Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu
    Amkeni!—2009 | Septemba
    • Sayansi Yaleta Mabadiliko Zaidi

      Kufikia mwaka wa 1850, mataifa fulani yalikuwa na ufanisi wa kutosha kugharimia utafiti wa kilimo. Uchunguzi wa kilimo umeendelea kuleta mabadiliko hata katika siku zetu. Kwa mfano, wazalishaji wa mimea wamechunguza mbegu za urithi na kutokeza mimea inayoweza kuzaa sana na kustahimili magonjwa. Watafiti pia wamegundua mchanganyiko unaofaa wa nitrati na fosfati kwa ajili ya mimea na udongo mbalimbali. Magugu yaliwafanya vibarua wa shambani wawe na kazi nyingi ya kuyaondoa. Lakini wengi wao walipoteza kazi zao baada ya wanasayansi kugundua dawa za kuua magugu. Wadudu, minyoo, na fukusi wamekuwa maadui wa mkulima tangu jadi. Hata hivyo, sasa wakulima wanaweza kuchagua kemikali mbalimbali za kuwaua wadudu wowote waharibifu.a

      Maisha ya wakulima wafugaji pia yamebadilika. Mashini za kulisha na kukamua maziwa zimewawezesha mchungaji na msaidizi wake kuchunga ng’ombe 200 hivi. Wafugaji wanaweza pia kunenepesha ndama na nguruwe haraka kuliko ilivyokuwa zamani kwa kuwafuga kwenye zizi badala ya kondeni, na hivyo wanaweza kudhibiti chakula na joto lao la mwili.

      Mara nyingi matokeo ya ukulima wa kutumia mbinu za kisayansi yamekuwa yenye kustaajabisha. Wakulima fulani waliongeza mazao yao mara mia au hata elfu moja zaidi kuliko kabla ya kuanza kutumia mbinu za kisayansi. Lakini maendeleo hayo yote yameathirije maisha ya watu?

      Maisha ya Mkulima Yalibadilika

      Mashini zimebadili maisha ya mkulima katika sehemu nyingi. Wakulima wengi na vibarua wamelazimika kujifunza kuendesha na kudumisha mashini za hali ya juu. Na mara nyingi, wao hufanya kazi wakiwa peke yao. Sasa hawafurahii tena ushirikiano waliokuwa nao pamoja na marafiki walipokuwa wakipanda, kupalilia, na kuvuna.

      Katika nchi nyingi, sasa mkulima pia ni mfanyabiashara mwenye elimu sana ambaye amebobea katika kuzalisha kwa wingi mazao machache tu au zao moja. Ametumia pesa nyingi kununua mashamba, majengo, na mashini. Hata hivyo, bado anawategemea watu wengine. Kampuni kubwa sana za kusindika vyakula na maduka makubwa huamua bei na pia aina, ukubwa, na rangi ya mazao yake. Mainjinia wa kilimo wanabuni mfumo wa kuzalisha mazao, na kampuni za pekee humtengenezea mbolea, dawa za kuua wadudu, na mbegu zinazotokeza mazao mengi ambazo atatumia katika shamba lake. Mbinu anazotumia kulima zimeboreshwa sana zinapolinganishwa na zile walizotumia mababu zake. Lakini bado anakabili hali ngumu, na watu fulani wanahofia kwamba huenda mbinu fulani za ukulima zikawa na madhara.

      Wakulima Bado Wakabili Matatizo

      Katika nchi zenye utajiri, bado wakulima wengi wanalazimishwa kuyaacha mashamba yao kwa kuwa hawawezi kushindana na mashirika makubwa ya kilimo. Wakulima fulani wanaweza tu kuendelea kuishi maisha ya kawaida kwa kugeuza mashamba yao kuwa mahali pa tafrija kutia ndani kujenga vyumba vya kukodi watalii au kuwa viwanja vya kupigia kambi, kucheza gofu, na kutokeza sanaa. Wengine huanza kukuza mazao ya pekee kama vile chakula kilichokuzwa kwa mbolea ya kiasili, maua, na kufuga mbuni, na alpaca.

      Katika nchi maskini, ambako asilimia 80 hivi ya idadi ya watu wanapata riziki yao kwa kukuza mazao yao, wakulima wengi pia wanakumbwa na badiliko kubwa. Kampuni za kimataifa zinazotumia mbinu za kulima mashamba makubwa zinaweza kununua mashamba bora zaidi na kukuza mimea itakayouzwa katika nchi za mbali. Kwa upande ule mwingine, wakulima wadogo-wadogo hulima mashamba madogo sana au yasiyo na rutuba mara nyingi bila kutumia mashini ili waandalie familia zao chakula.

  • Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu
    Amkeni!—2009 | Septemba
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

      MBINU MBILI ZA KILIMO

      Eusebio anaishi kwenye Milima ya Andes, ambako anakuza mimea na kulisha ng’ombe 14. “Wote wana majina,” anasema. “Ninapenda kulima. Tunakuza mboga zetu wenyewe. Mimi, mke wangu, na majirani husaidiana kulima na kuvuna. Hatuna mashini zozote. Tunalima kwa plau zinazokokotwa na mafahali, na kwenye miteremko mikali tunalima kwa majembe.

      “Wakati mmoja karibu mifugo yetu yote ilikufa kutokana na ugonjwa. Baada ya msiba huo, nilisomea jinsi ya kutibu wanyama wagonjwa. Hakuna mnyama ambaye amekufa tangu wakati huo, na sasa ninaweza kuwasaidia majirani kutunza mifugo yao. Tunauza jibini sokoni, lakini tunapata pesa kidogo sana. Siku zote sisi huwa na chakula cha kuwalisha watoto wetu sita.”

      Richard analima shamba lenye ukubwa wa ekari 1,300 hivi huko Kanada. Anafanya kazi peke yake ingawa ana kibarua mmoja ambaye humsaidia katika majira ya kupanda na kuvuna.

      “Siku hizi, mkazo wa kilimo unaathiri mtu kiakili kuliko kimwili,” anasema Richard. “Trekta yangu na mashini ya kuvuna ina mfumo wa kupunguza joto ambao hunilinda kutokana na vumbi na wadudu. Nina mashini zenye upana wa mita 9, kwa hiyo ninaweza kupanda au kuvuna upana wa ekari 160 hivi kwa siku moja. Lakini ninategemea sana mashini hizo, na jambo hilo ndilo husababisha mkazo. Mara kwa mara ninalazimika kukopa pesa ili kununua mashini nyingine. Kulipa mkopo huo kunategemea mambo ambayo siwezi kuyadhibiti kama vile, mvua, baridi kali, bei ya bidhaa sokoni, na riba ambayo benki itanitoza. Mkazo unaotokezwa na ukulima umesababisha matatizo mengi katika ndoa katika eneo hili, na hata kujiua.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki