Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wanyama wa Pori wa Dunia Wanaotoweka
    Amkeni!—1997 | Julai 8
    • Wanyama wa Pori wa Dunia Wanaotoweka

      NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

      JE, WEWE husisimuki kuona na kusikia wanyama halisi wa pori—simbamarara, nyangumi, au gorila? Je, husisimuki kumtunza koala? Kuhisi ardhi ikitetemeka chini ya kwato zenye kishindo za makundi ya wanyama wenye kuhama ambao ni wengi sana kufikia upeo wa macho? Lakini, kwa kusikitisha huenda watu wengi wasifurahie maono kama hayo—ila tu wazuru jumba la makumbusho, wasome kitabu, au wawaone katika kompyuta. Kwa nini?

      Hii ni kwa sababu usomapo makala hiihii, maelfu ya mimea na wanyama yanatoweka kwa kasi. Dakt. Edward O. Wilson, mwanabiolojia kwenye Chuo Kikuu cha Harvard, akadiria kwamba spishi 27,000 kwa mwaka, au spishi tatu kwa kila saa, hutoweka. Kwa kiwango hicho, kufikia asilimia 20 ya spishi za dunia zingeweza kutoweka katika miaka 30 ijayo. Lakini kutoweka hakudumu kwa kiwango kilekile; kunazidi kuongezeka. Inatabiriwa kwamba kufikia mwanzo-mwanzo wa karne ifuatayo, mamia ya spishi zitakuwa zikitoweka kila siku!

      Kifaru mweusi wa Afrika yumo hatarini mwa kutoweka. Uwindaji wa haramu ulipunguza idadi zao tokea 65,000 hadi 2,500 kwa muda unaopungua miaka 20. Orangutangu wanaopungua 5,000 ndio wamebaki katika misitu inayopunguka ya Borneo na Sumatra. Uharibifu huo umeathiri pia viumbe vya bahari za dunia. Mhasiriwa mmoja ni yule dolfini-baiji mwenye madaha apatikanaye katika Mto Yangtze wa China. Uchafuzi na uvuvi wa kiholela umeacha 100 pekee, na huenda wote wakafa kwa mwongo mmoja.

      “Wanasayansi wa nyanja mbalimbali hawakubaliani kuhusu mambo mengi,” asema Linda Koebner katika Zoo Book, “lakini kuhusu udharura wa kuokoa spishi na uhai wa sayari hii, wao husema hivi kwa kauli moja: Miaka hamsini [50] ijayo ni ya muhimu kabisa.”

      Ni Nani Apaswaye Kulaumiwa?

      Idadi ya watu yenye kuongezeka imeharakisha kiwango cha kutoweka kwa wanyama, lakini si msongo wa idadi ya watu pekee ambao unapaswa kulaumika. Viumbe vingi—njiwa aina ya passenger, moa, auk mkubwa, na thilasini, kwa kutaja vichache tu—vilitoweka muda mrefu kabla ya tatizo la idadi kubwa ya watu kuzuka. Dakt. J. D. Kelly, mkurugenzi wa Kamati ya Hifadhi za Wanyama ya New South Wales, Australia, asema hivi juu ya rekodi ya nchi hiyo: “Kupotezwa kwa aina nyingi za mimea na wanyama tangu makao hayo yaanze katika 1788 ni aibu kubwa ya kitaifa.” Bila shaka maoni hayo ni ya kweli kuhusu nchi nyinginezo nyingi. Pia yadokeza visababishi vingine vibaya zaidi vya kutoweka kwa wanyama—ukosefu wa ufahamu na pupa.

      Kwa sababu ya tatizo la kutoweka kwa wanyama duniani pote, kuna mteteaji mpya asiyetazamiwa ambaye anatetea hao wanyama wenye kung’ang’ania uhai—zile bustani za wanyama. Kwa kuongezeka, bustani hizo za wanyama zilizo katikati ya miji ndizo himaya za pekee za spishi nyingi. Lakini bustani nyingi za wanyama hazina nafasi za kutosha, na kuwatunza wanyama wa pori kuna gharama kubwa na vilevile ni kazi ngumu. Pia kuna maswala ya maadili kuhusu kuwafungia, hata kama wanatendewa kwa huruma. Isitoshe, wakiwa katika bustani za wanyama wao hutegemea kabisa upaji wa kifedha kutoka kwa wanadamu na mifumo dhaifu ya kisiasa na kiuchumi ambayo mara nyingi haitegemeki. Kwa hiyo hao wakimbizi kutoka porini wako salama kadiri gani?

      [Sanduku katika ukurasa wa 3]

      Je, Kutoweka kwa Wanyama Ni Jambo la Asili?

      “Je, kutoweka kwa wanyama si utaratibu wa kiasili? Jibu ni la, angalau si kwa kiwango ambacho kutoweka kumetukia katika nyakati za majuzi. Kwa muda mrefu katika miaka 300 ambayo imepita, kiwango cha kutoweka kwa spishi kilikuwa karibu spishi moja kwa mwaka. Kwa sasa, kiwango cha kutoweka kunakosababishwa na wanadamu ni angalau mara elfu moja kuliko cha awali. . . . Kisababishi cha ongezeko hilo la kutoweka kwa wanyama ni utendaji wa kibinadamu.”—The New York Public Library Desk Reference.

      “Nimevutiwa na viumbe vingi visivyo vya kawaida vilivyotoweka, na kuhuzunishwa, na mara nyingi nikikasirika kwa sababu vilitoweka. Kwa sababu katika visa vingi ni Mwanadamu ambaye kwa sababu ya pupa au ukatili, uzembe au kutojali amechangia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutoweka kwa viumbe hivyo.”—David Day, The Doomsday Book of Animals.

      “Utendaji wa kibinadamu unasababisha kutoweka kwa spishi kabla hazijarekodiwa.”—Biological Conservation.

  • Bustani ya Wanyama—Je, Ni Tumaini la Mwisho la Wanyama wa Pori?
    Amkeni!—1997 | Julai 8
    • Bustani ya Wanyama—Je, Ni Tumaini la Mwisho la Wanyama wa Pori?

      KATIKA nyakati za majuzi mabadiliko makubwa yametukia polepole katika bustani za wanyama zenye maendeleo zaidi ulimwenguni. Ukiwa wonyesho wa nje, wao wamerekebisha upya bustani hizo kwa kupatana na wazo lenye ufikirio la kuwa na “mandhari ya asili”—kule kufanyizwa kwa mazingira ya asili ya wanyama, yaliyo kamili kwa mimea, mawe, mimea yenye kutambaa, ukungu, kelele, na hata wanyama na ndege ambao huambatana pamoja. Ingawa ni gharama kubwa kufanya hivyo—dola bilioni 1.2 hivi hutumiwa ili kuboresha bustani za wanyama na matangi ya viumbe vya bahari kila mwaka Marekani pekee—mabadiliko hayo huonwa kuwa ya lazima kwa kufikiria daraka jipya la bustani za wanyama.

      Utume wa Karne Ijayo

      Huku uhaba wa wanyama na mimea ukitisha sayari, bustani za wanyama zilizo mashuhuri ulimwenguni zimeazimia kuhifadhi wanyama, kuelimisha watu, na kufanya utafiti wa kisayansi katika karne ya 21. Zikichochewa na mwito huo na kusukumwa na udharura wa hali, bustani nyingine za wanyama hata zimeacha kabisa kutumia jina bustani ya wanyama na badala ya hivyo zinatumia maneno kama “hifadhi ya wanyama wa pori” au “mbuga ya hifadhi.”

      Kichapo The World Zoo Conservation Strategy ndicho kinachoongoza harakati hizo mpya. Kikifafanuliwa na mwandikaji mmoja kuwa “hati muhimu zaidi ambayo jumuiya za bustani za wanyama zimepata kutokeza,” kichapo Strategy hasa ni mkataba wa masuala ya wanyama; hicho “chafafanua wajibu na madaraka ya bustani za wanyama na matangi ya viumbe vya bahari vya ulimwengu ili kuhifadhi aina nyingi za wanyama wa pori wa duniani kote.” Kikiondosha shaka zozote juu ya hayo mambo mapya, Strategy chaongezea: “Haki ya kuwapo kwa bustani ya wanyama au kuwapo kwa matangi ya viumbe vya bahari kwa hakika yategemea mchango wake katika kuhifadhi wanyama wa pori.”

      Kuelimisha umma na kufanya utafiti wa kisayansi, hasa kuhusu uzalishaji wa wanyama walio utekwani, ni muhimu sana katika daraka hili jipya. Miongoni mwa vijana wa leo mna wale watakaotunza bustani za wanyama kesho, ambao watakuwa na daraka la kuhifadhi mabaki yaliyookoka kati ya spishi nyingi zinazozidi kutoweka porini. Je, wao watatumia amana hiyo kwa hekima na kwa ujitoleaji? Na je, mwanadamu kwa ujumla atakuwa na ufahamu zaidi kuhusu mambo ya asili? Kwa kusudi hilo, Strategy chatia moyo kila bustani ya wanyama kuelimisha watu, na kujiona kuwa sehemu ya “mfumo wa ulimwenguni pote wa kutahadharisha watu.”

      Bustani za Wanyama Zaungana Katika Mfumo wa Duniani Kote

      Kwa sababu ya ukubwa sana wa kazi hiyo, bustani nyingi za wanyama zinaungana ili kufanyiza mfumo wa duniani kote, ambao sasa una ushirika wa bustani za wanyama zipatazo 1,000. Mashirika ya kimataifa, kama vile Shirika la Ulimwengu la Bustani za Wanyama na Muungano wa Kimataifa wa Hifadhi ya Asili na Maliasili, huunganisha bustani hizo pamoja na kuandaa mawasiliano na mwelekezo.

      Kikitaja sababu kubwa sana ya kuwa na ushirikiano kama huo, kitabu Zoo—The Modern Ark chasema: “Kuzalisha wanyama wa familia moja kusipokomeshwa, bustani hizo za wanyama haziwezi kuridhika kwa kudhibiti tu wanyama wachache zilizo nao kama vile simbamarara wa Siberia. Badala ya hivyo, simbamarara wote wa Siberia walio utekwani katika bustani zote za wanyama za kontinenti fulani—au hata ulimwenguni pote—waonwe kuwa wa familia moja.” Ndiyo, mamia ya kila spishi huhitajika ili kukomesha kuzalisha wanyama wa familia moja—ambako ni utangulizi wa kutoweza kuzaa na kutoweka kabisa kwa wanyama—na kwa wazi bustani moja ya wanyama haiwezi kutimiza jambo hilo. Kichapo Strategy chasema: “Kukusanywa kwa mali zote ziwezazo kutumika kutahitajika ili kuipa Dunia yetu . . . uwezekano mzuri zaidi wa kuokoka. Kuna wengi wanaoamini kwamba tukishindwa kuhifadhi spishi nyinginezo tutashindwa kujiokoa.” Bila shaka, mtazamo huu wa kutotazamia mazuri haufikirii ahadi ya Biblia ya dunia iliyorudishwa kuwa paradiso.—Ufunuo 11:18; 21:1-4.

      Vifaa vya Kusaidia Bustani za Wanyama Kufanikiwa

      Tatizo la kutoweka kwa wanyama limechochea pia uundaji wa vifaa fulani vya tekinolojia ya hali ya juu viwezavyo kutumika kimataifa katika uzalishaji wa wanyama walio utekwani: rekodi za uzalishaji wa wanyama, International Zoo Yearbook (IZY), na Mfumo wa Habari za Spishi Zipatikanazo Kimataifa (ISIS) unaotegemea kompyuta.

      Kila rekodi ya uzalishaji wa wanyama huorodhesha habari nyingi juu ya wanyama wote wa spishi moja wanaoishi katika bustani mbalimbali za wanyama, hata wawe wapi ulimwenguni. Hiyo ikiwa rekodi ya kimataifa, ndiyo ufunguo wa kuhifadhi chembe za urithi na kukomesha kuzalisha wanyama wa familia moja. Bustani ya Wanyama ya Berlin ilifungua rekodi ya kwanza kabisa ya kuzalisha wanyama mnamo 1923 ilipoanza kuzalisha nyatisinga wa Ulaya, ambaye karibu atoweshwe na Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.

      Ili kuboresha usambazaji wa habari za kisayansi kama vile rekodi za uzalishaji wa wanyama, IZY, na habari za idadi ya wanyama, shirika la ISIS lilijiunga na mfumo mkuu wa kompyuta katika 1974 Marekani. Mfumo wake wa kompyuta wenye kupanuka na ugavi mkubwa unaozidi kuongezeka wa habari unasaidia bustani za wanyama kuweza kufanya kazi pamoja ili ushirikiano wa bustani nyingi za wanyama utimizwe.

      Vifaa vya kibiolojia vinavyotumiwa na bustani za wanyama hutia ndani kupiga chapa za DNA, kupachika viinitete, utungishaji wa yai nje ya mwili, na cryogenics (kugandisha shahawa na viinitete). Kupiga chapa za DNA husaidia bustani za wanyama kutambulisha uzazi wa mnyama bila kukosea hata kidogo, jambo lililo muhimu katika kudhibiti kuzalisha wanyama wa familia moja, kama vile miongoni mwa wanyama ambao hutembea kwa makundi makubwa, ambao ni vigumu sana kujua uzazi wao. Kwa wakati uo huo kupachika kiinitete na kutungisha yai nje ya mwili huharakisha uzalishaji. Njia moja ya kutimiza hilo ni kuongeza “wazazi” wengi zaidi kwa spishi iliyo hatarini mwa kutoweka. Viinitete vyao vyaweza kuingizwa katika spishi zilizo na uhusiano wa karibu nao—hata wanyama wa kufugwa—ambao nao huwa mama-walezi. Mbinu hiyo imefanya ng’ombe amzae ng’ombe-mwitu na paka wa nyumbani kumzaa paka wa jangwa wa India ambaye yumo hatarini kabisa mwa kutoweka. Pia imepunguza gharama, hatari, na athari za kusafirisha mnyama aliye hatarini mwa kutoweka. Viinitete au shahawa zilizogandishwa ndizo huhitajika tu kusafirishwa.

      Kukiwa na uwezekano wa spishi fulani kutoweka kabisa, bustani fulani ya wanyama imeingilia sayansi ya kugandisha shahawa na viinitete na kuziweka akiba kwa muda mrefu. Vitu hivyo vilivyogandishwa hutoa tazamio la kuzaliwa kwa wazao miongo mingi, na labda hata karne nyingi baadaye, baada ya wanyama hao kutoweka! Ingawa imejaa tashwishi, hiyo imeitwa “jambo la pekee liwezalo kufanywa.”

      Uchunguzi Porini Husaidia Bustani za Wanyama Kuzalisha Watoto Zaidi

      Uchunguzi wa kisayansi wa wanyama, kutia ndani tabia zao wakiwa katika makao yao ya asili, ni muhimu sana katika kuzalisha wanyama walio utekwani na ndio kichocheo cha kufanyiza “mandhari ya asili” katika bustani za wanyama. Ili wanyama wadumishe afya nzuri na kuweza kuzaana, ni lazima bustani za wanyama zifikirie silika za wanyama hao na “kuwafurahisha.”

      Kwa mfano, duma wa kiume na duma wa kike hujitenga wakiwa porini nao huwasiliana kwa harufu tu iliyo katika mkojo wao na kinyesi chao. Harufu humjulisha duma wa kiume wakati ambapo duma wa kike yu tayari kujamiiana, kisha yeye hukaa na duma wa kike kwa siku moja au mbili tu. Bustani za wanyama zilipogundua tabia hiyo, zilirekebisha mahali walipo wanyama hao ili kutenganisha duma wa kiume na duma wa kike wakati wote ila tu katika pindi fupi za kujamiiana, na wakafaulu; watoto wakazaliwa.

      Ingawa kutoonana kwa duma hufanya wapendane zaidi, sivyo ilivyo na heroe. Wao hujamiiana tu katika makundi makubwa sana ambayo bustani za wanyama haziwezi kushughulikia. Kwa hiyo bustani fulani za wanyama katika Uingereza zilifanya majaribio—“zilirudufisha” ukubwa wa kundi kwa kioo kikubwa sana. Kwa mara ya kwanza, ndege hao walianza michezo ya kutazamisha ya kujamiiana! Je, mifano hiyo inakupa dokezo la utata wa wanyama wa pori wa dunia? Kwa hakika bustani za wanyama zinakabili ugumu mkubwa sana.

      Mradi wa Kuokoa Wanyama Ni Halisi Kadiri Gani?

      Ikionyesha uwezekano wa hiyo programu mpya kufaulu, spishi nyingine zilizozalishwa utekwani zimerudishwa katika bustani zao za asili. Miongoni mwa hao ni tai wa California, nyatisinga wa Ulaya, nyatisinga wa Marekani, choroa wa Arabia, golden lion tamarin, na farasi-mwitu. Hata hivyo, kuna shaka juu ya matazamio ya wakati ujao.

      “Jamii ya kibinadamu ni tata sana, na matatizo ya ulimwengu ni mengi sana,” chasema Strategy, “hivi kwamba japo ukuzi wa ufahamu na hangaiko kuhusu asili na mazingira, haijawezekana kukomesha hatua nyingi zenye kuleta uharibifu.” Tokeo ni kwamba, “ni lazima wahifadhi wajitayarishe kutafuta njia za kukabili kipindi cha matatizo kinachotazamiwa,” chaongezea. Kwa kawaida, jambo hilo lataka ushirikiano katika kila tabaka la jamii. Ushirikiano wa sasa, kulingana na mwandishi mmoja wa kisayansi, “ni mbali sana na ushirikiano unaohitajika.” Ikiwa misongo inayofanya wanyama watoweke yapungua tu lakini haikomi, hata jitihada bora zaidi huenda bado zisifaulu. Bustani kubwa na zilizo kamili—si maeneo madogo pekee, ambayo hutokeza kuzalisha wanyama wa familia moja—ni lazima zitayarishwe. Ndipo tu bustani za wanyama ziwezapo kuachilia wanyama bila wasiwasi ili warudi porini. Lakini, je, tumaini kama hilo ni halisi, au ni dhana tu ambayo haiwezi kufaulu?

      Isitoshe, ni vigumu hata zaidi kuamini kwamba suluhisho ni ushirikiano wa bustani zote za wanyama. “Ukweli mchungu,” asema Profesa Edward Wilson, “ni kwamba bustani zote za wanyama ulimwenguni pote leo zaweza kutoshea spishi 2,000 tu za wanyama, ndege, wanyama-watambaazi na amfibia”—na hizo ni spishi chache sana. Kwa hiyo bustani za wanyama zina jukumu gumu la kuamua ni spishi gani zitakazohifadhiwa na spishi zitakazojiunga na orodha ndefu ya wanyama wanaotoweka.

      Kwa wataalamu wa uhifadhi, hilo lazusha swali lenye kutisha, Kwa kufikiria kutegemeana kwa viumbe vyote vilivyo hai, ni lini wanyama na mimea watakapokuwa hatarini kufikia hatua ambapo wataanzisha kutoweka kwingi kwa wanyama ambako kutaharibu uhai ubakio duniani, kutia ndani na wanadamu? Wanasayansi wanaweza kukisia tu. “Kutoweka kwa spishi moja au mbili au hamsini kutakuwa na athari ambazo sisi hatuzijui,” asema Linda Koebner katika Zoo Book. “Kutoweka kwa wanyama kunatokeza badiliko hata kabla ya sisi kuelewa athari zake.” Kwa wakati uo huo, chasema kitabu Zoo—The Modern Ark, “bustani za wanyama zadumu kuwa hifadhi muhimu zaidi ya uhai katika vita vya dunia vya kuangamiza wanyama, vita ambavyo haviwezi kutabirika na ambavyo vizazi vya wakati ujao vitatulaumu kabisa.”

      Basi, je, kuna msingi wowote wa kuwa na tumaini? Au je, vizazi vya wakati ujao vitabaki na dunia isiyo na wanyama na mimea, vyenyewe vikingoja kutoweka?

  • Dunia Nzima Itakapokuwa Hifadhi
    Amkeni!—1997 | Julai 8
    • Dunia Nzima Itakapokuwa Hifadhi

      JE, UNATAKA kuona kiumbe kilicho hatari zaidi duniani? Basi tazama kioo! Ndiyo, sisi wanadamu ndio waharibifu wabaya zaidi wa dunia! Sisi hata huuana kwa wingi sana.

      Ili kufanya dunia iwe salama kwa wanyama wa pori, hata katika bustani ya wanyama—hasa kama hizo zaja kuwa makimbilio ya mwisho—ni lazima vita ambayo huathiri sana mwanadamu iondolewe. Ni wanyama 91 tu kati ya wanyama 12,000 wa Bustani ya Wanyama ya Berlin waliookoka Vita ya Ulimwengu ya Pili. Bustani nyingine nyingi ziliathirika vivyo hivyo. Katika vita ya majuzi katika nchi za Balkani, wafanyakazi wenye moyo mkuu wa bustani ya wanyama walihamisha wanyama wengi wakapata usalama; lakini mamia mengine, kutia ndani dia, jamii ya paka wakubwa, dubu na mbwa-mwitu, waliuawa. Majuzi, katika misitu ya Kambodia, kulingana na maofisa walionukuliwa katika gazeti la habari The Australian, wapiganaji wa Khmer Rouge wamewachinja kimakusudi wanyama wengi walio nadra kupatikana. Kwa nini? Ili kupata silaha kwa kutoa ngozi na viungo vinginevyo vya wanyama hao!

      Uporaji wa kimakusudi wa kimazingira, kama ule unaofanywa katika Visiwa vya Peron vilivyojitenga, vilivyoko kusini-magharibi mwa Darwin, Australia, ni uovu mwingine ambao ni lazima ukomeshwe iwapo wanyama watapata usalama—ndani au nje ya bustani ya wanyama. Mara mbili katika miaka mitatu, makazi ya mwari katika visiwa hivyo yamechomwa bila sababu yoyote ila tu kuua maelfu ya makinda kikatili.

      Hata hivyo, katika miongo ya majuzi upotezo mkubwa zaidi wa spishi hausababishwi na uovu; bali ni athari ya ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji sana mahali pa kuishi na ardhi ya kulima. Kwa sababu ya kuingilia daima makao ya wanyama na uchafuzi ambao hufuata, The World Zoo Conservation Strategy chaonya: “Karne ya 21 haionekani kuwa nzuri kwa habari ya mfumo wote wa asili wa dunia. Hakuna ishara yoyote ionyeshayo kwamba uharibifu unaotukia katika karibu sehemu zote za ulimwengu utakoma.”

      Kwa sababu ya hangaiko linalozidi kuongezeka kuhusu wakati ujao wa dunia, wakati ambapo dunia nzima itakapokuwa hifadhi waweza kuonekana kama ndoto tu. Lakini, tumaini hilo lina msingi mzuri, si kwa maoni ya wanadamu wasioweza kuona mbali—ambao hata kwa miaka michache kama 50 iliyopita, kulingana na mwandikaji fulani wa kisayansi, hawakuweza kuona uharibifu mkubwa wa sasa wa kiikolojia—bali kwa yule ambaye aliliona, Yehova Mungu. Zaidi ya miaka 1,900 iliyopita, yeye alitabiri kikweli kwamba katika wakati wetu mwanadamu angepatikana ‘akiharibu dunia.’ (Ufunuo 11:18) Unabii huo ulipotajwa wakati ambapo dunia haikuwa na watu wengi, huenda ulionekana kana kwamba ni ndoto tu kwa wengi walioishi wakati huo, lakini umethibitika kuwa sahihi kama nini!

      Kwa kinyume, uharibifu huo unatukia wakati ambapo sayansi na tekinolojia huonekana karibu kuweza kufanya muujiza: transmita ndogo-ndogo na setilaiti hufuatia miendo ya spishi zilizo hatarini mwa kutoweka, uharibifu wa misitu ya mvua waweza kupimwa barabara hadi meta za mraba kutoka anga za nje, na uchafuzi wa hewa kupimwa katika viwango vidogo sana. Lakini, isipokuwa katika visa vilivyo nadra sana, mwanadamu haonekani kama anaweza kurekebisha hali kwa kutegemea habari nyingi alizo nazo. Labda mwanadamu ni kama dereva wa gari-moshi ambalo limeharibika likiwa mwendoni. Yeye ana vifaa vya ajabu vya elektroni na vichunguzi vinavyomwonyesha kile kinachotendeka, lakini yeye hawezi kusimamisha gari-moshi!

      Kwa Nini Jitihada Zao Zaambulia Patupu?

      Ebu wazia kwamba katika kiwanda kikubwa, meneja mwenye kiburi asiyefuata kanuni atukia kumsikia mwenye kiwanda akisema kwamba huyo meneja hatapandishwa cheo bali atafutwa kazi katika miezi michache ijayo. Akiwa amekasirika na kuwa na uchungu, yeye atumia uwongo, hongo, na mbinu zozote zile zilizo chafu ili wafanyakazi fulani wasababishe mvurugo. Wao wafanya mashine zikwame, mazao yawe chini, na bidhaa kuwa na kasoro—lakini kwa ujanja hivi kwamba waepuka lawama. Kwa wakati uo huo, wafanyakazi wenye kufuatia haki, bila kujua kinachoendelea hasa, wajaribu kufanya marekebisho; lakini kwa kadiri wajitahidivyo, ndivyo na mambo yawavyo mabaya.

      “Meneja” mbaya wa ulimwengu huu ametunga hila kama hizo dhidi ya wanadamu na dunia. Lakini sisi hatupaswi kukaa bila “ujuzi kuhusu mbinu zake,” kwa kuwa Biblia yamfunua na kuonyesha kiumbe-roho mwenye uchungu—Shetani Ibilisi—malaika aliyekuja kutaka makuu na kutamani kuabudiwa. (2 Wakorintho 2:11; 4:4) Mungu alimwondosha kutoka kwa familia Yake ya kimbingu na kumhukumia uharibifu.—Mwanzo 3:15; Waroma 16:20.

      Kama yule meneja mbaya wa kiwanda, huyu “baba ya uwongo” pia hutumia mbinu nyinginezo mbaya ili kuonyesha hasira yake. Yeye amemchukia Yehova Mungu naye anataka kuharibu uumbaji Wake. (Yohana 8:44) Silaha kali zaidi za Shetani ni propaganda za uwongo, pupa, ufuatiaji wa vitu vya kimwili, na mafundisho ya kidini yenye kudhuru. Akitumia hizo yeye ‘ameiongoza vibaya dunia yote inayokaliwa’ na kugeuza wanadamu—wale waliokusudiwa kuihifadhi—kuwa waharibifu wakubwa zaidi, na hivyo kuwa kama wafuasi wa Nimrodi wa kale, aliyekuwa “mwindaji hodari dhidi ya Yehova.”—Ufunuo 12:9, 12; Mwanzo 1:28; 10:9, NW.

      Tumaini Halisi la Kipekee la Hifadhi ya Kidunia

      Hata hivyo, ushindi juu ya kani za kibinadamu na zizidizo za kibinadamu ambazo zinasababisha kutoweka kwa wanyama waweza kupatikana. Muumba mweza-yote wa vitu vyote vilivyo hai aweza kutuondoa kwenye hali hii mbaya sana, naye ameahidi kufanya hivyo kupitia serikali yake ya kimbingu. Yeye aahidi kuangamiza waharibifu hao wanaoharibu dunia. Sisi husali hilo litukie tusemapo: “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”—Mathayo 6:9, 10, Union Version; Ufunuo 11:18.

      Je, uliona kwamba kuja kwa Ufalme huo kunahusika na kufanywa kwa mapenzi ya Mungu duniani? Hiyo ni kwa sababu Ufalme wa Mungu ni serikali ya Mungu ya kutawala juu ya dunia. Na kwa kuwa huo ni ufalme, basi una mfalme—Yesu Kristo, ambaye ni “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.” (Ufunuo 19:16) Pia una raia. Hata Yesu alisema: “Wenye furaha ni wenye tabia-pole, kwa kuwa wao watairithi dunia.” (Mathayo 5:5) Ndiyo, hao wenye tabia-pole ndio raia watakaoishi duniani, na kwa msaada wa Ufalme wa Mungu, wao watatunza kwa upendo urithi wao, wakiugeuza kuwa paradiso iliyojaa viumbe. Kwa kupendeza, Strategy chasema: “Wakati ujao wa wanadamu na asili waweza tu kuhakikishiwa usalama ikiwa wanadamu wote waweza kuishi kwa upatano mpya na asili.”

      Historia na asili ya binadamu isiyokamilika zaonyesha kwamba haiwezekani kwa “wanadamu wote” leo kupata kuishi kwa “upatano mpya” na asili, kwa kuwa hao hawajamtia ndani Yehova. Kwa hakika, kuthibitisha ubatili wa wanadamu kujitawala ndiyo sababu moja inayomfanya Mungu aruhusu ulimwengu huu kuendelea kwa muda mrefu hivyo. Lakini karibuni, wale wanaotamani utawala wa Kristo watafurahia amani tele. Isaya 11:9 lathibitisha hilo, nalo pia laonyesha sababu inayofanya wao pekee waweze kuishi kwa “upatano mpya” na asili: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Italiki ni zetu.) Ndiyo, elimu ya kimungu ndiyo ufunguo. Na je, hilo si jambo lifaalo, kwa kuwa ni nani ila Muumba wa asili aliye na hekima kama hiyo?

      Vipi juu ya wale wanaodumu kumpuuza Yehova? “Bali waovu watatengwa na nchi,” lasema Mithali 2:22. Ndiyo, uchokozi wao au kutojali kwao kutawagharimu uhai katika “dhiki kubwa” inayokaribia upesi—njia ya Mungu ya kuhukumu wale wote wanaodumu kutumia vibaya na kuharibu uumbaji wake.—Ufunuo 7:14; 11:18.

      Je, unataka kushiriki katika programu ya kurekebisha dunia? Basi tafadhali jua yale ambayo Mungu ataka ufanye kwa kujifunza Biblia. Ni hiyo pekee iwezayo kukufanya uone maoni ya Muumba. (2 Timotheo 3:16; Waebrania 4:12) Kwa kuongezea, kwa kutumia yale unayojifunza, hutakuwa tu raia mzuri sasa bali pia utathibitisha kwamba kwa kweli wewe ni mtu ambaye ataaminishwa na Yehova “dunia mpya” yake inayokuja kwa kasi.—2 Petro 3:13.

      Ikiwa ungependa, wachapishaji wa gazeti hili au kutaniko la Mashahidi wa Yehova lililo karibu zaidi nawe litafurahia kukusaidia kuwa na funzo la Biblia nyumbani bila malipo au kukupa fasihi zaidi zenye kueleza mambo haya.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki