-
Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?Amkeni!—2003 | Oktoba 8
-
-
Matatizo ya Wakulima Yanasababishwa na Nini?
“Wafanyakazi wanaopokea simu katika kituo cha kushughulikia mfadhaiko wa wakulima wamezoezwa kukusaidia kukabiliana na matatizo yako. Sisi ni wakulima au tulikuwa wakulima kama wewe, na tunaelewa magumu yanayokumba familia za mashambani. Tunaweza kukujulisha kwa watu wanaoweza kukusaidia. . . . Hatutafichua habari zozote utakazotuambia.”—Kutoka kwa kituo cha Internet cha serikali ya Kanada.
WATAALAMU wengi wa afya wametambua kwamba mfadhaiko ni mojawapo ya matatizo ya wakulima. Ili kuwasaidia wakulima wakabiliane nao, kuna wanasaikolojia wanaoshughulikia mfadhaiko wa wakulima, na wanapanga mikutano ya kuwashauri wakulima na kuwapa namba za simu wanazoweza kupiga ili wapate msaada.
Jane, ambaye ni mke wa mkulima, huhudhuria mkutano wa kupata mashauri Alhamisi usiku. Jane anasema hivi: “Ninahudhuria kwa sababu mume wangu alijiua. Sikuzote alipenda sana kulima shamba letu, na ninadhani alijiua kwa sababu hakufaulu katika kilimo.”
Watu wengi wamegundua kwamba kuna ongezeko kubwa la wakulima wanaotaka msaada kwa sababu ya mfadhaiko. Matatizo ya wakulima yanasababishwa na nini?
Misiba ya Asili na Magonjwa
Kituo cha Internet cha serikali kilichonukuliwa pale mwanzoni kinasema: “Kuna mambo mengi ambayo mkulima hawezi kuyadhibiti maishani mwake, kama vile hali ya hewa, bei za mazao, viwango vya riba, na kuharibika kwa vifaa. Hata kuamua mambo kama vile mazao utakayopanda au kuuza shamba au kuwapa wakopeshaji shamba hilo kwa muda kunaweza kusababisha mfadhaiko, kwani unaweza kupata hasara au faida ikitegemea uamuzi uliofanya.” Matatizo hayo yanapozidishwa na hatari ya ukame mkali, magonjwa, au uwezekano wa kupoteza shamba, mfadhaiko unaweza kumlemea mkulima sana.
Kwa mfano, ukame unaweza kusababisha hasara maradufu. Mkulima Howard Paulsen alisema kwamba ukame wa mwaka wa 2001, ambao ulikuwa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya ukame kuwahi kutukia huko Kanada, uliathiri mimea na mifugo yake. Hakukuwa na malisho ya mifugo au mazao ya kuvuna, kwa hiyo ilibidi wakulima wanunue chakula cha mifugo. Alisema hivi: “Tayari nimetumia dola 10,000 za Kanada kununua chakula cha mifugo na sasa ninawalisha chakula ambacho wanapaswa kula wakati wa baridi kali. Ukifanya hivyo, huwezi kupata faida yoyote hata kutoka kwa mifugo wenyewe.” Katika sehemu nyingine, mafuriko yameharibu kabisa mashamba mengi na mavuno yote.
Kuzuka kwa ugonjwa wa midomo na miguu mwaka wa 2001 kulikuwa tu mojawapo ya matatizo ambayo wakulima Waingereza walikumbwa nayo hivi karibuni, kutia ndani kichaa cha ng’ombe na homa ya nguruwe. Mbali na kuharibu uchumi na kusababisha hofu, magonjwa hayo yanasababisha matatizo mengi zaidi. Gazeti Agence France-Presse lilisema hivi: “Wanaume wakakamavu wa mashambani ambao hawatokwi na machozi ovyoovyo, wameonekana wakilia wanapowatazama wataalamu wa mifugo wa serikali wakiteketeza marundo ya mifugo ambao wametumia maisha yao yote kuzalisha.” Baada ya ugonjwa wa midomo na miguu kuzuka, polisi hata walianza kuwapokonya bunduki wakulima waliokusudia kujiua. Wakulima wengi waliofadhaika walipiga simu wakiomba mashauri.
Kuzorota kwa Uchumi
Kumekuwa pia na mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Jalada la nyuma la kitabu Broken Heartland linasema hivi: “Kati ya mwaka wa 1940 hadi katikati ya miaka ya 1980, gharama za uzalishaji katika eneo kuu la kilimo la Marekani ziliongezeka mara tatu, gharama za vifaa ziliongezeka mara nne, malipo ya riba yaliongezeka mara kumi, faida zilipungua kwa asilimia 10, idadi ya wakulima ilipungua kwa thuluthi mbili, watu walihama maeneo mengi ya mashambani, biashara zilifungwa, na uchumi ukazorota.”
Kwa nini faida zinapungua na gharama zinaongezeka? Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa. Kwa hiyo wakulima hujikuta wakishindana na wazalishaji wa chakula katika maeneo ya mbali sana. Ni kweli kwamba masoko mapya ya bidhaa za kilimo yameanzishwa kwa sababu ya biashara ya kimataifa, lakini masoko ya kimataifa yanaweza kubadilika ghafula. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, wakulima kadhaa wa nafaka na wafugaji wa nguruwe nchini Kanada walikuwa karibu kufilisika wakati wateja wao huko Asia walipokumbwa na matatizo ya kiuchumi.
Wakazi wa Mashambani Wanahama
Profesa Mike Jacobsen wa Chuo Kikuu cha Iowa, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mashambani, anasema kwamba matatizo ya wakulima yanawaathiri pia wakazi wote wa mashambani. Anasema hivi: “Mashambani ni mahali panapowafaa watoto, ni mahali safi, ambapo watu wangependa kuoa na kulea watoto. Shule za mashambani ni nzuri na salama. Naam, huo ndio ukweli wa mambo. Lakini, uchumi wa miji ya mashambani unategemea hasa mashamba madogo yanayomilikiwa na familia mbalimbali.” Hivyo, matatizo ya wakulima yamefanya hospitali, shule, mikahawa, maduka, na makanisa ya mashambani yafungwe. Jamii zenye umoja, ambazo hufanya maisha ya mashambani yavutie, zinatoweka.
Basi, haishangazi kwamba gazeti Newsweek lilisema kwamba karibu asilimia 16 ya Wamarekani wanaoishi mashambani ni maskini hohehahe. Geoffrey Lawrence anasema hivi katika ripoti yenye kichwa “Matatizo ya Mashambani Huko Australia”: “Ukosefu wa kazi na umaskini umeongezeka sana mashambani kuliko mjini.” Familia nyingi, na hasa familia za vijana, zimelazimika kuhamia mjini kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi. Sheila, anayeisaidia familia yao kulima shamba lao, anauliza hivi: “Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”
Kwa kuwa vijana wengi sana wamehamia mijini, wakazi wengi wa miji ya mashambani ni wazee. Hivyo, hakuna vijana wa kufanya kazi wala watu wa kuwatunza wazee ambao wanahitaji sana msaada. Ndiyo sababu mabadiliko hayo ya haraka yamewafanya wazee wachanganyikiwe na kuogopa.
Kwa hiyo, matatizo ya wakulima yanasababisha matatizo makubwa kila mahali. Yanatuathiri sote. Hata hivyo, kama makala ifuatayo itakavyoonyesha, tunaweza kutumaini kwamba matatizo ya wakulima yatakoma.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
Katika ulimwengu wa leo ulio kama kijiji, wakulima wanaathiriwa na hali za masoko ya kimataifa
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Hali ikiendelea hivi, je, kweli kutakuwa na wakulima?”
-
-
Matatizo ya Wakulima YatakomaAmkeni!—2003 | Oktoba 8
-
-
Matatizo ya Wakulima Yatakoma
“BAADHI ya watu wanaoona matatizo ya wakulima kijuujuu, hawaelewi kwa nini wakulima huendelea kulima,” anasema Rodney, mkulima wa kizazi cha tatu. Hata hivyo, mamilioni ya watu ulimwenguni pote huendelea kulima. Katika nchi fulani zinazoendelea, hakuna kazi za kutosha; angalau familia zinazolima zinaweza kupata chakula kila siku.
Isitoshe, familia nyingi huona kilimo kuwa sehemu ya maisha wala si kazi tu. Idadi ya watu wanaoendelea kulima licha ya ukame, magonjwa, hali mbaya za kiuchumi, na matatizo mengine inaonyesha uvumilivu wao na kwamba wanapenda maisha ya mashambani. Kabla ya kuchunguza jinsi matatizo ya wakulima yatakavyosuluhishwa, na tuchunguze jinsi wakulima fulani wamesaidiwa kukabiliana na hali hiyo.
Jinsi Wengine Wanavyokabiliana na Matatizo
Wakulima hukabili matatizo fulani yasiyoepukika. Ni lazima tukubali kwamba hali ya hewa, uchumi, na mambo mengine mengi yanayosababisha mfadhaiko hayawezi kudhibitiwa. Ripoti iliyochapishwa na Mpango wa Elimu ya Ziada wa North Carolina inasema: “Wakulima wengi wametambua kwa masikitiko kwamba kazi ngumu haifanikiwi sikuzote. Jitihada nyingi ambazo kila mkulima huweka katika kazi yake, haziwi na matokeo mazuri nyakati zote. Kila mkulima hukabili hali ambazo hawezi kuzidhibiti.” Mkulima mmoja mzee alieleza siri ya furaha yake aliposema hivi: “Nimejifunza kubadilika kulingana na hali zisizoweza kuepukika.”
Mithali moja ya kale inasema hivi: “Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; naye ayatazamaye mawingu hatavuna.” (Mhubiri 11:4) Mtu mwenye wasiwasi na mwenye kusitasita hawezi kutenda lolote. Kuchukua hatua zinazofaa na kuepuka maoni mabaya kwaweza kupunguza mfadhaiko.
Kula vizuri, kupumzika vya kutosha, na kufanya mazoezi yafaayo kunasaidia sana pia. Gazeti The Western Producer linaripoti kwamba wakulima wenye afya “hufanya maamuzi mazuri.” Mkulima anayeitwa Eugene na mkewe, Candace, waliliambia gazeti la Amkeni! hivi: “Kupumzika vya kutosha hutusaidia kupunguza mfadhaiko. Matatizo huonekana madogo na rahisi kusuluhishwa baada ya kupumzika. Kula vizuri husaidia pia, hasa familia yote inapokula pamoja.” Shauri hilo linapatana na maneno haya ya Biblia: “Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.”—Mhubiri 3:13.
Kuiruzuku Familia
Mkulima mmoja aliliambia gazeti la Amkeni! hivi: “Familia nyingi za mashambani zimelazimika kufanya kazi nyingine mbali na kilimo. Ingawa hatua hiyo huchukuliwa ili kupunguza matatizo ya kifedha, inaweza kuathiri mahusiano katika familia. Familia fulani za mashambani zilikuwa na umoja hapo awali, lakini sasa zimesambaratika.” Familia zinawezaje kukabiliana na matatizo hayo?
Yapata miaka 2,700 iliyopita, vichwa vya familia walishauriwa hivi: “Tengeneza kazi yako huko nje, jifanyizie kazi yako tayari shambani, ukiisha, jenga nyumba yako.” (Mithali 24:27) Randy, ambaye ni baba na mkulima wa kizazi cha nne, anasema: “Ni lazima umshukuru kila mtu katika familia. Kila mtu katika familia anahitaji kutiwa moyo na kupendwa. Maneno na matendo ya fadhili huwafanya wote wahisi kwamba wanahitajiwa na kuthaminiwa.”
Watoto hasa wanahitaji kutiwa moyo mabadiliko makubwa yanapotokea. Familia inapopoteza shamba, watoto huathiriwa kama watoto wa wazazi waliotalikiana au kufa. Wanahitaji kujua kwamba hawakusababisha tatizo hilo na kwamba familia haitavunjika.
Jinsi Wengine Wanavyoweza Kusaidia
Huenda wakulima waliofadhaika wakajitenga na wengine, hata kuwaepuka marafiki zao. (Mithali 18:1) Hata hivyo, wakati wa shida mtu anahitaji sana kutiwa moyo na wengine!
Je, una marafiki au majirani wakulima ambao wamekumbwa na matatizo? Unaweza kuwatia moyo sana ukionyesha kwamba unawajali. Mkulima anayeitwa Ron anasema hivi: “Tunafarijiwa tunapojua kwamba marafiki zetu wanatambua matatizo yetu.” Naam, watembelee marafiki zako na uwasikilize wanapoeleza yaliyo moyoni mwao.
Jack alifaidika alipotembelewa na kutiwa moyo. Anasema hivi: “Nakumbuka vizuri sana wakati ambapo marafiki zangu waliona kwamba nimefadhaika na kwa upendo wakaja kunitia moyo.” Si lazima mtu awe na ujuzi mwingi kuhusu kilimo ili awafariji wengine. Rodney, aliyenukuliwa mwanzoni, anasema hivi: “Mimi hupata nguvu na tamaa ya kufanya yote niwezayo ninapojua kwamba marafiki zangu wanatambua kazi nyingi nilizo nazo.” Hilo linatukumbusha mithali hii ya Biblia: “Rafiki hupenda sikuzote; na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.”—Mithali 17:17.
Suluhisho la Kudumu
Matatizo ya wakulima ni kati ya mambo yanayoonyesha kwamba wanadamu hawawezi kuisimamia vizuri dunia na rasilimali zake. Nabii Yeremia alisema hivi: “Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Ama kwa hakika, mwanadamu anahitaji msaada wa Mungu. Hapana shaka kwamba msaada huo utatolewa hivi karibuni.
Biblia inasema: “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2:15) Naam, agizo hilo la Muumba wetu ndilo lililoanzisha kilimo! Karne nyingi baadaye, Mungu aliwaingiza watu wake Waisraeli katika nchi ya Kanaani. Biblia inasema hivi kuhusu nchi hiyo: “Hunyweshwa maji ya mvua ya mbinguni; nayo ni nchi itunzwayo na BWANA, Mungu wako; macho ya BWANA Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka.” (Kumbukumbu la Torati 11:11, 12) Yehova pia alitunga sheria zilizozuia Nchi ya Ahadi isiharibiwe. Kwa mfano, kila mwaka wa saba, Waisraeli hawakupaswa kulima mashamba yao, mashamba ya mizabibu, na mashamba ya mizeituni. (Kutoka 23:10, 11) Hivyo, udongo wa nchi hiyo uliendelea kuwa na rutuba.
Tunaweza kuwa na uhakika kwamba wakati ujao dunia itapata mazao mengi kutokana na kilimo wakati wa utawala wa Ufalme wa Mungu, serikali inayoongozwa na Yesu Kristo kutoka mbinguni. (Isaya 35:1-7) Yesu Kristo, Mtawala aliyewekwa kuongoza Ufalme huo, alipokuwa duniani, alionyesha kwamba anaweza kudhibiti nguvu za asili zinazoathiri kilimo. (Marko 4:37-41) Zaburi 72 inaeleza jinsi hali zitakavyokuwa wakati atakapotumia uwezo wake kurekebisha dunia na kuponya wakazi wake. Inatuhakikishia hivi: “Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima; matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni, na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.” (Zaburi 72:16) Watu wa Mungu watavuna kwa wingi na kwa shangwe katika ulimwengu huo mpya ulioahidiwa.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
“Wakulima wengi wametambua kwa masikitiko kwamba kazi ngumu haifanikiwi sikuzote”
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kushughulikia mahitaji ya kiroho na ya kihisia ya watu wa familia kunaweza kuwasaidia kukabiliana na matatizo
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wakati wa utawala wa Mungu, dunia itazaa chakula tele
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Garo Nalbandian
-