Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Uhai Wote Umetokana na Chanzo Kimoja?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • NAMNA GANI REKODI YA VISUKUKU?

      Wanasayansi wengi huona rekodi ya visukuku kuwa inaunga mkono dhana ya kwamba uhai ulitokana na chanzo kimoja. Kwa mfano, wao hudai kwamba rekodi ya visukuku huonyesha kwamba samaki waligeuka na kuwa amfibia na reptilia wakawa mamalia. Hata hivyo, visukuku huthibitisha nini hasa?

      Mwanamageuzi ambaye pia ni mtaalamu wa visukuku, David M. Raup anasema: “Badala ya kuchunguza jinsi uhai ulivyotokea hatua kwa hatua, kile ambacho wanajiolojia wa siku za Darwin na wa leo wanapata ni rekodi isiyolingana au isiyo na mpangilio; kwamba spishi zinaonekana ghafula kwa mfuatano, zinakuwa na mabadiliko madogo au hata bila mabadiliko yoyote, kisha zinatoweka ghafula kutoka katika rekodi.”32

      Kusema kweli, visukuku vingi huonyesha kwamba aina tofauti-tofauti za viumbe hazijabadilika hata baada ya muda mrefu sana. Uthibitisho hauonyeshi vikigeuka kutoka kwa aina moja hadi nyingine. Maumbo ya kipekee hutokea ghafula. Sehemu mpya hutokea ghafula. Kwa mfano, popo wenye mfumo wa sona ambao wana uwezo wa kugundua mahali kitu fulani kinapatikana kwa kutumia mawimbi ya sauti, hawana uhusiano ulio wazi na popo wa kale.

      Inaonekana zaidi ya nusu ya vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea kwa muda mfupi wa wakati. Kwa kuwa aina nyingi mpya za uhai zinazotofautiana sana zinatokea ghafula kwenye rekodi ya visukuku, wataalamu wa visukuku hukiita kipindi hicho “mlipuko wa Cambria.” Huo ulikuwa wakati gani?

      Tuchukulie kwamba makadirio ya watafiti ni sahihi. Hivyo basi, historia ya dunia inaweza kuwakilishwa na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha wakati kinachoweza kunyooshwa na kutoshana na uwanja wa mpira wa kandanda (1). Kwa kipimo hicho, utahitaji kutembea asilimia 88 ya uwanja huo kabla ya kufikia kile ambacho wataalamu wa visukuku wanakiita kipindi cha Cambria (2). Katika muda mfupi wa kipindi hicho, vikundi vikubwa vya wanyama vinaonekana katika rekodi ya visukuku. Vinatokea ghafula kadiri gani? Unapoendelea kutembea kwenye uwanja huo, viumbe vyote hivyo tofauti-tofauti vinatokea upesi kwa muda unaopungua hatua moja!

      Kutokea ghafula kwa aina hizo tofauti-tofauti za uhai kumefanya watafiti fulani wa nadharia ya mageuzi kutilia shaka masimulizi ya jadi ya nadharia ya Darwin. Kwa mfano, kwenye mahojiano ya mwaka 2008, mwanamageuzi, Stuart Newman, alizungumzia uhitaji wa kuwa na nadharia nyingine ya mageuzi inayoweza kufafanua kutokea ghafula kwa aina mpya mbalimbali za uhai. Alisema: “Nadharia ya Darwin iliyokuwa ikifafanua mabadiliko yote ya mageuzi itashushwa, iwe tu kama mojawapo ya nadharia nyingi—huenda hata isiyo muhimu sana inapohusu kuelewa mageuzi makubwa, mageuzi ya mabadiliko makubwa katika maumbo ya mwili.”33

      MATATIZO YA “UTHIBITISHO”

      Hata hivyo, namna gani visukuku vinavyotumiwa kuonyesha samaki wakibadilika kuwa amfibia, na reptilia kuwa mamalia? Je, vinaandaa uthibitisho thabiti kuhusu hatua za mageuzi? Rekodi ya visukuku inapochunguzwa kwa makini, matatizo mengi huwa wazi.

      Kwanza, nyakati nyingine ukubwa wa viumbe katika mfuatano wa mabadiliko kutoka reptilia-hadi-mamalia hupotoshwa katika vitabu. Badala ya kuwa sawa kwa ukubwa, viumbe fulani katika mfuatano huwa vikubwa, huku vingine vikiwa vidogo.

      Pili, tatizo kubwa hata zaidi ni ukosefu wa uthibitisho unaoonyesha kwamba viumbe hao wanahusiana kwa njia fulani. Kulingana na makadirio ya watafiti, mara nyingi wanyama walio kwenye mfuatano hutenganishwa na mamilioni ya miaka. Kuhusiana na wakati unaotenganisha visukuku hivyo, mwanazuolojia Henry Gee anasema: “Muda unaotenganisha visukuku ni mrefu sana hivi kwamba hatuwezi kusema kwa uhakika ikiwa vinahusiana kupitia nasaba na ukoo.”34c

      Akizungumzia visukuku vya samaki na amfibia, mwanabiolojia Malcolm S. Gordon, anasema kwamba visukuku vilivyopatikana vinawakilisha sehemu ndogo tu “huenda isiyowakilisha kabisa aina mbalimbali ya mimea na wanyama waliokuwako katika vikundi hivyo wakati huo.” Anaendelea kusema: “Hatuwezi kujua ni kwa kiasi gani viumbe hao walihusika katika ukuzi wa baadaye, au jinsi walivyohusiana.”35d

      “FILAMU” INAONYESHA NINI HASA?

      Makala iliyochapishwa mwaka wa 2004 katika jarida la National Geographic lilifananisha rekodi ya visukuku na “filamu ya mageuzi ambayo kati ya kila picha 1,000, imepoteza picha 999 katika chumba cha kuhariri.”36 Fikiria matokeo ya mfano huo.

      Wazia umepata picha 100 ya filamu ambayo mwanzoni ilikuwa na picha 100,000. Utajuaje mfuatano wa matukio katika filamu hiyo? Huenda ukawa na maoni fulani, lakini namna gani ikiwa ni 5 tu kati ya zile picha 100 ulizopata zinazoweza kupangwa ili kuunga mkono hadithi unayopendelea, huku zile nyingine 95 zikiwa na hadithi tofauti? Lingekuwa jambo la hekima kudai kwamba maoni yako kuhusu filamu hiyo ni sahihi kwa sababu tu ya hizo picha tano? Inawezekana kwamba uliweka picha hizo tano kwa mpangilio ambao unapatana na maoni yako? Je, halingekuwa jambo la busara kuacha zile picha nyingine 95 zikusaidie kuwa na maoni yanayofaa?

      Ni kwa njia gani mfano huo unatusaidia kuelewa jinsi wanamageuzi wanavyoiona rekodi ya visukuku? Kwa miaka mingi, watafiti hawakukubali kwamba visukuku vingi—zile picha 95 za filamu—vilionyesha kwamba spishi hubadilika kidogo sana baada ya muda. Kwa nini hawasemi lolote kuhusu uthibitisho huo muhimu? Mwandikaji Richard Morris anasema: “Yaelekea wataalamu wa visukuku walianza kushikilia maoni yaliyokubaliwa na wengi kwamba kulikuwa na mabadiliko ya hatua kwa hatua katika mageuzi, hata baada ya kupata uthibitisho unaokanusha jambo hilo. Wamekuwa wakijaribu kufafanua uthibitisho wa visukuku kulingana na maoni yanayokubaliwa kuhusu mageuzi.”37

      Namna gani wanamageuzi leo? Inawezekana kwamba wanapanga visukuku katika mpangilio fulani, si kwa sababu mfuatano huo unaungwa mkono na visukuku vingi na uthibitisho wa kinasaba, bali kwa sababu kufanya hivyo kunapatana na maoni yanayokubaliwa leo kuhusu mageuzi?e

  • Je, Uhai Wote Umetokana na Chanzo Kimoja?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • KILE KINACHOTHIBITISHWA HASA NA VISUKUKU

      ◼ Ukweli wa mambo: Mwanzoni mwa karne ya 20, visukuku vyote vilivyotumiwa kuunga mkono nadharia ya kwamba mwanadamu na sokwe waligeuka kutoka kwa mzazi mmoja vingeweza kutoshea kwenye meza ya biliadi. Tangu wakati huo, idadi ya visukuku vinavyotumiwa kuunga mkono nadharia hiyo imeongezeka. Inadaiwa kwamba sasa visukuku hivyo vinaweza kujaza behewa la gari-moshi.38 Hata hivyo, idadi kubwa ya visukuku hivyo ni mfupa mmojammoja na meno hapa na pale. Ni vigumu sana kupata mafuvu kamili au viunzi kamili vya mifupa.39

      Swali: Je, kupatikana kwa idadi kubwa ya visukuku vinavyodaiwa ni vya “ukoo” wa mwanadamu kumejibu swali ambalo baadhi ya wataalamu wa mageuzi wameuliza kuhusu wakati na jinsi ambavyo wanadamu waligeuka kutokana na sokwe?

      Jibu: Hapana. Kuhusiana na jinsi visukuku hivyo vinapaswa kuainishwa, Robin Derricourt wa Chuo Kikuu cha New South Wales, nchini Australia, aliandika hivi mnamo 2009: “Huenda makubaliano pekee ambayo yamefikiwa sasa ni kwamba, hakuna makubaliano.”40 Mwaka 2007 jarida la sayansi, Nature, lilichapisha makala ya wagunduzi wa vile vinavyodaiwa kuwa visukuku vilivyokuwa vikikosekana katika ule mti wa mageuzi. Jarida hilo lilisema kwamba hakuna chochote kinachojulikana kuhusu wakati au jinsi jamii ya mwanadamu ilivyotokea kutokana na sokwe.41 Gyula Gyenis, mtafiti katika Idara ya Biolojia ya Anthropolojia, ya Chuo Kikuu cha Eötvös Loránd, nchini Hungaria, aliandika hivi mwaka wa 2002: “Kufahamu uainishaji wa visukuku vya hominidi na kuelewa mahali ambapo mageuzi ya hominidi yalitokea, ni jambo linaloendelea kubishaniwa.”g Mwandikaji huyo anasema pia kwamba visukuku ambavyo vimekusanywa kufikia sasa havitusaidii kujua kwa hakika wakati, mahali, au jinsi ambavyo mwanadamu aligeuka kutokana na viumbe vinavyofanana na sokwe.42

  • Je, Uhai Wote Umetokana na Chanzo Kimoja?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • [Mchoro katika ukurasa wa 24]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      Kwa nini vitabu fulani hubadili kipimo cha visukuku kinachoonyeshwa katika mfuatano fulani uliopendekezwa?

      KAMA INAVYOONYESHWA KATIKA VITABU FULANI

      KADIRIO LA UKUBWA HALISI

      [Mchoro katika ukurasa wa 25]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      Mistari yenye nukta inaonyesha uhusiano unaodhaniwa

      Samaki asiye na taya

      Samaki aliyetoweka mwenye magamba na taya

      Samaki mwenye gegedu

      Samaki mwenye mifupa

      Amfibia

      Reptilia

      Ndege

      Mamalia

      VIPINDI VYA WAKATI VYA KIJIOLOJIA →→→→

      Uthibitisho wa visukuku halisi hauonyeshi uhusiano wowote

      Samaki asiye na taya

      Samaki aliyetoweka mwenye magamba na taya

      Samaki mwenye gegedu

      Samaki mwenye mifupa

      Amfibia

      Reptilia

      Ndege

      Mamalia

      [Picha katika ukurasa wa 26]

      Ikiwa “picha 95” za rekodi ya visukuku zinaonyesha kwamba wanyama hawageuki kutoka kwa aina moja hadi nyingine, kwa nini wataalamu wa visukuku wanapanga zile “picha 5” zinazobaki kuonyesha kwamba wanyama hao walitokana na mageuzi?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki