Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Matatizo ya Wakulima
    Amkeni!—2003 | Oktoba 8
    • Matatizo ya Wakulima

      RICHARD hulima shamba lililolimwa na babu wa baba yake miaka 100 hivi iliyopita. Lakini, mnamo mwaka wa 2001, mkulima huyo Mkanada alikuwa mtu wa kwanza kutovuna chochote katika vizazi vinne vya familia yao. Mimea yake iliharibiwa na ukame. Na matatizo yake yamezidi kwa sababu katika miaka iliyotangulia bei za mazao zimeshuka na gharama zimeongezeka. Richard alilalamika hivi: “Matatizo yanazidi kuongezeka na hakuna suluhisho.”

      Larry alikuwa na shamba ambalo lilikuwa limemilikiwa na familia yake kwa miaka 115 katika eneo linalokuza mahindi kwa wingi nchini Marekani. Anasema hivi: “Nilihisi nina wajibu wa kuendelea kulima shamba hilo na kulifanya litokeze faida nyingi . . . , lakini sikufua dafu.” Larry na mkewe walipoteza shamba lao.

      Wakulima wengi wanakabili matatizo kama ya Larry na Richard. Kuenea kwa ugonjwa wa mifugo wa midomo na miguu nchini Uingereza kuliwaletea wakulima hasara kubwa ya kifedha na mfadhaiko. Taarifa moja ya habari ilisema: “Kila siku wakulima nchini Uingereza wanakumbwa na mahangaiko, upweke, na matatizo ya madeni, hata wale ambao hawajakabili ugonjwa huo wa mifugo.” Katika nchi fulani zinazoendelea, vita, ukame, ongezeko la haraka la idadi ya watu, na matatizo mengine mengi yamewatatiza wakulima. Serikali zinalazimika kununua chakula kutoka nje, na familia nyingi haziwezi kukinunua.

      Kwa hiyo, matatizo ya wakulima yanawaathiri watu wengi. Hata hivyo, ni wakazi wachache wa mjini wanaojali dhiki za wakulima. Miaka 50 hivi iliyopita, Rais wa Marekani Dwight D. Eisenhower alitoa taarifa hii mwafaka: “Kilimo huonekana kuwa rahisi sana ikiwa unafanya kazi ofisini, na ikiwa unaishi mbali sana na shamba la mahindi.” Vivyo hivyo, leo wakulima wanahisi kwamba watu wengi ulimwenguni hawaelewi kilimo na umuhimu wa wakulima. Mkulima mmoja Mkanada analalamika hivi: “Hatujali chakula chetu chatoka wapi. Kazi kubwa huwa imefanywa kabla chakula hakijapakiwa na kuuzwa dukani.”

      Matatizo ya wakulima hayawezi kupuuzwa kwani sote tunategemea bidhaa za kilimo. Wanasoshiolojia Don A. Dillman na Daryl J. Hobbs wanaonya hivi: “Katika jamii yetu inayotegemeana sana, matatizo ya mashambani husambaa upesi mjini, na matatizo ya mjini husambaa haraka mashambani. Jamii za mjini au za mashambani haziwezi kuendelea kwa muda mrefu ikiwa mojawapo inakabili matatizo.” Isitoshe, katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, uchumi wa taifa moja unapozorota, unaweza kuathiri sana uuzaji wa mazao na gharama za uzalishaji katika nchi nyingine.

      Basi, si ajabu kwamba kituo fulani cha kilimo huko New York kilisema hivi: “Kilimo ni mojawapo ya kazi 10 zinazosababisha mfadhaiko mwingi nchini Marekani.” Ni nini baadhi ya visababishi vya matatizo ya wakulima? Wakulima wanawezaje kukabiliana na matatizo hayo? Je, kweli matatizo hayo yanaweza kukomeshwa?

      [Blabu katika ukurasa wa 4]

      “Kilimo huonekana kuwa rahisi sana ikiwa unafanya kazi ofisini, na ikiwa unaishi mbali sana na shamba la mahindi”

  • Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?
    Amkeni!—2003 | Oktoba 8
    • Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?

      “Wafanyakazi wanaopokea simu katika kituo cha kushughulikia mfadhaiko wa wakulima wamezoezwa kukusaidia kukabiliana na matatizo yako. Sisi ni wakulima au tulikuwa wakulima kama wewe, na tunaelewa magumu yanayokumba familia za mashambani. Tunaweza kukujulisha kwa watu wanaoweza kukusaidia. . . . Hatutafichua habari zozote utakazotuambia.”—Kutoka kwa kituo cha Internet cha serikali ya Kanada.

      WATAALAMU wengi wa afya wametambua kwamba mfadhaiko ni mojawapo ya matatizo ya wakulima. Ili kuwasaidia wakulima wakabiliane nao, kuna wanasaikolojia wanaoshughulikia mfadhaiko wa wakulima, na wanapanga mikutano ya kuwashauri wakulima na kuwapa namba za simu wanazoweza kupiga ili wapate msaada.

      Jane, ambaye ni mke wa mkulima, huhudhuria mkutano wa kupata mashauri Alhamisi usiku. Jane anasema hivi: “Ninahudhuria kwa sababu mume wangu alijiua. Sikuzote alipenda sana kulima shamba letu, na ninadhani alijiua kwa sababu hakufaulu katika kilimo.”

      Watu wengi wamegundua kwamba kuna ongezeko kubwa la wakulima wanaotaka msaada kwa sababu ya mfadhaiko. Matatizo ya wakulima yanasababishwa na nini?

      Misiba ya Asili na Magonjwa

      Kituo cha Internet cha serikali kilichonukuliwa pale mwanzoni kinasema: “Kuna mambo mengi ambayo mkulima hawezi kuyadhibiti maishani mwake, kama vile hali ya hewa, bei za mazao, viwango vya riba, na kuharibika kwa vifaa. Hata kuamua mambo kama vile mazao utakayopanda au kuuza shamba au kuwapa wakopeshaji shamba hilo kwa muda kunaweza kusababisha mfadhaiko, kwani unaweza kupata hasara au faida ikitegemea uamuzi uliofanya.” Matatizo hayo yanapozidishwa na hatari ya ukame mkali, magonjwa, au uwezekano wa kupoteza shamba, mfadhaiko unaweza kumlemea mkulima sana.

      Kwa mfano, ukame unaweza kusababisha hasara maradufu. Mkulima Howard Paulsen alisema kwamba ukame wa mwaka wa 2001, ambao ulikuwa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya ukame kuwahi kutukia huko Kanada, uliathiri mimea na mifugo yake. Hakukuwa na malisho ya mifugo au mazao ya kuvuna, kwa hiyo ilibidi wakulima wanunue chakula cha mifugo. Alisema hivi: “Tayari nimetumia dola 10,000 za Kanada kununua chakula cha mifugo na sasa ninawalisha chakula ambacho wanapaswa kula wakati wa baridi kali. Ukifanya hivyo, huwezi kupata faida yoyote hata kutoka kwa mifugo wenyewe.” Katika sehemu nyingine, mafuriko yameharibu kabisa mashamba mengi na mavuno yote.

      Kuzuka kwa ugonjwa wa midomo na miguu mwaka wa 2001 kulikuwa tu mojawapo ya matatizo ambayo wakulima Waingereza walikumbwa nayo hivi karibuni, kutia ndani kichaa cha ng’ombe na homa ya nguruwe. Mbali na kuharibu uchumi na kusababisha hofu, magonjwa hayo yanasababisha matatizo mengi zaidi. Gazeti Agence France-Presse lilisema hivi: “Wanaume wakakamavu wa mashambani ambao hawatokwi na machozi ovyoovyo, wameonekana wakilia wanapowatazama wataalamu wa mifugo wa serikali wakiteketeza marundo ya mifugo ambao wametumia maisha yao yote kuzalisha.” Baada ya ugonjwa wa midomo na miguu kuzuka, polisi hata walianza kuwapokonya bunduki wakulima waliokusudia kujiua. Wakulima wengi waliofadhaika walipiga simu wakiomba mashauri.

      Kuzorota kwa Uchumi

      Kumekuwa pia na mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Jalada la nyuma la kitabu Broken Heartland linasema hivi: “Kati ya mwaka wa 1940 hadi katikati ya miaka ya 1980, gharama za uzalishaji katika eneo kuu la kilimo la Marekani ziliongezeka mara tatu, gharama za vifaa ziliongezeka mara nne, malipo ya riba yaliongezeka mara kumi, faida zilipungua kwa asilimia 10, idadi ya wakulima ilipungua kwa thuluthi mbili, watu walihama maeneo mengi ya mashambani, biashara zilifungwa, na uchumi ukazorota.”

      Kwa nini faida zinapungua na gharama zinaongezeka? Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa. Kwa hiyo wakulima hujikuta wakishindana na wazalishaji wa chakula katika maeneo ya mbali sana. Ni kweli kwamba masoko mapya ya bidhaa za kilimo yameanzishwa kwa sababu ya biashara ya kimataifa, lakini masoko ya kimataifa yanaweza kubadilika ghafula. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, wakulima kadhaa wa nafaka na wafugaji wa nguruwe nchini Kanada walikuwa karibu kufilisika wakati wateja wao huko Asia walipokumbwa na matatizo ya kiuchumi.

      Wakazi wa Mashambani Wanahama

      Profesa Mike Jacobsen wa Chuo Kikuu cha Iowa, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mashambani, anasema kwamba matatizo ya wakulima yanawaathiri pia wakazi wote wa mashambani. Anasema hivi: “Mashambani ni mahali panapowafaa watoto, ni mahali safi, ambapo watu wangependa kuoa na kulea watoto. Shule za mashambani ni nzuri na salama. Naam, huo ndio ukweli wa mambo. Lakini, uchumi wa miji ya mashambani unategemea hasa mashamba madogo yanayomilikiwa na familia mbalimbali.” Hivyo, matatizo ya wakulima yamefanya hospitali, shule, mikahawa, maduka, na makanisa ya mashambani yafungwe. Jamii zenye umoja, ambazo hufanya maisha ya mashambani yavutie, zinatoweka.

      Basi, haishangazi kwamba gazeti Newsweek lilisema kwamba karibu asilimia 16 ya Wamarekani wanaoishi mashambani ni maskini hohehahe. Geoffrey Lawrence anasema hivi katika ripoti yenye kichwa “Matatizo ya Mashambani Huko Australia”: “Ukosefu wa kazi na umaskini umeongezeka sana mashambani kuliko mjini.” Familia nyingi, na hasa familia za vijana, zimelazimika kuhamia mjini kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi. Sheila, anayeisaidia familia yao kulima shamba lao, anauliza hivi: “Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”

      Kwa kuwa vijana wengi sana wamehamia mijini, wakazi wengi wa miji ya mashambani ni wazee. Hivyo, hakuna vijana wa kufanya kazi wala watu wa kuwatunza wazee ambao wanahitaji sana msaada. Ndiyo sababu mabadiliko hayo ya haraka yamewafanya wazee wachanganyikiwe na kuogopa.

      Kwa hiyo, matatizo ya wakulima yanasababisha matatizo makubwa kila mahali. Yanatuathiri sote. Hata hivyo, kama makala ifuatayo itakavyoonyesha, tunaweza kutumaini kwamba matatizo ya wakulima yatakoma.

      [Blabu katika ukurasa wa 6]

      Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa

      [Blabu katika ukurasa wa 6]

      “Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki