Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001 | Julai 8
    • Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?

      NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

      “KILA mtu hutumia dawa za kulevya.” Usemi huo wa kawaida unaweza kuwashawishi wale wasio na busara waonje dawa haramu za kulevya. Ikitegemea jinsi tunavyoelewa neno “dawa za kulevya,” usemi huo ni wa kweli kwa kadiri fulani.

      Neno “dawa za kulevya” linafafanuliwa kuwa: “Kitu chochote chenye kemikali, kiwe ni cha asili au cha sanisia, ambacho kinaweza kuvuruga uwezo wa kufikiri, hisia au hali nyingine za kisaikolojia.” Ufafanuzi huo muhimu sana hutumiwa na wengi kurejezea dawa zinazoathiri uwezo wa kufikiri ingawa hauhusu dawa nyingi za matibabu.

      Kupatana na ufafanuzi huo, pombe ni dawa ya kulevya. Hatari huzuka watu wanapokunywa pombe kupita kiasi. Ni wazi kwamba tatizo hilo linaongezeka. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika vyuo na vyuo vikuu katika nchi moja ya Ulaya ulifunua kwamba “sherehe za ulevi ni tatizo kubwa sana katika vyuo hivyo.” Uchunguzi huo ulifunua kwamba asilimia 44 ya wanafunzi ni walevi.a

      Kama pombe, sigareti imeidhinishwa kisheria ijapokuwa ina sumu kali sana ya nikotini. Shirika la Afya Ulimwenguni, linasema kwamba watu wapatao milioni nne hufa kila mwaka kwa sababu ya uvutaji wa sigareti. Lakini, wauzaji mashuhuri wa sigareti ni watu matajiri wanaoheshimiwa katika jamii. Uvutaji wa sigareti husababisha uraibu, labda hata kuliko dawa nyingi haramu za kulevya.

      Katika miaka ya karibuni, nchi nyingi zimepiga marufuku matangazo ya sigareti na kuweka vizuizi vingine. Lakini watu wengi wanaona kuvuta sigareti kuwa jambo linalokubaliwa na jamii. Watayarishaji wa sinema hutukuza uvutaji wa sigareti kana kwamba ni jambo zuri sana. Uchunguzi mmoja uliofanywa na Chuo Kikuu cha California huko San Francisco kuhusu sinema zilizovuma sana kati ya mwaka wa 1991 na 1996, ulifunua kwamba asilimia 80 ya waigizaji wakuu wa sinema hizo walionyeshwa wakivuta sigareti.

      Vipi Kuhusu Dawa “Zisizodhuru”?

      Bila shaka dawa za kitiba zimewasaidia watu wengi, lakini zinaweza kutumiwa vibaya. Nyakati nyingine madaktari huwapa wagonjwa dawa ovyoovyo, au wanashurutishwa na wagonjwa kuwapa dawa zisizohitajiwa. Daktari mmoja alisema hivi: “Mara nyingi madaktari hawachanganui kisababishi cha ugonjwa. Ni rahisi kusema, ‘Meza kidonge hiki.’ Lakini kisababishi cha ugonjwa hakishughulikiwi.”

      Hata dawa zinazotumiwa bila maagizo ya daktari, kama vile aspirini na paracetamol (Tylenol, Panadol), zinaweza kuwa hatari sana kwa afya zikitumiwa vibaya. Zaidi ya watu 2,000 ulimwenguni pote hufa kila mwaka kwa sababu ya kutumia vibaya dawa ya paracetamol.

      Kulingana na ufafanuzi wetu wa awali, kemikali ya kafeini iliyo katika chai na kahawa ni dawa ya kulevya pia, ingawa hatufikiri hivyo tunapokunywa chai au kahawa tunayopenda wakati wa kiamsha-kinywa. Na haingefaa kulinganisha vinywaji vinavyokubaliwa kama chai au kahawa na dawa kali za kulevya kama heroini. Kufanya hivyo kungekuwa kama kulinganisha kitoto cha paka na simba mkali. Hata hivyo, wataalamu fulani wa afya wanasema kwamba ukizoea kunywa zaidi ya vikombe vitano vya kahawa au vikombe tisa vya chai kwa siku, unaweza kupata madhara. Isitoshe, ukipunguza ghafula kiasi kikubwa unachokunywa, unaweza kusumbuliwa na dalili za kuacha kama zile zilizompata mnywaji mmoja wa chai. Alianza kutapika, kupata maumivu makali ya kichwa, na kuathiriwa na mwangaza.

      Vipi Kuhusu Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya?

      Jambo ambalo limezusha ubishi mkali zaidi ni matumizi ya dawa za kulevya michezoni. Jambo hilo lilitukia katika mashindano ya baiskeli ya Tour de France mwaka wa 1998, wakati waendeshaji tisa wa baiskeli wa timu iliyokuwa ikiongoza walipofukuzwa mashindanoni kwa sababu ya kutumia dawa zinazoongeza nguvu mwilini. Wanariadha wamebuni njia mbalimbali za kuepuka kunaswa wakati wanapopimwa kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya. Gazeti Time laripoti kwamba baadhi ya wanariadha hata huenda “‘kutiwa mkojo wa mtu mwingine,’ yaani mkojo ‘usio na dawa za kulevya’ hutiwa kwenye kibofu chao kupitia kifaa maalumu kiitwacho katheta. Kwa kawaida mtu huhisi maumivu makali sana.”

      Bado hatujazungumzia aina mbalimbali za dawa haramu za kulevya zinazotumiwa kama “kiburudisho.” Zatia ndani bangi, ecstasy (methylenedioxy-methamphetamine, au MDMA), LSD (lysergic acid diethylamide), dawa zinazochochea utendaji wa mwili kama vile kokeini na amphetamines, dawa zinazopumbaza akili (za kutuliza wasiwasi), na heroini. Hatupaswi pia kusahau zoea linalopendwa na vijana wengi la kupumua mvuke wa gundi na petroli. Bila shaka, bidhaa hizo zenye mvuke hazijapigwa marufuku na zinapatikana kwa urahisi.

      Maoni ya kawaida ya kwamba waraibu wa dawa za kulevya walionyong’onyea hujifungia katika chumba kichafu na kujidunga mishipani sindano zenye dawa za kulevya huenda yasiwe sahihi. Waraibu wengi wa dawa za kulevya huishi maisha ya kawaida tu, ijapokuwa uraibu wao huathiri maisha yao kwa kadiri fulani. Hata hivyo, hatuwezi kupuuza hatari ya dawa za kulevya. Mwandishi mmoja aeleza kwamba watumiaji fulani wa kokeini “wanaweza kujidunga sindano nyingi sana za kokeini kwa muda mfupi tu, kiasi cha kwamba mwili wao unajaa majeraha mengi sana ya sindano yanayovuja damu.”

      Matumizi haramu ya dawa za kulevya yalipungua sana mwishoni mwa miaka ya 1980, lakini sasa yanaongezeka tena ulimwenguni pote. Gazeti la Newsweek lilisema hivi: “Wenye mamlaka hawajui la kufanya kwa sababu ya kuenea sana kwa ulanguzi na matumizi ya dawa mbalimbali za kulevya. Hawana pesa—wala habari—za kupambana na ulanguzi na matumizi ya dawa hizo za kulevya.” Gazeti la The Star la Johannesburg, Afrika Kusini, lilisema kwamba takwimu za serikali zinaonyesha kwamba “mkazi mmoja kati ya kila wakazi wanne wa Afrika Kusini ni mraibu wa pombe au wa dawa za kulevya.”

      Taasisi ya UM ya Utafiti wa Maendeleo ya Kijamii ilisema kwamba “watengenezaji na walanguzi wa dawa za kulevya . . . wametapakaa ulimwenguni pote nao hurundika katika mabenki pesa nyingi wanazopata kutokana na biashara ya dawa hizo. Wao huchagua mabenki yanayotoa huduma za siri ambayo hulipa faida kubwa sana. . . . Hivi sasa walanguzi wa dawa za kulevya wanaweza kuhalalisha pesa wanazopata kwa njia haramu kwa kuhamisha pesa hizo kwenye mabenki mengineyo ulimwenguni kupitia mifumo ya kompyuta bila kudhibitiwa na serikali.”

      Yamkini Wamarekani wengi hugusa kokeini kila siku pasipo kujua. Makala moja katika gazeti Discover ilieleza kwamba noti nyingi za mabenki ya Marekani zina madoa ya kokeini.

      Ukweli ni kwamba watu wengi wanakubali na hata wanaona utumizi wa dawa za kitiba na hata dawa haramu za kulevya kuwa jambo la kawaida tu. Tuzingatiapo athari zinazotangazwa kote za dawa haramu za kulevya, sigareti na pombe, swali lifaalo ni, Kwa nini watu hutumia dawa za kulevya? Tunapotafakari swali hilo, inafaa pia kuchunguza maoni yetu wenyewe kuhusu dawa hizo za kulevya.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ulevi ulifafanuliwa kuwa ‘kunywa chupa tano au zaidi za pombe kwa wanaume, na chupa nne au zaidi kwa wanawake.’

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Sherehe za ulevi ni tatizo kubwa sana katika vyuo vingi

      [Picha katika ukurasa wa 5]

      Watu wengi hudhani sigareti na dawa za kulevya “za kujiburudisha” hazina madhara

  • Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001 | Julai 8
    • Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?

      “NILIPOKUWA na umri wa miaka 13, dada ya rafiki yangu mkubwa alitualika nyumbani kwao jioni moja. Kila mtu akaanza kuvuta bangi. Mwanzoni, nilikataa, lakini mwishowe nilionja baada ya kusihiwa mara kadhaa nijaribu.” Hivyo ndivyo, Michael, kutoka Afrika Kusini alivyosimulia jinsi alivyoanza kutumia dawa za kulevya.

      “Familia yetu ilizingatia mno desturi za kale. Tulipenda kucheza muziki bora wa kale. Nilikuwa mshiriki wa bendi moja ya muziki, na mwanamuziki fulani alizoea kuvuta bangi wakati wa mapumziko. Alinisihi sana kwa miezi mingi nijaribu kuvuta bangi. Hatimaye, nilijaribu halafu nikaanza kuivuta kwa ukawaida.” Hivyo ndivyo Darren, mkazi wa Kanada, alivyoanza kutumia dawa za kulevya.

      Watu hao wawili walianza kutumia dawa nyingine za kulevya, kama vile LSD, kasumba, na dawa zinazochochea utendaji wa mwili. Waliacha kutumia dawa hizo, lakini wanapokumbuka mambo yaliyotukia, wanakubali kwamba walianza kutumia dawa za kulevya kwa sababu ya msongo wa marafiki. Michael asema hivi: “Sikudhani kamwe kwamba ningeanza kutumia dawa za kulevya, lakini sikuwa na marafiki wengine ila hao, na ni jambo la kawaida tu kwa mtu kuiga marafiki wake.”

      Vitumbuizo

      Msongo wa marafiki ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wengi waanze kutumia dawa za kulevya, hasa vijana. Isitoshe, wanaiga watumbuizaji ambao huvutia mashabiki wao wachanga na kuathiri maoni na mwenendo wao.

      Dawa za kulevya hutumiwa sana katika vitumbuizo. Mara nyingi wanamuziki maarufu hutumia dawa kali za kulevya pindi fulani-fulani. Waigizaji wengi maarufu wa sinema ni waraibu wa dawa za kulevya.

      Watumbuizaji wanaweza kutukuza na kusifu sana dawa za kulevya kiasi cha kwamba vijana wanashawishiwa kuzitumia. Gazeti la Newsweek liliripoti hivi mnamo mwaka wa 1996: “Barabara za Seattle zimejaa vijana wanaokuja kutumia heroini, eti kwa sababu Cobain [mwimbaji wa muziki wa roki] alitumia heroini.”

      Utumizi wa dawa za kulevya unatukuzwa na magazeti, sinema, na televisheni. Wabuni maarufu wa mitindo ya mavazi hupendelea wanamitindo walio wembamba, na dhaifu kama waraibu wa dawa za kulevya.

      Kwa Nini Watu Fulani Huanza Kutumia Dawa za Kulevya?

      Kuna sababu nyingi zinazochangia ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya. Baadhi ya sababu hizo ni kutamauka sana, kushuka moyo, na kukosa kusudi maishani. Matatizo ya kifedha, ukosefu wa kazi, na mifano mibaya ya wazazi huchangia pia tatizo hilo.

      Watu fulani wanaoshindwa kushughulika na wengine hutumia dawa za kulevya ili kukabiliana na hali hiyo. Wanaamini kwamba dawa za kulevya huwasaidia kuwa na ujasiri, zinawafanya wawe wacheshi na wahisi wanapendwa. Wengine huona ni rahisi kutumia dawa za kulevya badala ya kujifunza jinsi ya kukabiliana na maisha.

      Pia vijana hutumia dawa za kulevya kwa sababu hawana la kufanya. Kitabu The Romance of Risk—Why Teenagers Do the Things They Do chasema hivi kuhusu kutokuwa na la kufanya na kutopata mwelekezo wa wazazi: “Wavulana na wasichana wanaporejea kutoka shuleni hawamkuti yeyote nyumbani. Ndiyo sababu wanahisi upweke na hawataki kuwa peke yao. Wanatembelewa na marafiki lakini bado wanahisi uchoshi wakiwa pamoja. Wanatazama televisheni na video za muziki kwa muda mrefu au kutafuta mambo yenye kusisimua kwenye Internet. Muda si muda, huenda wakaanza kuvuta sigareti, kutumia dawa za kulevya na kunywa pombe.”

      Michael, aliyetajwa awali, alisema kuwa yeye hakupata mwelekezo wa wazazi wake nyumbani: “Familia yetu ilikuwa na furaha. Tulikuwa na uhusiano wa karibu sana. Hata hivyo, wazazi wangu walifanya kazi ya kuajiriwa na sikuwaona mchana kutwa. Isitoshe, wazazi wetu walitupatia uhuru mkubwa sana. Hawakutuadhibu. Wazazi wangu hawakujua kamwe kwamba nilikuwa nikitumia dawa za kulevya.”

      Mara tu baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya, vijana wengi huendelea kuzitumia kwa sababu moja tu: Wanafurahia kufanya hivyo. Michael, aliyetumia dawa za kulevya kila siku, alitaja athari zake: “Nilipumbaa akili. Niliweza kusahau mikazo yoyote niliyokuwa nayo. Sikuhofu kamwe. Hali ilionekana kuwa sawa kabisa.”

      Dick, mwenyeji wa Afrika Kusini, aliyetumia dawa za kulevya awali asema jinsi bangi ilivyomwathiri tangu alipoanza kuivuta akiwa na umri wa miaka 13: “Nilicheka ovyoovyo. Kila jambo lilinichekesha.”

      Yaonekana vijana hata hawatishwi na maonyo yanayotolewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya. Wao hudhani kwamba ‘hawawezi kupatwa na madhara hayo.’ Kitabu Talking With Your Teenager chaeleza kwa nini vijana hupuuza maonyo kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa afya: “Wana afya nzuri na nguvu nyingi hivi kwamba wanafikiri afya yao haiwezi kuathiriwa. Kwa kawaida vijana wengi wanaobalehe hudhani kwamba hawawezi ‘kuumizwa.’ Matineja huona kansa ya mapafu, ulevi, uraibu wa dawa kali za kulevya, kuwa mambo yanayowapata watu wenye umri mkubwa, na hayawezi kuwapata.” Kwa kweli wengi hawajui hatari zilizopo, kama inavyothibitishwa na idadi inayoongezeka ya vijana wanaotumia dawa ya kulevya iitwayo ecstasy. Ecstasy ni nini?

      Dawa ya Kulevya ya Ecstasy na Dansi za Usiku Kucha

      Dawa ya kulevya ya MDMA inayotokana na kemikali ya amphetamine, hutumiwa sana kwenye tafrija za dansi za usiku kucha zinazoitwa kwa Kiingereza rave. Dawa hiyo huitwa ecstasy. Wauzaji wa dawa hiyo husema kwamba dawa ya kulevya ya ecstasy ni salama na humsisimua mtu na kumtia nguvu zaidi ili acheze dansi usiku kucha. Dawa hiyo huwasaidia wachezaji-dansi waendelee kucheza dansi kwa saa nyingi sana hadi wanapofikia ile hali iliyotajwa na mwandishi mmoja kuwa ‘hali ya kupumbaa kiakili’ au kuwa hoi kabisa. Kijana mmoja alisema kile kinachofanya ecstasy ivutie: ‘Msisimuko huanza miguuni, moyo wako hupiga-piga kasi, halijoto ya mwili wako hupanda na msukumo wa damu kuongezeka.’

      Uchunguzi wa ubongo wa watumiaji wa ecstasy umethibitisha kwamba dawa hiyo ni hatari sana tofauti na madai ya wauzaji. Kwa wazi, ecstasy huharibu nyuzi za neva ubongoni na kupunguza vipimo vya homoni ya serotonin. Yaelekea madhara hayo ni ya kudumu. Baada ya muda, hilo laweza kusababisha matatizo kama vile kushuka moyo na kuzorota kwa kumbukumbu. Imeripotiwa kwamba baadhi ya watumiaji wa ecstasy wamekufa. Na walanguzi kadhaa wa dawa za kulevya huchanganya ecstasy na heroini ili kuwafanya wateja wao wawe waraibu.

      Je, Ni Rahisi Kupata Dawa za Kulevya?

      Bei ya dawa za kulevya imeshuka katika nchi nyingi kwa sababu idadi ya wauzaji imeongezeka. Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yamechangia hali hiyo. Mfano mmoja ni nchi ya Afrika Kusini. Mabadiliko ya kisiasa nchini humo yameboresha biashara na mawasiliano kati yake na nchi nyingine. Mbali na hayo, kutokuwapo kwa sheria kali za kuzuia watu kuvuka mipaka kumesitawisha biashara ya dawa za kulevya. Maelfu ya watu hutegemea ulanguzi haramu wa dawa za kulevya ili kupata riziki kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa kazi ya kuajiriwa. Kwa kawaida uhalifu wenye jeuri unahusiana sana na biashara ya dawa za kulevya. Gazeti moja liliripoti kwamba watoto wa shule katika jimbo la Gauteng, Afrika Kusini—baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 13 tu—wanapelelezwa na polisi kwa sababu ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Shule kadhaa katika jimbo hilo zimekuwa zikiwapima wanafunzi kuona iwapo wanatumia dawa za kulevya.

      Ni Nini Kiini cha Tatizo Hilo?

      Bila shaka kuna sababu nyingi zinazowafanya watu watumie dawa za kulevya. Lakini sababu hizo zote ni dalili tu za kiini cha tatizo hilo. Mwandishi Ben Whitaker alitaja kiini hicho aliposema hivi: “Kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya leo ni ishara hatari ya kwamba jamii yetu ina kasoro, licha ya kwamba watu ni wapweke na wamevunjika moyo. Ikiwa hilo si kweli, kwa nini watu wengi wenye vipawa na fursa nzuri maishani watumie dawa za kulevya badala ya kukabiliana na maisha ya leo?”

      Hilo ni swali lenye kuchochea fikira sana, linalotusaidia tuelewe kwamba jamii yetu inayokazia mno ufuatiaji wa mali na umashuhuri, imeshindwa kutimiza mahitaji yetu ya kihisia-moyo na ya kiroho. Hata dini nyingi hazijafaulu kutimiza mahitaji hayo kwa sababu zimepuuza kiini cha matatizo ya wanadamu.

      Ni lazima tutambue na kukabiliana na kiini kabla hatujapata suluhisho la kudumu kwa tatizo la dawa za kulevya. Habari hiyo itazungumziwa kwenye makala inayofuata.

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Nyakati nyingine watu mashuhuri hutukuza matumizi ya dawa za kulevya

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Muziki wa kisasa unakazia sana matumizi ya dawa za kulevya

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Dawa ya kulevya ya “ecstasy” hupatikana sana kwenye dansi za usiku kucha

      [Hisani]

      AP Photo/Greg Smith

      Gerald Nino/U.S. Customs

  • Matumizi ya Dawa za Kulevya Yatakomeshwa!
    Amkeni!—2001 | Julai 8
    • Matumizi ya Dawa za Kulevya Yatakomeshwa!

      “KOKEINI Nyingi Haramu Yapatikana Katika Chupa za Divai.” Makala moja ya gazeti iliyozungumzia kichwa hicho ilieleza jinsi polisi huko Johannesburg, Afrika Kusini, walivyopata kasha kubwa lenye chupa 11,600 za divai ya kutoka Amerika Kusini. Divai hiyo ilikuwa imechanganywa na kilogramu 150 hadi 180 za kokeini. Yaaminika kuwa hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha kokeini kuwahi kuingizwa nchini humo.

      Ijapokuwa huenda ugunduzi huo ukaonyesha kwamba pambano dhidi ya dawa za kulevya linafaulu, ukweli ni kwamba polisi hupata asilimia 10 hadi 15 tu ya dawa haramu za kulevya ulimwenguni. Hilo linasikitisha kwa sababu ni sawa na mkulima anayekata majani machache ya gugu hatari linalomea haraka, na kuacha mizizi yake ardhini.

      Jitihada za serikali za kukomesha utengenezaji na uuzaji wa dawa za kulevya huzuiwa na faida kubwa inayotokana na uuzaji wa dawa hizo. Inakadiriwa kwamba dawa za kulevya zenye thamani ya mabilioni ya dola zinauzwa na kununuliwa kila mwaka nchini Marekani peke yake. Kwa sababu ya pesa nyingi zinazohusika, si ajabu kwamba polisi na maofisa wa serikali, hata wale wenye vyeo vya juu, kutumbukia katika ufisadi.

      Alex Bellos wa gazeti la The Guardian Weekly aliripoti kutoka Brazili kwamba uchunguzi mmoja wa bunge ulionyesha kwamba, “wabunge watatu, wasaidizi 12 wa serikali, na mameya watatu walitajwa . . . kwenye orodha yenye zaidi ya watu 800 ambao wanashukiwa kuhusika na uhalifu wa magenge na ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Brazili.” Orodha hiyo ilikuwa pia na majina ya “maofisa wa polisi, wanasheria, wafanyabiashara na wakulima kutoka majimbo 17 kati ya majimbo 27 nchini humo.” Profesa mmoja wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha Brasília alisema hivi: “Matokeo hayo yanaonyesha hali ya ujumla ya jamii nchini Brazili.” Ndivyo ilivyo katika jamii nyingi zinazokumbwa na matatizo makubwa ya dawa za kulevya. Sheria za uuzaji na ununuzi wa dawa za kulevya ndiyo inayoendeleza tatizo hilo.

      Baadhi ya watu huteta ili dawa fulani za kulevya zihalalishwe kwa sababu wanajua kwamba vizuizi vya kisheria haviwezi kudhibiti dawa hizo. Kwa ujumla wanataka watu mmoja-mmoja waruhusiwe kuwa na kiasi kidogo cha dawa hizo kwa matumizi ya kibinafsi. Wanahisi kwamba hatua hiyo itasaidia serikali kudhibiti dawa hizo kwa urahisi na itapunguza faida kubwa za wafanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya.

      Wengine Hufaulu

      Mwanzoni huenda kumsaidia mraibu kuacha kutumia dawa za kulevya kukaboresha afya yake. Lakini inasikitisha kwamba mara tu mraibu arejeapo nyumbani, kuna uwezekano mkubwa wa kwamba huenda akashawishiwa kuanza tena kutumia dawa za kulevya. Mwandishi Luigi Zoja aeleza sababu: “Kumsaidia mgonjwa kuacha zoea fulani ni kazi bure iwapo hatasaidiwa kubadili kabisa njia yake ya kufikiri.”

      Darren, aliyetajwa katika makala inayotangulia, alisitawisha ‘njia mpya ya kufikiri’ iliyobadili maisha yake. Aeleza hivi: “Mimi sikuamini kwamba Mungu yuko, lakini baada ya muda, niling’amua kwamba ni sharti Mungu awepo. Wakati huo nilikuwa mraibu wa dawa za kulevya. Kwa muda wa miezi miwili au mitatu, nilijaribu kuacha kutumia dawa za kulevya, lakini marafiki wangu hawakuniruhusu kuacha. Ingawa niliendelea kutumia dawa za kulevya, nilianza kusoma Biblia kwa ukawaida kabla ya kulala. Sikushirikiana na marafiki wangu mara nyingi. Jioni moja mimi na yule niliyeishi naye tulikuwa tumelewa kabisa baada ya kutumia dawa za kulevya. Nilimweleza kuhusu Biblia. Asubuhi iliyofuata alimpigia simu nduguye, ambaye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alituelekeza kwa Shahidi mmoja aliyeishi katika jiji letu, nami nikaenda kumwona.

      “Tulizungumza hadi saa 5:00 usiku, akanipa vichapo 12 hivi vya kujifunzia Biblia. Nilianza kujifunza naye Biblia na nikaacha kutumia dawa za kulevya na kuvuta sigareti. Miezi tisa hivi baadaye, nilibatizwa na kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.”

      Kuacha uraibu wa dawa za kulevya si rahisi. Michael, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, afunua matatizo aliyopata alipoacha dawa za kulevya baada ya kuzitumia kwa miaka 11: “Nilikonda kwa sababu ya kushindwa kabisa kula. Nilihisi maumivu makali kana kwamba ninadungwa na sindano, nilitoka jasho, na kuona mazingaombwe. Nilitamani sana dawa za kulevya, lakini kumkaribia Yehova kupitia sala na kujifunza Biblia kulinisaidia kuacha kabisa dawa za kulevya.” Watu hao waliokuwa wakitumia dawa za kulevya hapo awali wanakubali kwamba ilikuwa muhimu kwao kuachana kabisa na washiriki wao wa kale.

      Kwa Sababu Gani Jitihada za Wanadamu Hazifaulu

      Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni mojawapo tu ya matatizo makubwa yanayokumba ulimwengu. Hali mbaya sana ya uovu, jeuri, na ukatili imeenea kotekote ulimwenguni. Biblia yasema hivi: “Ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu.” (1 Yohana 5:19) Huyo “mwovu” anatajwa na mtume Yohana kwenye Ufunuo 12:9: “Kwa hiyo likavurumishwa chini hilo joka kubwa mno, nyoka wa awali, yeye aitwaye Ibilisi na Shetani, anayeiongoza vibaya dunia nzima inayokaliwa; akavurumishwa chini kwenye dunia, na malaika zake wakavurumishwa chini pamoja naye.”

      Mbali na udhaifu wake, mwanadamu amelazimika kukabiliana na adui huyu mwenye nguvu. Shetani ndiye aliyemfanya mwanadamu atumbukie katika dhambi hapo mwanzoni. Ameazimia kuwatumbukiza wanadamu kwenye uovu zaidi na kuwashawishi wamwache Mungu. Yaonekana kwamba hali ya wanadamu ya kutumia dawa za kulevya ni mojawapo ya mbinu anazotumia. Ana hasira kali sana kwa sababu anajua kwamba “ana kipindi kifupi cha wakati.”—Ufunuo 12:12.

      Mungu Atatatuaje Tatizo Hilo?

      Biblia inasema jinsi Muumba alivyoandaa kwa upendo njia ya kuwakomboa wanadamu kutoka kwa dhambi. Twasoma hivi kwenye 1 Wakorintho 15:22: “Kama vile katika Adamu wote wanakufa, ndivyo pia katika Kristo wote watafanywa kuwa hai.” Yesu alijitolea kuja duniani akiwa mwanadamu mkamilifu kisha akadhabihu uhai wake wa kidunia ili kuwakomboa wanadamu kutokana na matokeo ya dhambi na kifo.

      Watu wengi wamepata kichocheo na ujasiri wa kuacha uraibu wa dawa za kulevya baada ya kujua kisababishi cha kifo na kujua suluhisho la matatizo yanayowakumba wanadamu. Lakini Biblia huandaa msaada zaidi mbali na kutusaidia kibinafsi kupambana na tatizo la dawa za kulevya sasa. Biblia husema juu ya wakati ambapo matatizo yote ulimwenguni yatakoma kabisa, kutia ndani matumizi ya dawa za kulevya. Wakati huo uvutano wa Shetani utakuwa umekomeshwa kabisa.

      Kitabu cha Ufunuo chaeleza kuhusu “mto wa maji ya uhai, mwangavu kama fuwele, ukitiririka kutoka katika kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-kondoo.” (Ufunuo 22:1) Mto huo wa mfano hufananisha maandalizi ya Mungu kupitia Yesu Kristo ya kuwarejeshea wanadamu uhai mkamilifu kwenye paradiso duniani. Kitabu cha Ufunuo hueleza kuhusu miti ya uhai inayositawi kando ya mto huo, halafu chasema hivi: “Majani ya hiyo miti yalikuwa ya kuponya mataifa.” (Ufunuo 22:2) Majani hayo ya mfano hufananisha maandalizi ya Yehova ya kuponya na kuwarejeshea wanadamu ukamilifu wa kiroho na wa kimwili.

      Hatimaye, wanadamu watakuwa huru, si tu kutokana na dawa za kulevya bali pia kutokana na matatizo mengine yanayowakumba katika mfumo huu mwovu!

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      Je, Bangi Inadhuru?

      Nchi kadhaa zinafikiria kuhalalisha bangi, hasa kwa ajili ya matibabu. Uchunguzi umeonyesha kwamba dawa hiyo ya kulevya inaondoa kichefuchefu kinachosababishwa na matibabu ya kemikali, na yaonekana kwamba inawasaidia wagonjwa wenye UKIMWI kuwa na hamu ya kula. Imetumiwa pia kutuliza maumivu.

      Ijapokuwa kuna ubishi kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, majaribio yaliyoripotiwa kwenye gazeti la New Scientist yamethibitisha baadhi ya madhara ya bangi.

      Chuo Kikuu cha Harvard kilifanya majaribio ya kulinganisha kikundi kimoja cha watu waliovuta bangi kila siku na kikundi kingine cha watu wasiovuta bangi kwa ukawaida. Uchunguzi wa kawaida wa akili ulionyesha kwamba hawakutofautiana sana kiakili. Hata hivyo, jaribio moja lililobainisha uwezo wa kukabiliana na hali mpya, lilionyesha kwamba wavutaji sugu wa bangi walikuwa na uwezo mdogo sana wa kukabiliana na hali mpya.

      Kwa muda wa miaka 15, chuo kingine kikuu kilichunguza kikundi cha watu waliovuta bangi kwa ukawaida na kikundi cha watu waliovuta sigareti. Kwa kawaida wavutaji wa bangi walivuta misokoto mitatu au minne ya bangi kwa siku, ilhali wavutaji wa sigareti walivuta sigareti 20 au zaidi kwa siku. Watu kadhaa kutoka vikundi vyote viwili waliugua ugonjwa wa mkamba na kukohoa. Uchunguzi wa mapafu yao ulifunua kwamba chembe za mapafu ya watu wa vikundi vyote viwili zilikuwa zimeharibika.

      Ijapokuwa wavutaji wa bangi waliitumia mara chache, uchunguzi ulionyesha kwamba msokoto mmoja wa bangi ulikuwa na kiasi cha lami kinachozidi kile cha sigareti kwa mara tatu. Isitoshe, gazeti New Scientist liliripoti hivi: “Wavutaji wa bangi huvuta moshi mwingi sana kwa muda mrefu zaidi.”

      Zaidi ya hayo, uchunguzi huo ulionyesha kwamba uwezo wa chembe za kinga za mapafu ya wavutaji wa bangi wa kupambana na viini vya magonjwa, ulipungua kwa asilimia 35 uwezo wa chembe za kinga za wavutaji wa sigareti.

      [Hisani]

      U.S. Navy photo

      [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      “Lawama Mbaya” kwa Wazazi

      Safu ya mhariri katika gazeti la Afrika Kusini la Saturday Star ilionyesha wasiwasi uliopo kwa sababu ya idadi kubwa sana ya vijana wanaotumia dawa za kulevya nchini Afrika Kusini. Ilisema hivi:

      “Watoto wetu wanapotumia dawa za kulevya kwa kawaida jambo hilo linaelekeza lawama mbaya kwetu wazazi na kwa jamii kwa ujumla. Siku baada ya siku, tunajitahidi kutafuta pesa, na kujitoa mhanga kutafuta mali. Watoto wetu wanatuchosha kiakili na kimwili. Je, sisi hupata wakati wa kufanya nao mambo yanayonufaisha? Ni rahisi kwetu kuwapa pesa ili waache kutusumbua. Kuwapa pesa ni rahisi kuliko kuwasikiliza—kujua matatizo yao, matumaini yao, na mahangaiko yao. Leo usiku, tunapoketi mkahawani au tunapotazama televisheni, je, kweli tunajua mambo wanayofanya?”

      Au huenda tukauliza, je, tunajua wanachofikiria?

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Wengi wamechochewa kuacha kabisa dawa za kulevya

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki