Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kusoma kwa Usahihi
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • VITUO

      Nukta (.) inaonyesha kutua kabisa.

      Mkato (,) kwa kawaida hii huonyesha kutua kifupi, kwani kuna maandishi yanayofuata.

      Nukta-mkato (;) ni kituo kifupi kuliko nukta lakini kirefu kuliko mkato.

      Nukta-pacha (:) hutanguliza orodha fulani au mnukuo; ni kutua bila kubadili sauti.

      Alama ya mshangao (!) huonyesha mshangao.

      Kiulizio (?) mara nyingi inatakikana sentensi isomwe kwa sauti ya juu au inayoendelea kuinuka.

      Alama za mnukuo (“ ” au ‘ ’) zinaweza kuonyesha kwamba maneno yaliyo ndani ya alama hizo yanapasa kusomwa baada ya kutua (kituo kifupi sana kama maneno hayo ni sehemu ya sentensi; au kituo kirefu ikiwa maneno hayo ni sentensi kamili).

      Vistari (—), vinapotumiwa kutenganisha maneno, mara nyingi inatakikana kubadili kidogo sauti au mwendo.

      Parandesi ( ) na mabano [ ] yanaweza kutenga maneno yanayopasa kusomwa kwa sauti ya chini kidogo. Marejeo ya habari ambayo yamo ndani ya parandesi hayapasi kusomwa, na maneno yaliyo katika mabano ambayo yamewekwa kukamilisha maana ya mambo yanayosomwa hayahitaji ubadilifu wa sauti.

  • Kusoma kwa Usahihi
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • SOMO LA 1

      Kusoma kwa Usahihi

      Unahitaji kufanya nini?

      Soma kwa sauti na bila kukosea maandishi yaliyochapwa. Usiruke-ruke maneno, au kuacha sehemu fulani za maneno, au kubadilisha maneno. Tamka maneno vizuri. Zingatia vituo na alama za matamshi.

      Kwa Nini Ni Muhimu?

      Kusoma kwa makini na kwa usahihi ni njia muhimu ya kujulisha wengine ujuzi sahihi wa kweli ya Biblia.

      MAANDIKO yanasema kwamba Mungu anataka watu wa hali zote ‘waje kwenye ujuzi sahihi wa kweli.’ (1 Tim. 2:4) Kwa hiyo, tunaposoma Biblia kwa sauti, tamaa yetu ya kujulisha wengine ujuzi sahihi inapasa kutuchochea kusoma vizuri.

      Uwezo wa kusoma Biblia kwa sauti pamoja na vichapo vingine vinavyoifafanua ni muhimu sana kwa vijana na wazee. Sisi Mashahidi wa Yehova tuna daraka la kuwajulisha wengine ujuzi juu ya Yehova na njia zake. Mara nyingi sisi husomea mtu mmoja au watu kadhaa. Sisi husoma pia katika familia. Shule ya Huduma ya Kitheokrasi huwapa akina ndugu na dada, vijana kwa wazee, fursa nzuri ya kupokea mashauri yanayowasaidia kusoma vizuri kwa sauti.

      Ni jambo zito kusoma Biblia mbele ya watu au mbele ya kutaniko. Biblia imepuliziwa na Mungu. Na pia ‘neno la Mungu liko hai na hukazia nguvu na linaweza kufahamu fikira na makusudio ya moyo.’ (Ebr. 4:12) Neno la Mungu lina ujuzi wenye thamani sana ambao haupatikani mahali pengine popote. Pia linaweza kumsaidia mtu amjue Mungu wa pekee wa kweli na kujenga uhusiano mzuri naye. Hali kadhalika linaweza kumsaidia kukabiliana na matatizo ya maisha kwa mafanikio. Linaeleza jinsi ya kupata uhai wa milele katika ulimwengu mpya wa Mungu. Tunapaswa kuweka mradi wa kusoma Biblia kwa kadiri iwezekanavyo.—Zab. 119:140; Yer. 26:2.

      Jinsi ya Kusoma kwa Usahihi. Kusoma vizuri kunahusisha mambo mengi, lakini hatua ya kwanza ni kusoma kwa usahihi. Hiyo inamaanisha kujaribu kusoma maneno yaliyochapwa jinsi yalivyo hasa. Jihadhari usiruke-ruke maneno, usikose kutamka sehemu fulani za maneno, wala usisome maneno vibaya kwa sababu ya kuchanganyikiwa na maneno mengine yanayofanana nayo.

      Ili uweze kusoma maneno kwa usahihi, inatakikana uelewe muktadha. Hiyo inahitaji matayarisho mazuri. Baada ya muda utaweza kusoma kwa usahihi zaidi unapokuza uwezo wa kutazama maneno yanayofuata na kufahamu jinsi ambavyo mawazo yamefuatana.

      Vituo na alama za matamshi ni sehemu muhimu za maandishi. Vituo vinaweza kuonyesha mahali pa kutua, muda wa kutua, na labda mahali pa kubadili sauti. Katika lugha nyinginezo, swali linaweza kubadilika kuwa taarifa au maana ya sentensi inaweza kubadilika kabisa mtu asipobadili sauti anapofikia kituo. Nyakati nyingine vituo hutumiwa hasa kwa minajili ya sarufi. Katika lugha nyingi, huwezi kusoma kwa usahihi bila kufikiria kwa makini alama za matamshi zinazoonyeshwa na pia zile ambazo zinaeleweka tu kutokana na muktadha. Alama hizo hubadili sauti za herufi zinazohusika. Hakikisha unajua kutumia vituo katika lugha yenu. Hiyo ndiyo njia ya kusoma vizuri. Kumbuka kwamba kusudi lako ni kuwasilisha mawazo, si kusema tu maneno.

      Ili uweze kukuza uwezo wa kusoma kwa usahihi, unahitaji kufanya mazoezi sana. Soma fungu moja tu, kisha urudie kulisoma tena na tena mpaka uweze kulisoma bila kufanya kosa lolote. Kisha usome fungu linalofuata. Hatimaye, jaribu kusoma kurasa kadhaa bila kuruka-ruka maneno, bila kujirudia-rudia, au bila kusoma maneno vibaya. Baada ya kufanya hivyo, omba mtu mwingine akusikilize unaposoma ili akukosoe unapokosea.

      Katika sehemu nyingine za ulimwengu, matatizo ya macho na kukosa mwangaza wa kutosha kunaweza kutokeza matatizo ya kusoma. Hali hizo zikiboreshwa, bila shaka wengi wanaweza kusoma vizuri.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki