Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Waliyaita Vitumbuizo
    Amkeni!—1997 | Mei 22
    • Waliyaita Vitumbuizo

      UWANJA huo wa duara ulijawa na msisimko. Makumi ya maelfu yalikuwa yamekusanyika kwa ajili ya mojawapo tamasha zenye kusisimua zaidi za Roma ya kale. Bendera, waridi, na mazulia ya ukutani yenye rangi yaliremba uwanja kwa furaha. Chemchemi zilirusha maji yaliyotiwa manukato, yakibadili hewa kidogo kwa harufu zenye kupendeza. Matajiri walijipamba kwa mavazi yao ya kifahari kupita yote. Kelele za umati ziliingiliwa pindi kwa pindi na mianguo ya vicheko, lakini furaha hiyo ilikuwa kinyume cha mambo yenye kuogofya yaliyokuwa karibu kutukia.

      Muda si muda mlio wa tarumbeta wenye kuashiria hali mbaya uliita wapiganaji wawili waje kwenye pigano. Umati ulikuwa katika hali ya kichaa washindanaji hao walipoanza kukatana-katana kwa ukatili usio na huruma. Kugongana kwa panga hakukuweza kusikika kwa sababu ya kelele za kushangilia zenye kutia uziwi za watazamaji. Ghafula, kwa mbinu yenye wepesi, mshindani mmoja alimwangusha mpinzani wake. Matokeo ya baadaye ya mpiganaji aliyeangushwa yalikuwa mikononi mwa watazamaji. Ikiwa wangepunga vitambaa vyao vya mkononi, angeishi. Kwa ishara moja tu ya vidole gumba vyao, kusanyiko hilo—wanawake na wasichana wakiwa ndani—liliamuru pigo la kifo. Kwa dakika chache tu mwili usio na uhai uliburutwa kutoka kwenye sakafu ya uwanja, mchanga uliolowa damu ulilimwa kwa sepetu, mchanga mwingine ulitapakazwa, na umati ulijiandaa kwa machinjo yaliyobaki.

      Kwa watu wengi walioishi katika Roma ya kale, hayo yalionwa kuwa kitumbuizo. “Hata wafundishaji kamili wa maadili hawakupinga ufurahiaji huu wa umwagikaji wa damu,” chasema kitabu Rome: The First Thousand Years. Na mchezo wa upiganaji hadi kifo ulikuwa aina moja tu ya vitumbuizo vilivyozorota ambavyo Roma iliandaa. Mapigano halisi ya kimanowari yalifanywa ili watazamaji wenye tamaa ya kumwagwa kwa damu wafurahie. Hata ufishaji wa hadharani ulifanywa, ambapo mhalifu aliyehukumiwa kifo angefungwa kwenye mti wa mateso na kunyafuliwa na mahayawani-mwitu walioshindishwa njaa.

      Kwa wale ambao hawakupendelea umwagikaji wa damu, Roma iliandaa mchanganyiko wa michezo ya jukwaani. Kwenye maigizo hayo—michezo mifupi kuhusu maisha ya kila siku—“uzinzi na mahusiano ya kimapenzi ndiyo yalikuwa vichwa vikuu,” akaandika Ludwig Friedländer katika Roman Life and Manners Under the Early Empire. “Lugha iliyotumiwa ilijaa usemi wenye matusi, na vichekesho vilikuwa vya utovu wa adabu, kukiwa na wingi wa kukunja uso, ishara za mwili zenye matusi, na zaidi ya yote, dansi za kustaajabisha za mwambatano wa filimbi.” Kulingana na The New Encyclopædia Britannica, “kuna uthibitisho kwamba vitendo vya uzinzi vilifanywa kihalisi kwenye jukwaa la maigizo wakati wa Milki ya Roma.” Kwa sababu nzuri Friedländer aliyaita maigizo hayo “kwa wazi aina ya mwigizo wa kushangaza ulio mbaya sana kuliko yote katika ukosefu wa adili na uchafu,” na akaongeza: “Maonyesho yaliyokuwa machafu zaidi ndiyo yaliyoshangiliwa zaidi.”a

      Namna gani leo? Je, upendezi wa mwanadamu katika vitumbuizo umebadilika? Fikiria uthibitisho, kama unavyozungumziwa kwenye makala ifuatayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Nyakati fulani, ufishaji ulikuwa ukifanywa jukwaani ili kufanya maonyesho ya kidrama yawe halisi. Kitabu The Civilization of Rome chaonelea hivi: “Lilikuwa jambo la kawaida kwa mhalifu aliyehukumiwa kifo kuchukua mahali pa mwigizaji wakati wa msiba.”

  • Ni Nini Kimepata Vitumbuizo?
    Amkeni!—1997 | Mei 22
    • Ni Nini Kimepata Vitumbuizo?

      WAROMA wa kale, ambao walipaswa kuwa kwenye kilele cha kustaarabika, wangewezaje kuona maumivu ya binadamu wenzao kuwa kitumbuizo? “Yaweza kuelezwa tu na tamaa ya kupata visisimuaji vipya vyenye nguvu zaidi,” aandika Gerhard Uhlhorn katika The Conflict of Christianity With Heathenism. “Wakiwa wamekinai ufurahio wote uwezekanao, watu walitafuta . . . msisimko ambao hawakuupata kwingineko kote.”

      Watu wengi leo hudhihirisha “tamaa [kama hiyo] ya visisimuaji vipya na vyenye nguvu.” Ni kweli, huenda wasikusanyike kutazama machinjo halisi au uzinifu. Lakini chaguo lao la vitumbuizo hufunua tamaa kama hiyo ya jeuri na ngono. Fikiria baadhi ya vielelezo.

      Sinema. Katika miaka ya hivi majuzi watengeneza filamu wamedhihirisha “upendezi kuelekea upotovu,” asisitiza mchambuzi wa sinema Michael Medved. “Wazo kuu katika fungu la sinema,” yeye aongeza, “laonekana kuwa kwamba maonyesho ya ukatili na kichaa yastahili kufikiriwa zaidi, kupokea staha zaidi, kuliko jitihada zozote za kuwasilisha wema au uzuri.”

      Kushindana na televisheni kumelazimisha watengeneza filamu wafanye chochote kile ili kushawishi watu waende kwenye majumba ya sinema. “Twahitaji sinema zenye kustaajabisha, zenye ukali, ambazo zinatofautiana sana na programu ambazo watu huona kwenye televisheni,” asema mwenyekiti wa studio moja ya sinema. “Si kwamba tumejitoa kuonyesha umwagikaji wa damu na lugha [chafu], bali hayo ndiyo yanayohitajiwa leo ili kutengeneza filamu.” Kwa hakika, wengi hata hawashtuliwi tena na jeuri nyingi ya waziwazi kabisa ya sinema. “Watu wanakufa ganzi kwa habari ya jeuri ya sinema,” asema mkurugenzi wa sinema Alan J. Pakula. “Kiasi cha wanaouawa kimeongezeka mara nne, nguvu za mlipuko zimeongezeka sana, na watu hawashtuki. Wamesitawisha tamaa kubwa sana ya msisimko wenye ukatili.”

      Televisheni. Maonyesho mabaya sana ya ngono kwenye televisheni sasa ni ya kawaida katika sehemu nyingi za ulimwengu, kutia ndani Brazili, Ulaya, na Japani. Mtazamaji wa wastani wa televisheni katika Amerika huona marejezeo ya kingono yapatayo 14,000 kwa mwaka mmoja tu. “Kuongezeka kwa vichwa vikuu kuhusu ngono na maonyesho ya waziwazi hakuonyeshi ishara yoyote ya kukoma,” charipoti kikundi kimoja cha utafiti. “Mambo ambayo wakati mmoja yalikuwa mwiko kama vile ngono ya maharimu, kupata raha kwa kutendea wengine kwa ukatili, na ngono na mnyama yamekuwa njia ya kupata faida ya vipindi vya televisheni vya wakati wa jioni.”

      Kulingana na kitabu Watching America, kuna sababu ya kuruhusu kila kitu katika programu zinazoonyeshwa kwenye televisheni. Hicho husema: “Kuonyesha ngono huleta faida nyingi. . . . Kampuni za kutokeza vipindi vya televisheni zilipogundua kwamba zilikuwa zikisisimua watazamaji wengi zaidi ya wale wenye kuchukizwa, zimeongeza hatua kwa hatua uwezekano wa kupata faida kwa vipindi vyao kwa kuruhusu miiko mingi zaidi na zaidi ivunjwe na katika namna ya waziwazi sana.”

      Michezo ya Vidio. Muhula ulioonekana kuwa usio mbaya wa michezo ya vidio aina ya Pac-Man na Donkey Kong umeachia nafasi muhula mpya wa michezo yenye ukatili mbaya sana. Profesa Marsha Kinder afafanua michezo hii kuwa “mibaya zaidi kuliko televisheni au sinema. Hiyo huwasilisha ujumbe kwamba njia pekee ya kupata udhibiti na uwezo ni kupitia jeuri.”

      Kwa sababu ya hangaiko la umma, kampuni moja mashuhuri ya utengenezaji katika Marekani sasa inatumia mfumo wa kuainisha michezo yayo ya vidio. Kibandiko “MA-17”—kinachoonyesha kwamba mchezo huo wa “waliokomaa” haufai kwa wale walio chini ya umri wa miaka 17—chaweza kuwa na jeuri nyingi mno, habari za kingono, na lugha chafu. Hata hivyo, watu fulani wanahofu kwamba uainishaji wa “waliokomaa” utaongezea uvutio wa mchezo huo. “Kama ningekuwa na umri wa miaka 15 na nione kibandiko MA-17,” asema shabiki mmoja mchanga wa michezo, “ningefanya juu chini kuupata mchezo huo.”

      Muziki. Gazeti moja ambalo huchunguza sana yaliyomo katika muziki upendwao sana ladai kwamba mwishoni mwa mwaka 1995, ni rekodi 10 tu katika rekodi bora 40 ambazo hazikuwa na lugha chafu au marejezo ya dawa za kulevya, jeuri, au ngono. “Muziki upatikanao kwa wale hawajafikia ubalehe unashtua sana, mwingi wao unaonyesha waziwazi kwamba maadili ya kidesturi hayana msingi na hayafai,” laripoti St. Louis Post-Dispatch. “[Muziki] unaovutia wabalehe fulani umejaa hasira na hali ya kutokuwa na tumaini nao huchochea hisia za kwamba ulimwengu pamoja na yule anayesikia muziki huo wanaelekea kwenye maangamizi.”

      Mdundo wa kifo, roki ambayo gitaa inapigwa kwa mvurugo na muziki kuimbwa kivivu, na rapu ya magenge ya mitaani yaonekana hutukuza sana jeuri. Na kulingana na ripoti ya San Francisco Chronicle, “washiriki wa biashara ya vitumbuizo wanatabiri kwamba vikundi vya kuhofisha zaidi hivi karibuni vitakuwa na mafanikio na umashuhuri.” Nyimbo zenye kutukuza hasira na kifo sasa zimependwa na wengi katika Australia, Ulaya, na Japani. Ni kweli, bendi fulani zimejaribu kuwa na ujumbe ufaao. Hata hivyo, Chronicle laonelea, “Uthibitisho wadokeza kwamba hakuna uwezekano wa kupata faida kwa muziki usio na hatia.”

      Kompyuta. Hivi ni vifaa vyenye thamani na vyenye matumizi mengi yafaayo. Hata hivyo, zimetumiwa na watu wengine ili kusambaza habari zenye utovu wa adabu. Kwa kielelezo, gazeti Maclean’s laripoti kwamba hiyo yatia ndani “picha na maandishi kuhusu chochote kuanzia vitu vinavyopendwa na kuheshimiwa mno hadi ukahaba hadi kuvutiwa kingono na watoto—habari ziwezazo kushtua watu wazima wengi, licha ya kushtua watoto wao.”

      Habari ya Kusoma. Vitabu vingi vinavyopendwa na wengi vimejaa ngono na jeuri hadi pomoni. Mtindo wa hivi majuzi katika Marekani na Kanada ni ule ambao umeitwa “hadithi ya kubuni ya kushtua”—hadithi zenye kuogofya mno zinazoelekezwa kwa vijana wachanga wa umri wa miaka minane. Diana West, akiandika katika New York Teacher, adai kwamba vitabu hivi “vinatia ganzi watoto, vikizuia uwezo wa kiakili hata kabla ya huo kuanza.”

      Vitabu vingi vya ucheshi vinavyochapishwa katika Hong Kong, Japani, na Marekani huonyesha “habari nyingi mno za vita vikatili, ulaji wa nyama ya binadamu, kukatwa kichwa, ibada ya Shetani, ubakaji, na lugha chafu,” waripoti uchunguzi uliofanywa na National Coalition on Television Violence (NCTV). “Wingi wa jeuri na habari zilizopotoka kingono katika magazeti haya unashtua,” asema Dakt. Thomas Radecki, mkurugenzi wa utafiti wa NCTV. “Inaonyesha jinsi tumejiruhusu tufe ganzi.”

      Uhitaji wa Kutahadhari

      Kwa wazi, katika ulimwengu wa leo kuna hali ya kuvutiwa na ngono na jeuri, na hiyo yaonekana katika biashara ya vitumbuizo. Hali hiyo inafanana na ile iliyofafanuliwa na mtume Mkristo Paulo: “Wakiisha kuishiwa na hisia zote za adili, walijikabidhi wenyewe kwenye mwenendo mlegevu ili wafanye ukosefu wa usafi wa kila namna pamoja na pupa.” (Waefeso 4:19) Wakiwa na sababu ifaayo wengi leo hutafuta kitu bora zaidi. Je, ndivyo ilivyo na wewe? Ikiwa ndivyo, utafurahi kujua kwamba waweza kupata vitumbuizo vifaavyo, kama makala ifuatayo itakavyoonyesha.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      Televisheni Yaweza Kudhuru

      TELEVISHENI ilitokea hadharani mara ya kwanza Marekani kwenye maonyesho ya ulimwengu ya 1939 katika New York. Mwandishi mmoja wa habari aliyekuwapo alieleza tashwishi yake kuhusu wakati ujao wa kifaa hiki kipya. “Tatizo na televisheni,” akaandika, “ni kwamba ni lazima watu wakae na kukaza macho yao kwenye kiwambo; familia ya kawaida ya Marekani haina wakati kwa jambo hilo.”

      Alikosea kama nini! Kwa hakika, imesemekana kwamba kufikia wakati Mmarekani wa kawaida amalizapo shule, atakuwa ametumia asilimia 50 zaidi ya wakati mbele ya televisheni kuliko mbele ya mwalimu. “Watoto ambao ni watazamaji wa televisheni wa kupindukia ni wakali zaidi, wasiotazamia mazuri, ni wazito zaidi, hawana uwezo wa mawazo ya kubuni, hawana hisia-mwenzi sana, na ni wanafunzi wasio na uwezo sana kuliko wenzao ambao hawatazami sana televisheni,” adai Dakt. Madeline Levine katika kitabu chake Viewing Violence.

      Yeye atoa shauri gani? “Watoto wahitaji kufunzwa kwamba televisheni, kama tu kifaa kingine nyumbani, ina kazi hususa. Hatuachi kikausha nywele kikiendelea kufanya kazi wakati nywele zimekauka, au kioka mkate kikiendelea kufanya kazi wakati kipande cha mkate kimeokwa. Twatambua matumizi hususa ya vifaa hivi na twajua wakati wa kuvizima. Watoto wetu wahitaji kufunzwa vivyohivyo kuhusu televisheni.”

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Vitumbuizo Ulimwenguni

      Amkeni! liliomba waleta-habari walo kutoka sehemu kadhaa za ulimwengu wafafanue mielekeo ya vitumbuizo mahali walipo. Yafuatayo ni baadhi ya maelezo yao.

      Brazili: “Vipindi vya televisheni vimezidi kupotoka. Hata hivyo, huku wazazi wengi wakifanya kazi mbali na nyumbani, watoto mara nyingi wanaachwa wajitumbuize na televisheni. CD-ROM zilizo na habari kuhusu mambo ya kimafumbo na michezo ya vidio yenye kuonyesha jeuri mbaya zapendwa na wengi.”

      Jamhuri ya Cheki: “Tangu kuanguka kwa Ukomunisti, nchi hii imejawa na vitumbuizo ambavyo havijapata kuonwa hapa tena, kutia ndani vipindi vya televisheni kutoka Magharibi na maduka ya ponografia. Vijana huenda kwa ukawaida kwenye majumba ya disko, vilabu vya biliadi, na baa. Matangazo ya kupita kiasi na msongo wa marika mara nyingi huwa na uvutano mkubwa kwao.”

      Ujerumani: “Kwa kuhuzunisha, wazazi wengi wamechoka sana kupangia watoto wao vitumbuizo, kwa hiyo vijana wanategemeana ili kupata wakati wa kufurahia. Wengine wanajitenga wakiwa na michezo ya kompyuta. Wengine wanahudhuria vipindi vya usiku kucha vya dansi viitwavyo raves, ambapo dawa za kulevya ni nyingi mno.”

      Japani: “Vitabu vya ucheshi ni kipitisha wakati kipendwacho sana na vijana na watu wazima, lakini vimejaa jeuri, ukosefu wa adili, na lugha chafu. Kucheza kamari kumeenea pia. Mwelekeo mwingine wenye kusumbua ni kwamba wasichana fulani wanapiga simu kwenye vilabu vinavyotangazwa sana ambavyo hushughulikia wanaume wenye makusudi yasiyo ya adili. Wengine wanapiga ili kufurahia tu, ilhali wengine wanafikia hatua ya kupeana miadi ya kijinsia ili kulipwa, jambo ambalo katika visa fulani huongoza kwenye ukahaba.”

      Nigeria: “Majumba ya vidio yasiyodhibitiwa yanaenea Afrika Magharibi. Vibanda hivi hafifu huruhusu watu wa umri wote kuingia, kutia ndani watoto. Vidio za ponografia na za maogofyo huonyeshwa kwa ukawaida. Kwa kuongezea, filamu zilizotengenezwa hapa zinazoonyeshwa kwenye televisheni kwa kawaida huonyesha uwasiliani-roho.”

      Afrika Kusini: “Vipindi vya usiku kucha vya dansi vinasitawi hapa, na dawa za kulevya mara nyingi hupatikana kwa urahisi hapo.”

      Sweden: “Baa na vilabu vya usiku vinafanikiwa katika Sweden, na mara nyingi wahalifu na walanguzi wa dawa za kulevya humiminika mahali kama hapo. Vitumbuizo vya televisheni na vidio vimejaa jeuri, uwasiliani-roho, na ukosefu wa adili.”

  • Waweza Kupata Vitumbuizo Vifaavyo
    Amkeni!—1997 | Mei 22
    • Waweza Kupata Vitumbuizo Vifaavyo

      BIBLIA haishutumu raha za vitumbuizo, wala haioni ufurahio wa tafrija kuwa kupoteza wakati. Badala ya hivyo, Mhubiri 3:4 husema kwamba kuna “wakati wa kucheka” na “wakati wa kucheza.”a Watu wa Mungu katika Israeli la kale walifurahia aina tofauti-tofauti za vitumbuizo, kutia ndani muziki, kucheza dansi, na michezo. Yesu mwenyewe alihudhuria karamu kubwa ya arusi na, katika pindi nyingine, “karamu kubwa ya makaribisho.” (Luka 5:29; Yohana 2:1, 2) Kwa hiyo Biblia haipingi kuwa na wakati wa kufurahisha.

      Hata hivyo, kwa kuwa vingi vya vitumbuizo vya leo hutukuza mwenendo usiompendeza Mungu, swali lazuka, Waweza kufanya nini ili kuhakikisha kwamba viwango vyako vya kuchagua vitumbuizo vyabaki vikiwa vyenye kufaa?

      Uwe Mteuzi

      Katika kuteua vitumbuizo vyao, Wakristo watataka kuongozwa na kanuni za Biblia. Kwa kielelezo, mtunga-zaburi Daudi aliandika: “Yehova mwenyewe humchunguza mwadilifu na vilevile mwovu, na yeyote apendaye jeuri nafsi Yake kwa hakika humchukia.” (Zaburi 11:5, NW) Na Paulo aliandikia Wakolosai hivi: “Kwa hiyo, fisheni viungo vya mwili wenu vilivyo juu ya dunia kwa habari ya uasherati, ukosefu wa usafi, hamu ya ngono, tamaa yenye kuumiza, na tamaa . . . Yawekeni mbali nanyi hayo, hasira ya kisasi, hasira, ubaya, usemi wenye kuudhi, na maongezi yenye aibu kutoka katika kinywa chenu.”—Wakolosai 3:5, 8.

      Vitumbuizo vingi vipatikanavyo leo kwa wazi huvunja shauri hili lililopuliziwa. ‘Lakini sitafanya kamwe mambo yanayoonyeshwa kwenye kiwambo,’ huenda wengine wakapinga. Huenda ikawa hivyo. Lakini hata ikiwa vitumbuizo vyako havionyeshi utakuwa mtu wa aina gani, huenda vikafunua jambo fulani kuhusu aina ya mtu uliye tayari. Kwa mfano, huenda vikaonyesha kama umo miongoni mwa wale ambao ‘wanapenda jeuri’ au wale ambao akili zao zimejaa ‘uasherati, hamu ya ngono, tamaa, maongezi yenye’ aibu au ikiwa umo miongoni mwa wale ambao ‘huchukia uovu’ kikweli.—Zaburi 97:10.

      Paulo aliwaandikia Wafilipi: “Mambo yoyote yaliyo ya kweli, mambo yoyote yaliyo ya hangaikio zito, mambo yoyote yaliyo ya uadilifu, mambo yoyote yaliyo safi kiadili, mambo yoyote yaliyo ya kupendeka, mambo yoyote yaliyo ya kusemwa vema, wema wa adili wowote ulioko na jambo lolote la kustahili sifa likiwako, endeleeni kufikiria mambo haya.”—Wafilipi 4:8.

      Lakini je, andiko hilo lamaanisha kwamba kila sinema, kitabu au kipindi cha televisheni ambacho habari inazungumzia namna fulani ya kutofuatia uadilifu, labda uhalifu, ni mbaya moja kwa moja? Au je, sinema zote za vichekesho hazipasi kuonwa kwa sababu si za “hangaikio zito”? La, kwa kuwa muktadha waonyesha kwamba Paulo hakuwa akizungumzia vitumbuizo lakini mambo ambayo moyo hutafakari, ambayo yapasa kukazia mambo ambayo yanampendeza Yehova. (Zaburi 19:14) Hata hivyo, alichosema Paulo chaweza kutusaidia kwa habari ya kuchagua kitumbuizo. Kwa kutumia kanuni iliyoko kwenye Wafilipi 4:8, twaweza kujiuliza, ‘Je, chaguo langu la kitumbuizo hunifanya nitafakari mambo yasiyo safi?’ Ikiwa ndivyo, basi twahitaji kufanya marekebisho.

      Ingawa hivyo, katika kuchanganua vitumbuizo, Wakristo wapaswa kuacha ‘hali yao ya kukubali sababu ijulikane kwa watu wote.’ (Wafilipi 4:5) Bila shaka, kuna upitaji kiasi katika vitumbuizo ambavyo kwa wazi havifai Wakristo wa kweli. Kando na hilo, kila mtu anapaswa kuchanganua mambo kwa uangalifu na kufanya maamuzi ambayo yatamwacha akiwa na dhamiri safi mbele ya Mungu na mwanadamu. (1 Wakorintho 10:31-33; 1 Petro 3:21) Haingefaa kuhukumu wengine kwa mambo madogo-madogo au kuweka sheria kwa uthabiti kuamua kile wapaswacho kufanya wengine.b—Waroma 14:4; 1 Wakorintho 4:6.

      Daraka la Wazazi

      Wazazi wana daraka muhimu sana kwa habari ya vitumbuizo. Paulo aliandika hivi: “Hakika ikiwa yeyote hawaandalii kitu wale walio wake mwenyewe, na hasa kwa ajili ya wale walio washiriki wa nyumbani mwake, ameikana imani naye ni mbaya zaidi kuliko mtu asiye na imani.” (1 Timotheo 5:8) Hivyo, wazazi wana wajibu wa kuandalia washiriki wa familia si tu kimwili bali pia kiroho na kihisia-moyo. Hilo latia ndani kuandaa pumziko lifaalo.—Mithali 24:27.

      Nyakati fulani sehemu hii ya maisha ya familia hupuuzwa. “Kwa kuhuzunisha,” asema mishonari mmoja katika Nigeria, “wazazi fulani huona tafrija kuwa kupoteza wakati. Likiwa tokeo, watoto fulani huachwa peke yao, nao hupata namna mbaya ya marafiki na namna mbaya ya raha.” Wazazi, msiache hilo litukie! Hakikisheni kwamba watoto wenu wanapata tafrija ifaayo ambayo itawaburudisha kikweli.

      Lakini kutahadhari kwahitajiwa. Wakristo hawapaswi kuwa kama wengi leo ambao ni “wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu.” (2 Timotheo 3:1-4) Ndiyo, vitumbuizo vyapasa kuwekwa mahali pavyo. Vyapasa kuburudisha—si kutawala maisha ya mtu. Kwa hiyo watoto na vilevile watu wazima wahitaji si tu aina ifaayo ya vitumbuizo bali pia kiasi kifaacho.—Waefeso 5:15, 16.

      Furahia Utendaji Mwingineo

      Vitumbuizo vipendwavyo na wengi huzoesha watu kujikalia tu wala si kuwa watendaji. Kwa kielelezo, fikiria televisheni. Kitabu What to Do After You Turn Off the TV chaonelea: “Kwa asili yayo yenyewe [televisheni] huzoesha watu kujikalia tu: Vitumbuizo, na hata kujifunza, huwa jambo tunalopokea bila jitihada, si ubuni wetu wenye utendaji.” Bila shaka, kuna mahali pa hata vitumbuizo vya kujikalia tu. Lakini ikiwa vinatumia wakati mwingi wa mtu, humnyima fursa zenye kusisimua.

      Mtungaji Jerry Mander, ambaye asema kwamba yeye ni “wa kizazi cha kabla ya televisheni,” afafanua vipindi vya mara kwa mara vya uchoshi vilivyompata utotoni: “Hangaiko liliambatana nao,” yeye asema. “Ilikuwa hali isiyofurahisha kabisa, isiyofurahisha kiasi cha kwamba hatimaye ningeamua kuchukua hatua—kufanya jambo fulani. Ningempigia rafiki simu au kwenda nje. Ningekwenda kucheza mpira. Ningesoma. Ningefanya jambo fulani. Nikikumbuka, naona wakati huo wa uchoshi, wa ‘kukosa la kufanya,’ kuwa hali ambayo katika hiyo tendo la ubuni huzuka.” Leo, Mander aonelea, watoto hutumia televisheni kuwa suluhisho rahisi la uchoshi. “Televisheni huzima hangaiko na ubuni uwezao kutokea,” yeye aongeza.

      Hivyo, wengi wamegundua kwamba utendaji unaohitaji kushiriki badala ya kujikalia tu waweza kuridhisha kuliko walivyofikiri. Wengine wamepata kwamba kusoma kwa sauti kubwa pamoja na wengine ni chanzo cha furaha. Wengine hufuatia hobi, kama vile kucheza ala ya muziki, au kuchora picha. Kisha kuna fursa za kupangia vikusanyiko vifaavyo.c (Luka 14:12-14) Tafrija ya nje pia ina manufaa. Mleta-habari wa Amkeni! katika Sweden aripoti: “Familia fulani huenda kupiga kambi, au kuvua samaki au kutembea-tembea msituni, kufanya visafari vya mitumbwi, matembezi milimani, na kadhalika. Wachanga hufurahi.”

      Kuwapo kwa sehemu zenye kupotosha katika vitumbuizo hakupaswi kutushangaza. Mtume Paulo aliandika kwamba watu wa mataifa ‘hutembea katika ukosefu wa faida wa akili zao.’ (Waefeso 4:17) Kwa hivyo, ni jambo la kutarajiwa tu kwamba sehemu kubwa ya wanachoona kuwa chenye kutumbuiza inashughulikia “kazi za mwili.” (Wagalatia 5:19-21) Hata hivyo, Wakristo waweza kujizoeza kufanya maamuzi timamu kwa habari ya ubora na kiasi cha vitumbuizo vyao. Wao pia wanaweza kufanya tafrija kuwa jambo la kupanga wakiwa familia na waweza hata kujaribu utendaji mpya mbalimbali ambao utakuwa wenye kuburudisha na kuandaa kumbukumbu nzuri kwa miaka itakayokuja. Ndiyo, wewe waweza kupata vitumbuizo vifaavyo!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki