Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kazini Au vitani?
    Amkeni!—2004 | Mei 8
    • Kazini Au vitani?

      NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UJERUMANI

      “Singevumilia tena. Nilifanya kazi katika kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 30. Hata nilikuwa msimamizi kazini. Kisha tukapata meneja mpya. Alikuwa kijana mwenye uwezo na akili nyingi. Aliniona kuwa kizuizi kwa maendeleo ya kampuni, kwa hiyo akaanza kunionea. Baada ya kunitusi, kusema uwongo juu yangu, na kuniaibisha kwa miezi kadhaa, nilichoka kiakili. Nilipoahidiwa na kampuni hiyo kwamba ningepata malipo ya kustaafu, nilikubali kuacha kazi.”—Peter.a

      PETER, anayeishi Ujerumani, alikuwa akidhulumiwa kazini. Inakadiriwa kwamba watu milioni 1.2 hudhulumiwa kazini nchini humo. Nchini Uholanzi, mtu 1 kati ya 4 atadhulumiwa kazini wakati fulani maishani. Na kulingana na ripoti moja ya Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi, tatizo la kudhulumiwa kazini linaongezeka nchini Australia, Austria, Denmark, Marekani, Sweden, na Uingereza. Lakini, ni nini hutokea mtu anapodhulumiwa kazini?

      ‘Kuteseka Akili’

      Kulingana na gazeti Focus la Ujerumani, mtu anayedhulumiwa kazini “huonewa mara nyingi kwa njia maalumu.” Kudhulumiwa kazini kunahusisha mengi zaidi ya kudhihakiwa, kuchambuliwa, kuchokozwa, na kufanyiwa mzaha. Wafanyakazi hupanga kumtesa mfanyakazi mwenzao kiakili. Lengo ni kumfanya yule anayedhulumiwa ahisi kwamba hafai hata kidogo.b

      Mbinu za kumdhulumu mtu hutia ndani dhihaka za kitoto na hata jeuri. Anayedhulumiwa huharibiwa jina, hutukanwa, huchokozwa, na kunyamaziwa. Wengine hupewa kazi nyingi kupita kiasi au kila wakati wanapewa kazi mbaya-mbaya ambazo wafanyakazi wengine hawataki kuzifanya. Huenda wafanyakazi wengine wakamzuia mtu kufanya kazi vizuri, labda kwa kutompa habari anazohitaji. Katika visa fulani, wafanyakazi wengine wamepasua tairi za gari au kuingilia na kuharibu kompyuta ya mtu wanayemdhulumu.

      Watu fulani hudhulumiwa na mtu mmoja. Lakini mara nyingi mtu hudhulumiwa na wafanyakazi wengi.

      Jambo la kushangaza ni kwamba mara nyingi mameneja huruhusu dhuluma kazini. Katika uchunguzi uliofanywa huko Ulaya, wasimamizi walihusika sana katika asilimia 50 hivi ya visa vya dhuluma, na mara nyingi wao ndio waliowadhulumu wengine. Kulingana na gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani, mbinu hizo zote za dhuluma huwafanya wafanyakazi “wateseke sana kiakili.”

      Madhara ya Kudhulumiwa

      Mara nyingi, dhuluma inayotokea kazini husababisha madhara mengine maishani. Watu wengi hupatwa na magonjwa mabaya sana kwa sababu ya kudhulumiwa. Baadhi ya madhara ya kudhulumiwa ni kushuka moyo, kukosa usingizi, na kushtuka mara kwa mara. Ni madhara gani yaliyompata Peter, aliyetajwa mwanzoni? Alijiona kuwa hafai kabisa. Mwanamke mmoja anayeitwa Margaret, ambaye anaishi Ujerumani pia, alishauriwa na daktari wake apate matibabu kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili. Kwa nini? Kwa sababu ya kudhulumiwa kazini. Pia kudhulumiwa kunaweza kuathiri ndoa au maisha ya familia.

      Huko Ujerumani, dhuluma imeongezeka sana kazini hivi kwamba kampuni moja ya bima ya afya imeanzisha huduma za kuwashauri watu wenye matatizo au maswali kupitia simu. Kampuni hiyo iligundua kwamba zaidi ya nusu ya watu waliopiga simu hawakuweza kufanya kazi kwa majuma sita, thuluthi moja hivi hawakuweza kufanya kazi kwa miezi mitatu, na zaidi ya asilimia 10 hawakuweza kufanya kazi kwa zaidi ya miezi mitatu. Jarida moja la kitiba la Ujerumani linakadiria kwamba “asilimia 20 ya visa vya kujiua husababishwa na kudhulumiwa kazini.”

      Kwa kweli, mtu anaweza kuogopa sana anapodhulumiwa kazini. Je, dhuluma hiyo inaweza kuzuiwa? Wafanyakazi wanaweza kufanya nini ili kuwe na amani kazini?

      [Maelezo ya Chini]

      a Majina yaliyotumiwa katika mfululizo huu wa makala yamebadilishwa.

      b Ripoti zinaonyesha kwamba wanawake ndio hudhulumiwa zaidi kazini kuliko wanaume, labda kwa sababu wanawake huzungumzia tatizo hilo na kutafuta msaada kuliko wanaume.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Watu wanaodhulumiwa kazini huteseka kiakili

  • Jinsi Watu Wanavyolengwa
    Amkeni!—2004 | Mei 8
    • Jinsi Watu Wanavyolengwa

      Mara tu baada ya kumaliza shule, Monika alianza kuzoezwa kuwa karani katika kampuni moja ya sheria. Monika alitazamia kufanya kazi baada ya kumaliza shule.

      Horst alikuwa daktari akiwa na umri wa miaka 30 na kitu. Alikuwa na mke na watoto, na ilionekana wazi kwamba angepata sifa na mshahara mnono.

      Monika na Horst walidhulumiwa kazini.

      TUNAJIFUNZA jambo muhimu kutokana na visa vya Monika na Horst: Haijulikani ni nani atakayedhulumiwa kazini. Mfanyakazi yeyote anaweza kudhulumiwa. Basi unaweza kujilindaje? Njia moja ni kujifunza jinsi ya kuwa mwenye amani kazini hata kukiwa na wafanyakazi wagumu.

      Kusikilizana na Wafanyakazi Wenzako

      Watu wengi hulazimika kufanya kazi na watu kadhaa na kushirikiana ili wafanikishe kazi. Wafanyakazi wakielewana, wanafanya kazi vizuri. Wasipoelewana, hawafanyi kazi vizuri na kuna uwezekano mkubwa wa kudhulumiwa.

      Ni nini kinachoweza kuwafanya watu washindwe kufanya kazi vizuri pamoja? Sababu moja ni kwamba huenda wafanyakazi wakabadilishwa mara nyingi. Katika hali kama hiyo, inakuwa vigumu kuwa na marafiki. Isitoshe, wafanyakazi wapya hawajui utaratibu wa kazi, na hilo huwazuia wafanyakazi wote kufanya kazi haraka. Kazi ikiongezeka, wanaweza kuwa na mfadhaiko kila wakati.

      Isitoshe, wafanyakazi hao wasipokuwa na miradi hususa, hakutakuwa na umoja. Kwa mfano, hilo linaweza kutokea wakati msimamizi asiyejiamini anapotumia muda mwingi kutetea cheo chake badala ya kusimamia kazi. Hata huenda akajaribu kufanya hivyo kwa kuwagonganisha wafanyakazi. Pia, huenda wafanyakazi fulani wasijue majukumu yao kwa sababu hayajabainishwa waziwazi. Kwa mfano, wafanyakazi wawili wanaweza kugombana ikiwa kila mmoja wao anadhani kwamba yeye ndiye mwenye jukumu la kuidhinisha invoisi.

      Katika hali hiyo, wafanyakazi hunyamaziana na mara nyingi hawasuluhishi mambo. Wivu huwafanya wasielewane na kuwachochea kushindana ili kupata kibali cha mkubwa. Makosa madogo huonwa kuwa makubwa. Basi, matatizo madogo yanakuwa matatizo makubwa. Hivyo, dhuluma inaweza kutokea.

      Jinsi Dhuluma Inavyoanza

      Baada ya kipindi fulani, huenda mfanyakazi mmoja akaanza kudhulumiwa. Huenda jambo hilo likampata mtu wa aina gani? Inaelekea ni mtu aliye tofauti na wengine. Kwa mfano, anaweza kuwa mwanamume anayefanya kazi na wanawake au mwanamke anayefanya kazi na wanaume. Huenda mtu anayejiamini akaonekana kuwa mchokozi, hali mtu mnyamavu akaonwa kuwa mdanganyifu. Huenda mtu anayeweza kudhulumiwa akawa mwenye umri mkubwa au kijana kuliko wengine au hata ndiye anayestahili zaidi kazi hiyo.

      Haidhuru ni nani anayedhulumiwa, jarida la kitiba la mta la Ujerumani linasema kwamba wafanyakazi “huanza kumtesa na kumwonea mtu waliyechagua kudhulumu ili kujituliza kutokana na mfadhaiko wao.” Mtu anayedhulumiwa anapojaribu kusuluhisha hali hiyo huenda asifanikiwe sana na hata huenda mambo yakachacha. Kadiri dhuluma inavyozidi, ndivyo yule anayedhulumiwa anavyojihisi mpweke zaidi. Wakati huo, huenda anayedhulumiwa akashindwa kupambana na hali hiyo akiwa peke yake.

      Bila shaka, watu wamekuwa wakidhulumiwa kazini sikuzote. Lakini huenda wengi wakakumbuka wakati ambapo wafanyakazi walishirikiana. Wafanyakazi hawakupanga kuwadhulumu wengine. Lakini kama vile daktari mmoja alivyosema, kwa miaka mingi “watu wameacha kuwa na umoja na hawajali.” Sasa watu hawajali hata wakipigana kazini.

      Hivyo, wote walioajiriwa wangependa sana kupata majibu kwa maswali haya: Je, dhuluma inaweza kuzuiwa? Watu wanawezaje kufanya kazi pamoja kwa amani?

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Lengo la dhuluma ni kumfanya mtu ahisi kwamba hafai hata kidogo

  • Kuwa Wenye Amani Kazini
    Amkeni!—2004 | Mei 8
    • Kuwa Wenye Amani Kazini

      KWA nini watu fulani huwadhulumu wengine? Biblia inatusaidia kuelewa jambo hilo. Inaeleza kwamba tunaishi katika “siku za mwisho” za mfumo huu wa mambo na ndiyo sababu tunakabili “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” Watu wengi ni “wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda pesa, wenye kujidai, wenye majivuno, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio washikamanifu, wasio na upendo wa asili, wasiotaka makubaliano yoyote, wachongezi, wasiojizuia, wakali, wasiopenda wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kujivuna kwa kiburi.” (2 Timotheo 3:1-5) Katika nyakati hizi ngumu, tabia hizo zimezidi na dhuluma ni mojawapo ya matokeo yake. Basi unawezaje kuwa mwenye amani kazini?

      Kutatua Hali ya Kutoelewana

      Mara nyingi dhuluma huanza wakati ambapo wafanyakazi hawatatui hali ya kutoelewana. Hivyo, badala ya kujiingiza katika mambo ya wengine, tatua mambo haraka usipoelewana na wengine. Tatua hali hiyo kwa busara na heshima. Zungumza na mtu mmoja-mmoja wala si kikundi. Ukiona kwamba mtu ana jambo dhidi yako, jaribu kusuluhisha mambo kabisa. Kumbuka shauri hili la Yesu: “Uwe tayari kusuluhisha mambo upesi pamoja na mtu anayekushtaki.”—Mathayo 5:25.

      Isitoshe, kila mtu kazini hufaidika kunapokuwa na mawasiliano mazuri. Basi, jaribu kuzungumza vizuri na msimamizi wako bila kuonyesha kwamba unajaribu kujipendekeza kwake. Pia, kumbuka kwamba mawasiliano mazuri pamoja na wafanyakazi wenzako na wasaidizi wako yatakusaidia kushinda mfadhaiko. Mfalme Sulemani aliandika hivi: “Mipango huvunjika mahali ambapo hapana mazungumzo ya siri, lakini katika wingi wa washauri mambo hutimizwa.”—Methali 15:22.

      Hivyo, jitahidi juu chini kupatana na wafanyakazi wenzako. Hiyo haimaanishi ufanye mambo ili kuwapendeza watu tu kwa kukubali kila kitu shingo upande huku ukivunja kanuni zako eti ili udumishe amani. Lakini ukiwa mchangamfu na mwenye urafiki unaweza kuboresha hali. Uwe mwangalifu kuhusu yale unayosema na jinsi unavyoyasema. Biblia inatoa mashauri haya ya busara: “Jibu, linapokuwa la upole, hugeuza ghadhabu.” (Methali 15:1) “Utulivu wa ulimi ni mti wa uzima.” (Methali 15:4) “Kwa subira kiongozi hushawishiwa.” (Methali 25:15) “Maneno yenu na yawe yenye neema sikuzote, yenye kukolezwa chumvi, ili mjue jinsi mnavyopaswa kumjibu kila mtu.”—Wakolosai 4:6.

      “Usawaziko Wenu na Ujulikane”

      Mtume Paulo aliwashauri hivi Wakristo huko Filipi: “Usawaziko wenu na ujulikane kwa watu wote.” (Wafilipi 4:5) Ukifuata kanuni hiyo, jiwekee viwango vya mwenendo unaofaa. Epuka kujiamini kupita kiasi au kuwa mwenye haya sana. Wafanyakazi wenzako wakikuudhi, usijaribu kulipiza kisasi. Hutapata faida yoyote kwa kutenda maovu. Watendee wengine kwa heshima na staha, na inaelekea watakutendea vivyo hivyo.

      Zaidi ya kufikiria mwenendo wako, fikiria pia mavazi yako. Jiulize: ‘Mavazi yangu yanaonyesha nini? Je, mavazi yangu yanaamsha tamaa mbaya? Je, ninavalia shaghalabaghala? Je, nijiwekee sheria kuhusiana na mavazi nitakayovaa kazini?’

      Katika tamaduni nyingi, wafanyakazi wenye bidii wanaheshimiwa na kuthaminiwa sana. Kwa hiyo, jaribu kupata heshima kwa kufanya kazi kwa ustadi. Uwe mwenye kutegemeka na mwenye kuaminika. Hiyo haimaanishi ujaribu kufanya kila kitu kikamilifu. Mwanamke mmoja aliyedhulumiwa alikubali baadaye kwamba yeye ndiye aliyesababisha hali hiyo. Anasema: “Nilitaka kuwa mkamilifu.” Baadaye, mwanamke huyo alitambua kwamba haiwezekani kuwa mkamilifu: “Mimi hufanya kazi vizuri, lakini si lazima nifanye kila kitu kikamilifu.”

      Usiathiriwe kupita kiasi na maneno yanayoumiza. Wakati mwingine unapochambuliwa bila sababu, hiyo haimaanishi unadhulumiwa. Mfalme Sulemani aliandika hivi katika Biblia: “Usiwe na haraka kuudhika katika roho yako . . . Pia, usiweke moyoni mwako maneno yote ambayo huenda watu wakasema, . . . kwa maana moyo wako mwenyewe unajua vema kwamba hata mara nyingi wewe, naam hata wewe, umewalaani wengine.”—Mhubiri 7:9, 21, 22.

      Kwa kweli, kufuata kanuni hizo nzuri hakumaanishi kwamba hutadhulumiwa kamwe. Licha ya jitihada zako nzuri, huenda wafanyakazi wengine wakakudhulumu. Ufanye nini?

      Tafuta Msaada

      Gregory anasema hivi: “Nilipopuuzwa na wafanyakazi wenzangu kwa miezi kadhaa, niliumia kihisia.” Yaliyompata ni kama yale yanayowapata wale wanaodhulumiwa ambao hukasirika, hujiona kuwa wenye hatia, huaibika, huchanganyikiwa na kujiona kuwa hawafai. Kudhulumiwa kunaweza kumfanya hata mtu aliye imara kufadhaika. Biblia inasema kwamba “uonevu mtupu unaweza kumfanya mtu mwenye hekima atende kiwazimu.” (Mhubiri 7:7) Kwa hiyo ufanye nini?

      Uchunguzi unaonyesha kwamba haifai kushughulikia dhuluma bila kuomba msaada. Anayedhulumiwa anaweza kupata wapi msaada? Makampuni fulani makubwa yanawasaidia wafanyakazi wao wanaohisi kwamba wanadhulumiwa. Makampuni hayo yanajua kwamba yatafaidika kwa kukomesha dhuluma. Kulingana na kadirio moja, wafanyakazi wanaowadhulumu wengine hutumia asilimia 10 ya muda wa kazi kufanya hivyo. Ikiwa kuna mpango wa kuwasaidia wanaodhulumiwa, mtu anaweza kuomba msaada huo. Mshauri wa kampuni hiyo au kampuni nyingine ambaye hana upendeleo, anaweza kuwasaidia wote wanaohusika kuzungumzia hali hiyo na kuwa na mwenendo mzuri kazini.

      Hakuna Suluhisho Kamili

      Inafaa tutambue kwamba hakuna suluhisho kamili la dhuluma. Hata wale wanaotumia kanuni za Biblia zinazopatikana katika makala hii huenda wakaendelea kudhulumiwa kazini. Hapana shaka kwamba Yehova Mungu anaona uvumilivu wao na jitihada zao za kuonyesha sifa za Kikristo licha ya hali ngumu.—2 Mambo ya Nyakati 16:9; Yeremia 17:10.

      Dhuluma inapozidi, wengine huamua kutafuta kazi nyingine. Wengine hawana la kufanya kwa kuwa huenda si rahisi kupata kazi nyingine au msaada. Monika, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, aliona kwamba tatizo lake lilisuluhishwa baada ya muda wakati mmoja wa wale waliokuwa wakimdhulumu sana alipoacha kazi. Hivyo, kukawa na amani kazini na alimaliza mafunzo yake kabla ya kuamua kutafuta kazi mahali pengine.

      Peter, aliyetajwa katika makala ya kwanza, alitulia kabisa alipostaafu mapema. Hata hivyo, Peter alisaidiwa na mke wake alipokuwa akidhulumiwa. Anasema: “Alijua mambo yaliyokuwa yakinipata, naye aliniimarisha sana.” Kwa kuwa Monika na Peter ni Mashahidi wa Yehova, waliimarishwa na imani yao walipokuwa wakivumilia majaribu hayo. Walipofanya kazi ya kuhubiri walijiheshimu zaidi, na waliposhirikiana na waamini wenzao walihakikishiwa kwamba wana marafiki wenye kutegemeka.

      Hata uwe katika hali gani, jitahidi uwezavyo kupatana na wafanyakazi wenzako. Ukidhulumiwa, jitahidi kufuata shauri hili la mtume Paulo: “Msimlipe yeyote uovu kwa uovu. . . . Ikiwezekana, kwa kadiri inavyowategemea ninyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote. . . . Usiache ushindwe na uovu, bali endelea kuushinda uovu kwa wema.”—Waroma 12:17-21.

      [Blabu katika ukurasa wa 8]

      Ukiwa mchangamfu na mwenye urafiki unaweza kuboresha hali

      [Blabu katika ukurasa wa 9]

      “Ikiwezekana, kwa kadiri inavyowategemea ninyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote.”—WAROMA 12:18

      [Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Shughulikia haraka hali ya kutoelewana

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki