Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuufanya Ulimwengu Uwe na Uraibu wa Dawa za Kulevya
    Amkeni!—1999 | Novemba 8
    • Kuufanya Ulimwengu Uwe na Uraibu wa Dawa za Kulevya

      NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA

      MTOTO mchanga aliyezaliwa hivi karibuni alia kwa sauti kubwa katika hospitali moja huko Madrid, Hispania. Muuguzi mmoja ajaribu kumtuliza kwa juhudi lakini bila mafanikio. Mtoto huyo anateseka kwa sababu ya kuacha kupewa heroini. Jambo lililo baya hata zaidi ni kwamba ana virusi vya HIV. Mama yake alikuwa mraibu wa heroini.

      Mama mmoja huko Los Angeles aendesha gari lake bila kujua kwenye barabara inayodhibitiwa na genge linalouza dawa za kulevya. Arushiwa risasi mfululizo, ambazo zamwua binti yake mchanga.

      Maelfu ya kilometa mbali na huko, katika Afghanistan, mkulima mmoja alima shamba la mmea unaotumika kutengenezea kasumba. Umekuwa mwaka wenye mazao; uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 25. Mimea hiyo ya kasumba ina faida nyingi na familia ya mkulima huyo inajitahidi kujikimu. Lakini mimea hiyo mizuri itatumiwa kutengenezea heroini, na heroini huharibu maisha.

      Msichana mmoja mwenye haya huko Sydney, Australia, huenda kwenye disko kila Jumamosi usiku. Alikuwa akiona ugumu wa kuchangamana na umati, lakini hivi karibuni, tembe inayoitwa ecstasy imempa uhakika. Tembe anazotumia ziliingizwa Australia kwa njia ya magendo kutoka Uholanzi, ijapokuwa maabara za huko pia zimeanza kuzigawanya. Tembe ya ecstasy hufanya muziki uvutie zaidi, na kumfanya ashindwe kujizuia. Hata huhisi akiwa na sura nzuri zaidi.

      Kwa upande wa Manuel, mkulima hodari ambaye hupata riziki kwa taabu kutoka kwenye shamba lake dogo huko Andes, maisha yalikuwa afadhali alipoanza kulima koka. Manuel angependa kuacha kuvuna zao hilo, lakini anaogopa kwamba jambo hilo litawakasirisha wanaume wakatili wanaodhibiti uzalishaji wa koka katika eneo lake.

      Hawa ni baadhi ya watu wachache tu walioathiriwa na dawa za kulevya ambazo zinaharibu sayari yetu.a Iwe watu hawa ni wanunuzi, wazalishaji, au watu wasiojihusisha na wasiokuwa na hatia, dawa za kulevya zinadhibiti maisha yao daima.

      Tatizo la Dawa za Kulevya ni Kubwa Kadiri Gani?

      Katibu Mkuu wa UM Kofi Annan asema hivi: “Dawa za kulevya zinaharibu jamii zetu, zinaongeza uhalifu, zinaeneza maradhi kama vile UKIMWI, na kuua vijana wetu na kuharibu wakati wetu ujao.” Aongezea hivi: “Leo kuna watumiaji wa dawa za kulevya wanaokadiriwa kuwa milioni 190 ulimwenguni pote. Wako katika kila nchi. Na hakuna nchi yoyote kwa kujitegemea yenyewe, inayoweza kukomesha kwa mafanikio biashara ya dawa za kulevya katika mipaka yake. Biashara ya dawa za kulevya ambayo ni ya tufeni pote yahitaji itikio la kimataifa.”

      Jambo linalofanya hali iwe mbaya zaidi, ni kwamba katika miaka ya hivi majuzi, kumekuwako dawa za kulevyab za kubuniwa. Kemikali hizo za sanisia zimebuniwa kumfanya mtumiaji apumbae au ahisi furaha. Kwa kuwa dawa za kulevya za kubuniwa zinaweza kutengenezwa kwa bei rahisi karibu mahali popote, polisi hawana uwezo kabisa wa kuzidhibiti. Mnamo 1997, Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulika na Dawa za Kulevya ilionya kwamba katika nchi nyingi dawa hizi za kubuniwa zimekuwa sehemu ya “utamaduni wa watumiaji wengi” na kwamba zapasa kuonwa kuwa “tisho kubwa kwa jumuiya ya kimataifa katika karne ijayo.”

      Dawa za kulevya mpya zaidi ni zenye matokeo sawa na zile zilizotangulia. Kokeini iliyosafishwa hutokeza uraibu hata zaidi ya kokeini ya kawaida. Aina mpya za bangic zinatokeza njozi nyingi zaidi, na dawa mpya ya kulevya ya kubuniwa inayoitwa ice huenda ikawa miongoni mwa dawa zenye madhara makubwa zaidi.

      Pesa na Uwezo wa Dawa za Kulevya

      Ijapokuwa watumiaji wa dawa za kulevya huenda wakawa wachache, idadi yao inatosha kuwapa nguvu viongozi wa dawa za kulevya, watu wanaopanga uzalishaji na ugawaji wa dawa za kulevya. Watu hao wasio na maadili huendesha biashara ya ulaghai ambayo imekuwa yenye faida zaidi—na inakaribia kuwa biashara kubwa zaidi duniani. Biashara ya dawa za kulevya huenda sasa ikawa na mapato ya asilimia 8 ya biashara yote ya kimataifa, au takriban dola za Marekani 400,000,000,000 kila mwaka. Pesa zinazotokana na dawa za kulevya zinapozunguka ulimwenguni, zinatajirisha magenge, zinafisidi polisi, zinatumiwa kuhonga wanasiasa, na hata kulipia gharama za ugaidi.

      Je, jambo lolote laweza kufanywa ili kukomesha tatizo la dawa za kulevya? Biashara ya dawa za kulevya inaathiri kadiri gani mapato yako, usalama wako, na maisha ya watoto wako?

      [Maelezo ya Chini]

      a Katika makala haya, twarejezea dawa zinazotumiwa kwa makusudi yasiyo ya kitiba na ambazo zinagawanywa kwa njia haramu.

      b Dawa ya kulevya ambayo imefanyiwa marekebisho madogo katika muundo wake wa kemikali, mara nyingi hutokezwa ili kukwepa vizuizi vya dawa za kulevya haramu au dawa zenye kuleta njozi.

      c Sehemu za juu zilizokaushwa za mmea wa bangi ambazo hutokeza maua ndizo hutumiwa kutengenezea bangi. Utomvu wa mmea huohuo ni bangi. Bangi huvutwa na watumiaji wa dawa za kulevya.

      [Ramani katika ukurasa wa 4, 5]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      Uzalishaji na Ulanguzi wa Dawa za Kulevya Ulimwenguni Pote

      MAENEO MAKUU YA UZALISHAJI:

      Bangi

      Heroini

      Kokeini

      Alama hizo za mishale zaonyesha njia kuu zinazotumiwa kwa ulanguzi.

  • Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako
    Amkeni!—1999 | Novemba 8
    • Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako

      KAMA vile kuvu inayosababisha kuoza kwa mihimili ya nyumba, ndivyo dawa za kulevya ziwezavyo kudhoofisha muundo mzima wa jamii. Ili jamii ya kibinadamu itende kwa njia inayofaa, lazima iwe na familia zilizo imara, wafanyakazi wenye afya, serikali zinazoweza kutumainika, polisi wenye kufuatia haki, na raia wanaotii sheria. Dawa za kulevya hudhoofisha kila moja ya mambo hayo ya msingi.

      Sababu moja inayofanya serikali zipige marufuku dawa zisizotumiwa kwa matibabu ni madhara ya afya yanayowapata raia zake. Kila mwaka maelfu ya waraibu wa dawa za kulevya hufa kwa kutumia dawa kupita kiasi. Wengi zaidi hufa kwa UKIMWI. Kwa kweli, asilimia 22 ya watu walio na HIV ulimwenguni ni watumiaji wa dawa za kulevya waliojidunga sindano zilizokuwa zimeambukizwa. Akiwa na sababu halali, kwenye mkutano wa hivi majuzi wa Umoja wa Mataifa, Nasser Bin Hamad Al-Khalifa, wa kutoka Qatar, alionya kwamba “soko la dunia nzima linakaribia kuwa kaburi la ujumla la mamilioni ya wanadamu likiwa tokeo la biashara ya dawa za kulevya haramu.”

      Lakini haiathiri tu afya ya mtumiaji. Takriban asilimia 10 ya watoto wote wanaozaliwa Marekani wanakabili hatari ya dawa za kulevya haramu—katika visa vingi, kokeini—wanapokuwa wangali kwenye tumbo la uzazi. Tatizo wanalokabili si athari za kuacha peke yake, kwa kuwa hatari ya dawa za kulevya katika tumbo la uzazi yaweza kusababisha watoto wanaozaliwa wapatwe na matokeo mengine yenye kudhuru—ya kiakili na ya kimwili.

      Pesa Zinazopatikana kwa Urahisi Kupitia Dawa za Kulevya—Kishawishi Kisichozuilika

      Je, wewe huhisi ukiwa salama katika ujirani wako baada ya giza kuingia? Ikiwa sivyo, labda ni kwa sababu ya wauzaji wa dawa za kulevya. Uvamizi na jeuri ya mitaani inahusiana sana na dawa za kulevya. Mara nyingi watumiaji wa dawa za kulevya hugeukia uhalifu au ukahaba ili kuendeleza zoea lao, huku magenge yenye kushindana yakipigana na kuuana ili kudhibiti ugawaji wa dawa za kulevya. Kwa kueleweka, polisi katika miji mingi huona dawa za kulevya kuwa zinachangia visa vingi vya uuaji ambavyo wanachunguza.

      Katika mabara fulani, waasi wameona faida za kutumia nguvu ili kujinufaisha na biashara yenye faida ya mihadarati. Kikundi kimoja cha waasi huko Amerika Kusini sasa kinajipatia nusu ya mapato yake kwa kuwalinda walanguzi wa dawa za kulevya. “Mapato yanayotokana na dawa za kulevya haramu hutumiwa kuendeleza baadhi ya mapambano makali zaidi ulimwenguni ya kidini na ya kikabila,” laripoti Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Ulanguzi wa Dawa za Kulevya Ulimwenguni.

      Msiba Unaotokana na Athari za Dawa za Kulevya

      Watumiaji wa dawa za kulevya hufanya barabara zisiwe salama katika njia nyingine. “Kuendesha gari ukiwa chini ya uvutano wa bangi au LSD kwaweza kuwa hatari kama vile kuendesha ukiwa umekunywa kileo,” asema Michael Kronenwetter, katika kitabu chake Drugs in America. Haishangazi basi kwamba watumiaji wa dawa za kulevya wanaelekea kupatwa na aksidenti wakiwa kazini mara tatu au nne zaidi.

      Hata hivyo, labda nyumbani ndipo dawa za kulevya hutokeza madhara makubwa zaidi. “Maisha ya familia yenye kasoro na utumiaji wa dawa za kulevya mara nyingi huhusiana,” chasema kichapo World Drug Report. Wazazi wanaotatanishwa na tamaa ya kutumia dawa za kulevya huwaandalia watoto wao maisha imara kwa nadra sana. Kifungo kati ya mtoto mchanga na mzazi—kilicho cha maana sana katika majuma ya kwanza ya maisha ya mtoto—kinaweza kukatizwa. Kwa kuongezea, wazazi walio waraibu mara nyingi huwa na madeni na waweza kuibia marafiki wao na familia au waweza kupoteza kazi zao. Watoto wengi wanaokulia katika mazingira hayo hutoroka nyumbani na kwenda kuishi barabarani au hata huanza kutumia dawa za kulevya.

      Matumizi mabaya ya dawa za kulevya yanaweza kuongoza kwenye kutendwa vibaya kimwili—kwa mwenzi au watoto. Kokeini hasa inapochanganywa na kileo, inaweza kumfanya mtu ambaye kwa kawaida ni mtulivu akawa na tabia mwitu. Kulingana na uchunguzi wa Kanada uliofanyiwa watumiaji wa kokeini, asilimia 17 ya waliohojiwa walikiri kwamba walikuwa wachokozi baada ya kutumia dawa za kulevya. Hali kadhalika, ripoti moja kuhusu kutenda watoto vibaya huko New York City ilipiga hesabu na kupata kwamba asilimia 73 ya watoto waliopigwa hadi wakafa walikuwa na wazazi waliotumia vibaya dawa za kulevya.

      Ufisadi na Uchafu

      Ikiwa nyumba inaweza kudhoofishwa na ufisadi, hali kadhalika serikali zinaweza. Katika kisa hiki ni pesa za dawa za kulevya, badala ya dawa za kulevya zenyewe, ndizo hufisidi mfumo. “Dawa za kulevya zimefisidi maofisa wa serikali, polisi na jeshi,” akalalamika balozi mmoja kutoka nchi moja ya Amerika Kusini. Anaongezea kwamba pesa zinazopatikana ni “kishawishi kikubwa sana” kwa wale walio na tatizo la kujikimu.

      Nchi moja baada ya nyingine, mahakimu, mameya, polisi, na hata maofisa wa kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya wamenaswa katika hali ya ufisadi. Wanasiasa ambao huenda uchaguzi wao ulifanywa kwa kutumia pesa za viongozi wa ulanguzi wa dawa za kulevya hukataa wanapoombwa wachukue hatua kali za kinidhamu dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Maofisa wengi wenye kufuatia haki ambao wameunga mkono kwa ujasiri harakati dhidi ya dawa za kulevya wameuawa.

      Hata udongo wetu, misitu yetu, na aina mbalimbali za viumbe wanaoishi humo wanateseka kutokana na pigo la tufeni pote la dawa za kulevya. Asilimia kubwa ya uzalishaji wa afyuni na kokeini hufanywa katika maeneo mawili ambayo yanaweza kupatwa na madhara ya kimazingira kwa urahisi: misitu ya mvua ya magharibi mwa Amazon na ile ya Kusini-mashariki ya Asia. Uharibifu katika sehemu hizo umekuwa mkubwa. Hata jitihada zenye kusifika za kuondoa mimea ya dawa za kulevya haramu huleta madhara makubwa kwa sababu ya dawa zinazotumika kuua mimea.

      Ni Nani Hulipia Madhara Hayo?

      Ni nani hulipia madhara yote yanayoletwa na dawa za kulevya? Ni sisi sote. Naam, sote hulipia hasara ya uzalishaji, gharama za kitiba, mali zilizoibwa au kuharibiwa, na gharama ya kutekeleza sheria. Ripoti ya Wizara ya Kazi ya Marekani ilipiga hesabu na kupata kwamba “matumizi ya dawa za kulevya kazini yaweza kugharimu biashara na viwanda vya Marekani kati ya dola bilioni 75 hadi 100 kila mwaka . . . ikiwa ni hasara ya uzalishaji, aksidenti na gharama za juu za kitiba, na gharama za kulipa wafanyakazi ridhaa.”

      Hatimaye pesa hizo zote hulipwa na watu wanaotozwa kodi pamoja na wanunuzi. Uchunguzi uliofanywa Ujerumani katika mwaka wa 1995 ulipiga hesabu ya ujumla ya gharama ya mwaka mmoja ya dawa za kulevya katika nchi hiyo kuwa dola za Marekani 120 kwa kila raia. Huko Marekani, kadirio la tarakimu moja lilikuwa juu hata zaidi—dola za Marekani 300 kwa kila mtu.

      Hata hivyo, gharama iliyo kubwa hata zaidi ni madhara ya jamii ambayo huletwa na dawa za kulevya. Ni nani ambaye angetoa thamani ya fedha ya kuvunjika kwa familia nyingi namna hiyo, kutendwa vibaya kwa watoto wengi namna hiyo, ufisadi wa maofisa wengi kadiri hiyo, na vifo vya mapema vya watu wengi kadiri hiyo? Mambo hayo yote yanamaanisha nini kwa semi za kibinadamu? Makala yetu ifuatayo itachunguza jinsi dawa za kulevya huathiri maisha ya wale wanaozitumia.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      DAWA ZA KULEVYA NA UHALIFU

      DAWA ZA KULEVYA ZIMEHUSIANISHWA NA UHALIFU ANGALAU KWA NJIA NNE:

      1. Kuwa na dawa za kulevya bila idhini na ulanguzi wa dawa za kulevya ni makosa ya jinai karibu katika kila nchi ulimwenguni. Huko Marekani peke yake, polisi hukamata takriban watu milioni moja kila mwaka kwa mashtaka ya kuhusika na dawa za kulevya. Katika nchi nyingine mifumo ya kisheria ya kushughulika na uhalifu inalemewa na ongezeko la visa vya dawa za kulevya hivi kwamba polisi na mahakama haziwezi kuvishughulikia.

      2. Kwa kuwa dawa za kulevya ni ghali sana, mara nyingi waraibu hugeukia uhalifu ili kuendeleza zoea lao. Mraibu wa kokeini huenda akahitaji dola za Marekani 1,000 kila juma ili kulipia uraibu wake! Haishangazi kwamba visa vya kuvunja nyumba, uvamizi, na ukahaba huongezeka kwa ghafula dawa za kulevya zinapoanza kutumiwa kwa ukawaida katika jumuiya.

      3. Uhalifu mwingine hufanywa ili kuendeleza ulanguzi wa dawa za kulevya, mojawapo ya biashara zenye faida zaidi duniani. “Shirika la dawa za kulevya haramu na uhalifu uliopangwa hutegemeana,” chaeleza kichapo World Drug Report. Ili kusafirisha dawa za kulevya kutoka sehemu moja hadi nyingine bila matatizo, walanguzi hujaribu kuhonga au kuogopesha maofisa. Wengine hata wana majeshi yao ya kibinafsi. Faida kubwa ambazo viongozi wa dawa za kulevya hupata hutokeza matatizo pia. Kiasi kikubwa cha fedha wanazopata zingeweza kuwahatarisha ikiwa fedha hizo hazingebadilishwa ziwe halali, kwa hiyo mabenki na mawakili huajiriwa ili kuficha kubadilishwa kwa fedha hizo zinazotokana na dawa za kulevya.

      4. Matokeo yenyewe ya dawa za kulevya yaweza kuongoza kwenye uhalifu. Washiriki wa familia waweza kutendwa vibaya na watumiaji sugu wa dawa za kulevya. Katika nchi fulani za Afrika zilizokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, uhalifu wenye kuogofya umefanywa na askari matineja walioduwazwa na dawa za kulevya.

  • Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa
    Amkeni!—1999 | Novemba 8
    • Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa

      “DAWA za kulevya ni kama nyundo kubwa,” asema Dakt. Eric Nestler. Kwa kweli, kiasi kidogo cha kemikali hizo zilizo kama nyundo kubwa chaweza kufisha. “Kwa kielelezo, kokeini iliyosafishwa, imejulikana kuwa iliua watu mara ya kwanza walipoitumia,” chaeleza kitabu Drugs in America.

      Dawa mpya za sanisia zaweza kutokeza hatari kubwa hivyo. “Vijana wanaoweza kudanganywa kwa urahisi ambao hununua dawa za kulevya kwenye karamu za ‘rave’ hawawezi kuwa na habari yoyote kuhusu jambo ambalo mchanganyiko wa kemikali utafanyia ubongo wao,” chaonya kichapo World Drug Report cha Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kwa vijana wengi uraibu wa dawa za kulevya hutukia hatua kwa hatua, kama ionyeshwavyo na mifano ifuatayo.

      “Kukwepa Uhalisi wa Mambo”

      Pedro,a mmojawapo wa watoto tisa, alizaliwa katika ujirani wenye jeuri katika jiji la Córdoba, Hispania. Hali yake ya utotoni ilikuwa yenye kufadhaisha kwa sababu ya uraibu wa alkoholi wa baba yake. Pedro alipokuwa na umri wa miaka 14, binamu yake alimzoeza kuvuta bangi. Baada ya mwezi mmoja akawa mraibu.

      “Kutumia dawa za kulevya kulikuwa njia ya kupitisha wakati,” aeleza Pedro, “kukwepa uhalisi wa mambo, na njia moja ya kuwa mshiriki wa kikundi. Nilipokuwa na umri wa miaka 15, mbali na bangi nilianza kutumia LSD na amfetamini. Dawa ya kulevya niliyoipenda zaidi ilikuwa LSD, na ili kupata pesa za kuinunua, nikawa mwuzaji wa muda wa dawa za kulevya. Nililangua hasa bangi. Wakati mmoja, baada ya kutumia LSD kupita kiasi, sikuweza kulala usiku kucha, na nilihisi kana kwamba nilikuwa nimerukwa na akili. Jambo hilo liliniogofya. Nilihisi kwamba nikiendelea kutumia dawa za kulevya, ningeishia ama jela ama ningekufa. Lakini tamaa ya dawa za kulevya ilinifanya nipuuze hofu hiyo. Nikawa mraibu mkubwa sana wa LSD na kuhitaji dawa hiyo ya kulevya zaidi ili niwe katika hali ya kupumbaa. Licha ya matokeo yenye kuogopesha, sikuweza kuacha. Sikujua jinsi ya kuepuka hali hiyo.

      “LSD haikuwa bei rahisi, kwa hiyo nilijifunza kuiba kwenye maduka ya kuuza vito, kuwanyang’anya watalii mikoba, na kuibia wapita njia saa na vibeti. Nilipofikia umri wa miaka 17, nilikuwa nimejiimarisha nikiwa muuzaji wa dawa za kulevya katika mji wa kwetu, na nyakati nyingine nilishiriki unyang’anyi wa kutumia silaha. Kwa sababu ya sifa ya kuwa mhalifu mwenye tabia mwitu katika ujirani wangu, nilipewa jina la utani el torcido, linalomaanisha ‘aliyepotoka.’

      “Unapochanganya dawa za kulevya na vileo, utu wako hubadilika, mara nyingi unakuwa na tabia mwitu. Na tamaa ya kupata dawa za kulevya zaidi ni kubwa sana hivi kwamba inashinda kabisa dhamiri yako. Maisha yanakuwa na mabadiliko ya ghafula, na unaishi kwa kuduwazwa na dawa za kulevya.”

      “Kujihusisha Sana na Dawa za Kulevya”

      Ana mke wa Pedro, alikulia Hispania katika mazingira mazuri ya familia. Alipokuwa na umri wa miaka 14, Ana alikutana na wavulana wachache kutoka shule iliyokuwa karibu ambao walivuta bangi. Mwanzoni alichukizwa na tabia yao ya kiajabu-ajabu. Lakini Rosa mmojawapo wa marafiki wasichana wa Ana, alivutiwa na mmoja wa wavulana hao. Alimsadikisha Rosa kwamba kuvuta bangi hakungemdhuru na kwamba angefurahia kufanya hivyo. Kwa hiyo, Rosa alijaribu dawa hiyo ya kulevya na kumpa Ana.

      “Ilinifanya nihisi vizuri, na baada ya majuma machache, nilikuwa nikivuta bangi kila siku,” asema Ana. “Baada ya mwezi mmoja hivi, bangi haikuniduwaza tena, kwa hiyo nikaanza kutumia amfetamini pamoja na kuvuta bangi.

      “Punde si punde mimi na rafiki zangu tulikuwa tumejihusisha kabisa na dawa za kulevya. Tungezungumza kuhusu ni nani ambaye angetumia dawa za kulevya nyingi zaidi bila kupatwa na madhara yoyote na aliyelewa zaidi. Hatua kwa hatua, nilijitenga na watu kwa ujumla, na kwenda shuleni kwa nadra sana. Sikutosheka na bangi na amfetamini tena, kwa hiyo nilianza kujidunga sindano za dawa iliyotengenezwa kwa afyuni niliyoipata katika maduka mbalimbali ya kuuzia dawa. Wakati wa kiangazi tungeenda kwenye maonyesho ya roki, mahali ambapo ilikuwa rahisi daima kupata dawa za kulevya kama vile LSD.

      “Siku moja mama alinishika nikivuta bangi. Wazazi wangu walifanya jitihada zote walizoweza ili kunilinda. Waliniambia kuhusu hatari za dawa za kulevya, na wakanihakikishia upendo na hangaiko lao. Lakini niliona jitihada zao kuwa zinaingilia maisha yangu isivyofaa. Nilipokuwa na umri wa miaka 16 niliamua kutoroka nyumbani. Nilijiunga na kikundi fulani cha vijana waliosafiri Hispania kote wakiuza mikufu ya kujitengenezea na kutumia dawa za kulevya. Miezi miwili baada ya hapo, nilikamatwa na polisi huko Málaga.

      “Polisi waliponipeleka kwa wazazi wangu, walinipokea kwa moyo mkunjufu, na nikaaibika kwa yale niliyokuwa nimefanya. Baba yangu alikuwa akilia—jambo ambalo sikuwa nimewahi kuliona. Nilijuta kuumiza hisia zao, lakini majuto hayo hayakuwa makubwa vya kutosha kunifanya niache kutumia dawa za kulevya. Niliendelea kutumia dawa za kulevya kila siku. Nilipokuwa sijalewa, nyakati nyingine nilifikiri juu ya hatari hizo—lakini si kwa muda mrefu.”

      Kutoka Kuwa Mwashi Hadi Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya

      José, mwanamume mwenye familia na mwenye urafiki, alilangua dawa za kulevya kutoka Morocco hadi Hispania kwa muda wa miaka mitano. Alipata kujihusishaje? “Nilipokuwa nikifanya kazi ya uashi, mfanyakazi mwenzi alianza kulangua dawa za kulevya,” aeleza José. “Kwa kuwa nilihitaji pesa, nilijiambia ‘Kwa nini nisifanye kazi hiyo?’

      “Ilikuwa rahisi kununua bangi huko Morocco—nyingi kadiri ambavyo ningeweza. Nilikuwa na mashua ya kasi ambayo ingeweza kukwepa polisi kwa urahisi. Baada ya kusafirisha dawa za kulevya hadi Hispania, niliziuza kwa kiasi kikubwa, takriban kilogramu 600 kwa wakati mmoja. Nilikuwa na wateja watatu au wanne tu, na walichukua dawa zote za kulevya nilizoweza kuwaletea. Ijapokuwa polisi walifanya upelelezi, dawa hizo za kulevya hazikugunduliwa. Sisi walanguzi wa dawa za kulevya tulikuwa na vifaa bora zaidi kuliko polisi.

      “Nilipata pesa nyingi sana kwa urahisi. Safari moja kutoka Hispania hadi Afrika Kaskazini ingeweza kuleta pesa zipatazo dola za Marekani 25,000 hadi 30,000. Punde si punde, nilikuwa na wanaume 30 wa kunifanyia kazi. Sikuwahi kukamatwa kwa sababu nilimlipa mtoa habari mmoja ili kunishauri nilipokuwa ninasakwa.

      “Nyakati fulani nilifikiri kuhusu mambo ambayo dawa hizi za kulevya zingeweza kuwafanyia wengine, lakini nilijifariji kwamba bangi ni dawa ya kulevya ambayo si kali na isiyoua mtu yeyote. Kwa kuwa nilikuwa nikipata pesa nyingi, sikufikiri sana juu ya hilo. Mimi mwenyewe sikuwa nikitumia dawa za kulevya kamwe.”

      Pesa Zako na Uhai Wako!

      Kama ionyeshwavyo na mifano hiyo, dawa za kulevya zinadhibiti maisha ya watu. Mara tu unapokuwa mraibu, kujiponyoa huwa jambo gumu na lenye kufadhaisha. Kama kisemavyo kitabu Drugs in America, “katika sehemu za Magharibi mwa Marekani, magaidi walielekezea watu bunduki zao kwenye nyuso na kudai, ‘Pesa zako au uhai wako.’ Dawa za kulevya haramu ni mbaya zaidi kuliko waasi wa kale. Hudai vyote viwili.”

      Je, kuna kitu chochote kinachoweza kukomesha tatizo lisilozuilika la dawa za kulevya? Makala ifuatayo itachunguza baadhi ya utatuzi.

      [Maelezo ya Chini]

      a Baadhi ya majina katika mfululizo huu wa makala yamebadilishwa.

      [Blabu katika ukurasa wa 8]

      “Katika sehemu za Magharibi mwa Marekani, magaidi walielekezea watu bunduki zao kwenye nyuso na kudai, ‘Pesa zako au uhai wako.’ Dawa za kulevya haramu ni mbaya zaidi kuliko waasi wa kale. HUDAI VYOTE VIWILI”

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

      JE, MTOTO WAKO ATAKATAA DAWA ZA KULEVYA?

      NI MATINEJA GANI WANAOWEZA KUWA HATARINI ZAIDI?

      a. Wale wanaotaka kuonyesha kwamba wanajitegemea na wako tayari kukabili hatari zozote.

      b. Wale wasiopendezwa sana na miradi ya masomo au ya kiroho.

      c. Wale wasiopatana na jamii.

      d. Wale wasiofahamu waziwazi lililo sawa na lililo baya.

      e. Wale wanaoona kwamba wazazi wao hawawategemezi na ambao hutiwa moyo na rafiki zao watumie dawa za kulevya. Wachunguzi wameona kwamba “ubora wa uhusiano wa kijana mbalehe pamoja na wazazi wake waonekana kuwa ulinzi bora zaidi dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.”—Italiki zimeongezwa.

      UNAWEZA KUWALINDAJE WATOTO WAKO?

      a. Kwa kuwa na uhusiano wa karibu na mawasiliano mazuri pamoja nao.

      b. Kwa kuwaelewesha waziwazi lililo sawa na lililo baya.

      c. Kwa kuwasaidia wawe na miradi hususa.

      d. Kwa kuwafanya wahisi kwamba wao ni sehemu ya familia yenye upendo na jumuiya yenye uchangamfu.

      e. Kwa kuwafundisha juu ya hatari za matumizi mabaya ya dawa za kulevya. Watoto wanahitaji kujua waziwazi kwa nini wanapaswa kukataa dawa za kulevya.

  • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?
    Amkeni!—1999 | Novemba 8
    • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?

      KUSHINDA vita dhidi ya dawa za kulevya ni mradi wa kusifika, lakini si jambo rahisi. Mambo mawili ndiyo huchochea biashara haramu ya dawa za kulevya—ugavi na mahitaji. Kwa muda upatao nusu karne, serikali na polisi wamejitahidi kupunguza ugavi huo. Dhana yao ilikuwa sahili: Bila dawa za kulevya, hakutakuwa na waraibu.

      Kupambana na Ugavi

      Ili kutimiza kusudi hilo, vikosi vya polisi wa kupambana na dawa za kulevya, wamenasa mizigo ya dawa za kulevya, na ushirikiano wa kimataifa umefanya walanguzi mashuhuri wa dawa za kulevya watiwe kizuizini. Lakini ukweli mchungu ni kwamba ingawa uangalizi wenye matokeo waweza kuwalazimisha walanguzi wa dawa za kulevya wahamie kwingineko, watafute masoko mengine, au wawe werevu zaidi, hauwazuii. “Hatutawahi kupambana kwa mafanikio na wauzaji wa dawa za kulevya maadamu wao wana pesa za kutosha nasi lazima tujitahidi kupata pesa kutoka kwa bajeti ya taifa,” akakiri mtaalamu mmoja wa mihadarati.

      Joe de la Rosa, ofisa wa kuzuia uhalifu wa Polisi wa Gibraltar, alizungumza na Amkeni! kuhusu ugumu wa kudhibiti ulanguzi wa dawa za kulevya kati ya Afrika na Peninsula ya Iberia. “Mnamo mwaka wa 1997 tulinasa kilogramu 400 za bangi ya sanisia,” akasema. “Kwa kweli nyingi yake haikunaswa kutoka kwa walanguzi wa dawa za kulevya; ilipatikana ikielea baharini au imebebwa kwenye fuo za bahari. Jambo hilo lakupa wazo fulani kuhusu kiasi cha dawa za kulevya kinachovuka Mlango Bahari wa Gibraltar kila mwaka. Kiasi tunachonasa ni kidogo sana kwa kuzingatia kiasi kinachoingizwa. Wasafirishaji ambao hufunga safari hizo kutoka Afrika hadi Hispania wana mashua za kasi zinazokimbia zaidi ya mashua za maofisa wa forodha. Na wahisipo kwamba wako hatarini ya kukamatwa, wanatupa tu dawa hizo za kulevya baharini, kwa hiyo tunakosa uthibitisho wa kuwashtaki.”

      Polisi hukabili matatizo kama hayo katika sehemu nyingine za ulimwengu. Wasafiri wanaoonekana kuwa wa kawaida, ndege ndogo, meli za kubebea kontena, na hata nyambizi hulangua dawa za kulevya kwenye bahari au kupita kwenye mipaka inayoweza kuvukwa. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa ilipiga hesabu kwamba “angalau asilimia 75 ya dawa za kulevya zinazosafirishwa kati ya mataifa yote zitahitaji kuzuiwa ili kupunguza kwa kiasi kikubwa faida inayotokana na ulanguzi wa dawa za kulevya.” Kwa wakati uliopo, kiwango cha kuzizuia labda hakizidi asilimia 30 kuhusu kokeini—na kuhusu dawa nyingine za kulevya ni kidogo zaidi ya hicho.

      Kwa hiyo kwa nini serikali isishambulie chanzo cha tatizo hilo na kuharibu mimea yote ya bangi, mipopi ya kasumba, na mimea ya koka? Hivi majuzi Umoja wa Mataifa ulipendekeza hatua hiyo, lakini si hatua rahisi. Bangi yaweza kukuzwa karibu katika shamba lolote. Sehemu moja kuu ambapo koka hukuzwa huko Andes iko mahali panapoelezwa kuwa pako “nje ya udhibiti wa serikali.” Hali kama hizo ziko katika maeneo ya mbali ya Afghanistan na Burma, ambayo ni maeneo makuu ya kasumba na heroini.

      Jambo linalotatanisha hata zaidi ni kwamba walanguzi wa dawa za kulevya wanaweza kubadilika kwa urahisi na kuanza kutumia dawa za kubuniwa ambazo uhitaji wake unazidi kuongezeka. Na maabara za siri zinaweza kutengeneza dawa hizi za sanisia karibu kila mahali ulimwenguni.

      Je, uangalizi wenye matokeo zaidi na vifungo vya gereza vikali zaidi vingeweza kupunguza biashara ya dawa za kulevya? Kuna watumiaji wengi sana wa dawa za kulevya, waraibu wengi, na polisi wachache kuwezesha njia hiyo ifanikiwe. Kwa mfano, nchi ya Marekani, ina wafungwa wapatao milioni mbili—wengi wao walifungwa kwa sababu ya makosa yanayohusisha dawa za kulevya. Lakini hofu ya kufungwa gerezani haijazuia watu kutumia dawa za kulevya. Katika nchi nyingi zinazositawi ambapo mauzo ya dawa za kulevya yanaongezeka haraka, polisi wachache sana wasiolipwa mshahara wa kutosha hujikuta hawana nguvu za kuzuia zoea hilo.

      Je, Mahitaji ya Dawa za Kulevya Yaweza Kupunguzwa?

      Ikiwa jitihada za kupunguza ugavi wa dawa za kulevya zimekosa kufua dafu, vipi juu ya kupunguza mahitaji? “Vita vinavyohusu dawa za kulevya kwa kweli ni pambano la moyoni na akilini, na si suala tu la polisi na mahakama na magereza,” lasema gazeti Time.

      Joe de la Rosa, aliyenukuliwa mapema, hali kadhalika aamini kwamba elimu ndiyo njia pekee ya kupambana na dawa haramu za kulevya. “Uraibu wa dawa za kulevya ni tatizo la jamii linalosababishwa na jamii, kwa hiyo tunahitaji kubadili jamii au angalau kubadili njia ya watu ya kufikiri,” asema. “Tunajaribu kuhusisha shule, wazazi, na walimu ili wote wafahamu kwamba kuna hatari, kwamba dawa za kulevya zinapatikana, na kwamba watoto wao wangeweza kuathiriwa.”

      Yale Ambayo Mashahidi wa Yehova Wamefanya

      Kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova wamejihusisha kwa bidii kuelimisha watu waepuke dawa za kulevya. Wametayarisha habari iliyokusudiwa kusaidia wazazi wawafundishe watoto wao kuhusu hatari za dawa za kulevya.a Zaidi ya hayo, huduma yao imefaulu kusaidia watumiaji na walanguzi wengi wa dawa za kulevya waishi maisha ya kawaida.

      Ana, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, alijulishwa kwa Mashahidi wa Yehova kwa sababu dada yake alikuwa amesikia jinsi walivyofanikiwa kusaidia waraibu wa dawa za kulevya. Ana hakupendezwa na Biblia haswa, lakini alienda kwa kusitasita kwenye kusanyiko moja lililofanywa na Mashahidi wa Yehova. Akiwa huko alimwona mwanamume mmoja aliyekuwa mtumiaji sugu wa dawa za kulevya lakini ambaye alikuwa amebadili sura yake na mtindo wake wa maisha. “Nilifikiri kwamba ikiwa angeweza kubadilika, mimi pia ningeweza,” asema Ana. “Badiliko alilofanya lilinisadikisha kwamba nilipaswa kukubali funzo la Biblia.

      “Tangu nilipoanza funzo la Biblia mara ya kwanza, niliamua kukaa nyumbani, kwa kuwa nilijua kwamba ikiwa ningeondoka nyumbani, ningekutana na watumiaji wengine wa dawa za kulevya na kuanza kutumia dawa za kulevya tena. Tayari nilijua kwamba dawa za kulevya zilikuwa mbaya na kwamba Mungu hakukubali zoea hilo. Pia nilikuwa nimeona madhara yanayowapata watu wanaotumia dawa za kulevya na madhara niliyokuwa nimesababishia familia yangu. Lakini nilihitaji nguvu za kiroho ili kujiondoa katika utumwa wa dawa za kulevya. Lilikuwa jambo gumu kuondoa sumu hiyo. Kwa muda fulani nililala mchana kutwa huku matokeo ya dawa za kulevya yakipungua. Lakini jitihada nilizofanya zilifaa.”

      Tumaini na Kusudi Halisi

      Mume wa Ana, Pedro, aliyetajwa pia katika makala iliyotangulia, alijiponyoa kwa njia hiyo hiyo. “Siku moja nilipokuwa nikivuta bangi katika nyumba ya ndugu yangu, niliona kitabu chenye kichwa kilichonivutia,” akumbuka Pedro. “Kilikuwa na kichwa Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. Nilienda nacho nyumbani, nikakisoma, na kuyachunguza maandiko. Nilikuwa na hakika kwamba nimepata kweli.

      “Kusoma Biblia na kuzungumza na wengine kuhusu yale niliyokuwa nikijifunza kulinifanya nihisi vizuri zaidi na kupunguza tamaa ya dawa za kulevya. Nikaamua sitaendelea na mpango wangu wa kuiba kwenye kituo cha petroli kwa kutumia silaha. Rafiki mmoja alikuwa akijifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, na punde si punde nikaiga kielelezo chake. Katika muda wa miezi tisa nilibadili mtindo wangu wa maisha na kubatizwa. Katika pindi hiyo, marafiki wengi wa zamani walinipa dawa za kulevya, lakini nilianza kuzungumza nao juu ya Biblia mara moja. Baadhi yao waliitikia kwa njia ifaayo. Mmoja wao hata alifaulu kuacha uraibu wake.

      “Ili kuvunja zoea la uraibu wa dawa za kulevya, unahitaji kuwa na tumaini. Biblia ilinipa tumaini hilo, ilinipa kusudi maishani, na kunionyesha waziwazi maoni ya Mungu juu ya dawa za kulevya na jeuri. Niliona kwamba nilihisi vizuri zaidi nilipokuwa nikijifunza juu ya Mweza Yote—na hakukuwa na madhara yoyote. Baadaye, kushirikiana na watu wanaoishi maisha safi kwenye mikutano ya Mashahidi wa Yehova kulinisaidia nifuatie mwendo huo.”

      Kutoka Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya Hadi Kuwa Mwashi

      José, mlanguzi wa dawa za kulevya aliyetajwa katika makala iliyotangulia, sasa ni mwashi kwa mara nyingine tena. Haikuwa rahisi kwa upande wake kuacha biashara yenye faida. “Dawa za kulevya hukuletea pesa nyingi sana,” akiri hivyo, “lakini si njia nzuri ya kuchuma pesa. Nawaona vijana wakiwa na bastola na magari yenye kuvutia sana. Familia huvunjika, uhalifu umeenea mitaani pote, na waraibu wengi wa dawa za kulevya huvunja magari, huiba madukani au kunyang’anya watu ili wapate pesa za dawa za kulevya. Wengi huanza na bangi, kisha ecstasy au tembe nyingine, na kisha hujaribu kokeini au hata heroini. Natambua kwamba nilihusika kuingiza wengi katika zoea hilo.

      “Kadiri nilivyojifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, nilizidi kusadiki kwamba ni vibaya kujihusisha na dawa za kulevya. Nilitaka kuwa na dhamiri safi, na mke wangu, ambaye pia alikuwa akijifunza, alitamani dhamiri safi. Bila shaka ni vigumu kuacha kulangua dawa za kulevya. Niliwaeleza wateja wangu na walanguzi wengine kwamba nilikuwa nikijifunza Biblia na nilikuwa nimeacha biashara ya dawa za kulevya. Mwanzoni, hawakuniamini, na hata kufikia sasa wengine bado hawaniamini. Hata hivyo, niliacha karibu miaka miwili iliyopita, na sijajutia hilo kamwe.

      “Tangu mwaka uliopita, nimekuwa nikifanya kazi ya uashi ambayo nimesomea. Sasa kwa mwezi mmoja mimi hupata robo ya pesa nilizopata kwa siku moja nikiwa mwuzaji wa dawa za kulevya. Lakini hiyo ni njia bora ya maisha, nami nina furaha zaidi.”

      Suluhisho la Tufeni Pote Litakalofaulu

      Walanguzi wachache wa dawa za kulevya wenye moyo mkuu wameacha biashara ya dawa za kulevya. Na njia mbalimbali za kufanya watumiaji wa dawa za kulevya waishi maisha ya kawaida zimewasaidia washinde uraibu wao. Lakini, kama kikirivyo kitabu World Drug Report, “kwa watumiaji wa dawa za kulevya wa muda mrefu, kujiepusha nazo kwa muda mrefu si jambo la kawaida.” Kwa kusikitisha, kwa kila mraibu anayesaidiwa kuishi maisha ya kawaida, watu wapya kadhaa hunaswa kwenye zoea hilo. Ugavi na mahitaji yanazidi kuongezeka.

      Ikiwa vita dhidi ya dawa za kulevya itashinda, lazima kuwe na suluhisho la tufeni pote kwa sababu tatizo hilo tayari ni la tufeni pote. Kwa habari hii, Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulika na Dawa za Kulevya yasema: “Ingawa matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu unaohusiana na tatizo la dawa za kulevya katika nchi nyingi yalionwa kuwa vitisho vikuu kwa usalama, umma haukufahamu uhakika wa kwamba dawa haramu za kulevya zilikuwa tatizo la tufeni pote ambalo halingeweza kutatuliwa tena na jitihada za kitaifa peke yake.”

      Lakini je, serikali za ulimwengu zitaungana ili kuondoa pigo hilo la tufeni pote? Kufikia sasa matokeo yaliyopatikana hayatii moyo. Hata hivyo, Biblia inaelekeza kwenye serikali ya kimbingu itakayovuka mipaka yote ya kitaifa kuwa suluhisho la mwisho. Biblia inatuhakikishia kwamba Ufalme wa Mungu, unaotawalwa na Yesu Kristo, utadumu “milele na milele.” (Ufunuo 11:15) Kwa sababu hiyo, chini ya Ufalme wa Mungu, elimu ya kimungu itahakikisha kwamba hakutakuwa na mahitaji ya dawa za kulevya. (Isaya 54:13) Na matatizo ya kijamii na ya kihisia-moyo ambayo huwafanya watu washindwe na tamaa ya kutumia dawa za kulevya, yatatoweka milele.—Zaburi 55:22; 72:12; Mika 4:4.

      Je, Unahitaji Msaada?

      Hata sasa, tumaini katika Ufalme wa Mungu mikononi mwa Kristo linawachochea watu wakatae dawa za kulevya. Ikiwa ungependa habari zaidi, tafadhali wasiliana na Mashahidi wa Yehova katika eneo lako.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki