ya Kijapani yaonyesha wazo hilo: “Kwa kinywa chako, utaangamia.”
Utamaduni wetu huamua jinsi tuonavyo wakati. Katika Uswisi, ukichelewa kwa dakika kumi kwa miadi fulani, unatarajiwa uombe radhi. Katika nchi nyinginezo unaweza kuchelewa kwa muda wa saa moja au mbili na usitarajiwe kuomba radhi.
Utamaduni wetu pia hutufundisha maadili. Fikiria jinsi ambavyo ungehisi mtu akikuambia: “Unaongeza uzito sana. Unanenepa kwelikweli!” Ikiwa ulilelewa katika utamaduni wa Kiafrika ambako ukubwa wa mwili huthaminiwa, yaelekea ungefurahia hayo maneno. Lakini ikiwa ulilelewa katika utamaduni wa Magharibi ambako wembamba huthaminiwa sana, yaelekea maneno hayo ya unyoofu yangekuudhi.
‘Njia Yetu Ndiyo Bora!’
Kile ambacho mara nyingi huzuia mawasiliano kati ya watu wa tamaduni tofauti ni kwamba kila mahali watu hufikiria kwamba utamaduni wao ndio bora. Wengi wetu hufikiri kwamba itikadi zetu, maadili, mapokeo, na namna ya kuvaa, na mawazo juu ya urembo ni sawa, yafaa, na bora kuliko mengine yote. Pia sisi huelekea kuhukumu tamaduni nyinginezo kwa kuzilinganisha na maadili ya kikundi chetu. Kufikiri hivyo ni kuona utamaduni wetu kuwa bora kuliko nyinginezo. The New Encyclopædia Britannica huonelea: “Kuona utamaduni wetu kuwa bora . . . ni jambo linalopata karibu ulimwengu mzima. Washiriki wa karibu tamaduni zote za ulimwengu huona njia zao wenyewe za maisha kuwa bora kuliko hata zile za majirani wao wa karibu.”
Miaka 200 iliyopita, Mwingereza mmoja mwenye cheo alieleza jambo hilo waziwazi, akisema: “[Kwa] maoni yangu, wageni ni wapumbavu.” Mhariri wa kitabu chenye manukuu hayo aliandika: “Ni lazima [hiyo] iwe hisia ya karibu ulimwengu wote.”
Vielelezo vya kutovumilia wale wa tamaduni nyinginezo vimejaa. Ingawa liliandikwa awali na mwandikaji wa vitabu Mjerumani katika miaka ya 1930, nukuu lifuatalo mara nyingi husemwa kuwa lilitajwa na kiongozi wa Nazi Hermann Göring: “Nisikiapo neno utamaduni, mimi hutwaa bastola yangu.”
Maoni ya kishupavu ya kuona utamaduni wako kuwa bora yaweza kutokeza ubaguzi, ambao nao unaweza kutokeza chuki na pambano. Richard Goldstone ni kiongozi wa mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa inayochunguza uhalifu wa vita katika Rwanda na ile iliyokuwa Yugoslavia. Kuhusu matendo makatili katika mapambano hayo yote mawili, yeye alisema: “Jambo hili laweza kutokea mahali popote. Hapa pana nchi mbili tofauti, zikiwa na tamaduni na historia tofauti, lakini ukatili unaofanana [una]fanywa na jirani dhidi ya jirani mwenzake. Aina hii ya vita vikatili vya kikabila au kidini ni ubaguzi tu ulioongezeka ukawa wenye jeuri. Kile kikundi cha watu kinachohasiriwa ni lazima kishushiwe hadhi kabisa au kuonwa kuwa cha kishetani. Mara hilo lifanywapo, hilo huondolea watu wa kawaida vizuizi vya kiadili ambavyo kwa kawaida vingewazuia wasitende matendo ya kuogofya kama hayo.”
Kupanua Mtazamo Wetu
Mara nyingi watu tuwachaguao kuwa marafiki wetu ni wale walio kama sisi, watu wenye kushiriki mitazamo yetu na maadili yetu. Sisi huwatumaini na kuwaelewa. Sisi hustarehe tukiwa pamoja nao. Tukiona tabia ya mtu mwingine kuwa isiyo ya kawaida au isiyo nzuri, yaelekea marafiki wetu watakubaliana nasi kwa sababu wao wana ubaguzi uleule kama sisi.
Basi, twaweza kupata manufaa gani katika kuwasiliana na wengine wanaotofautiana na sisi kwa sababu ya malezi ya kitamaduni? Kwanza, mawasiliano mazuri yatatusaidia kuelewa sababu zinazofanya wengine wafikiri na kutenda jinsi wafanyavyo. Kunle, kutoka Afrika Magharibi, asema: “Watoto wengi katika Afrika hukatazwa sana wasiongee wanapokula chakula. Lakini, katika baadhi ya nchi za Ulaya, kuongea wakati wa kula kunapendekezwa. Basi ni nini hutukia wakati Mzungu anapokula pamoja na Mwafrika? Yule mzungu anashangaa kwa nini huyu Mwafrika anakula chakula kwa mawazo mazito na kwa ukimya. Wakati uo huo, yule Mwafrika anashangaa ni kwa nini huyo Mzungu anaongea kama kasuku!” Kwa wazi katika hali kama hizo, kuelewa malezi ya kitamaduni ya kila mmoja kwaweza kuondoa ubaguzi wa kijamii.
