-
Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha YakoAmkeni!—1999 | Novemba 8
-
-
Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako
KAMA vile kuvu inayosababisha kuoza kwa mihimili ya nyumba, ndivyo dawa za kulevya ziwezavyo kudhoofisha muundo mzima wa jamii. Ili jamii ya kibinadamu itende kwa njia inayofaa, lazima iwe na familia zilizo imara, wafanyakazi wenye afya, serikali zinazoweza kutumainika, polisi wenye kufuatia haki, na raia wanaotii sheria. Dawa za kulevya hudhoofisha kila moja ya mambo hayo ya msingi.
-
-
Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha YakoAmkeni!—1999 | Novemba 8
-
-
Lakini haiathiri tu afya ya mtumiaji. Takriban asilimia 10 ya watoto wote wanaozaliwa Marekani wanakabili hatari ya dawa za kulevya haramu—katika visa vingi, kokeini—wanapokuwa wangali kwenye tumbo la uzazi. Tatizo wanalokabili si athari za kuacha peke yake, kwa kuwa hatari ya dawa za kulevya katika tumbo la uzazi yaweza kusababisha watoto wanaozaliwa wapatwe na matokeo mengine yenye kudhuru—ya kiakili na ya kimwili.
Pesa Zinazopatikana kwa Urahisi Kupitia Dawa za Kulevya—Kishawishi Kisichozuilika
Je, wewe huhisi ukiwa salama katika ujirani wako baada ya giza kuingia? Ikiwa sivyo, labda ni kwa sababu ya wauzaji wa dawa za kulevya. Uvamizi na jeuri ya mitaani inahusiana sana na dawa za kulevya. Mara nyingi watumiaji wa dawa za kulevya hugeukia uhalifu au ukahaba ili kuendeleza zoea lao, huku magenge yenye kushindana yakipigana na kuuana ili kudhibiti ugawaji wa dawa za kulevya. Kwa kueleweka, polisi katika miji mingi huona dawa za kulevya kuwa zinachangia visa vingi vya uuaji ambavyo wanachunguza.
Katika mabara fulani, waasi wameona faida za kutumia nguvu ili kujinufaisha na biashara yenye faida ya mihadarati. Kikundi kimoja cha waasi huko Amerika Kusini sasa kinajipatia nusu ya mapato yake kwa kuwalinda walanguzi wa dawa za kulevya. “Mapato yanayotokana na dawa za kulevya haramu hutumiwa kuendeleza baadhi ya mapambano makali zaidi ulimwenguni ya kidini na ya kikabila,” laripoti Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Ulanguzi wa Dawa za Kulevya Ulimwenguni.
Msiba Unaotokana na Athari za Dawa za Kulevya
Watumiaji wa dawa za kulevya hufanya barabara zisiwe salama katika njia nyingine. “Kuendesha gari ukiwa chini ya uvutano wa bangi au LSD kwaweza kuwa hatari kama vile kuendesha ukiwa umekunywa kileo,” asema Michael Kronenwetter, katika kitabu chake Drugs in America. Haishangazi basi kwamba watumiaji wa dawa za kulevya wanaelekea kupatwa na aksidenti wakiwa kazini mara tatu au nne zaidi.
Hata hivyo, labda nyumbani ndipo dawa za kulevya hutokeza madhara makubwa zaidi. “Maisha ya familia yenye kasoro na utumiaji wa dawa za kulevya mara nyingi huhusiana,” chasema kichapo World Drug Report. Wazazi wanaotatanishwa na tamaa ya kutumia dawa za kulevya huwaandalia watoto wao maisha imara kwa nadra sana. Kifungo kati ya mtoto mchanga na mzazi—kilicho cha maana sana katika majuma ya kwanza ya maisha ya mtoto—kinaweza kukatizwa. Kwa kuongezea, wazazi walio waraibu mara nyingi huwa na madeni na waweza kuibia marafiki wao na familia au waweza kupoteza kazi zao. Watoto wengi wanaokulia katika mazingira hayo hutoroka nyumbani na kwenda kuishi barabarani au hata huanza kutumia dawa za kulevya.
Matumizi mabaya ya dawa za kulevya yanaweza kuongoza kwenye kutendwa vibaya kimwili—kwa mwenzi au watoto. Kokeini hasa inapochanganywa na kileo, inaweza kumfanya mtu ambaye kwa kawaida ni mtulivu akawa na tabia mwitu. Kulingana na uchunguzi wa Kanada uliofanyiwa watumiaji wa kokeini, asilimia 17 ya waliohojiwa walikiri kwamba walikuwa wachokozi baada ya kutumia dawa za kulevya. Hali kadhalika, ripoti moja kuhusu kutenda watoto vibaya huko New York City ilipiga hesabu na kupata kwamba asilimia 73 ya watoto waliopigwa hadi wakafa walikuwa na wazazi waliotumia vibaya dawa za kulevya.
Ufisadi na Uchafu
Ikiwa nyumba inaweza kudhoofishwa na ufisadi, hali kadhalika serikali zinaweza. Katika kisa hiki ni pesa za dawa za kulevya, badala ya dawa za kulevya zenyewe, ndizo hufisidi mfumo. “Dawa za kulevya zimefisidi maofisa wa serikali, polisi na jeshi,” akalalamika balozi mmoja kutoka nchi moja ya Amerika Kusini. Anaongezea kwamba pesa zinazopatikana ni “kishawishi kikubwa sana” kwa wale walio na tatizo la kujikimu.
Nchi moja baada ya nyingine, mahakimu, mameya, polisi, na hata maofisa wa kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya wamenaswa katika hali ya ufisadi. Wanasiasa ambao huenda uchaguzi wao ulifanywa kwa kutumia pesa za viongozi wa ulanguzi wa dawa za kulevya hukataa wanapoombwa wachukue hatua kali za kinidhamu dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Maofisa wengi wenye kufuatia haki ambao wameunga mkono kwa ujasiri harakati dhidi ya dawa za kulevya wameuawa.
Hata udongo wetu, misitu yetu, na aina mbalimbali za viumbe wanaoishi humo wanateseka kutokana na pigo la tufeni pote la dawa za kulevya. Asilimia kubwa ya uzalishaji wa afyuni na kokeini hufanywa katika maeneo mawili ambayo yanaweza kupatwa na madhara ya kimazingira kwa urahisi: misitu ya mvua ya magharibi mwa Amazon na ile ya Kusini-mashariki ya Asia. Uharibifu katika sehemu hizo umekuwa mkubwa. Hata jitihada zenye kusifika za kuondoa mimea ya dawa za kulevya haramu huleta madhara makubwa kwa sababu ya dawa zinazotumika kuua mimea.
Ni Nani Hulipia Madhara Hayo?
Ni nani hulipia madhara yote yanayoletwa na dawa za kulevya? Ni sisi sote. Naam, sote hulipia hasara ya uzalishaji, gharama za kitiba, mali zilizoibwa au kuharibiwa, na gharama ya kutekeleza sheria. Ripoti ya Wizara ya Kazi ya Marekani ilipiga hesabu na kupata kwamba “matumizi ya dawa za kulevya kazini yaweza kugharimu biashara na viwanda vya Marekani kati ya dola bilioni 75 hadi 100 kila mwaka . . . ikiwa ni hasara ya uzalishaji, aksidenti na gharama za juu za kitiba, na gharama za kulipa wafanyakazi ridhaa.”
Hatimaye pesa hizo zote hulipwa na watu wanaotozwa kodi pamoja na wanunuzi. Uchunguzi uliofanywa Ujerumani katika mwaka wa 1995 ulipiga hesabu ya ujumla ya gharama ya mwaka mmoja ya dawa za kulevya katika nchi hiyo kuwa dola za Marekani 120 kwa kila raia. Huko Marekani, kadirio la tarakimu moja lilikuwa juu hata zaidi—dola za Marekani 300 kwa kila mtu.
Hata hivyo, gharama iliyo kubwa hata zaidi ni madhara ya jamii ambayo huletwa na dawa za kulevya. Ni nani ambaye angetoa thamani ya fedha ya kuvunjika kwa familia nyingi namna hiyo, kutendwa vibaya kwa watoto wengi namna hiyo, ufisadi wa maofisa wengi kadiri hiyo, na vifo vya mapema vya watu wengi kadiri hiyo? Mambo hayo yote yanamaanisha nini kwa semi za kibinadamu? Makala yetu ifuatayo itachunguza jinsi dawa za kulevya huathiri maisha ya wale wanaozitumia.
-