-
Mpendwa AnapokufaMnara wa Mlinzi—2008 | Julai 1
-
-
Mpendwa Anapokufa
Jumanne (Siku ya 2), Julai 17, 2007 (17/7/2007), karibu saa moja jioni, ndege ya abiria iliteleza kwenye uwanja wa ndege wa Brazili wenye shughuli nyingi zaidi huko São Paulo. Ndege hiyo ilivuka barabara yenye shughuli nyingi na kugonga depo ya mizigo. Watu 200 hivi walikufa katika aksidenti hiyo.
TUKIO hilo linalosemekana kuwa msiba mbaya zaidi wa ndege nchini Brazili halitawahi kusahauliwa na wale waliowapoteza wapendwa wao. Mmoja wao ni Claudete. Alikuwa akitazama TV aliposikia habari kuhusu aksidenti hiyo ya ndege. Mwana wake, Renato, alikuwa ndani ya ndege hiyo. Alikuwa na umri wa miaka 26 tu. Alikuwa akipanga kufunga ndoa mnamo Oktoba (Mwezi wa 10). Claudete alijaribu juu chini kuwasiliana naye kwenye simu ya mkononi, lakini hakufaulu. Alianguka kwenye sakafu na kulia sana.
Antje alimpoteza mchumba wake katika aksidenti mbaya ya gari mnamo Januari (Mwezi wa 1) 1986. Aliposikia habari hizo, alipatwa na mshtuko wa akili. “Kwanza sikuamini. Nilihisi kana kwamba ni ndoto mbaya na ningeamka na kukuta mambo yako tofauti. Nilitetemeka na kuhisi uchungu mbaya ni kama mtu alikuwa amenigonga tumboni.” Antje alipatwa na mshuko wa moyo kwa miaka mitatu iliyofuata. Ingawa zaidi ya miaka 20 imepita tangu aksidenti hiyo, bado anatetemeka anapokumbuka yaliyotokea.
Hatuwezi kueleza hisia za mshtuko, kutokuamini, na kupoteza tumaini zinazoweza kuletwa na misiba mibaya kama hiyo isiyotarajiwa. Hata hivyo, hata tunapotarajia kwamba mpendwa atakufa, kama vile kutokana na ugonjwa wa muda mrefu, bado huzuni inaweza kuwa nyingi sana jambo hilo linapotendeka. Hakuna mtu ambaye huwa tayari kabisa kwa ajili ya kifo cha mpendwa. Mama ya Nanci alikufa mnamo 2002 baada ya ugonjwa wa muda mrefu. Hata hivyo, siku ambayo mama yake alikufa, Nanci aliketi kwenye sakafu ya hospitali akiwa katika hali ya mshtuko. Kwake ni kana kwamba maisha yalipoteza maana. Miaka mitano imepita, lakini bado analia anapofikiri kumhusu mama yake.
“Uchungu wa kumpoteza mpendwa hautoweki kabisa, watu huzoea tu kwamba mpendwa wao hayupo,” akasema Dakt. Holly G. Prigerson. Ikiwa umempoteza mpendwa katika kifo, iwe ni bila kutarajia au la, huenda ukajiuliza: ‘Je, ni kawaida kuomboleza? Mtu anaweza kukabiliana na kumpoteza mpendwa wake jinsi gani? Je, nitawahi kumwona tena mpendwa wangu?’ Habari inayofuata itajibu maswali haya na mengine ambayo huenda ukajiuliza.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
EVERTON DE FREITAS/AFP/Getty Images
-
-
Kukabiliana na HuzuniMnara wa Mlinzi—2008 | Julai 1
-
-
“Nao wanawe wote [wa Yakobo] na binti zake wote wakawa wakiondoka ili kumfariji, lakini akawa akizidi kukataa kufarijiwa na kusema: ‘Kwa maana nitashuka kuingia katika Kaburi nikimwombolezea mwanangu!’ Na baba yake akaendelea kumlilia.”—MWANZO 37:35.
MZEE wa ukoo Yakobo aliomboleza sana kwa kumpoteza mwanawe. Alitazamia kwamba ataendelea kuhuzunika hadi atakapokufa. Kama Yakobo, huenda ukahisi kwamba uchungu wa kumpoteza mpendwa ni mwingi sana hivi kwamba hautawahi kwisha. Je, huzuni nyingi kama hiyo inaonyesha kwamba mtu hana imani katika Mungu? La!
Biblia inaonyesha kwamba Yakobo alikuwa mtu mwenye imani. Kama tu babu yake Abrahamu na baba yake Isaka, Yakobo anasifiwa kwa imani yake yenye nguvu. (Waebrania 11:8, 9, 13) Pindi moja, alipigana mweleka usiku kucha na malaika ili apate baraka kutoka kwa Mungu! (Mwanzo 32:24-30) Ni wazi kwamba Yakobo alikuwa mtu wa kiroho sana. Basi, tunajifunza nini kutokana na huzuni ya Yakobo? Mtu anaweza kuwa na imani yenye nguvu katika Mungu na bado awe na hisia nyingi za huzuni mpendwa anapokufa. Ni kawaida kuwa na huzuni mpendwa wetu anapokufa.
Huzuni Ni Nini?
Huzuni inaweza kutuathiri kwa njia nyingi, lakini kwa wengi hisia kubwa huwa ile ya uchungu mwingi wa kihisia. Fikiria mfano wa Leonardo, ambaye alikuwa na umri wa miaka 14 baba yake alipokufa ghafula kutokana na matatizo ya moyo na ya mfumo wa kupumua. Leonardo hawezi kusahau siku ambayo shangazi yake alimpasha habari hiyo. Kwanza, alikataa kuamini alichoambiwa. Aliona mwili wa baba yake wakati wa maziko, lakini ni kana kwamba mambo hayakuwa halisi. Kwa karibu miezi sita, Leonardo hakuweza kulia. Mara nyingi, alijikuta akimsubiri baba yake arudi nyumbani kutoka kazini. Ilimchukua karibu mwaka mmoja kutambua kikamili kwamba alikuwa amempoteza baba yake. Alipotambua hilo alijihisi mpweke sana. Mambo ya kawaida, kama vile kutompata mtu nyumbani, yalimkumbusha kwamba baba yake hayuko. Nyakati kama hizo, mara nyingi alilia. Alimkosa baba yake kwelikweli!
Kama hali ya Leonardo inavyoonyesha, mtu anaweza kukumbwa na huzuni nyingi sana. Jambo linalotia moyo ni kwamba mtu anaweza kushinda hali hiyo. Hata hivyo, huenda ikachukua muda. Kama tu jeraha baya mwilini linavyohitaji muda kupona, ndivyo ilivyo na hisia za kumpoteza mpendwa. Mtu anaweza kupata nafuu kutokana na huzuni hiyo baada ya miezi, miaka kadhaa, au hata muda mrefu zaidi. Lakini uchungu mwingi unaohisi mwanzoni utapungua kadiri wakati unavyopita, na hatua kwa hatua maisha yataanza kuonekana kuwa yenye maana na yenye tumaini.
Kwa sasa, huzuni inasemwa kuwa sehemu muhimu ya hatua za kupona na ya kujifunza kukabiliana na hali yako mpya. Kuna pengo mahali ambapo kulikuwa na mwanadamu. Tunahitaji kuzoea kuishi bila mtu huyo. Huzuni inaweza kutusaidia kuonyesha hisia zetu. Bila shaka, watu wanaomboleza kwa njia zinazotofautiana. Hata hivyo, jambo moja linaonekana kuwa la kweli: Kufungia huzuni yako kunaweza kukudhuru kiakili, kihisia, na kimwili.
-