Tupatapo kuwajua watu wa tamaduni nyinginezo, hatuboreshi tu jinsi tunavyowaelewa wengine bali pia sisi wenyewe hujielewa vizuri zaidi. Mstadi mmoja wa mambo ya kibinadamu aliandika: “Kitu ambacho yule mkazi wa ndani ya bahari hawezi kugundua ni maji. Yeye angefahamu maji yapo ikiwa tu aksidenti fulani ingemleta juu na kumwonyesha hewa. . . . Uwezo wa kuona utamaduni wa jamii yetu kwa ujumla . . . hutaka kiasi fulani cha uwezo wa kushughulikia mambo bila ubaguzi ambao mara nyingi haupo kamwe.” Hata hivyo, kwa kufahamu tamaduni nyinginezo, sisi ni kama yule mkazi wa bahari anayeonyeshwa hewa; twatambua “maji” ya kitamaduni tunamoishi. Mwandikaji Thomas Abercrombie alieleza jambo hilo vizuri: “Mtu ambaye hajavutiwa na utamaduni wa kigeni hawezi kamwe kujua vizuizi vya utamaduni wake.”
Kwa ufupi, kuthamini tamaduni nyinginezo kwaweza kuboresha maisha zetu kwa kupanua mtazamo wetu, ili tuweze kujielewa na kuelewa wengine vizuri zaidi. Ingawa urithi wa kitamaduni na mawazo ya kwamba utamaduni wako ndio bora yaweza kuwa vizuizi vinavyozuia mawasiliano, lakini si lazima yawe hivyo. Vizuizi hivyo vyaweza kushindwa.
-
-
Kushinda Vizuizi vya MawasilianoAmkeni!—1996 | Julai 8
-
-
Kushinda Vizuizi vya Mawasiliano
HATUKUCHAGUA familia au taifa ambalo tulizaliwa ndani yalo, wala hatukuamua ni utamaduni gani ungefanyiza njia yetu ya kufikiri. Hatukuwa na uwezo wowote juu ya mambo hayo. Sote hupatwa na wakati na hali. Lakini twaweza kudhibiti jinsi tunavyowaona wengine na kuwatendea.
Biblia hufafanua jinsi tuwezavyo kufanya hivyo. Fikiria kanuni chache zitakazotusaidia kuwasiliana na wale ambao huenda wanatoka katika malezi yanayotofautiana na yetu.
“Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo . . . alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote.” (Matendo 17:24, 26) Sisi sote ni washiriki wa familia ileile ya kibinadamu na basi tuna mambo mengi yanayofanana. Kutazama mambo tuliyo nayo ambayo yafanana hufanya mawasiliano yawe rahisi zaidi. Sisi sote twataka marafiki wazuri nasi twahitaji kuhisi tunapendwa na kustahiwa. Kila mtu hujaribu kuepuka maumivu ya kimwili na ya kihisia-moyo. Watu wa tamaduni zote hupenda muziki na sanaa, kusema mambo yachekeshayo, na kuamini kutendeana kwa adabu, nao hutafuta njia za kuwa na furaha.
‘Usitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, umhesabu mwenzako kuwa bora kuliko nafsi yako.’ (Wafilipi 2:3) Hili halimaanishi kwamba tuwaone wengine kuwa bora kuliko sisi kwa kila kitu. Badala ya hivyo, twapaswa kung’amua kwamba katika maeneo fulani ya maisha, wengine ni bora. Hatupaswi kamwe kufikiri kwamba ama sisi ama utamaduni wetu hufanya mambo yote vizuri kushinda wengine.
“Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema.” (Wagalatia 6:10) Kuchukua tu hatua ya kuwa mwenye urafiki na mwenye kusaidia wengine, hata wawe wa malezi gani ya kitamaduni kwaweza kusaidia sana kuziba pengo la mawasiliano.
“Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika.” (Yakobo 1:19) Wawasilianaji wazuri ni lazima wafanye mengi zaidi ya kusema tu; ni lazima wawe wasikilizaji wenye hisia-mwenzi.
“Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; lakini mtu mwenye ufahamu atayateka.” (Mithali 20:5) Uwe chonjo kufahamu hisia na masuala yanayomfanya mtu awe na tabia fulani kwa nje. Jaribu kujua watu vizuri zaidi.
“Mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.” (Wafilipi 2:4) Uwe mwenye hisia-mwenzi kwa kutazama masuala jinsi mwingine ayaonavyo. Usiwe mwenye ubinafsi.
Utofauti wa Kitamaduni Miongoni mwa Mashahidi wa Yehova
Jambo la kwamba kanuni hizo kwa kweli zinafanya kazi laonekana katika muungano wenye kustaajabisha wa Mashahidi wa Yehova, ambao wanatenda katika nchi 232 za dunia. Wao ni watu ambao wametoka “kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha” na ambao wameazimia kujipatanisha na mwongozo wenye upendo wa Yehova katika mambo yote.—Ufunuo 7:9; 1 Wakorintho 10:31-33.
Mashahidi mmoja-mmoja hawadharau utamaduni wa wengine. Wala wale wanaokuwa Mashahidi hawakatai utamaduni ambamo walilelewa, ila tu kama huo unapinga kanuni za Biblia. Katika hali kama hizo wao hufanya mabadiliko maishani mwao. Wao hutambua kwamba katika kila utamaduni kuna mambo mazuri sana na kwamba hayo hukuzwa hata zaidi katika watu wanaokubali ibada ya kweli.
Wao hujaribu kuona dunia yetu jinsi ambavyo lazima Mungu awe anaiona—yenye kung’aa na buluu na maridadi—ikizunguka angani. Ni dunia yenye watu na tamaduni tofauti-tofauti ajabu. Mashahidi wa Yehova watazamia wakati ambapo wote walio duniani watafurahia maisha wakiwa familia ambayo kikweli imeungana.
-