-
Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?Amkeni!—1999 | Novemba 8
-
-
Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?
KUSHINDA vita dhidi ya dawa za kulevya ni mradi wa kusifika, lakini si jambo rahisi. Mambo mawili ndiyo huchochea biashara haramu ya dawa za kulevya—ugavi na mahitaji. Kwa muda upatao nusu karne, serikali na polisi wamejitahidi kupunguza ugavi huo. Dhana yao ilikuwa sahili: Bila dawa za kulevya, hakutakuwa na waraibu.
Kupambana na Ugavi
Ili kutimiza kusudi hilo, vikosi vya polisi wa kupambana na dawa za kulevya, wamenasa mizigo ya dawa za kulevya, na ushirikiano wa kimataifa umefanya walanguzi mashuhuri wa dawa za kulevya watiwe kizuizini. Lakini ukweli mchungu ni kwamba ingawa uangalizi wenye matokeo waweza kuwalazimisha walanguzi wa dawa za kulevya wahamie kwingineko, watafute masoko mengine, au wawe werevu zaidi, hauwazuii. “Hatutawahi kupambana kwa mafanikio na wauzaji wa dawa za kulevya maadamu wao wana pesa za kutosha nasi lazima tujitahidi kupata pesa kutoka kwa bajeti ya taifa,” akakiri mtaalamu mmoja wa mihadarati.
Joe de la Rosa, ofisa wa kuzuia uhalifu wa Polisi wa Gibraltar, alizungumza na Amkeni! kuhusu ugumu wa kudhibiti ulanguzi wa dawa za kulevya kati ya Afrika na Peninsula ya Iberia. “Mnamo mwaka wa 1997 tulinasa kilogramu 400 za bangi ya sanisia,” akasema. “Kwa kweli nyingi yake haikunaswa kutoka kwa walanguzi wa dawa za kulevya; ilipatikana ikielea baharini au imebebwa kwenye fuo za bahari. Jambo hilo lakupa wazo fulani kuhusu kiasi cha dawa za kulevya kinachovuka Mlango Bahari wa Gibraltar kila mwaka. Kiasi tunachonasa ni kidogo sana kwa kuzingatia kiasi kinachoingizwa. Wasafirishaji ambao hufunga safari hizo kutoka Afrika hadi Hispania wana mashua za kasi zinazokimbia zaidi ya mashua za maofisa wa forodha. Na wahisipo kwamba wako hatarini ya kukamatwa, wanatupa tu dawa hizo za kulevya baharini, kwa hiyo tunakosa uthibitisho wa kuwashtaki.”
Polisi hukabili matatizo kama hayo katika sehemu nyingine za ulimwengu. Wasafiri wanaoonekana kuwa wa kawaida, ndege ndogo, meli za kubebea kontena, na hata nyambizi hulangua dawa za kulevya kwenye bahari au kupita kwenye mipaka inayoweza kuvukwa. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa ilipiga hesabu kwamba “angalau asilimia 75 ya dawa za kulevya zinazosafirishwa kati ya mataifa yote zitahitaji kuzuiwa ili kupunguza kwa kiasi kikubwa faida inayotokana na ulanguzi wa dawa za kulevya.” Kwa wakati uliopo, kiwango cha kuzizuia labda hakizidi asilimia 30 kuhusu kokeini—na kuhusu dawa nyingine za kulevya ni kidogo zaidi ya hicho.
Kwa hiyo kwa nini serikali isishambulie chanzo cha tatizo hilo na kuharibu mimea yote ya bangi, mipopi ya kasumba, na mimea ya koka? Hivi majuzi Umoja wa Mataifa ulipendekeza hatua hiyo, lakini si hatua rahisi. Bangi yaweza kukuzwa karibu katika shamba lolote. Sehemu moja kuu ambapo koka hukuzwa huko Andes iko mahali panapoelezwa kuwa pako “nje ya udhibiti wa serikali.” Hali kama hizo ziko katika maeneo ya mbali ya Afghanistan na Burma, ambayo ni maeneo makuu ya kasumba na heroini.
Jambo linalotatanisha hata zaidi ni kwamba walanguzi wa dawa za kulevya wanaweza kubadilika kwa urahisi na kuanza kutumia dawa za kubuniwa ambazo uhitaji wake unazidi kuongezeka. Na maabara za siri zinaweza kutengeneza dawa hizi za sanisia karibu kila mahali ulimwenguni.
Je, uangalizi wenye matokeo zaidi na vifungo vya gereza vikali zaidi vingeweza kupunguza biashara ya dawa za kulevya? Kuna watumiaji wengi sana wa dawa za kulevya, waraibu wengi, na polisi wachache kuwezesha njia hiyo ifanikiwe. Kwa mfano, nchi ya Marekani, ina wafungwa wapatao milioni mbili—wengi wao walifungwa kwa sababu ya makosa yanayohusisha dawa za kulevya. Lakini hofu ya kufungwa gerezani haijazuia watu kutumia dawa za kulevya. Katika nchi nyingi zinazositawi ambapo mauzo ya dawa za kulevya yanaongezeka haraka, polisi wachache sana wasiolipwa mshahara wa kutosha hujikuta hawana nguvu za kuzuia zoea hilo.
Je, Mahitaji ya Dawa za Kulevya Yaweza Kupunguzwa?
Ikiwa jitihada za kupunguza ugavi wa dawa za kulevya zimekosa kufua dafu, vipi juu ya kupunguza mahitaji? “Vita vinavyohusu dawa za kulevya kwa kweli ni pambano la moyoni na akilini, na si suala tu la polisi na mahakama na magereza,” lasema gazeti Time.
Joe de la Rosa, aliyenukuliwa mapema, hali kadhalika aamini kwamba elimu ndiyo njia pekee ya kupambana na dawa haramu za kulevya. “Uraibu wa dawa za kulevya ni tatizo la jamii linalosababishwa na jamii, kwa hiyo tunahitaji kubadili jamii au angalau kubadili njia ya watu ya kufikiri,” asema. “Tunajaribu kuhusisha shule, wazazi, na walimu ili wote wafahamu kwamba kuna hatari, kwamba dawa za kulevya zinapatikana, na kwamba watoto wao wangeweza kuathiriwa.”
-
-
Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?Amkeni!—1999 | Novemba 8
-
-
Suluhisho la Tufeni Pote Litakalofaulu
Walanguzi wachache wa dawa za kulevya wenye moyo mkuu wameacha biashara ya dawa za kulevya. Na njia mbalimbali za kufanya watumiaji wa dawa za kulevya waishi maisha ya kawaida zimewasaidia washinde uraibu wao. Lakini, kama kikirivyo kitabu World Drug Report, “kwa watumiaji wa dawa za kulevya wa muda mrefu, kujiepusha nazo kwa muda mrefu si jambo la kawaida.” Kwa kusikitisha, kwa kila mraibu anayesaidiwa kuishi maisha ya kawaida, watu wapya kadhaa hunaswa kwenye zoea hilo. Ugavi na mahitaji yanazidi kuongezeka.
Ikiwa vita dhidi ya dawa za kulevya itashinda, lazima kuwe na suluhisho la tufeni pote kwa sababu tatizo hilo tayari ni la tufeni pote. Kwa habari hii, Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulika na Dawa za Kulevya yasema: “Ingawa matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu unaohusiana na tatizo la dawa za kulevya katika nchi nyingi yalionwa kuwa vitisho vikuu kwa usalama, umma haukufahamu uhakika wa kwamba dawa haramu za kulevya zilikuwa tatizo la tufeni pote ambalo halingeweza kutatuliwa tena na jitihada za kitaifa peke yake.”
-