Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Usafi—Kwa Nini Ni Muhimu?
    Mnara wa Mlinzi—2008 | Desemba 1
    • Ushirikiano Katika Familia Ni Muhimu

      Kulingana na mama ya Max, familia nzima inahusika katika kudumisha usafi. Mara kwa mara, familia fulani zinaketi na kuzungumzia mahitaji yao na marekebisho wanayohitaji kufanya, ndani na nje ya nyumba. Jambo hilo pia linaleta umoja katika familia na linamkumbusha kila mmoja jambo analopaswa kufanya ili kuwatunza wengine katika familia. Kwa mfano, Mama anaweza kuwaeleza watoto wakubwa kwa nini wanapaswa kunawa mikono baada ya kutumia choo, kugusa pesa, na kabla ya kula. Watoto hao wanaweza kuhakikisha kwamba watoto wadogo wanachukua jambo hilo kwa uzito.

      Wote katika familia wanaweza kugawiwa majukumu mbalimbali. Huenda familia ikaamua kusafisha nyumba kila juma na kuwa na ratiba ya kuisafisha kabisa mara moja au mbili kwa mwaka. Namna gani nje ya nyumba? Mhifadhi wa mazingira Stewart L. Udall, alisema hivi kuhusu Marekani: “Tunaishi katika nchi inayopoteza umaridadi wake, inayozidi kuwa na sura mbaya, isiyo na maeneo mengi yaliyo wazi, na mazingira yanayozorota kila siku kwa sababu ya uchafuzi na kelele.”

      Je, hali za kwenu zinafanana na ufafanuzi huo? Zamani na hata leo katika miji fulani ya Afrika ya Kati, mpiga-mbiu wa mji anapiga kengele ili watu wamsikilize. Kwa sauti kubwa anawakumbusha raia wasafishe mji, wafagie mitaro, wakate matawi ya miti, wang’oe magugu, na washughulikie takataka.

      Mifumo ya kuondoa takataka ni tatizo la ulimwenguni pote linalohangaisha serikali nyingi. Manispaa fulani zinachelewa kuokota takataka na hivyo zinarundamana mitaani. Raia wanaweza kuombwa wasaidie. Kwa kuwa Wakristo ni raia wazuri, wao huwa kati ya wale wanaoongoza kutii sheria za Kaisari bila kulalamika. (Waroma 13:3, 5-7) Wakristo wa kweli wako tayari kufanya mengi zaidi ili wasaidie katika jambo hilo. Wanapendezwa na mazingira safi nao wanachukua hatua ya kwanza kufanya usafi, bila kukumbushwa na mpiga-mbiu wa mji. Wanatambua kwamba usafi unaonyesha wamezoezwa vizuri na wana tabia nzuri. Jambo hilo linaanza na kila mtu na kila familia. Kudumisha usafi nyumbani kutachangia afya nzuri na vilevile kuboresha mazingira ya eneo ambalo mtu anaishi.

  • Usafi—Kwa Nini Ni Muhimu?
    Mnara wa Mlinzi—2008 | Desemba 1
    • [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      Vikumbusho Kutoka kwa Daktari

      Maji ni muhimu kwa uhai, lakini maji machafu yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa na kifo. Dakt. J. Mbangue Lobe, mkuu katika idara ya matibabu katika bandari ya Douala, Kamerun, alitaja mambo fulani muhimu katika mahojiano.

      “Chemsha maji ya kunywa ikiwa huna hakika kuwa maji hayo ni safi.” Lakini alionya hivi: “Kutumia kemikali za kuua viini ni sawa lakini kunaweza kutokeza madhara zisipotumiwa vizuri. Nawa mikono yako kwa sabuni na maji kabla ya kula na baada ya kutumia choo. Kipande cha sabuni si bei ghali, hivyo hata maskini wanaweza kununua. Fua nguo zako kwa ukawaida, tumia maji moto ikiwa una matatizo ya ngozi au magonjwa mengine.”

      “Usafi ndani na nje ya nyumba unapaswa kuchukuliwa kwa uzito na washiriki wote wa familia,” anaendelea daktari huyo. “Mara nyingi vyoo vinapuuzwa na vinakuwa makao ya mende na nzi.” Akiongezea jambo moja muhimu kuhusu watoto, alionya hivi: “Jihadharini msiogee katika mitaro katika ujirani wenu. Vijito hivyo vina viini hatari. Oga usiku kabla ya kwenda kulala, piga mswaki vizuri usiku, na ujifunike kwa neti ya mbu unapolala.” Wazo kuu ni kwamba unapaswa kufikiria mapema, kuchukua hatua, na kuepuka matatizo.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki