Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Unapokumbwa na Ugonjwa
    Amkeni!—2001 | Januari 22
    • Unapokumbwa na Ugonjwa

      John, baada ya kugundua kwamba alikuwa na ugonjwa wenye kudhoofisha—“Nilishtuka sana.”

      Beth, baada ya kufahamu hatari ya ugonjwa wake.—“Nilihofu sana.”

      KUFAHAMU kwamba una ugonjwa wa kudumu au wa kulemaza au kufahamu kwamba utalemaa kabisa kwa sababu ya majeraha uliyoyapata katika aksidenti ni mojawapo ya mambo yenye kuhuzunisha zaidi maishani. Iwe utapokea habari za ugonjwa wako katika ofisi tulivu ya daktari au utagundua ulemavu wako katika chumba cha tiba ya dharura chenye hekaheka, yamkini utapigwa na bumbuazi. Maisha hayakutayarishi kukabiliana na hisia-moyo kali zinazokukumba wakati unaposhikwa na tatizo baya sana la kiafya.

  • Kufadhaishwa na Hisia-Moyo
    Amkeni!—2001 | Januari 22
    • Kufadhaishwa na Hisia-Moyo

      “BAADA ya kuambiwa kwamba nilikuwa na ugonjwa wenye kufisha,” akumbuka mwanamume mmoja mzeemzee, “nilijaribu kushinda hofu yangu, lakini hisia za shaka zilinilemea.” Maneno yake yakazia uhakika wa kwamba ugonjwa mbaya haumlemazi mtu kimwili tu bali pia humwumiza kihisia. Hata hivyo, kuna watu ambao wanakabiliana kwa mafanikio na hali hizo. Wengi wao wangependa kukuhakikishia kwamba kuna njia za kukabiliana kwa mafanikio na ugonjwa wenye kudumu. Lakini kabla ya kuzungumzia unaloweza kufanya, acheni kwanza tuchunguze kinagaubaga baadhi ya hisia ambazo yaelekea zitakupata mwanzoni.

      Kutoamini, Kutokubali, Kuhuzunika

      Waweza kuwa na hisia-moyo tofauti sana na za wengine. Hata hivyo, wataalamu wa afya na watu wanaougua wanasema kwamba watu wanaokumbwa na ugonjwa huwa na hisia-moyo mbalimbali za kawaida. Mwanzoni wao hushtuka na kutoamini kisha wanakuwa na hisia za kutokubali: ‘Haiwezi kuwa kweli.’ ‘Lazima wawe wamekosea.’ ‘Labda walichanganya matokeo ya upimaji kwenye maabara.’ Mwanamke mmoja alieleza alivyohisi alipoambiwa ana kansa: “Unataka tu kujifunika kichwa kwa blanketi, na unatumaini kwamba ukijifunua itakuwa imetokomea.”

      Lakini unapoanza kung’amua kuwa ni kweli, unahuzunika sana kwa sababu ya mabaya yatakayokupata. ‘Nitaishi muda mrefu kadiri gani?’ ‘Je, nitaishi kwa maumivu hadi nifapo?’ na maswali mengine kama hayo yaweza kukusumbua. Huenda ukatamani kuishi jinsi ulivyoishi kabla ya kugunduliwa kwa ugonjwa wako, lakini huwezi. Punde si punde waweza kujikuta umelemewa sana na hisia nyingine kali na zenye kuumiza. Hisia kama zipi?

      Kukosa Uhakika, Kufadhaika, Hofu

      Ugonjwa mbaya sana hukufanya ukose uhakika kabisa na ufadhaike. “Nyakati nyingine, hali yangu isiyojulikana hufanya maisha yawe yenye kutamausha sana,” asema mwanamume mwenye ugonjwa wa kutetemeka. “Kila siku, nina wasiwasi kuhusu hali yangu.” Ugonjwa wako waweza pia kukuogopesha. Endapo utazuka ghafula, waweza kulemewa mno na hofu. Hata hivyo, ikiwa ugonjwa wako umegunduliwa baada ya kusumbuliwa kwa miaka mingi sana na dalili ambazo hazikupimwa vizuri, huenda hofu hiyo isiwe dhahiri. Mwanzoni, huenda hata ukatulia kwa kuhisi kwamba hatimaye watu wataamini kwamba kwa kweli wewe ni mgonjwa na wala si kisingizio. Lakini, baada ya muda utulivu huo waweza kufuatwa na hofu kuu unapogundua matokeo ya ugonjwa wako.

      Hofu ya kushindwa kudhibiti maisha yako yaweza pia kukutia wasiwasi. Hasa ikiwa unapenda kujitegemea, huenda ukahofu ufikiripo uwezekano wa kuwategemea wengine zaidi na zaidi. Huenda ukahangaika kwamba ugonjwa wako unaanza kudhibiti maisha yako na kukuwekea mipaka.

      Hasira, Aibu, Upweke

      Waweza pia kushikwa na hasira unapong’amua kwamba huwezi kudhibiti maisha yako. ‘Mbona iwe mimi? Kwani nilifanya nini ili nistahili hali hii?’ huenda ukajiuliza. Pigo hilo kwa afya yako huonekana kuwa lisilo la haki na lisilofaa. Aibu na kukata tamaa kwaweza kukupata ghafula. Mtu mmoja aliyepooza akumbuka hivi: “Niliaibika sana kwamba nilipatwa na hali hiyo kwa sababu ya aksidenti moja ya kipumbavu!”

      Huenda ukaanza kujitenga na wengine. Kujitenga na wengine kwaweza kusababisha upweke kwa urahisi. Iwapo ugonjwa wako wakuzuilia nyumbani, huenda usiweze tena kushirikiana na marafiki wa zamani. Lakini, huo ndio wakati unapotamani sana ushirika wa wengine kuliko wakati mwingine wowote. Baada ya kukutembelea na kukupigia simu kwa bidii sana mwanzoni, sasa ni watu wachache zaidi na zaidi wanaokutembelea au kukupigia simu.

      Kwa kuwa inaumiza kuona marafiki wakijitenga nawe, huenda hali hiyo yenye kutia uchungu ikakufanya ujitenge kabisa na wengine. Bila shaka, inaeleweka kwamba waweza kuhitaji kuwa peke yako kabla ya kushirikiana na wengine tena. Lakini ikiwa utajitenga na wengine zaidi wakati huu, huenda hali yako ya kukosa marafiki (ambapo wengine hawakutembelei) ikutumbukize katika upweke wa kihisia-moyo (ambapo hutaki kuwaona wengine). Vyovyote vile, yaelekea unapambana na hisia kali mno za upweke.a Nyakati nyingine, huenda ukawa na tashwishi iwapo utaendelea kuishi.

      Kujifunza Kutokana na Wengine

      Hata hivyo, kuna tumaini. Iwapo umekumbwa na ugonjwa hivi karibuni, kuna hatua madhubuti unazoweza kuchukua ambazo zitakusaidia kudhibiti tena maisha yako kwa kadiri fulani.

      Bila shaka, mfululizo huu wa makala hautasuluhisha ugonjwa wowote ule wa kudumu ulio nao. Lakini, habari iliyotolewa yaweza kukusaidia kujua jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wako. Mwanamke mmoja mwenye kansa alisema hivi kwa ufupi kuhusu mawazo na hisia zake: “Baada ya kutokubali hali yangu nilishikwa na hasira kali kisha nikaanza kutafuta msaada.” Wewe pia waweza kutafuta msaada, kwa kuzungumza na watu ambao wamepatwa na hali hiyohiyo na ujifunze kutokana nao jinsi unavyoweza kunufaika na msaada wa wengine walio karibu nawe.

      [Maelezo ya Chini]

      a Bila shaka, watu wengi hupatwa na hisia hizo mbalimbali kwa njia na hali mbalimbali.

  • Kuishi kwa Mafanikio na Ugonjwa Wako—Jinsi Gani?
    Amkeni!—2001 | Januari 22
    • Kuishi kwa Mafanikio na Ugonjwa Wako—Jinsi Gani?

      UWE na hakika kwamba hisia ambazo yaelekea zinakukumba zinatarajiwa kuwapo. Ijapokuwa huenda ukawa mgonjwa au ukawa umelemaa kimwili, akili yako hukinza mabadiliko ambayo yamesababishwa na ugonjwa wako. Huenda ikaonekana kana kwamba unapambana kufa kupona na ugonjwa wako, huku ukifikiria sana hali yako ya awali na hali yako ya baadaye. Na hivi sasa huenda ikaonekana kana kwamba ugonjwa wako unakulemea. Lakini unaweza kubadili hali hiyo. Jinsi gani?

      “Ugonjwa unapomwathiri mtu vibaya,” asema Dakt. Kitty Stein, “anahisi ni kama amefiwa.” Hivyo basi, afya yako ambayo ni ya thamani sana inapozorota, ni kawaida kuomboleza na kulia kwa muda fulani, kama vile ambavyo ungefanya endapo ungefiwa na mpendwa wako. Kwa kweli, huenda ukaathiriwa kwa njia nyingine mbali na afya yako. Ni kama mwanamke mmoja anavyoeleza, “Ilinibidi kuacha kazi yangu. . . . Ilinibidi kupoteza uhuru ambao nilikuwa nikifurahia daima.” Hata hivyo, uwe na maoni yaliyosawazika kuhusu matokeo hayo yote. “Omboleza kuhusu hali uliyopoteza,” aongezea Dakt. Stein, ambaye ana ugonjwa wa kukakamaa kwa tishu (multiple sclerosis), “lakini wahitaji pia kufahamu uwezo ambao ungali nao.” Kwa kweli, baada ya kupambana na kilio chako mwanzoni, utagundua kwamba ungali na uwezo muhimu sana. Kwanza, una uwezo wa kunyumbulika.

      Baharia hawezi kudhibiti dhoruba, bali anaweza kustahimili dhoruba kwa kurekebisha matanga ya merikebu yake. Vivyo hivyo, huenda usiweze kudhibiti ugonjwa ambao umekukumba kama dhoruba, lakini unaweza kukabiliana nao kwa kurekebisha “matanga” yako, yaani, uwezo wako wa kimwili, kiakili, na kihisia-moyo. Nini kimewasaidia watu wengine wenye ugonjwa wa kudumu kufanya hivyo?

      Jifunze Kuhusu Ugonjwa Wako

      Baada ya kustahimili uchungu wanaohisi ugonjwa wao unapogunduliwa, watu wengi huhisi kwamba kujua ukweli huo mchungu ni bora kuliko kuhofu bila msingi. Hofu yaweza kukuzuia kutenda, ilhali kujua hali yako kwaweza kukusaidia kufikiria hatua unayoweza kuchukua—na kufanya hivyo tu hunufaisha. “Fikiria furaha unayokuwa nayo unapobuni mbinu ya kusuluhisha tatizo linalokuhangaisha,” asema Dakt. David Spiegel wa Chuo Kikuu cha Stanford. “Kabla hujafanya lolote, punguza wasiwasi wako kwa kupanga hatua ya kuchukua.”

      Huenda ukaona uhitaji wa kujifunza mengi kuhusu hali yako. Ni kama tu mithali moja ya Biblia inavyosema, “mtu mwenye maarifa huongeza uwezo.” (Mithali 24:5) “Azima vitabu kutoka kwenye maktaba. Jifunze mengi kadiri uwezavyo kuhusu ugonjwa wako,” ashauri mwanamume mmoja aliye mgonjwa kitandani. Kadiri unavyojifunza kuhusu matibabu yaliyopo na mbinu za kukabiliana na ugonjwa, huenda ukaona kwamba hali yako labda si mbaya kama ulivyohofia. Huenda hata ukapata sababu za kutarajia mema.

      Hata hivyo, lengo lako kuu si kuwa tu na maarifa ya ugonjwa wako. Dakt. Spiegel aeleza hivi: “Ukusanyaji huo wa habari ni sehemu muhimu ya kukabiliana na ugonjwa, kuuelewa, na kuwa na maoni yanayofaa kuuhusu.” Kukubali kwamba maisha yako yamebadilika ujapokuwa hai si jambo rahisi na kwa kawaida huchukua muda. Lakini hatua hii ya ziada—ya kutokuwa tu na maarifa ya ugonjwa wako bali kuukubali kihisia—ni hatua unayoweza kuchukua. Vipi?

      Kupata Usawaziko Unaofaa

      Huenda ukalazimika kurekebisha maoni yako kuhusu maana ya kukubali ugonjwa wako. Kwani, kukubali kwamba wewe ni mgonjwa hakumaanishi umeshindwa, kama vile tu haimaanishi baharia ameshindwa kwa kukubali uhakika wa kwamba yuko katika dhoruba. Badala yake, kukubali kwamba anakabili dhoruba humchochea kutenda. Hali kadhalika, kukubali kwamba wewe ni mgonjwa hakumaanishi umeshindwa, lakini humaanisha “kupiga hatua kuelekea upande mwingine,” ndivyo alivyosema mwanamke mmoja mwenye ugonjwa wa kudumu.

      Hata ingawa uwezo wako wa kimwili umedidimia, yamkini utahitaji kujikumbusha kwamba sifa zako za kiakili, kihisia-moyo, na kiroho hazihitaji kuathiriwa. Mathalani, je, uwezo wako wa kufikiri na wa kupanga mambo na kusababu ungalipo? Labda ungali unatabasamu kwa uchangamfu, ungali unawajali wengine, ungali na uwezo wako wa kusikiliza wengine kwa makini na kuwa rafiki wa kweli. Na la muhimu zaidi ni kwamba ungali na imani katika Mungu.

      Zaidi ya hayo, kumbuka kwamba ijapokuwa huwezi kubadili hali yako, bado unaweza kuamua jinsi ya kuitikia hali hiyo. Irene Pollin wa Taasisi ya Taifa ya Kansa asema: “Ni jukumu lako kuamua utakavyoitikia ugonjwa wako. Unaweza kufanya hivyo haidhuru athari ya ugonjwa wako.” Helen, mwanamke mwenye umri wa miaka 70 aliyedhoofishwa sana na ugonjwa wa kukakamaa kwa tishu, athibitisha hilo: “Kuwa tena na usawaziko wa kiakili na kihisia-moyo hakutegemei ugonjwa wako bali jinsi unavyoitikia ugonjwa huo.” Mtu mmoja ambaye amekabiliana na ulemavu kwa miaka kadhaa asema hivi: “Mtazamo chanya ni kama mkuku unaosawazisha merikebu.” Kwa kweli, Mithali 18:14 yasema hivi: “Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki