-
Je, Wajua?Mnara wa Mlinzi—2012 | Januari 1
-
-
Kuna uthibitisho gani kwamba matofali yalitengenezwa katika Misri ya kale?
▪ Katika Biblia, kitabu cha Kutoka kinataja kwamba Wamisri waliwalazimisha watumwa wao Waebrania kufanya kazi ya kutengeneza matofali. Watumwa hao walipaswa kutengeneza kiasi fulani cha matofali kila siku, wakitumia saruji ya udongo na nyasi.—Kutoka 1:14; 5:10-14.
Katika nyakati za Biblia, kazi ya kutengeneza matofali ya udongo na kuyakausha kwa jua, ilikuwa kazi muhimu katika eneo la Bonde la Mto Nile. Majengo ya kale yaliyojengwa kwa matofali hayo, bado yanapatikana leo nchini Misri. Mchoro wa karne ya 15 K.W.K. ulio kwenye ukuta wa kaburi la Rekhmire huko Thebes, ambao ulichorwa karibu na wakati ambapo matukio yaliyoandikwa katika kitabu cha Kutoka yalitokea, unaonyesha hatua kwa hatua jinsi matofali yalivyotengenezwa.
Kitabu The International Standard Bible Encyclopedia kinasema hivi kuhusu mchoro huo: “Maji yanaletwa kutoka mtoni, udongo unachanganywa na maji kwa kutumia jembe, kisha unabebwa hadi mahali panapofaa kutengenezea matofali. Udongo huo unawekwa ndani ya kisanduku cha mbao, kisha mtengenezaji wa matofali anakiweka kisanduku hicho chini, upande wa juu ukiwa umeangalia chini, halafu anakiinua ili tofali libaki chini likaushwe na jua. Kwa njia hiyo, matofali mengi yanatengenezwa, kisha yanapokauka yanapangwa vizuri yakingoja wakati ambapo yatahitajika. Mbinu hiyo ya kutengeneza matofali bado inatumika huko Mashariki ya Karibu.”
Pia, hati tofauti-tofauti zilizotengenezwa kwa mafunjo kuanzia mwaka wa 2,000 K.W.K. zinataja kazi ya kutengeneza matofali iliyofanywa na watumwa, matumizi ya nyasi na udongo, na pia kiasi cha matofali kilichopaswa kutengenezwa kila siku.
-
-
Je, Wajua?Mnara wa Mlinzi—2012 | Januari 1
-
-
[Picha katika ukurasa wa 22]
Mchoro kwenye ukuta ndani ya kaburi la Rekhmire
[Hisani ya Picha]
Erich Lessing/Art Resource, NY
-