Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Tisho la Nyuklia Halijaisha
    Amkeni!—1999 | Agosti 22
    • Tisho la Nyuklia Halijaisha

      “Kuenea kwa silaha hatari sasa ndilo jambo lililo hatari zaidi linalotisha sayari hii.”—CRITICAL MASS, CHA WILLIAM E. BURROWS NA ROBERT WINDREM.

      KWENYE mapambazuko katika Januari 25, 1995, mmweko wenye kuogofya ulitokea kwa ghafula kwenye viwambo vya rada za kutoa onyo la mapema katika kaskazini mwa Urusi. Roketi ilikuwa imerushwa mahali fulani kutoka pwani ya Norway! Wafanyakazi wa rada walitahadharisha Moscow juu ya uwezekano wa kuwasili kwa bomu la nyuklia. Katika muda wa dakika chache, rais wa Urusi alipewa sanduku lenye vifaa vya elektroni ambavyo vingemruhusu kuagiza kulipiza kisasi shambulizi hilo kwa kutumia silaha za nyuklia zenye kuangamiza. Ikaonekana kama vita vikubwa vya nyuklia vilikuwa karibu sana kutukia.

      Kwa uzuri, kujidhibiti kukashinda, na njia ambayo roketi hiyo ilichukua ikawa si tisho kwa Urusi. Baadaye ikajulikana kwamba hicho kilikuwa chombo kilichobeba vifaa vya kuchunguza hali ya hewa. Ijapokuwa hivyo, makala katika The Washington Post ilisema: “Huenda hizi zilikuwa mojawapo ya pindi zilizo hatari zaidi katika enzi ya nyuklia. Zinatuonyesha jinsi mfumo wa kurushia makombora ya nyuklia wa Vita Baridi ungali tayari kutumika, na jinsi unavyoweza kutokeza msiba kwa makosa, hata ingawa ushindani kati ya mataifa yenye uwezo mkubwa umekoma.”

      Tahadhari Kubwa

      Kwa miongo mingi hali inayohusu nyuklia ya Muungano wa Sovieti wa zamani na Marekani ilitegemea dhana iliyowazuia wasiangamizane inayojulikana kuwa angamizano hakika (MAD). Sehemu kuu ya MAD ilikuwa mbinu inayoitwa kurusha kombora onyo linapotolewa. Jambo hili liliupa kila upande uhakikisho wenye kuogofya kwamba ikiwa wangeshambulia, adui wao angelipiza kisasi kwa kiwango kikubwa sana hata kabla ya makombora yenye kushambulia kufikia shabaha zao. Sehemu kuu ya pili ya MAD ilikuwa mbinu iliyoitwa rusha kombora wakati wa shambulizi. Hiyo ilirejezea uwezo wa kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi hata baada ya makombora ya adui kusababisha uharibifu.

      Licha ya uadui wa Vita Baridi kukoma, bado sera ya MAD ni jambo linalosumbua wanadamu. Naam, zana za nyuklia za Marekani na Urusi zimepunguzwa kwa kiwango kikubwa—wengine wanasema kufikia nusu—lakini maelfu ya makombora ya nyuklia yangalipo. Basi kuna uwezekano kwamba silaha hizo zingeweza kurushwa kwa aksidenti au bila idhini. Na kwa sababu hayo mataifa yote mawili yanahofu uwezekano wa kushambuliwa kwanza na mwenzake, idadi kubwa ya makombora huwekwa yakiwa tayari kufyatuliwa.

      Ni kweli, mnamo 1994 Marekani na Urusi zilikubaliana kuacha kuelekezeana makombora. “Ingawa hilo ni badiliko zuri, si la maana sana kijeshi,” lasema Scientific American. “Makamanda wa makombora wanaweza kuweka tena nambari za kuwasaidia kulenga shabaha kwenye kompyuta za kuzielekeza kwa muda wa sekunde chache tu.”

      Je, Silaha Mpya Zitaundwa Hivi Karibuni?

      Hatupaswi kupuuza uhakika wa kwamba utafiti na usitawishaji wa silaha za nyuklia waendelea. Kwa mfano, nchini Marekani, bajeti ya kila mwaka kwa silaha hizo ni takriban dola bilioni 4.5! Mnamo 1997, The Toronto Star liliripoti: “Kumbe, Marekani sasa inatumia pesa nyingi zaidi kuliko wakati wa vita ya maneno na propaganda ili kuhifadhi silaha zake za nyuklia. Na baadhi ya pesa hizo zimetengwa kwa makusudi ya programu tata ambazo wachambuzi wanasema zingeweza kuongoza kwenye mashindano mapya ya silaha tufeni pote.”

      Kwa mfano, kulizuka ubishi mkubwa sana juu ya mradi wa serikali ya Marekani ambao ungegharimu mabilioni ya dola ulioitwa Stockpile Stewardship and Management Program. Ijapokuwa kusudi la programu hiyo eti ni kudumisha silaha za nyuklia zilizopo, wachambuzi wanasema kwamba pia ina kusudi baya. Kichapo The Bulletin of the Atomic Scientists charipoti: “Kuna mipango ya kufanyia mabadiliko silaha za nyuklia, na kuzirekebisha, na kuziboresha, na kubadilisha zile ambazo hazifai—si kurefusha tu muda wa silaha ya nyuklia . . . bali pia ‘kuiboresha’ vilevile.”

      Mnamo 1997 bishano kali lilitokea juu ya kuundwa kwa bomu la nyuklia linaloitwa B-61, ambalo lina uwezo wa kupenya ndani ya ardhi kabla halijalipuka. Hivyo linaweza kuharibu vituo vya kamanda vilivyo chini ya ardhi, viwanda, na maabara. Ingawa watetezi wanadai kwamba ni kurekebisha tu bomu zee, wapinzani wanadai kwamba kwa kweli hilo ni bomu jipya—ukiukaji mkubwa wa ahadi iliyofanywa na serikali ya Marekani kwamba haitatengeneza silaha mpya za nyuklia.

      Kwa vyo vyote vile, Ted Taylor, mwanafizikia wa nyuklia kwenye Chuo Kikuu cha Princetown alisema: “Nasadiki kwamba utafiti unaoendelea sasa (Marekani) pia unaendelea katika Urusi, Ufaransa, Ujerumani na sehemu nyinginezo, na nasadiki kwamba baadhi ya miradi yetu inaongoza ulimwengu kwenye mashindano mapya ya silaha.” Wachambuzi wanadai pia kwamba utafiti huo, usitawishaji, na kubuniwa kwa silaha mpya kunaendelezwa sana na wenye kubuni silaha wenyewe. Huenda kichocheo kikubwa cha kuwafanya wanasayansi hawa wahimize kuanzishwa tena kwa utafiti wa silaha kikawa ni fedheha ambayo wamepata, kudidimia kwa fahari yao na magumu ya kiuchumi.

      Mataifa Mapya Yenye Nyuklia

      Kisha kuna mabadiliko katika hali ya kisiasa ulimwenguni. Hapo zamani kulikuwa na mataifa matano yaliyokuwa na silaha za nyuklia: China, Marekani, Ufaransa, Uingereza, na Urusi. Hata hivyo, imetambuliwa kwamba nchi nyingine pia zimeunda silaha za nyuklia. Kwa mfano, hivi karibuni India na Pakistan zilifanya majaribio ya nyuklia ambayo yalichochea hofu ya mashindano makali sana ya silaha katika Kusini-Mashariki mwa Asia. Mataifa mengine yanayoshukiwa kuwa na programu za nyuklia yanatia ndani Algeria, Iran, Iraki, na Korea Kaskazini. Zaidi ya mataifa 180 yametia sahihi Mkataba wa Kutoongezeka kwa Mataifa Yenye Nyuklia, ulioanza kutumika mnamo 1970. Mpaka sasa, mataifa kadhaa yanayoshukiwa sana kuwa yanaficha tamaa yao ya kutengeneza silaha za nyuklia hayajatia sahihi mkataba huo.

      Kichapo Asiaweek charipoti: “Wataalamu wanaoshughulikia kuenea kwa nyuklia wangali wanaamini kwamba tisho halisi linatokana na idadi inayoongezeka ya nchi ambazo viongozi wao wangependa kuwa na uwezo wa kutengeneza nyuklia.” Watazamaji fulani wanahisi kwamba kujapokuwa adhabu, Mkataba wa Kutoongezeka kwa Mataifa Yenye Nyuklia hautaweza kuzuia serikali ambazo zimeazimia, kupata tekinolojia na vifaa vinavyohitajiwa ili kutengeneza nyuklia bila kujulikana. James Clapper, mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Jeshi la Marekani, alitabiri hivi: “Kufikia mwisho wa karne hii huenda tukaona nchi nyingi sana zikiwa na uwezo wa kutengeneza kichwa cha kombora [la sumu, viini au nyuklia] kutokana na kombora walilojitengenezea.”

      Wala haielekei kwamba mataifa yote yatakubali kusongwa ili kupiga marufuku majaribio ya nyuklia. Wakati mataifa kadhaa yaliposhawishwa kutia sahihi Mkataba wa Kukomesha Majaribio ya Nyuklia mnamo 1966, makala ya mhariri katika Asiaweek ilisema: “Ni sawa kwa Wamarekani na Wazungu kutangaza kupiga marufuku majaribio, kwa kuwa tayari wamelipua silaha za nyuklia za kutosha na kuacha kufanya majaribio kwa kuwa tayari wana habari waliyokusanya.”

      Magendo ya Nyuklia na Ugaidi

      Wengine wanahisi kuwa tisho kubwa zaidi ni kwamba huenda kikundi fulani cha magaidi kikapata silaha ya nyuklia na kuamua kuilipua—au angalau kutisha kuilipua—ili kutimiziwa madai yao ya kisiasa. Vivyo hivyo, kuna hofu kwamba kikundi cha wahalifu kingeweza kutumia vifaa vya nururishi kwa kiwango kikubwa ili kutimiziwa madai yao kwa nguvu na serikali au shirika fulani. Makala moja katika Scientific American yaeleza hivi: “Lingekuwa jambo rahisi sana watu kumsadiki mfanya-magendo wa nyuklia ikiwa angeacha sampuli ya nyuklia ili kuchunguzwa. Baadaye, vitisho vya kuchafua hewa au maji, au hata kulipua silaha ndogo ya nyuklia, vingekuwa na matokeo makubwa.” Tayari mashirika ya utekelezaji sheria yamegundua majaribio ya kupitisha kimagendo vifaa vya nyuklia. Jambo hilo huongezea hofu kwamba vikundi vya watu wabaya huenda kwa kweli vikajaribu kutengeneza silaha za nyuklia.

      Ni kweli kwamba wachunguzi wanapuuza tisho la nyuklia kwa kuliona kuwa dogo tu. Wanasema, si kwamba tu vifaa vidogo vilitoka kwa wenyewe, bali pia isipokuwa visa vichache, vingi vyake havijakaribia ubora unaotakikana ili kutengeneza silaha hizo. Hata hivyo Scientific American, lawakumbusha wasomaji kwamba “karibu katika masoko yote ya magendo, ni jambo dogo tu linaloonekana, na hakuna sababu inayofanya vifaa vya nyuklia kwenye soko la magendo visiwe vinauzwa kwa wingi. . . . Kuamini kwamba wenye mamlaka wanazuia zaidi ya asilimia 80 ya biashara kungekuwa jambo la upumbavu. Isitoshe, hata kupitishwa kidogo-kidogo kwa nyuklia kungekuwa na matokeo makubwa sana.”

      Ijapokuwa kiwango hususa cha kutengeneza bomu la nyuklia ni siri kubwa, inakadiriwa kwamba unahitaji kati ya kilogramu 3 hadi 25 za urani au kati ya kilogramu 1 hadi 8 za plutonia ya gredi ya kutengeneza silaha. Jambo lenye kupendeza wafanya-magendo ni kwamba kilogramu saba za plutonia zinachukua nafasi inayotoshana na mkebe wa kawaida wa alumini wa kuwekea vinywaji baridi. Wengine wanafikiri kwamba hata plutonia ya gredi ya kudhibiti nguvu za nyuklia—ambayo hupatikana kwa urahisi zaidi kuliko ya gredi ya silaha—ingeweza kutumiwa kwa urahisi kutengeneza bomu la nyuklia lisilokuwa la hali ya juu lakini liwezalo kusababisha uharibifu. Ikiwa, kama wataalamu wengi wanavyodai, vifaa vya nururishi havilindwi ifaavyo, huenda vikaibwa kwa urahisi kuliko jinsi watu wanavyofikiri. Mikhail Kulik, ofisa Mrusi, alisema hivi kwa kukejeli: “Labda hata viazi vinalindwa zaidi kuliko vifaa vya nururishi.”

      Kwa wazi, basi hatari ya nyuklia ingali inakabili wanadamu. Je, kuna tumaini lolote kwamba litapata kuondolewa?

  • Hatimaye Wakati Ujao Ulio Salama!
    Amkeni!—1999 | Agosti 22
    • “WETU ni ulimwengu wa majitu walio wajuzi wa nyuklia lakini vitoto vichanga katika kufuata tabia zifaazo. Sisi twajua mengi zaidi kuhusu vita kuliko yale tuyajuayo kuhusu amani, mengi zaidi kuhusu kuua kuliko yale tuyajuayo kuhusu kuishi.” Maneno hayo yaliyosemwa na jenerali wa Kijeshi wa Marekani mnamo 1948, hutukumbusha maoni yanayopatikana katika Biblia: ‘Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.’ (Mhubiri 8:9) Wanadamu wanapokuwa na silaha za nyuklia, wanaweza kusababisha madhara zaidi kuliko kuwajeruhi tu wanadamu wenzao; wanaweza kuwaangamiza!

      Watu wengi wanaamini kwamba kuwa na silaha za nyuklia na kuzitumia ni kosa la kiadili. Kwa mfano, jenerali mstaafu wa Jeshi la Wanaanga la Marekani George Lee Butler alisema: “Mtu anapokuwa na silaha za nyuklia akibani anatoa ujumbe kwamba tunaweza kuwazia hali ambazo . . . kwa njia fulani tunaweza kufikiria kutumiwa kwa silaha hiyo. Hilo ni kosa kabisa.”

      Hata hivyo, mwandishi wa makala za gazeti Mwingereza Martin Woollacatt asema: “Bado silaha za nyuklia zinapendeza, bila kujali wataalamu na watu wenye kutetea maadili wanasemaje kuhusu kutofaa na hatari zake. Serikali zinaamini kwamba zinahitaji silaha hizo kwa sababu ya kujilinda; pia wanazing’ang’ania kwa sababu bila shaka silaha za nyuklia zina uvutano mbaya ambao wanasiasa na majeshi hutambua na kutaka kuwa nao.”

      Ni kweli kwamba kwa miongo mitano iliyopita, kwa njia fulani mwanadamu amefaulu kuepusha vita vya nyuklia. Lakini katika kipindi hichohicho, silaha za kawaida zimetumiwa kuua maelfu yasiyojulikana ya watu. Kwa kufikiria historia ya binadamu, ni jambo linalofaa kudhania kwamba pindi moja, silaha hizi za nyuklia zenye kuogofya zitatumiwa.

      Sababu za Msingi

      Je, mielekeo ya mwanadamu ya kupenda vita inaweza kuzuiwa? Watu fulani wanadai kwamba wanadamu hupigana kwa sababu ya upumbavu, ubinafsi, na uchokozi unaofaa. “Ikiwa hizi ndizo sababu za msingi za vita,” asema msomi Kenneth Waltz, “basi kukomeshwa kwa vita kwapaswa kutokana na kuboresha hali ya wanadamu na kuwaelimisha.”

      Wengine wanasema kwamba visababishi vya vita vyategemea sera za siasa za kimataifa. Kwa sababu kila nchi inayojitawala hufuatia mapendezi yake yenyewe, mapambano hayawezi kuepukwa. Kwa kuwa hakuna njia yenye kutegemeka ya kutatua matatizo, vita huzuka. William E. Burrows na Robert Windrem waandika hivi katika kitabu chao Critical Mass: “Jambo gumu ni la kisiasa. Hakuna usimamizi wenye udhibiti unaowezekana bila kuwa na azimio la msingi la kisiasa la kukomesha na hata kutangua kuenea kwa silaha za nyuklia.”

      Fikiria majadiliano yanayoendelea ya kutekeleza Mkataba wa Kukomesha Kabisa Majaribio. Gazeti la Guardian Weekly liliyafafanua kuwa “kipindi cha majadiliano makali kati ya mataifa yenye uwezo wa nyuklia na mataifa ambayo tayari yana silaha za nyuklia kisiri au yaliyo na tekinolojia ya kuzitengeneza haraka.” Makala hiyohiyo inakiri: “Hakuna [kikundi] chochote kilicho na mpango wa kuacha silaha zake au uwezo wake wa nyuklia, au kuboresha ama silaha zake ama uwezo wake.”

      Bila shaka, ushirikiano wa kimataifa wahitajiwa ikiwa vitisho vyote vya nyuklia vitaondolewa kabisa. Kitabu Critical Mass chasema: “Kuaminiana lazima kuchukue mahali pa kuangamizana wenyewe kwa wenyewe kila mahali, . . . au baada ya pindi fulani msiba mkubwa utatokea.” Kwa kusikitisha, uhusiano wa kimataifa leo na majadiliano mara nyingi unafanana na kile nabii Danieli alichokifafanua karne 26 zilizopita: ‘Wanasema uongo wakiwa katika meza moja.’—Danieli 11:27, Byington.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki