Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Uhai Ulianzaje?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • Wanasayansi wengi husema nini? Wengi wanaoamini mageuzi watakuambia kwamba uhai ulianza mabilioni ya miaka iliyopita kwenye ukingo wa kidimbwi cha kale kilichojaa maji wakati wa kupwa au katika sehemu za chini ya bahari. Wao huhisi kwamba katika maeneo yasiyojulikana kama hayo, kemikali zilijikusanya na kuwa vitu vinavyofanana na mapovu, vikafanyiza molekuli tata, na kuanza kujigawanya-gawanya. Wanaamini kwamba uhai wote duniani ulijitokeza wenyewe tu kutokana na chembe “sahili,” moja au zaidi.

      Wanasayansi wengine wanaoheshimika ambao pia wanaunga mkono mageuzi hawakubaliani na wazo hilo. Wanakisia kwamba chembe za kwanza au angalau sehemu zake kuu zilikuja duniani kutoka anga la nje. Kwa nini? Kwa sababu, licha ya jitihada zao nyingi, wanasayansi hawajaweza kuthibitisha kwamba uhai unaweza kutokea ghafula kutokana na molekuli zinazodhaniwa zilitokeza uhai. Katika mwaka wa 2008, Alexandre Meinesz, Profesa wa Biolojia, alizungumzia utata huo. Alisema kwamba kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, “hakuna uthibitisho wowote uliopatikana kupitia majaribio yaliyofanywa unaounga mkono nadharia ya kwamba uhai ulitokea ghafula Duniani kutokana na molekuli fulani, wala hakuna maendeleo ya kisayansi yanayoweza kuthibitisha hilo.”1

      Uthibitisho unafunua nini? Jibu la swali, Watoto hutoka wapi? limethibitishwa na haliwezi kupingwa. Sikuzote uhai hutokana na uhai ambao tayari upo. Hata hivyo, tukirudi nyuma miaka mingi iliyopita, inawezekana kwamba sheria hiyo ya msingi ilivunjwa? Inawezekana kweli kwamba uhai ulijitokeza wenyewe kutokana na kemikali zisizo hai? Kuna uwezekano wowote kwamba jambo hilo linaweza kutokea?

      Watafiti wamegundua kwamba ili chembe iendelee kuwa hai, angalau aina tatu tofauti za molekuli tata lazima zifanye kazi pamoja—DNA au deoksiribonyukilia asidi, RNA (ribonucleic acid), na protini. Leo, ni wanasayansi wachache wanaoweza kudai kwamba chembe kamili iliyo hai ilijitokeza yenyewe kutokana na mchanganyiko wa kemikali zisizo hai. Hata hivyo, kuna uwezekano gani kwamba RNA au protini zinaweza kujitokeza zenyewe?a

      Wanasayansi wengi huhisi kwamba huenda uhai ulijitokeza wenyewe kwa sababu ya jaribio fulani lililofanywa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1953. Mwaka huo, Stanley L. Miller aliweza kutengeneza asidi-amino, kemikali za msingi zinazofanyiza protini, kwa kupitisha nguvu za umeme ndani ya mchanganyiko wa gesi zilizodhaniwa kuwa zingewakilisha anga la dunia. Tangu wakati huo, asidi-amino zimepatikana pia katika vimondo. Ugunduzi huo unamaanisha kwamba kemikali za msingi za uhai zinaweza kujitokeza tu zenyewe?

      Robert Shapiro, aliyekuwa profesa wa kemia katika Chuo Kikuu cha New York, asema: “Baadhi ya waandikaji wameamini kwamba kemikali zote za msingi za uhai zinaweza kutengenezwa kwa urahisi kwa kutumia majaribio kama yale ya Miller na kwamba zinapatikana katika vimondo. Hata hivyo sivyo ilivyo.”2b

      Fikiria molekuli ya RNA. Imefanyizwa na molekuli ndogo zinazoitwa nukliotidi. Nukliotidi ni aina tofauti ya molekuli na ni tata zaidi kidogo kuliko asidi-amino. Shapiro anasema kwamba “hakuna nukliotidi za aina yoyote zinazoripotiwa kuwa zilitokana na majaribio yanayohusisha umeme wala katika uchunguzi wa vimondo.”3 Pia anasema kwamba uwezekano wa molekuli kujifanyiza bila mpangilio maalum na kujikusanya kutoka kwa kemikali nyingi za msingi “ni mdogo sana hivi kwamba hata kama ungetokea mahali popote katika ulimwengu unaoonekana, lingeonwa bahati njema.”4

      Namna gani molekuli za protini? Zinaweza kufanyizwa kutokana na asidi-amino 50 hivi au maelfu kadhaa ya amino-asidi zilizokusanywa pamoja katika mpangilio hususa wa hali ya juu. Protini ya wastani katika chembe yoyote ina amino-asidi 200. Hata katika chembe hizo kuna maelfu ya aina tofauti-tofauti za protini. Uwezekano wa kwamba protini moja tu iliyo na amino-asidi 100 pekee ingeweza kujifanyiza kwa njia isiyo na mpangilio maalum duniani, umekadiriwa kuwa mara moja tu hivi baada ya kufanya majaribio hayo mara milioni bilioni.

      Mtafiti Hubert P. Yockey, anayeunga mkono fundisho la mageuzi ana maelezo zaidi. Anasema: “Haiwezekani kwamba chanzo cha uhai ni ‘protini tu.’”5 RNA inahitajika kutengeneza protini, hata hivyo, protini zinahusika katika utengenezaji wa RNA. Namna gani ikiwa, licha ya uwezekano huo mdogo sana, protini na molekuli ya RNA zingetokea mahali pamoja wakati uleule? Kuna uwezekano wowote kwamba zinaweza kufanyiza uhai unaoweza kutokeza chembe ambazo zinaweza kuzaana na kuendeleza uhai? “Yaelekea uwezekano wa jambo hilo kujitokeza lenyewe (kukiwa na mchanganyiko usio na mpangilio maalum wa protini na RNA) ni mdogo sana,” asema Dkt. Carol Clelandc, mshiriki wa NASA (National Aeronautics and Space Administration’s Astrobiology Institute). “Hata hivyo,” aendelea, “yaelekea watafiti wengi wanafikiri kwamba ikiwa wataelewa jinsi protini na RNA zinavyojifanyiza kupitia njia za asili, basi kwa njia fulani haitakuwa vigumu kuelewa jinsi kemikali hizo zinavyoshirikiana.” Kuhusu nadharia za leo zinazoeleza jinsi huenda kemikali hizo za msingi zilivyojitokeza zenyewe, anasema: “Hakuna yoyote kati ya nadharia hizo inayoeleza kwa usahihi jinsi jambo hilo lilivyotukia.”6

      Kwa nini ukweli huu ni muhimu? Wazia changamoto inayowakabili watafiti ambao huamini kwamba uhai ulijitokeza wenyewe. Wamepata amino-asidi fulani ambazo zinapatikana pia katika chembe zilizo hai. Kupitia majaribio yaliyofanywa kwa ustadi mkubwa, wametengeneza molekuli tata zaidi katika maabara zao. Hatimaye, wanatarajia kutengeneza sehemu zote zinazohitajiwa ili kuunda chembe “sahili.” Hali yao inaweza kulinganishwa na ya mwanasayansi anayechukua vitu vya asili na kuvigeuza kuwa chuma, plastiki, silikoni, na waya; kisha anatengeneza roboti. Halafu anairatibu roboti hiyo ili iweze kutengeneza roboti nyingine zinazofanana nayo. Kwa kufanya hivyo, anathibitisha nini? Kwamba mtu mwenye akili anaweza kutengeneza mashini yenye kuvutia.

      Vivyo hivyo, ikiwa wanasayansi watawahi kutengeneza chembe, watakuwa wametimiza jambo lenye kustaajabisha kwelikweli—hata hivyo, je, watakuwa wakithibitisha kwamba chembe hiyo inaweza kujitokeza yenyewe bila mwelekezo wowote? Kinyume cha hilo, watakuwa wanathibitisha jambo lililo tofauti kabisa, sivyo?

      Una maoni gani? Uthibitisho wote wa kisayansi kufikia sasa unaonyesha kwamba uhai unaweza kutokezwa tu na uhai ambao tayari upo. Kuamini kwamba hata chembe “sahili” iliyo hai ilijitokeza yenyewe kutokana na kemikali zisizo na uhai, kunahitaji imani kubwa isiyo na msingi.

      Ukiwa na ukweli huo, uko tayari kuwa na imani kama hiyo? Kabla ya kujibu swali hilo, chunguza kwa makini jinsi ambavyo chembe zimetengenezwa. Kufanya hivyo kutakusaidia kuamua ikiwa nadharia ambazo wanasayansi fulani wamefundisha kuhusu chanzo cha uhai ni za kweli, au ni kama hadithi za kubuniwa ambazo wazazi fulani huwaambia watoto wao kuhusu mahali ambapo watoto hutoka.

      [Maelezo ya Chini]

      a Uwezekano wa DNA kujifanyiza yenyewe utazungumziwa katika sehemu ya 3, “Maagizo Yalitoka Wapi?”

      b Profesa Shapiro haamini kwamba uhai ulitokana na Muumba. Anaamini kuwa uhai ulijitokeza wenyewe kwa njia fulani ambayo bado haijaeleweka. Mwaka wa 2009 wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza, waliripoti kwamba wametengeneza nukliotidi katika maabara yao. Hata hivyo, Shapiro anasema kwamba viambato vyao “bila shaka havifikii viwango vyangu vinavyokubalika vya kutengeneza RNA.”

      c Dkt. Cleland haamini masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji. Anaamini kwamba uhai ulijitokeza wenyewe katika njia fulani ambayo bado haijaeleweka vizuri.

  • Je, Kweli Kuna Aina Yoyote ya Uhai Inayoweza Kuitwa Duni?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • Wanasayansi wengi husema nini? Chembe zote zilizo hai ziko katika vikundi viwili—zenye kiini na zisizo na kiini. Chembe za wanadamu, wanyama, na mimea zina kiini. Chembe za bakteria hazina kiini. Chembe zenye kiini huitwa eukaryotic. Chembe zisizo na kiini huitwa prokaryotic. Kwa kuwa chembe zisizo na kiini si tata sana kama zile zenye kiini, watu wengi huamini kwamba chembe za wanyama na mimea zilitokana na chembe za bakteria.

      Wengi hufundisha kwamba kwa mamilioni ya miaka, baadhi ya chembe “sahili” zisizo na kiini zilimeza chembe nyingine lakini hazikuzimeng’enya. Badala yake, kulingana na nadharia hiyo, tukio fulani la “asili” lisilotegemea akili, lilifanyiza mabadiliko muhimu kuhusiana na utendaji-kazi wa chembe zilizomezwa na pia kuendelea kuzihifadhi chembe hizo ndani ya chembe “kimelewa” (iliyozimeza) ilipokuwa ikijigawanya.9a

  • Je, Kweli Kuna Aina Yoyote ya Uhai Inayoweza Kuitwa Duni?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • Uthibitisho unafunua nini? Maendeleo katika elimu ya mikrobiolojia yamewawezesha wanasayansi kuchunguza sehemu yenye kustaajabisha ya ndani ya chembe hai sahili za prokaryotic zinazojulikana. Wanasayansi wanaounga mkono mageuzi wanakisia kwamba chembe za kwanza zilizo hai zilifanana na chembe hizo.10

      Ikiwa nadharia ya mageuzi ni ya kweli, basi inapaswa kueleza kinagaubaga jinsi chembe “sahili” ya kwanza ilivyojitokeza yenyewe. Kwa upande mwingine, ikiwa uhai ulitokana na Muumba, kunapaswa kuwa na uthibitisho wa ubunifu wa hali ya juu hata katika viumbe vidogo sana. Kwa nini usitembelee chembe ya prokaryotic? Unapoichunguza, jiulize ikiwa chembe hiyo inaweza kujitokeza yenyewe.

      UKUTA UNAOILINDA CHEMBE

      Ili uingie ndani na kuchunguza chembe ya prokaryotic, utahitaji kusinyaa na kuwa mdogo zaidi ya nukta iliyo mwishoni mwa sentensi hii. Chembe hiyo inalindwa na utando wenye kunyumbulika unaotenda kama ukuta wa matofali unaokizunguka kiwanda. Utando huo ni mwembamba sana hivi kwamba matabaka 10,000 ya utando huo yanalingana na unene wa karatasi moja. Hata hivyo, utando wa chembe ni tata sana kuliko ukuta wa matofali. Jinsi gani?

      Kama ukuta unaolinda kiwanda, utando wa chembe hulinda vitu vilivyo ndani dhidi ya hatari inayoweza kutokea. Hata hivyo, utando huo si mgumu; unaruhusu chembe “kupumua” na hivyo kuwezesha molekuli ndogo, kama oksijeni, kuingia au kutoka. Lakini utando huo huzuia molekuli zilizo tata zaidi zinazoweza kusababisha madhara zisiingie bila chembe kuziruhusu. Utando huo pia huzuia molekuli zenye manufaa zisitoke nje ya chembe. Utando huo hufanya hivyo jinsi gani?

      Kifikirie tena kiwanda. Huenda kina walinzi wanaochunguza bidhaa zinazoingia na kutoka kiwandani kupitia milango iliyo kwenye ukuta. Vivyo hivyo, utando wa chembe una protini za molekuli maalum zinazotenda kama milango na walinzi.

      Baadhi ya protini hizo (1) zina tundu katikati linaloruhusu aina fulani tu ya molekuli kuingia ndani na kutoka nje ya chembe. Protini nyingine ziko wazi upande mmoja wa utando wa chembe (2) na upande mwingine umefungwa. Zina maeneo ya kutia nanga (3) yenye maumbo yanayotoshea dutu fulani hususa. Dutu hiyo inapotia nanga, upande ule mwingine wa protini hufunguka na kuiachilia dutu hiyo kupitia utando (4). Mambo yote hayo hufanyika katika sehemu ya nje ya hata chembe sahili zaidi.

      NDANI YA KIWANDA

      Tuseme “walinzi” wamekuruhusu kuingia na sasa uko ndani ya chembe. Ndani ya chembe ya prokaryotic kumejaa umajimaji ambao una virutubisho vingi, chumvi, na dutu nyingine. Chembe hutumia viambato hivyo vya msingi kutengeneza bidhaa inazohitaji. Hata hivyo, mambo hayo hayatendeki kiholela. Kama kiwanda kinachoendeshwa vizuri, chembe hupanga utendaji mbalimbali wa maelfu ya kemikali ili ufanyike kwa utaratibu hususa na kulingana na wakati ulioratibiwa.

      Chembe hutumia muda mwingi kutengeneza protini. Inafanya hivyo jinsi gani? Kwanza, utaona chembe ikitengeneza kemikali za msingi 20 hivi zinazoitwa asidi-amino. Kemikali hizo za msingi hupelekwa hadi kwenye ribosomu (5), zinazoweza kulinganishwa na mashine zinazojiendesha zenyewe ambazo zinaunganisha asidi-amino katika utaratibu fulani ili kutengeneza protini hususa. Kama vile ambavyo huenda utendaji wote wa kiwanda ukaongozwa na programu ya kompyuta, utendaji mwingi wa chembe unaongozwa na “programu ya kompyuta” au molekuli ya DNA (6). Ribosomu hupokea kutoka kwa DNA nakala yenye maagizo kamili inayoiambia ni protini gani itakayotengeneza na jinsi ya kuitengeneza (7).

      Kinachotokea protini inapotengenezwa ni chenye kustaajabisha! Kila moja hujikunja na kufanyiza umbo la kipekee lenye nyuso tatu (8). Umbo hilo ndilo linaloamua kazi hususa ambayo protini hiyo itafanya.b Wazia sehemu za injini zikiunganishwa pamoja. Kila sehemu inapaswa kutengenezwa kwa usahihi kabisa ili injini hiyo ifanye kazi. Vivyo hivyo, ikiwa protini haijatengenezwa kwa usahihi kamili na kukunjwa katika umbo hususa, haitaweza kufanya kazi yake vizuri na huenda hata ikaharibu chembe.

      Protini inajuaje njia kutoka mahali ilipotengenezewa mpaka mahali inapohitajika? Kila protini inayotengenezwa na chembe inakuwa na “anwani” ili kuhakikisha kwamba protini hiyo itafika mahali inapohitajika. Ingawa maelfu ya protini hutengenezwa na kutumwa kila dakika, kila moja hufika mahali inapohitajika.

      Kwa nini ukweli huu ni muhimu? Molekuli tata zilizo ndani ya vitu sahili vilivyo hai haziwezi kujizalisha. Zikiwa nje ya chembe, molekuli hizo hujigawanya. Zikiwa ndani ya chembe, haziwezi kujizalisha bila msaada wa molekuli nyingine tata. Kwa mfano, vimeng’enya vinahitajiwa ili kutengeneza molekuli ya pekee ya nishati inayoitwa adenosine triphosphate (ATP), hata hivyo, nishati kutoka kwa ATP inahitajika ili kutengeneza vimeng’enya. Vivyo hivyo, DNA (sehemu ya 3 inazungumzia molekuli hiyo) inahitajika ili kutengeneza vimeng’enya, hata hivyo, vimeng’enya vinahitajika ili kutengeneza DNA. Pia, protini nyingine zinaweza tu kutengenezwa na chembe, hata hivyo, chembe inafanyizwa kwa protini.c

      Mwanasayansi Radu Popa hakubaliani na masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji. Hata hivyo, katika mwaka wa 2004 aliuliza: “Mambo ya asili yanawezaje kutokeza uhai ikiwa baada ya kufanya majaribio yote hayo kwa makini sana tumeshindwa?”13 Pia alisema: “Mifumo tata inayohitajika kwa ajili ya utendaji wa chembe iliyo hai ni ya hali ya juu sana hivi kwamba haingeweza kujitokeza yenyewe kwa wakati uleule.”14

      Una maoni gani? Watu wanaoamini nadharia ya mageuzi husema kwamba Mungu hakuhitaji kuingilia kati ili kutokeza uhai duniani. Hata hivyo, kadiri wanasayansi wanavyozidi kuelewa mambo fulani kuhusu uhai, ndivyo wanavyotambua kwamba haiwezekani kuwa ulijitokeza wenyewe. Ili kuepuka utata huo, wanasayansi fulani wanaoamini mageuzi, wangependa kutenganisha nadharia ya mageuzi na suala la chanzo cha uhai. Lakini kwa maoni yako, hilo linapatana na akili?

      Nadharia ya mageuzi inategemea dhana ya kwamba mfuatano wa matukio mengi yasiyoelekezwa yalianzisha uhai. Kisha nadharia hiyo inadokeza kwamba mfuatano mwingine wa matukio ya kiholela ulitokeza aina mbalimbali zenye kustaajabisha na tata za vitu vyote vilivyo hai. Hata hivyo, ikiwa nadharia hiyo haina msingi, namna gani zile nadharia nyingine zinazoitegemea? Kama vile ghorofa lililojengwa bila msingi litakavyoporomoka, ndivyo nadharia ya mageuzi ambayo haiwezi kueleza chanzo cha uhai itakavyoporomoka.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki