Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Udugu Wenye Umoja Usioweza Kuvunjwa
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • Udugu Wenye Umoja Usioweza Kuvunjwa

      Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini El Salvador

      MNAMO JANUARI 13, 2001, SAA 5:34 ASUBUHI, TETEMEKO LA ARDHI LENYE KIPIMO CHA RICHTER CHA 7.6 LILITINGISHA NCHI YA EL SALVADOR NA LILIENEA HADI PANAMA NA MEXICO. HAKUNA ATAKAYESAHAU ALICHOKUWA AKIFANYA TETEMEKO HILO LILIPOTOKEA.

      “WAKATI tetemeko hilo lenye kishindo lilipotulia, tulitazama mlimani, kilele chake kilikuwa kimegawanyika na ni kana kwamba kiliganda kwa sekunde chache,” akumbuka Miriam Quezada. “Binti yangu alilia kwa sauti, ‘Mama! Kimbia! Kimbia!’” Kisha sehemu ya juu ya mlima ikaanguka kuwaelekea. Karibu watu 500 walipoteza maisha yao katika jumuiya ya Las Colinas ya Nueva San Salvador, au Santa Tecla, na nyumba zipatazo 300 ziliharibiwa kabisa.

      “Nilikuwa nimetoka tu nyumbani na nilikuwa kwenye kituo cha basi wakati tetemeko lilipotokea,” asimulia Roxana Sánchez. “Tetemeko lilipokoma, nilimsaidia mwanamke mmoja kubeba mifuko yake na nikaamua kurudi nyumbani kwa sababu familia yangu wangekuwa na wasiwasi kunihusu.’” Roxana alipopiga kona, aliona kwamba barabara yao iliishia ghafula chini ya rundo la mchanga. Nyumba yao ilikuwa imetoweka!

      Kuandaa Msaada wa Haraka

      Kuna Mashahidi wa Yehova 28,000 nchini El Salvador na wengi wao wanaishi katika sehemu iliyokumbwa na msiba—sehemu iliyo karibu na pwani ya Salvador. Ingawa wengi bado waliteseka kutokana na mfadhaiko, upesi walianza kufikiria mahitaji ya wengine. Mario Suarez, mwangalizi asafiriye wa Mashahidi wa Yehova anayetumikia huko Santa Tecla, asimulia: “Saa moja hivi baada ya tetemeko la ardhi kutukia, niliitwa ili kusaidia. Ilisemekana kwamba baadhi ya akina ndugu na dada Wakristo walikuwa wamenaswa ndani ya nyumba zao. Mara moja kikundi cha wajitoleaji kilifanyizwa.

      “Tulifikiri kwamba huenda kuta fulani zilikuwa zimeanguka na kwamba ilihitaji tu kuondoa vifusi na kufanyiza njia ili walionaswa waweze kutoka nje. Kumbe hatukujua kwamba ulikuwa msiba mkubwa sana. Tulipofika mahali hapo tuliuliza nyumba zilipokuwa. Tulishtuka tulipoambiwa kwamba zilikuwa zimefukiwa mahali tuliposimama! Nyumba zilifukiwa kabisa kufikia orofa ya pili kwa meta tatu ya udongo. Lilikuwa jambo lenye kufadhaisha!”

      Kufikia mchana, Mashahidi wapatao 250 kutoka kwa makutaniko jirani walimiminika katika eneo hili ili kusaidia. Wajitoleaji walijaribu sana kuwaokoa manusura kwa kutumia sururu, sepetu, sinia za plastiki na mikono bila vifaa. Hata hivyo ni wachache tu waliookolewa huko Santa Tecla. Mashahidi wa Yehova watano walikuwa miongoni mwa mamia ya watu waliokufa kwa kukosa hewa au kwa kufukiwa.

  • Udugu Wenye Umoja Usioweza Kuvunjwa
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • Tetemeko la Pili Kubwa

      Katika Februari 13, 2001, saa 2:22 asubuhi, mwezi mmoja baada ya lile tetemeko la ardhi la kwanza, tetemeko la ardhi lilitikisa kitovu cha El Salvador kwa mara ya pili, likiwa na ukubwa wa kipimo cha Richter cha 6.6. Kwa mara nyingine tena, Mashahidi wa Yehova wakajitolea upesi kuandaa misaada na uokoaji. Mzee mmoja wa kutaniko aitwaye Noé Iraheta alieleza hivi: “Kila kiongozi wa Funzo la Kitabu la Kutaniko alienda kutafuta Mashahidi wa kikundi chake kuhakikisha kwamba wote walikuwa salama.”

      Majiji ya San Vicente na Cojutepeque na vitongoji vyake yaliathiriwa zaidi. Miji ya San Pedro Nonualco, San Miguel Tepezontes, na San Juan Tepezontes yalikuwa magofu. Katika Candelaria, Cuscatlán ambapo uharibifu ulienea karibu kila mahali, shule moja ya parokia iliporomoka na watoto 20 wakafa. Salvador Trejo, Shahidi anayeishi huko aeleza: “Saa moja hivi baadaye, nilisikia mtu akiniita, ‘Ndugu Trejo!’ Mwanzoni, sikuweza kuona kwa sababu ya vumbi. Halafu, ghafula, Mashahidi kutoka Cojutepeque wakatokea. Walikuja kutuona!”

      Makutaniko jirani yalipanga tena kuandaa mahitaji ya lazima kwa wahasiriwa wa huu msiba wa pili. Walifuata mfano wa Wakristo wa Makedonia katika karne ya kwanza waliofurahia pendeleo la kutoa, ingawaje wao pia walikuwa na uhitaji. Kwa mfano, wale wa makutaniko ya jiji la Santiago Texacuangos, waliopoteza vitu vingi wakati wa tetemeko la ardhi la kwanza, walipika vyakula na kuwapelekea ndugu zao katika mji wa karibu wa San Miguel Tepezontes.

      Kwa jumla, inakadiriwa kwamba zaidi ya watu 1,200 walikufa kutokana na tetemeko la ardhi huko El Salvador, na wengine wanane wakaripotiwa kufa katika nchi jirani ya Guatemala.

  • Udugu Wenye Umoja Usioweza Kuvunjwa
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • [Picha katika ukurasa wa 23]

      Poromoko la ardhi lililosababishwa na tetemeko lililofukia zaidi ya nyumba 300 huko Las Colinas

      [Hisani]

      Sehemu ya chini ya ukurasa wa 23-25: Courtesy El Diario de Hoy

      [Picha katika ukurasa wa 24]

      Wanakijiji walitumia sururu, sepetu na ndoo katika kazi yao ya uokoaji

      [Hisani]

      Courtesy of La Prensa Gráfica (photograph by Milton Flores/Alberto Morales/Félix Amaya)

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki