-
Je, Mfungo Ni Jambo la Kale?Mnara wa Mlinzi—1996 | Novemba 15
-
-
Je, Mfungo Ni Jambo la Kale?
NIMEKUWA nikifunga kila Jumatatu tangu nilipokuwa tineja,” asema Mrudulaben, mwanamke Mhindi aliyefana mwenye umri wa miaka 78. Mfungo umekuwa sehemu ya ibada yake, njia ya kuhakikisha kwamba alikuwa na ndoa nzuri na watoto wenye afya, na vilevile ulinzi kwa ajili ya mumewe. Sasa akiwa mjane, yeye huendelea kufunga siku za Jumatatu kwa ajili ya afya njema, na kwa ajili ya ufanisi wa watoto wake. Sawa na yeye, wanawake Wahindu walio wengi hufanya mifungo ya ukawaida iwe sehemu ya maisha yao.
Prakash, mfanyabiashara wa makamo anayeishi katika kiunga cha Mumbai (Bombay), India, asema kwamba yeye hufunga kila mwaka kwenye Jumatatu za Sawan (Shravan). Huo ni mwezi wenye umaana wa pekee wa kidini kwenye kalenda ya Kihindu. Prakash aeleza hivi: “Nilianza kufunga kwa sababu za kidini, lakini sasa napata kichocheo cha ziada cha kuendelea kwa sababu za kiafya. Kwa kuwa Sawan huja kuelekea mwishoni mwa kuvuma kwa upepo wa monsuni, mfungo huupa mwili wangu fursa ya kuondolea mbali magonjwa ya kawaida ya msimu wa mvua.”
Watu fulani huhisi kwamba mfungo humsaidia mtu kimwili, kiakili, na kiroho. Mathalani, kitabu Grolier International Encyclopedia chataarifu hivi: “Uchunguzi wa juzijuzi wa kisayansi wadokeza kwamba mfungo waweza kuleta afya na, ufanywapo kwa uangalifu, waweza kuleta viwango vya juu vya kuwa macho kiakili na kuwa na maitikio ya kihisia.” Yasemekana kwamba mwanafalsafa Mgiriki Plato aliweza kufunga kwa siku kumi au zaidi na kwamba yule mwanahisabati Pythagoras aliwalazimisha wanafunzi wake wafunge kabla ya kuwafundisha.
Kwa watu fulani, mfungo humaanisha kuepuka chakula na maji kabisa kwa kipindi fulani cha wakati, hali wengine hunywa vinywaji wakati wa mifungo yao. Kukosa milo fulani au kujinyima aina fulani ya chakula kunaonwa na wengi kuwa ni mfungo. Lakini kufunga kwa muda mrefu bila uangalifu kwaweza kuwa hatari. Mwanajarida Parul Sheth asema kwamba baada ya mwili kutumia ugavi wao wa kabohidrati, huanza kubadili protini ya misuli iwe glukosi na kisha huugeukia ugavi wa mafuta ya mwili. Kubadili mafuta yawe glukosi hutokeza sumuvija ziitwazo magimba ya ketoni. Hayo yakusanyikapo, yanasonga kuelekea kwenye ubongo, na kuudhuru mfumo wa neva wa kati. “Huo ndio wakati ambapo mfungo waweza kuwa hatari,” asema Sheth. “Waweza kuchanganyikiwa, kuvurugika, na hata kuwa vibaya zaidi. . . . [waweza kusababisha] kupoteza fahamu na kifo hatimaye.”
Silaha na Desturi
Mfungo umetumiwa kuwa silaha yenye nguvu ya kutimiza makusudio ya kisiasa na kijamii. Mtumiaji maarufu wa silaha hiyo alikuwa Mohandas K. Gandhi katika India. Akiwa anastahiwa sana na mamia ya mamilioni ya watu, alitumia mfungo ili kutokeza uvutano wenye nguvu juu ya matungamano ya Wahindu wa India. Akifafanua matokeo ya mfungo wake ili kusuluhisha bishano kati ya wafanyakazi wa kiwanda na wenye kiwanda, Gandhi alisema hivi: “Tokeo la jumla la mfungo lilikuwa kwamba watu wote waliohusika walikuwa na hali ya nia njema. Mioyo ya wenye kiwanda iliguswa . . . Mgomo ukakomeshwa baada ya mimi kufunga kwa siku tatu tu.” Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alishiriki katika mgomo wa siku tano wa kutokula wakati wa miaka yake akiwa mfungwa wa kisiasa.
Hata hivyo, walio wengi wa wale ambao wamezoea kufunga, wamefanya hivyo kwa sababu za kidini. Mfungo ni desturi maarufu katika Dini ya Hindu. Siku fulani-fulani, chasema kitabu Fast and Festivals of India, “watu hufunga kabisa . . . hata maji hayanywewi hata kidogo. Wanaume na pia wanawake hufunga kabisa-kabisa . . . ili kuhakikisha kuna furaha, ufanisi na msamaha wa ukiukaji-sheria na dhambi.”
Katika dini ya Jain wengi hufunga. Jarida The Sunday Times of India Review laripoti hivi: “Muni [mwenye hekima] wa Jain katika Bombay [Mumbai] alikunywa gilasi mbili tu za maji yaliyochemshwa kila siku—kwa siku 201. Alipoteza uzito wa kilo 33 [pauni 73].” Wengine hata hufunga kufikia kiwango cha kufa njaa, wakiwa na usadikisho wa kwamba hilo litatokeza wokovu.
Kwa watu wazima Waislamu kwa ujumla, mfungo ni lazima wakati wa mwezi wa Ramadhani. Hakuna chakula wala maji yapaswayo kunywewa kuanzia macheo hadi machweo kwa huo mwezi mzima. Yeyote aliye mgonjwa au aliye safarini wakati huo lazima alipie siku za mfungo. Kwaresima, kile kipindi cha siku 40 kinachotangulia Ista, ni wakati wa mfungo kwa watu fulani katika Jumuiya ya Wakristo, na vikundi vingi vya kidini hufunga kwenye siku nyingine hususa.
Bila shaka mfungo haujatoweka. Na kwa kuwa ni sehemu ya dini nyingi, twaweza kuuliza hivi, Je, Mungu hutaka mfungo? Je, kuna nyakati ambapo Wakristo waweza kuamua kufunga? Je, kufanya hivyo kwaweza kunufaisha? Makala ifuatayo itazungumzia maswali hayo.
Picha katika ukurasa wa 3]
Dini ya Jain huona mfungo kuwa njia ya kupata wokovu wa nafsi
[Picha katika ukurasa wa 4]
Mohandas K. Gandhi alitumia mfungo kuwa silaha yenye nguvu ya kutimiza makusudio ya kisiasa na kijamii
[Picha katika ukurasa wa 4]
Katika Uislamu, mfungo ni lazima wakati wa mwezi wa Ramadhani
-
-
Je, Mungu Hutaka Mfungo?Mnara wa Mlinzi—1996 | Novemba 15
-
-
Je, Mungu Hutaka Mfungo?
SHERIA ya Mungu iliyotolewa kupitia Musa ilitaka mfungo kwenye pindi moja tu—kwenye Siku ya Kufunika ya kila mwaka. Sheria iliamuru kwamba katika siku hiyo Waisraeli walipaswa ‘kujitaabisha roho zao,’ jambo ambalo laeleweka kumaanisha kwamba walifunga. (Mambo ya Walawi 16:29-31; 23:27; Zaburi 35:13) Hata hivyo, mfungo huo haukuwa jambo rasmi tu. Kusherehekea Siku ya Kufunika kuliwasukuma watu wa Israeli wafahamu zaidi hali yao yenye dhambi na ule uhitaji wa kupata ukombozi. Pia walifunga kwenye siku hiyo ili kuonyesha huzuni kwa sababu ya dhambi zao na kuonyesha toba mbele ya Mungu.
Ingawa huo ndio mfungo pekee wa lazima chini ya Sheria ya Kimusa, Waisraeli walifunga kwenye pindi nyinginezo. (Kutoka 34:28; 1 Samweli 7:6; 2 Mambo ya Nyakati 20:3; Ezra 8:21; Esta 4:3, 16) Ihusishwayo katika pindi hizo ni ile mifungo ya hiari ikiwa njia ya kuonyesha toba. Yehova aliwasihi sana watu wenye kukosea wa Yuda: “Nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea.” Hilo halikupaswa kuwa wonyesho wa nje, kwa kuwa Mungu aendelea kusema hivi: “Rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu.”—Yoeli 2:12-15.
Hatimaye, wengi walifunga, likiwa jambo rasmi la kuonekana nje. Yehova alichukia mfungo huo usio wa moyo mweupe na hivyo akawauliza hivi Waisraeli wanafiki: “Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA?” (Isaya 58:5) Badala ya kufanya wonyesho wa kujivunia wa mfungo wao, watu hao wapotovu waliombwa watokeze kazi zinazofaa toba.
Mifungo fulani iliyoanzishwa na Wayahudi haikupata kibali cha Mungu tangu mwanzo. Kwa kielelezo, wakati mmoja watu wa Yuda walikuwa na mifungo minne ya kila mwaka ya kukumbuka matukio yenye msiba yaliyoshirikishwa na mazingiwa na kuachwa ukiwa kwa Yerusalemu katika karne ya saba K.W.K. (2 Wafalme 25:1-4, 8, 9, 22-26; Zekaria 8:19) Baada ya Wayahudi kuachiliwa kutoka utekwa katika Babiloni, Yehova alisema hivi kupitia nabii Zekaria: “Hapo mlipofunga . . . katika miaka hiyo sabini, je! mlinifungia mimi kwa lo lote; mlinifungia mimi?” Mungu hakukubali mifungo hiyo kwa sababu Wayahudi walikuwa wakifungia na kuombolezea hukumu zilizokuwa zimetoka kwa Yehova mwenyewe. Walikuwa wakifunga kwa sababu ya msiba uliowapata, wala si kwa sababu ya kukosa kwao wenyewe kulikoongoza kwenye msiba huo. Baada ya kurudishwa katika nchi ya kwao, ulikuwa wakati wao wa kushangilia badala ya kuombolezea wakati uliopita.—Zekaria 7:5.
Je, Mfungo Ni kwa Ajili ya Wakristo
Ingawa Yesu Kristo hakuamuru wanafunzi wake wafunge, yeye na wafuasi wake walifunga kwenye Siku ya Kufunika kwa sababu walikuwa chini ya Sheria ya Kimusa. Kwa kuongezea, baadhi ya wanafunzi wake walifunga kwa hiari kwenye pindi nyinginezo, kwa kuwa Yesu hakuwaelekeza waache zoea hilo kabisa. (Matendo 13:2, 3; 14:23) Hata hivyo, hawakupaswa kamwe ‘kujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga.’ (Mathayo 6:16) Wonyesho huo wa nje wa uchaji waweza kuleta kibali kutoka kwa wanadamu wengine. Hata hivyo, Mungu hapendezwi na wonyesho huo wa kujivunia.—Mathayo 6:17, 18.
Pia Yesu alizungumzia mfungo wa wanafunzi wake wakati wa kifo chake. Hapo hakuwa akianzisha mfungo wa kidesturi. Badala ya hivyo, alikuwa akionyesha itikio kwa huzuni kubwa ambayo wangepata. Mara alipofufuliwa angekuwa pamoja nao tena, na kusingekuwako tena na sababu hiyo ya kuwafanya wafunge.—Luka 5:34, 35.
Sheria ya Kimusa iliisha ‘Kristo alipotolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi.’ (Waebrania 9:24-28) Na pamoja na mwisho wa Sheria, ile amri ya kufunga kwenye Siku ya Kufunika iliisha. Hivyo, ule mfungo pekee wa lazima katika Biblia uliondolewa.
Namna Gani Kwaresima?
Basi, ni nini ulio msingi wa zoea la kufunga la Jumuiya ya Wakristo wakati wa Kwaresima? Kanisa la Katoliki na la Protestanti hutambua Kwaresima, ingawa njia ya kuiadhimisha hutofautiana toka kanisa moja hadi jingine. Watu fulani hula mlo mmoja tu kwa siku wakati wote huo wa siku 40 zinazotangulia Ista. Wengine hufunga kabisa wakati wa Jumatano ya Majivu na Ijumaa Njema tu. Kwa wengine, Kwaresima hutaka wajiepushe na nyama, samaki, mayai, na bidhaa za maziwa.
Yadhaniwa kwamba Kwaresima ina msingi katika ule mfungo wa siku 40 wa Yesu baada ya ubatizo wake. Basi je, alikuwa akianzisha desturi ya kufuatwa kila mwaka? Sivyo hata kidogo. Hilo ni wazi kutokana na uhakika wa kwamba Biblia hairekodi zoea lolote la aina hiyo miongoni mwa Wakristo wa mapema. Kwaresima iliadhimishwa mara ya kwanza katika karne ya nne baada ya Kristo. Sawa na mafundisho mengine mengi ya Jumuiya ya Wakristo, Kwaresima iliazimwa kutoka katika vyanzo vya kipagani.
Ikiwa Kwaresima ni mwigo wa mfungo wa Yesu nyikani baada ya ubatizo wake, mbona hiyo huadhimishwa majuma yanayoongoza kwenye Ista—idhaniwayo kuwa wakati wa ufufuo wake? Yesu hakufunga katika siku zilizotangulia kifo chake. Masimulizi ya Gospeli yaonyesha kwamba yeye na wanafunzi wake walitembelea nyumba mbalimbali na kula milo huko Bethania siku chache tu kabla hajafa. Naye alikula mlo wa Sikukuu ya Kupitwa usiku uliotangulia kifo chake.—Mathayo 26:6, 7; Luka 22:15; Yohana 12:2.
Kuna jambo la kujifunza katika mfungo wa Yesu baada ya ubatizo wake. Alikuwa akianza huduma ya maana. Utetezi wa enzi kuu ya Yehova na wakati ujao wa wanadamu wote ulihusika. Huo ulikuwa wakati wa kutafakari kwa uzito na kumgeukia Yehova katika sala ili apate msaada na mwongozo. Wakati huo Yesu alifunga kwa kufaa. Hilo laonyesha kwamba mfungo waweza kunufaisha ufanywapo kukiwa na kusudio zuri na kwenye pindi inayofaa.—Linganisha Wakolosai 2:20-23.
Wakati Ambapo Mfungo Waweza Kunufaisha
Acheni tufikirie pindi fulani leo ambazo katika hizo mwabudu wa Mungu aweza kufunga. Mtu ambaye amefanya dhambi huenda asitake kula kwa kipindi fulani cha wakati. Hilo lisingekuwa ili kuwapendeza wengine au kwa sababu ya kukasirikia nidhamu iliyopokewa. Na, bila shaka, mfungo wenyewe usingenyoosha mambo pamoja na Mungu. Hata hivyo, mtu mwenye toba kwelikweli angehisi kuhuzunika sana kwa sababu ya kumuumiza Yehova na huenda hata marafiki na familia. Majonzi na sala zenye kuendelea ili kupata msamaha huenda zikazuia tamaa ya chakula.
Mfalme wa Israeli Daudi alipatwa na jambo hilo. Alipokabiliwa na taraja la kumpoteza mwana wake aliyempata kupitia Bath-sheba, alielekeza jitihada zake zote katika kusali kwa Yehova ili apate rehema kuhusiana na yule mtoto. Alipokuwa katika kusali kabisa-kabisa, alifunga. Vivyo hivyo, kula chakula huenda kusionekane kuwa jambo linalofaa chini ya hali fulani zenye kuleta mkazo leo.—2 Samweli 12:15-17.
Huenda pia kukawa na nyakati ambapo mtu wa kimungu anataka kukazia fikira jambo fulani la kiroho lenye uzito. Huenda kukawa na lazima ya kufanya utafiti katika Biblia na vichapo vya Kikristo. Huenda kipindi cha wakati kikahitajiwa kwa ajili ya kutafakari. Wakati wa funzo hilo lenye kushughulisha sana, huenda mtu akachagua kutokengeushwa fikira na kule kula milo.—Linganisha Yeremia 36:8-10.
Kuna vielelezo vya Kimaandiko vya watumishi wa Mungu wakifunga wakati ambapo maamuzi mazito yalihitaji kufanywa. Katika siku ya Nehemia kiapo kilipaswa kufanywa kwa Yehova, nao Wayahudi wangepatwa na laana ikiwa wangekivunja. Walipaswa kuahidi kuwataliki wake wao wa kigeni na kujitenga na mataifa yaliyozunguka. Kabla ya kufanya kiapo hicho na wakati wa kuungama hatia yao, kutaniko lote zima lilifunga. (Nehemia 9:1, 38; 10:29, 30) Akabiliwapo na maamuzi mazito, Mkristo aweza kutokula kwa kipindi kifupi cha wakati.
Nyakati nyingine kufanya maamuzi kwa mabaraza ya wazee katika kutaniko la mapema la Kikristo kuliambatana na mfungo. Leo, wazee wa kutaniko wanaokabili uamuzi mzito, labda unaohusiana na kesi ya kihukumu, huenda wakaepuka chakula wafikiriapo jambo hilo.
Kuchagua kufunga katika hali fulani ni uamuzi wa kibinafsi. Mtu mmoja hapaswi kumhukumu mwingine juu ya jambo hilo. Hatupaswi kutaka ‘kuonekana na watu kuwa wenye haki’; wala hatupaswi kufanya chakula kiwe cha maana sana hivi kwamba chaingiliana na kushughulikia kwetu wajibu mbalimbali ulio mzito. (Mathayo 23:28; Luka 12:22, 23) Nayo Biblia huonyesha kwamba Mungu wala hataki tufunge wala hatukatazi tusifunge.
-