-
Mageuzi—Dhana na Ukweli wa MamboUhai—Ulitokana na Muumba?
-
-
Dhana ya 1. Mabadiliko ya chembe za urithi hutokeza jamii mpya. Fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi—au mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum katika chembe za urithi za mimea na wanyama—yanaweza kutokeza spishi mpya au hata makundi mapya kabisa ya wanyama na mimea.19
Mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kuleta mabadiliko kwenye mimea—kama huu mmea wenye maua makubwa—lakini mabadiliko hayo yana mipaka
Ukweli wa mambo. Sifa na tabia nyingi za mimea na wanyama hutegemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi zilizo katika kiini cha kila chembe.c Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya baadaye vya wanyama na mimea. Hata hivyo, je, kweli mabadiliko katika chembe za urithi hutokeza spishi mpya kabisa? Utafiti ambao umefanywa kwa karne moja hivi kuhusu chembe za urithi umefunua nini?
Kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1930, wanasayansi walianza kuunga mkono wazo jipya. Tayari walikuwa wakiamini kwamba ule mchakato wa uteuzi wa kiasili, yaani, kwamba viumbe bora zaidi katika mazingira yake ndio wanaoweza kuendelea kuishi na kuzaana, ungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum. Kwa hiyo, walikata kauli kwamba uteuzi mnemba, au unaofanywa na wanadamu, unaweza kutokeza spishi mpya kwa njia bora zaidi. “Msisimko huo ulienea miongoni wa wanabiolojia wengi, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama,” akasema Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika taasisi moja nchini Ujerumani (Max Planck Institute for Plant Breeding Research).d Kwa nini kukawa na msisimko hivyo? Lönnig, ambaye kwa miaka 30 hivi amekuwa akichunguza mabadiliko ya chembe za urithi za mimea, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama umewadia. Walifikiri kwamba kwa kudukiza mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora zaidi.”20 Hata wengine kati yao wananuia kutokeza spishi mpya kabisa.
Nzi ambao chembe zao za urithi zimebadilika, ijapokuwa wana kasoro, bado ni nzi
Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyogharimu pesa nyingi, wakitumia mbinu walizodhani zingeharakisha mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti huo ambao umechukua zaidi ya miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutumia unururishaji [ili kubadili chembe za urithi] kutokeza aina mbalimbali zinazoweza kuzaana, yaliambulia patupu.”21 Pia, Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yalikuwa yamegonga mwamba ulimwenguni pote. Utafiti kuhusu uzalishaji wa kudukiza ukiwa kitengo tofauti cha utafiti ulitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi . . . walikufa au walikuwa dhaifu kuliko wale wenye chembe za asili.”e
Hata hivyo, data ambazo kufikia sasa zimekusanywa kwa miaka 100 hivi ya kutafiti mabadiliko ya chembe za urithi kwa ujumla, na hasa miaka 70 ya uzalishaji wa mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi, zimewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza matokeo ya utafiti huo, Lönnig alikata kauli hii: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambayo yamefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za welekeo.”
Hivyo basi, je, mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kubadili spishi moja iwe kiumbe kingine kipya kabisa? Matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba haiwezekani. Kutokana na utafiti mbalimbali ambao amefanya, Lönnig amekata kauli kwamba “spishi zinazotambulika waziwazi zina mipaka ambayo haiwezi kufutiliwa mbali wala kukiukwa na mabadiliko yoyote katika chembe za urithi yanayotokea bila mpangilio wowote.”22
Fikiria kinachomaanishwa na uthibitisho huo. Ikiwa wanasayansi stadi wameshindwa kutokeza spishi mpya kwa kudukiza mabadiliko na kuteua chembe bora za urithi, itawezekanaje basi mchakato usiotegemea akili yoyote ufaulu kufanya hivyo? Ikiwa utafiti unaonyesha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza spishi mpya kabisa, basi, yale mageuzi makubwa yatawezekanaje?
-
-
Mageuzi—Dhana na Ukweli wa MamboUhai—Ulitokana na Muumba?
-
-
e Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ndiyo iliyoteuliwa kwa ajili ya utafiti zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo iliyoteuliwa ndiyo iliyofaa kwa matumizi ya kibiashara. Hata hivyo, hakuna hata spishi moja mpya kabisa iliyotokezwa. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa duni hata kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yalitupiliwa mbali.
-