Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mtoto Anapokosa Kufurahia Maisha Yake ya Utotoni
    Amkeni!—2003 | Aprili 22
    • Mtoto Anapokosa Kufurahia Maisha Yake ya Utotoni

      “Kufurahia maisha ya utotoni ndiyo haki ya kwanza kabisa ya watoto.”—Kitabu “The Hurried Child.”

      AMA kweli utakubali kwamba watoto wote wanapaswa kufurahia maisha yao ya utotoni bila kuwa na mahangaiko yoyote. Hata hivyo, inahuzunisha kuona kwamba wavulana na wasichana wengi hawafurahii maisha yao ya utotoni. Hebu fikiria kuhusu maelfu au hata mamilioni ya watoto, ambao wameathiriwa na vita na hivyo matarajio yao maishani kudidimia. Fikiria pia kuhusu watoto ambao maisha yao yameharibiwa na utumwa au mateso.

      Wengi wetu hatuwezi kuwazia jinsi watoto wanavyohisi wanapolazimika kuishi barabarani kwa kuhisi kwamba maisha ya barabarani ni salama kuliko ya nyumbani. Huo ni wakati ambao wanahitaji kupendwa na kuhisi wakiwa salama. Badala yake, watoto hao wamelazimika kujifunza kuishi barabarani na kujilinda na wavamizi wowote ambao wangetaka kuwashambulia. Tena na tena, watoto wamevurugwa na matukio ya nyakati zetu ngumu.

      “Laiti Ningalirudia Maisha Yangu ya Utotoni”

      Carmen, mwenye umri wa miaka 22, alitaabika sana alipokuwa mtoto.a Kwa kuwa baba yao aliwatesa na mama yao akawapuuza, Carmen na dada yake walilazimika kuishi barabarani. Ijapokuwa kulikuwa na hatari nyingi, wao waliepuka madhara mengi ambayo huwapata watoto wengi ambao hutoroka nyumbani.

      Hata hivyo, Carmen bado anajuta kwa kukosa kufurahia maisha yake ya utotoni. “Ni kana kwamba niliruka kutoka utotoni hadi umri wa miaka 22,” yeye asema akisikitika. “Sasa nimeolewa na nina mtoto, lakini bado natamani kufanya mambo yanayofanywa na wasichana wadogo, kama kucheza na wanasesere. Nataka kupendwa na kukumbatiwa na wazazi wangu. Laiti ningalirudia maisha yangu ya utotoni.”

      Watoto wengi sana wanateseka kama Carmen na dada yake. Wanaishi barabarani, na hawafurahii maisha yao ya utotoni. Wengi wao hujiruzuku kwa kufanya uhalifu. Habari na takwimu zinaonyesha kwamba watoto wadogo sana wanajihusisha na uhalifu. Na isitoshe, wasichana wengi wanapata watoto wakiwa wadogo mno—wakiwa bado ni watoto.

      Tatizo Lililofichika

      Si ajabu kwamba watoto wengi wanapelekwa kwenye vituo vya utunzaji. Tahariri iliyochapishwa katika gazeti la Week-end Australian ilisema hivi: “Matatizo ya utunzaji yamezuka bila ya sisi kujua. Watoto wengi zaidi kutoka familia zilizovunjika au zenye matatizo wanapuuzwa.” Gazeti hilo pia lilisema hivi: “Wafanyakazi waliopewa daraka la kuwatunza watoto hao hukaa kwa miezi au hata miaka bila kuwajulia hali watoto hao, huku watoto wengine wakihamishwa huku na huku, na hivyo kukosa makao ya kudumu.”

      Habari fulani ilisema kwamba msichana mmoja mwenye umri wa miaka 13 alipitia makao 97 kwa kipindi cha miaka mitatu. Alikaa usiku mmoja tu katika makao mengine. Sasa anakumbuka jinsi alivyokuwa mwenye majonzi mengi kwa sababu ya kudharauliwa na kukosa usalama. Watoto kama hao hawafurahii maisha yao ya utotoni hata kidogo.

      Basi haishangazi kwamba wataalamu wanasema kuwa watoto wengi zaidi hawafurahii maisha yao ya utotoni. Ikiwa wewe ni mzazi, unapofikiria mambo hayo yenye kusikitisha, unapaswa kuona kwamba umebarikiwa kwa kuwa unaweza kuwaandalia watoto wako makao na mahitaji mengine. Lakini kuna hatari nyingine. Katika ulimwengu wa leo, si watoto wote wanaokosa kufurahia maisha yao ya utotoni kabisa. Wakati mwingine, maisha yao ya utotoni huharakishwa. Jinsi gani, na kukiwa na matokeo gani?

      [Maelezo ya Chini]

      a Jina limebadilishwa.

  • Maisha ya Utotoni Yanapoharakishwa
    Amkeni!—2003 | Aprili 22
    • Maisha ya Utotoni Yanapoharakishwa

      NDEGE ndogo yenye injini moja ilipita kasi kwenye barabara ya uwanja wa ndege na kuanza kupaa chini ya anga lenye mawingu meusi. Waandishi wa habari walikuwepo kunasa tukio hilo na kupiga picha, huku wakiuliza maswali na kustaajabu sana. Kwa nini wakastaajabu? Si kwa sababu ya rubani aliyekuwa ndani ya ndege hiyo wala abiria mwanamume aliyekuwepo, bali ni kwa sababu ya binti ya abiria huyo. Msichana huyo alikuwa na umri wa miaka saba.

      Msichana huyo alikuwa aendeshe ndege hiyo. Angekuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuendesha ndege nchini Marekani. Waandishi wa habari walikuwa na shughuli nyingi kwani wangeisubiri ndege hiyo mahali ambapo ingetua. Ijapokuwa kulikuwa na mawingu meusi, watu hao watatu waliipanda ndege hiyo. Msichana huyo alikalia mto ili aweze kuona mbele na aliwekewa vifaa vya kukanyagia vilivyomsaidia kufikia pedali.

      Kwa kusikitisha, safari yao ilikuwa fupi sana. Kwa ghafula, ndege hiyo ikaanza kuyumbayumba, ikashindwa kusonga mbele na ikaanguka kwa sababu ya dhoruba kali, na wote watatu wakafa. Waandishi wa habari waliripoti kisa hicho upesi. Badala ya kutangaza habari njema zilizokuwa zikitarajiwa, waliripoti habari zenye kuhuzunisha. Hata waandishi wachache wa habari waliona ni kana kwamba waandishi wenzao wamechangia mkasa huo. Watu wengi walianza kusema kwamba watoto hawapaswi kuruhusiwa kuendesha ndege. Nchini Marekani, sheria zilitungwa ili kutekeleza jambo hilo. Ijapokuwa watu walikuwa na huzuni nyingi na walitoa masuluhisho ya muda mfupi, bado masuala makubwa yalihusika.

      Tukio hilo liliwafanya wengi wafikirie mwelekeo ambao watu wanao siku hizi. Watoto wachanga sana wanapewa madaraka ya watu wazima. Huenda matokeo yasije ghafula sikuzote au yawe mabaya sana. Hata hivyo, huenda yakawa mazito na yakadumu kwa muda mrefu. Hebu tuchunguze mambo machache yanayoonyesha jinsi ambavyo maisha ya utotoni yanaweza kuharakishwa.

      Wanaelimishwa Haraka-Haraka

      Ni kawaida kwa wazazi kutamani watoto wao wafanikiwe maishani. Lakini wanapohangaikia jambo hilo kupita kiasi, huenda wakawalemea watoto wao wachanga mno. Hata wanaweza kuwa na nia nzuri wanapofanya hivyo. Kwa mfano, siku hizi wazazi wengi wanawaandikisha watoto wao kwenye shughuli za baada ya shule, kama vile michezo, muziki, au kucheza dansi. Wengi wanawapeleka watoto wao kwenye mafunzo ya ziada.

      Bila shaka si vibaya kuwatia moyo watoto wakuze uwezo au mapendezi yao. Hata hivyo, hatari hutokea mambo hayo yanapofanywa kupita kiasi, hasa watoto wanapokuwa na mahangaiko mengi kama watu wazima. Gazeti Time lasema hivi: “Ingawa zamani watoto walifurahia maisha yao ya utotoni, siku hizi wanalemewa na masomo; watoto ambao wanapaswa kutumia nguvu zao za ujana kwa uhuru, sasa wanafanya kazi kama siafu.”

      Wazazi wengine hutarajia watoto wao wawe mabingwa wa riadha, muziki, au wa sarakasi. Hata kabla watoto wao hawajazaliwa, wazazi wanawaandikisha katika shule, ili wafanikiwe wakati ujao. Isitoshe, akina mama wengine hujiandikisha kwenye “vyuo vikuu vya wanawake wajawazito” ili vijusi visomeshwe muziki vikiwa vingali tumboni. Wanafanya hivyo ili kuchemsha bongo za watoto wao zinazokua.

      Katika nchi fulani, watoto wanapewa mitihani ya kusoma na ya hesabu kabla hawajafikisha umri wa miaka sita. Mambo hayo yamezusha maswali fulani kuhusu afya ya kihisia ya mtoto. Kwa mfano, vipi mtoto akianguka mtihani akiwa kwenye shule ya watoto wadogo? David Elkind, mwandishi wa kitabu The Hurried Child, asema kwamba shule zinaamua mapema mno jinsi maisha ya watoto yatakavyokuwa. Elkind anasema wao hufanya hivyo kwa sababu wanataka shule zao zionekane kuwa bora badala ya kuwaelimisha watoto hao vizuri.

      Je, watoto wanaathiriwa kwa njia yoyote wanapolazimishwa kufanya mambo ya watu wazima wakiwa bado wachanga mno? Elkind analalamika kwamba jamii inawaona watoto kuwa watu wazima wanaoweza kubeba majukumu mazito. Anasema: “Inaonyesha tunaona kwamba mwelekeo wa kuwalemea vijana na mambo mengi ni jambo la ‘kawaida.’” Kwa kweli, maoni ya watu kuhusu mambo yaliyo ya kawaida kwa watoto yanabadilika.

      Wanaharakisha Kuwa Mabingwa

      Yaelekea wazazi wengi wanaona kuwa ni jambo la kawaida, ama hata linalofaa, kuwafundisha watoto kwamba kuwa bingwa ndilo jambo la maana zaidi, hasa michezoni. Leo watoto wengi wanawekewa miradi ya kushinda medali katika michezo ya Olimpiki. Ili wapate sifa ya kuwa mabingwa kwa muda mfupi na kuhakikisha kwamba watachuma mapato mazuri wanapokuwa watu wazima, watoto fulani hulazimishwa kufanya mambo ambayo huwazuia kufurahia maisha yao ya utotoni.

      Kwa mfano, wanasarakasi wa kike huanza kufanya mazoezi mapema sana. Mazoezi hayo ya kuendelea huwa mazito sana na hufanya miili yao michanga iwe na mkazo mwingi sana. Kwa muda wa miaka mingi, wao hujitayarisha kiakili na kimwili kwa ajili ya michezo ya Olimpiki. Ukweli wa mambo ni kwamba ni wachache tu ndio hushinda. Je, kweli wale walioshindwa watahisi kwamba ilifaa wajinyime maisha yao ya utotoni? Baada ya muda fulani, hata washindi hujiuliza kama kweli walistahili kufanya jitihada hizo zote ili washinde tu.

      Hisia za wasichana hao wachanga huathiriwa pia kwani maisha yao ya utotoni huharakishwa wanapochochewa sana kuwa mabingwa. Mazoezi hayo mazito huenda yakaathiri ukuzi wao wa kimwili. Mifupa ya wengine hukosa kukua vizuri. Wengine hupata matatizo ya ulaji. Baadhi yao huchelewa kubalehe, hata kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, wasichana wengi leo huwa na tatizo tofauti kabisa: kubalehe mapema.—Ona sanduku lililo juu.

      Ni Matajiri Lakini Hawafurahii Maisha ya Utotoni

      Ni kana kwamba vyombo vya habari vinataka tuamini kwamba ili mtu afurahie maisha yake ya utotoni, ni lazima aishi maisha ya starehe. Wazazi wengine hufanya kazi kwa bidii sana ili waweze kuwanunulia watoto wao vitu vya kuwastarehesha, kama nyumba nzuri, kuwaandalia burudani za kila aina, na mavazi ya bei ghali.

      Hata hivyo, watoto wengi waliolelewa kwa njia hiyo, hujiingiza katika unywaji wa kupindukia, hutumia dawa za kulevya, na huwa waasi na hukosa furaha. Kwa nini? Wengi huwa na hasira mno kwa kuwa wanahisi wamepuuzwa. Watoto wanahitaji wazazi wanaowapenda na kuwatunza. Wazazi wenye shughuli nyingi ambao hawana nafasi ya kuwapenda na kuwatunza watoto huamini kwamba wakifanya kazi kwa bidii watawafanya watoto wao wafurahi, lakini matokeo huwa kinyume kabisa.

      Dakt. Judith Paphazy anasema kuhusu “wazazi wanaofanya kazi, na walio matajiri,” ambao mara nyingi “huwapa watoto wao vitu vingi kwa kuwa wanatambua kwamba familia zao zinaathiriwa kwa sababu wanatumia wakati mwingi sana kazini.” Anaonelea kwamba wazazi hao “wanaepa daraka lao kwa kuwanunulia vitu.”

      Watoto ndio huathiriwa zaidi. Ingawa wana vitu vingi vya starehe, wanakosa mambo muhimu ambayo yangefanya maisha yao ya utotoni yafurahishe: kupendwa na wazazi na kutumia wakati pamoja nao. Kwa sababu ya kukosa mwongozo, nidhamu, na mwelekezo, wao hukabili masuala magumu ya watu wazima mapema mno, kabla hawajawa tayari kama vile, ‘Je, nitumie dawa za kulevya? Nifanye ngono? Niwe mjeuri ninapokasirika?’ Huenda wakatafuta majibu yao wenyewe kutoka kwa marafiki, kwenye televisheni, au katika sinema. Mara nyingi matokeo huwa ni maisha mafupi ya utotoni, labda hata yenye kuhuzunisha.

      Mtoto Anapolazimika Kuwa Yule Mzazi Mwingine

      Familia yenye wazazi wote wawili inapobadilika ghafula na kuwa familia ya mzazi mmoja kwa sababu ya kifo, kutengana, au talaka, mara nyingi hisia za watoto huumia. Bila shaka, familia nyingi za mzazi mmoja hufaulu sana. Lakini katika familia nyingine, maisha ya utotoni huharakishwa.

      Mara kwa mara, huenda mzazi aliye peke yake akahisi upweke. Hata hivyo, wazazi wengine humfanya mtoto, hasa yule mkubwa, achukue daraka la yule mzazi mwingine. Labda akihisi mambo yamemlemea, mzazi anaweza kumwambia mwanawe au binti yake kuhusu matatizo ambayo mtoto huyo mchanga hayawezi. Wazazi wengine huenda wakawalemea watoto kihisia.

      Wazazi wengine huachilia madaraka yao, huku wakimlazimisha mtoto achukue daraka la yule mzazi mwingine kabisa. Carmen na dada yake, waliotajwa awali, walipatwa na jambo hilo walipoamua kuishi barabarani. Wakiwa wangali watoto, walipewa daraka la kuwatunza wale watoto wengine wadogo. Huo ulikuwa mzigo mkubwa sana.

      Ama kwa hakika, kuharakisha maisha ya watoto ni hatari, na ni jambo linalopaswa kuepukwa ikiwezekana. Lakini, kuna habari njema: Wazazi wanaweza kuchukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kwamba watoto wao wanafurahia maisha yao ya utotoni. Ni hatua gani hizo? Acheni tuchunguze baadhi ya hatua ambazo zimethibitika kuwa na matokeo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Matatizo ya Kubalehe Mapema

      Je, wasichana wanabalehe mapema siku hizi? Wanasayansi wanatofautiana kuhusu jambo hilo. Wengine wanasema kwamba katikati ya karne ya 19, kwa wastani, wasichana walibalehe kuanzia umri wa miaka 17, ilihali leo wanabalehe kabla hawajafikisha miaka 13. Uchunguzi uliofanywa katika mwaka wa 1997 wa wasichana 17,000, ulionyesha kwamba karibu asilimia 15 ya wasichana Wazungu na asilimia 50 ya wasichana Wamarekani wenye asili ya Kiafrika nchini Marekani huonyesha dalili za kubalehe mapema wakiwa na umri wa miaka minane! Hata hivyo, baadhi ya madaktari wanapinga matokeo hayo na kuwaonya wazazi wasione dalili za mapema sana za kubalehe kuwa jambo la “kawaida.”

      Vyovyote vile, hali hiyo inatokeza magumu kwa wazazi na watoto. Gazeti la Time linasema: “Mbali na mabadiliko ya kimwili, tatizo kubwa zaidi ni madhara ya kiakili yanayowapata watoto wadogo sana wanaobalehe mapema, ambao husumbuliwa na wanaume. . . . Wakati wao wa utotoni ni mfupi mno.” Makala hiyo inazusha swali hili tata: “Wasichana wadogo wanapokuwa na miili kama ya watu wazima kabla hawajakomaa kihisia na kiakili, watapatwa na nini?”

      Mara nyingi wao husumbuliwa kingono. Mama mmoja anasema hivi waziwazi: “Wasichana wenye miili mikubwa kwa sababu ya kubalehe mapema ni kama asali [kwa nyuki]. Wao huwavutia wavulana wenye umri mkubwa zaidi.” Mtoto mdogo anapochochewa kufanya ngono, matokeo huwa mabaya. Msichana mdogo anaweza kujihisi hafai kitu. Anaweza kuwa na dhamiri mbaya na afya yake ya kimwili na ya kihisia kuathiriwa.

  • Kumwezesha Mtoto Afurahie Maisha Yake ya Utotoni
    Amkeni!—2003 | Aprili 22
    • Kumwezesha Mtoto Afurahie Maisha Yake ya Utotoni

      KUFURAHIA maisha ya utotoni hutegemea sana malezi mazuri. Lakini malezi mazuri yanahusisha nini? Huenda umesikia mashauri mbalimbali kuhusu kulea watoto. Tumia wakati pamoja na watoto wako. Wasikilize. Wape mwongozo thabiti. Furahi pamoja nao na usikitike pamoja nao. Uwe rafiki yao wa kweli bila kuachilia madaraka yako ukiwa mzazi. Bila shaka kanuni hizo ambazo hurudiwa-rudiwa zitawasaidia wazazi wawalee watoto wao vizuri. Lakini kuna jambo jingine la msingi na la muhimu zaidi.

      Mamilioni ya wazazi ulimwenguni pote wametambua kwamba kufuata kanuni za Biblia ni muhimu ili kutoa malezi bora. Kwa nini? Kwa sababu Mtungaji wa Biblia mwenye hekima, Yehova Mungu, ndiye aliyeanzisha mpango wa familia. (Mwanzo 1:27, 28; 2:18-24; Waefeso 3:15) Kwa hiyo, Neno lililoandikwa kwa uongozi wake linafaa zaidi kutoa mwelekezo wa kulea watoto. Hata hivyo, kitabu cha zamani kama Biblia chawezaje kutoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa kisasa wa kuwaharakisha watoto? Acheni tuchunguze kanuni za Kimaandiko zinazohusu jambo hilo.

      “Kwa Kadiri ya Mwendo wa Watoto”

      Yakobo, mwana wa Isaka, alikuwa baba ya watoto zaidi ya kumi na wawili. Biblia inaeleza maneno yake yenye hekima aliyoyasema wakati familia yake ilipokuwa safarini: “Watoto ni wachanga [dhaifu, NW] . . . Tafadhali Bwana wangu [Esau, ndugu mkubwa wa Yakobo] na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole . . . kwa kadiri ya mwendo wa watoto.”—Mwanzo 33:13, 14.

      Yakobo alijua ya kuwa watoto wake hawangeweza kufanya mambo kama watu wazima. Walikuwa “dhaifu”—wadogo, hafifu, na wenye mahitaji mengi zaidi kuliko watu wazima. Badala ya kuwalazimisha watoto wasafiri kwa mwendo wake, alipatanisha mwendo wake na mwendo wao. Kwa kufanya hivyo, alionyesha hekima ambayo Mungu huwapa watoto wake walio duniani. Baba yetu wa mbinguni anajua kwamba kuna mambo fulani tusiyoweza kutimiza. Yeye hatarajii tufanye mambo ambayo hatuwezi.—Zaburi 103:13, 14.

      Hata wanyama fulani wana hekima kama hiyo kwa sababu Mungu aliwaumba na “hekima ya kisilika.” (Mithali 30:24, NW) Kwa mfano, wataalamu wa wanyama wamechunguza tembo na kuona kwamba kundi la tembo hutembea kulingana na mwendo wa tembo mchanga anayetembea katikati ya kundi. Wao huendelea kutembea polepole mpaka tembo huyo mdogo anapojimudu kutembea pamoja nao.

      Siku hizi watu wengine hupuuza hekima ya kimungu. Hata hivyo, si lazima uwaige. Kumbuka kwamba watoto wako ni “dhaifu” na hawayawezi matatizo na madaraka ya watu wazima. Kwa mfano, iwapo wewe ni mzazi aliye peke yake na una tatizo kubwa la kibinafsi ambalo unahisi ni lazima umweleze mtoto wako, kinza mwelekeo huo. Badala yake, tafuta msaada wa rafiki mkomavu ambaye anaweza kukusaidia, hasa yule atakayekusaidia kutumia mashauri yenye hekima ya Biblia.—Mithali 17:17.

      Vilevile, usimlemee mtoto wako na matatizo chungu nzima, shughuli nyingi sana, au kumbana sana kiasi cha kumfanya asifurahie maisha yake ya utotoni. Mlee mtoto wako kwa kuzingatia uwezo wake, bali si kulingana na ulimwengu wa leo unaosonga mbio. Biblia inashauri hivi kwa hekima: “Usiruhusu ulimwengu unaokuzunguka ukufinyange kulingana na mtindo wake.”—Waroma 12:2, Phillips.

      “Kwa Kila Jambo Kuna Majira Yake”

      Shauri lingine la hekima la Biblia linasema: “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.” Bila shaka kuna wakati wa kufanya kazi pia. Watoto wana kazi nyingi ya kufanya, kutia ndani kazi ya shule, kazi za nyumbani, na mambo ya kiroho. Hata hivyo, kitabu hicho chasema pia kwamba kuna “wakati wa kucheka” na “wakati wa kucheza.”—Mhubiri 3:1, 4.

      Watoto wana uhitaji wa pekee wa kucheza, kucheka, na kutumia nguvu zao za ujana kwa furaha. Ikiwa wakati wao wote utapangiwa mambo ya shule, shughuli za baada ya shule, na madaraka mengine mazito, basi uhitaji wa kucheza hautatimizwa. Hiyo inaweza kuwafanya wakasirike, au hata washuke moyo.—Wakolosai 3:21.

      Ona jinsi unavyoweza kutumia kanuni hiyo kwa njia nyingine. Kwa kuwa kila jambo lina wakati wake, je, hiyo haionyeshi kwamba wakati wa utotoni ni wakati wa kuwa mtoto? Labda utajibu ndiyo, lakini huenda watoto wako wasikubaliane nawe sikuzote. Mara nyingi, wavulana na wasichana wadogo hupenda kuiga yale wanayoona watu wazima wakifanya. Kwa mfano, wasichana wachanga huenda wakashawishiwa kuvalia na kujipamba kana kwamba ni wanawake. Wale wanaobalehe mapema wanaweza kuhisi kwamba wanapaswa kuwa kama watu wazima.

      Wazazi wenye hekima hutambua hatari ya mwelekeo huo. Matangazo fulani ya biashara na burudani nyingine katika ulimwengu huu uliopotoka huonyesha kwamba watoto wanafahamu kuhusu ngono na wamekomaa. Watoto wengi zaidi hujipodoa na kuvalia mavazi yanayoonyesha uchi. Mbona tuwafanye watoto wavutie watu ambao wanaweza kuwasumbua kingono? Wazazi wakiwasaidia watoto wao wavalie mavazi yanayofaa umri wao, watakuwa wanatumia kanuni ya Biblia inayosema: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha.”—Mithali 27:12.

      Mfano mwingine ni huu: Ukiwaruhusu watoto waone michezo kuwa jambo la maana zaidi, hawataishi kwa usawaziko. Hawatatambua kwamba kila jambo lina wakati wake. Biblia inashauri hivi kwa hekima: “Kwa maana mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa kidogo; lakini ujitoaji-kimungu ni wenye manufaa kwa mambo yote, kwa kuwa una ahadi ya uhai wa sasa na ule utakaokuja.”—1 Timotheo 4:8.

      Usiwaruhusu watoto wako wafikiri kwamba “kushinda ndilo jambo muhimu zaidi.” Wazazi wengi huwafanya watoto wasifurahie michezo kwa kuwachochea wawe washindani mno na washinde kwa vyovyote vile. Hivyo watoto wengine huona kwamba ni lazima watumie ujanja au wawaumize wachezaji wenzao ili washinde. Ama kweli, mtu hahitaji kutumia njia hizo ili ashinde!

      Kujifunza Kujidhibiti

      Mara nyingi watoto hushindwa kutambua kwamba kuna wakati wa kila jambo. Haiwi rahisi kwao kungojea wanapotaka kitu fulani. Jambo baya hata zaidi ni kwamba wanadamu wana mwelekeo wa kutimiziwa mahitaji yao papo kwa hapo. Vyombo vya habari mara nyingi huwapa watu ujumbe huu: “Jipatie unachokitaka haraka!”

      Usiige mwelekeo huo wa kuwaendekeza na kuwaharibu watoto. “Mtu anayeweza kudhibiti hisia zake hutambua kwamba ni muhimu awe na subira,” chasema kitabu The Child and the Machine. “Kujitia nidhamu na kupatana na watu wengine ni dawa muhimu ya kuzuia jeuri ya watoto ndani na nje ya shule.” Biblia inatoa kanuni hii muhimu: “Ambembelezaye mtumwa wake tangu utoto, mwishowe mtumwa huyo atamrithi.” (Mithali 29:21, Biblia Habari Njema) Ingawa mstari huo unazungumzia jinsi ya kuwashughulikia watumishi wachanga, wazazi wengi wameona kwamba kanuni hiyo huwafaidi sana watoto wao.

      Mojawapo ya mahitaji muhimu zaidi ya watoto ni “nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova,” kama Biblia inavyosema. (Waefeso 6:4) Nidhamu yenye upendo huwasaidia watoto wasitawishe sifa kama vile kujidhibiti na subira. Sifa hizo zitawasaidia wafurahi na kuridhika maishani.

      Mambo Yanayotishia Maisha ya Utotoni Yatakapokoma

      Hata hivyo huenda ukajiuliza, ‘Je, Mungu mwenye upendo na mwenye hekima ambaye alitoa kanuni hizo alitaka ulimwengu uwe jinsi ulivyo? Je, alitaka watoto walelewe katika mazingira hatari kama haya?’ Unaweza kufarijiwa kufahamu kwamba Yehova Mungu na Mwanaye, Kristo Yesu, wanawapenda sana wanadamu, kutia ndani watoto wa umri wote. Hivi karibuni watawaondoa waovu wote duniani.—Zaburi 37:10, 11.

      Je, ungependa kujua jinsi hali zitakavyokuwa wakati huo wenye amani na furaha? Hebu wazia hali hii kama inavyoelezwa kwa njia yenye kuvutia katika Biblia: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.” (Isaya 11:6) Tukiwa katika ulimwengu ambamo maisha ya utotoni yanaharibiwa au kuharakishwa kikatili, inafariji kama nini kujua kwamba Mungu ameahidi wakati ujao mzuri kama huo kwa wanadamu hapa duniani! Ni wazi kwamba Muumba anataka watoto wafurahie maisha yao ya utotoni, na badala ya kuharakishwa, yawe na baraka.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki