-
Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19Amkeni!—2010 | Oktoba
-
-
Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19
Ulikuwa mwaka wa 1854, na kwa mara nyingine London ilikumbwa na mlipuko wa kipindupindu—ugonjwa wa tumbo unaomfanya mtu aharishe na kupoteza maji mwilini. Ugonjwa huo ulienea kwa kasi sana. Watu wengi waliokuwa na afya nzuri asubuhi walikuwa wamekufa kufikia usiku. Hakukuwa na tiba.
ULIKUWA ndio ugonjwa wenye kuogopesha katika karne yote, na hakuna aliyejua jinsi ulivyotokea. Wengine walifikiri mtu alipatwa na kipindupindu kwa sababu ya kupumua hewa yenye harufu ya vitu vilivyooza. Huenda makisio yao yakawa yalionekana kuwa yanapatana na akili. Mto Thames, uliopitia London, ulikuwa ukinuka vibaya sana. Je, harufu hiyo mbaya ndiyo iliyosababisha ugonjwa huo?
Miaka mitano mapema, daktari anayeitwa John Snow alikuwa amesema kwamba kipindupindu kinasababishwa, si na hewa chafu, bali maji machafu. Daktari mwingine, William Budd, alisema kwamba kuna kiini fulani kinachofanana na kuvu ambacho kilibeba ugonjwa huo.
Ugonjwa huo ulipolipuka katika mwaka wa 1854, Snow alijaribu kuthibitisha wazo lake kwa kuchunguza maisha ya watu waliopatwa na kipindupindu katika wilaya ya Soho, huko London. ‘Walikuwa wameshiriki katika utendaji gani unaofanana?’ alijiuliza. Uchunguzi wa Snow ulimfanya agundue jambo fulani lenye kushangaza. Wote walioambukizwa kipindupindu katika wilaya hiyo walikuwa wamechota maji ya kunywa katika bomba lilelile, na maji hayo yalikuwa yamechafuliwa na maji-taka yaliyo na kipindupindu!a
Mwaka huohuo hatua nyingine kubwa ya kitiba ilifikiwa wakati mwanasayansi Mwitaliano Filippo Pacini alipochapisha maandishi kuhusu kiini kinachosababisha kipindupindu. Hata hivyo, watu wengi walipuuza uchunguzi wake pamoja na mambo ambayo Snow na Budd walikuwa wamegundua. Kipindupindu kiliendelea kuenea, hadi mwaka wa 1858.
“Uvundo Mkuu”
Bunge halikuwa na haraka ya kujenga mfumo mpya wa kuondoa maji-taka ili kusafisha Mto Thames, lakini joto kali lililotokea katika kiangazi cha mwaka wa 1858 liliwalazimisha wachukue hatua. Uvundo uliotoka katika mto huo uliopita mbele ya Bunge ulikuwa mkali sana hivi kwamba wanasiasa walilazimika kuweka pazia zilizoloweshwa sabuni ya kuua viini ili kupunguza uvundo huo. Huo, ulioitwa Uvundo Mkuu, uliwasukuma Wabunge wachukue hatua. Katika muda wa siku 18, waliamuru kwamba mfumo mpya wa kuondoa maji-taka ujengwe.
Mifereji mikubwa ilijengwa iliyozuia maji-taka yasifike kwenye mto, kisha ikayasafirisha hadi mashariki ya London, ambako mwishowe yaliingia baharini, wakati ambapo maji ya bahari yalijaa. Matokeo yalikuwa yenye kushangaza. Sehemu zote za London zilipounganishwa kwenye mfumo huo mpya, kipindupindu kilikwisha.
Sasa hakukuwa na shaka: Kipindupindu hakikusababishwa na hewa chafu bali kilisababishwa na maji au chakula kichafu. Pia ilikuwa wazi kwamba siri ya kuzuia ugonjwa huo ni kudumisha usafi.
-
-
Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19Amkeni!—2010 | Oktoba
-
-
a Ingawa kufikia mwaka wa 1854 vyoo vya kupiga maji vilikuwa vimebuniwa, mfumo wa kale wa kupitisha maji-taka uliruhusu uchafu wa wanadamu kutiririka kupitia katika mabomba na mifereji hadi ndani ya Mto Thames, uliokuwa chanzo kikuu cha maji ya kunywa.
-