Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Jitihada za Kutafsiri Biblia Katika Kigiriki cha Kisasa
    Mnara wa Mlinzi—2002 | Novemba 15
    • Miaka 34 baadaye, viongozi wa Kanisa Othodoksi waliokutana huko Jerusalem ili kujadiliana kuhusu tafsiri hiyo, walitangaza kwamba Maandiko “hayapaswi kusomwa na mtu yeyote yule, lakini yanapasa kusomwa na watu wanaochunguza mambo mazito sana ya kiroho baada ya kufanya utafiti ufaao.” Walimaanisha kwamba Maandiko yanapaswa kusomwa tu na makasisi wenye elimu.

      Seraphim, mtawa Mgiriki kutoka kisiwa cha Lesbos, alijaribu kuchapisha tafsiri mpya ya Maximus huko London mnamo mwaka wa 1703. Wakuu wa serikali walipokataa kumpa msaada wa kifedha ambao walimwahidi, alitumia fedha zake mwenyewe kuchapisha tafsiri hiyo mpya. Seraphim aliandika maneno makali katika utangulizi wake, akikazia kwamba “kila Mkristo anayempenda Mungu” anapaswa kusoma Biblia. Aliwashutumu makasisi wenye vyeo vya juu kanisani ambao “walijaribu kuficha uovu wao kwa kutowaelimisha watu.” Kama ilivyotarajiwa, adui zake Waothodoksi walipanga njama, naye akakamatwa huko Urusi na kupelekwa uhamishoni huko Siberia, ambako alifia mwaka wa 1735.

      Akizungumzia njaa kali ya kiroho ambayo watu waliozungumza Kigiriki walikuwa nayo, kasisi mmoja Mgiriki alisema hivi kuhusu tafsiri ya baadaye ya Maximus: “Wagiriki na wengineo walipokea Biblia hii Takatifu kwa hamu na uchangamfu sana. Nao wanaisoma. Uchungu waliokuwa nao moyoni ulitulizwa, na imani yao katika Mungu . . . iliongezeka.” Hata hivyo, viongozi wao wa kidini waliogopa kwamba matendo ya makasisi na mafundisho yao yasiyo ya kimaandiko yangejulikana kama watu wangeanza kuielewa Biblia. Kwa hiyo, katika mwaka wa 1823 na pia mwaka wa 1836, askofu mkuu wa Constantinople aliagiza tafsiri hizo zote ziteketezwe.

      Mtafsiri Jasiri

      Licha ya upinzani mkali, watu walikuwa na hamu kubwa ya kujifunza Biblia. Hivyo mtu mmoja mashuhuri alijitokeza kufanya kazi muhimu ya kutafsiri Biblia katika Kigiriki cha kisasa. Mtu huyo jasiri alikuwa Neofitos Vamvas, mtaalamu wa lugha na msomi maarufu wa Biblia, ambaye alionwa na wengi kuwa miongoni mwa “Walimu wa Taifa.”

      Vamvas aliamini kwamba Kanisa Othodoksi ndilo lililowatumbukiza watu katika giza la kiroho. Aliamini kabisa kwamba Biblia ilihitaji kutafsiriwa katika Kigiriki cha kawaida ili kuwaamsha watu kiroho. Mnamo mwaka wa 1831, yeye pamoja na wasomi wengine, walianza kutafsiri Biblia kwa Kigiriki cha wasomi. Tafsiri yake nzima ilichapishwa mwaka wa 1850. Alishirikiana na Chama cha Biblia cha Uingereza na cha Lugha za Kigeni (BFBS) katika kuchapisha na kugawanya tafsiri yake kwa kuwa Kanisa Othodoksi la Ugiriki lilikataa kumsaidia. Kanisa lilimwita “Mprotestanti,” na baada ya muda alitengwa na kanisa.

  • Jitihada za Kutafsiri Biblia Katika Kigiriki cha Kisasa
    Mnara wa Mlinzi—2002 | Novemba 15
    • Makasisi Waothodoksi waliwaonya watu wasichukue tafsiri hizo. Kwa mfano, katika jiji la Athens, Biblia zote zilikusanywa kwa nguvu. Katika mwaka wa 1833, askofu Mwothodoksi wa Crete aliteketeza Biblia za “Agano Jipya” alizopata kwenye nyumba moja ya watawa. Kasisi mmoja na wakazi wa vijiji vya karibu walificha nakala zao hadi askofu huyo alipoondoka kisiwani.

      Miaka kadhaa baadaye, kwenye kisiwa cha Corfu, tafsiri ya Biblia ya Vamvas ilipigwa marufuku na Sinodi Takatifu ya Kanisa Othodoksi la Ugiriki. Uuzaji wa Biblia hiyo ulipigwa marufuku, na nakala zilizosalia zikaharibiwa. Biblia ziliteketezwa kwenye visiwa vya Chios, Síros, na Mykonos kwa sababu ya upinzani wa makasisi. Lakini kazi ya kutafsiri Biblia ilikumbwa na upinzani mwingi baadaye.

      Malkia Apendezwa na Biblia

      Katika miaka ya 1870, Malkia Olga wa Ugiriki aligundua kwamba Wagiriki wengi hawakuijua vizuri Biblia. Alijitahidi kuhakikisha kwamba Biblia imetafsiriwa kwa lugha rahisi kuliko tafsiri ya Vamvas kwa sababu aliamini kwamba ujuzi wa Maandiko ungeliimarisha na kulitia nguvu taifa hilo.

      Askofu mkuu wa Athens na msimamizi wa Sinodi Takatifu, Prokopios, alimtembelea kwa faragha malkia na kumtia moyo aendelee na jitihada zake. Hata hivyo, malkia alipoomba idhini rasmi kutoka kwa Sinodi Takatifu, ombi lake lilikataliwa. Lakini hakukata tamaa, alitoa ombi jingine, na likakataliwa tena mnamo mwaka wa 1899. Alipuuza katazo hilo, akaamua kugharimia uchapishaji wa nakala chache. Alimaliza kazi hiyo mwaka wa 1900.

      Wapinzani Sugu

      Mnamo mwaka wa 1901, gazeti maarufu la Athens, The Acropolis, lilichapisha Injili ya Mathayo katika Kigiriki cha kawaida. Injili hiyo iliandikwa na Alexander Pallis, mtafsiri aliyekuwa akifanya kazi huko Liverpool, Uingereza. Pallis na wenzake walikuwa na nia ya ‘kuwaelimisha Wagiriki’ na “kuliokoa taifa” lisizorote.

      Wanafunzi wa theolojia wa Othodoksi na maprofesa wao walisema tafsiri hiyo “iliaibisha vitu vitakatifu vya taifa hilo,” na ilikufuru Biblia. Askofu mkuu wa Constantinople, Joakim wa Tatu aliandika barua ya kupinga tafsiri hiyo. Ubishi huo uligeuka kuwa wa kisiasa, na vyama vya kisiasa vyenye kuzozana viliutumia kwa ujanja.

      Magazeti maarufu ya Athens yalianza kushambulia tafsiri ya Pallis. Yalisema kwamba watu waliounga mkono tafsiri hiyo “hawakumwamini Mungu,” walikuwa “wasaliti,” na “vibaraka wa serikali za kigeni” ambao walitaka kuvuruga amani nchini Ugiriki. Makundi yasiyopenda kamwe mabadiliko katika Kanisa Othodoksi la Ugiriki yaliwachochea wanafunzi wafanye ghasia jijini Athens kuanzia Novemba 5 hadi 8, mwaka wa 1901. Walishambulia ofisi za gazeti la The Acropolis, wakaandamana kwenye makao ya mfalme, wakateka Chuo Kikuu cha Athens huku wakidai serikali ijiuzulu. Watu wanane waliuawa katika mapambano hayo baina ya wanafunzi na wanajeshi. Siku iliyofuata, mfalme alimwagiza Askofu Mkuu Prokopios ajiuzulu, na siku mbili baadaye Baraza lote la Mawaziri likajiuzulu.

      Baada ya mwezi mmoja, wanafunzi waliandamana tena na kuiteketeza tafsiri moja ya Pallis hadharani. Waliazimia kukomesha ugawanyaji wa tafsiri hiyo na wakapendekeza kwamba mtu yeyote atakayejaribu kufanya hivyo wakati ujao aadhibiwe vikali. Kusudi lao lilikuwa kupiga marufuku matumizi ya tafsiri yoyote ya kisasa ya Kigiriki. Ulikuwa wakati mwovu sana.

      “Usemi wa Yehova Hudumu Milele”

      Amri iliyopiga marufuku Biblia ya kisasa ya Kigiriki ilifutiliwa mbali mwaka wa 1924. Tangu wakati huo, Kanisa Othodoksi la Ugiriki limeshindwa kabisa kuwazuia watu kuisoma Biblia.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki