-
Kwa Nini Ni Vigumu Kuwa na Maisha Yenye Kuridhisha?Jinsi ya Kupata Maisha Yenye Kuridhisha
-
-
6 Ghafla matunda ya mti huo yakavutia, yakatamanika sana! Hawa akachukua tunda, akala, baadaye akampa mume wake. Ingawa Adamu alijua vizuri kabisa matokeo, alimsikiliza mke wake naye akala. Matokeo yakawaje? Yehova alimhukumu hivi mwanamke: “Nitazidisha sana uchungu wa mimba yako; utazaa watoto kwa uchungu, nawe utamtamani sana mume wako, naye atakutawala.” Namna gani mwanamume? “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako. Kwa maumivu utakula mazao yake sikuzote za maisha yako. Itakuzalia miiba na michongoma, nawe utakula mimea ya shambani. Kwa jasho la uso wako utakula chakula mpaka utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitolewa humo. Kwa maana wewe ni mavumbi nawe utarudi mavumbini.” Sasa Adamu na Hawa waliachwa wajitafutie wenyewe furaha na kuridhika. Je, jitihada za wanadamu za kuishi maisha yenye kuridhisha bila kusudi la Mungu zingefanikiwa? Badala ya kufanya kazi yenye kufurahisha ya kutunza Paradiso iliyo kama bustani na kuipanua hadi miisho ya dunia, sasa walifanya kazi ya kuchosha ili tu waendelee kuishi, bila kufanya chochote cha kumtukuza Muumba.—Mwanzo 3:6-19.
7 Siku waliyokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, machoni pa Mungu Adamu na Hawa walikufa wakaanza kudhoofika wakielekea kufa kihalisi. Walipatwa na nini walipokufa hatimaye? Biblia inatufahamisha hali ya wafu. “Walio hai wanajua kwamba watakufa, lakini waliokufa hawajui jambo lolote kamwe, wala hawana thawabu tena, kwa sababu kumbukumbu lote kuwahusu limesahauliwa.” (Mhubiri 9:5; Zaburi 146:4) “Nafsi” haiendelei kuishi mtu anapokufa. Adhabu ya dhambi ni kifo, wala si kuteswa katika moto wa milele. Isitoshe, mtu akifa haendi mbinguni kuishi raha mustarehe.a
8 Kama vile sufuria iliyobonyea inayotumiwa kuokea mikate inavyotokeza mikate iliyobonyea, ndivyo Adamu na Hawa wasio wakamilifu wangetokeza wazao wasio wakamilifu. Biblia inafafanua hali hiyo: “Kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, basi kifo kikaenea kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi.” (Waroma 5:12) Kwa hiyo, sisi sote huzaliwa tukiwa na dhambi katika hali ya kutokamilika. Maisha ya wazao wa Adamu yakawa magumu na yenye kuchosha. Lakini, je, kuna suluhisho?
-
-
Maisha Yenye Kuridhisha YarudishwaJinsi ya Kupata Maisha Yenye Kuridhisha
-
-
Mungu aliwapa wanadamu tumaini ili waweze kukombolewa kutokana na utumwa wa dhambi na kifo
2 Adamu na Hawa walipotenda dhambi, waliwanyima wazao wao fursa ya kuishi maisha yenye kuridhisha duniani milele. Kwa sababu ya kutaka haki ya kujiamulia mema na mabaya, waliiuza familia yao ya wakati ujao katika utumwa wa dhambi na kifo. Kwa kuwa walizaliwa katika familia hiyo, wazao wao wanaweza kufananishwa na watumwa waliofungiwa katika kisiwa cha mbali kinachotawaliwa na wafalme wakatili. Kwa kweli, kifo kimetawala kama mfalme juu ya wanadamu walio watumwa wa mfalme mwingine—dhambi. (Waroma 5:14, 21) Inaonekana hakuna mtu atakayewaokoa. Kwa sababu babu yao ndiye aliyewauza utumwani!
-