-
Kanuni za Adili Zinazostahili StahaMashahidi wa Yehova na Elimu
-
-
Kusalimu Bendera
Kwa ujumla Mashahidi wa Yehova si shabaha ya mnyanyaso mkali wa jinsi hiyo leo. Hata hivyo, nyakati nyingine kuelewa vibaya hutokea kwa sababu ya uamuzi wenye kudhamiria wa Mashahidi wachanga wa kutoshiriki katika sherehe za kizalendo kama vile kusalimu bendera.
“Rudishieni Kaisari vilivyo vya Kaisari—na Mungu vilivyo vya Mungu”—Mathayo 22:21, Jerusalem Bible
Watoto wa Mashahidi wa Yehova hufundishwa wasizuie wengine kusalimu bendera; hilo ni jambo la kuamuliwa na kila mtu mmoja-mmoja. Hata hivyo, msimamo wa Mashahidi wenyewe ni imara: Wao hawasalimu bendera ya taifa lolote. Hilo kwa hakika halina nia ya kuonyesha ukosefu wa staha. Wao huistahi bendera ya nchi yoyote wanamoishi, nao huonyesha staha hiyo kwa kutii sheria za nchi hiyo. Hawashiriki kamwe katika aina yoyote ya utendaji wa kupinga serikali. Kwa kweli, Mashahidi huamini kwamba serikali za binadamu zilizopo hufanyiza “mpango wa Mungu” ambao yeye ameruhusu uweko. Kwa hiyo wao hujiona kuwa chini ya amri ya kimungu ya kulipa kodi na kustahi “mamlaka [hizo] zilizo kubwa.” (Warumi 13:1-7, NW) Hilo lapatana na taarifa maarufu ya Kristo: “Rudishieni Kaisari vilivyo vya Kaisari—na Mungu vilivyo vya Mungu.”—Mathayo 22:21, Jerusalem Bible ya Katoliki.
‘Lakini, kwa nini,’ huenda wengine wakauliza, ‘Mashahidi wa Yehova hawaiheshimu bendera kwa kuisalimu?’ Ni kwa sababu wao huona kusalimu bendera kuwa tendo la ibada, na ibada ni ya Mungu; hawawezi kwa kudhamiria kuabudu yeyote au chochote isipokuwa Mungu. (Mathayo 4:10; Matendo 5:29) Kwa hiyo, wao huthamini wakati waelimishaji wanapostahi sadikisho hili na kuruhusu watoto Mashahidi wafuate itikadi zao.
Haishangazi kwamba si Mashahidi wa Yehova peke yao wanaoamini kwamba kusalimu bendera kuna uhusiano na ibada, kama vile maelezo yafuatayo yaonyeshavyo:
“Bendera za mapema karibu zilikuwa za aina ya kidini kabisa. . . . Msaada wa dini ulikuwa daima ukitafutwa ili kuzipa utakatifu bendera za kitaifa.” (Italiki ni zetu.)—Encyclopædia Britannica.
“Bendera ni takatifu, kama vile msalaba. . . . Kanuni na amri zinazohusu mtazamo wa binadamu kuelekea viwango vya kitaifa hutumia maneno yenye nguvu na yaliyo dhahiri, kama vile, ‘Utumishi kwa Bendera,’ . . . ‘Kicho kwa Bendera,’ ‘Ujitoaji kwa Bendera.’” (Italiki ni zetu.)—The Encyclopedia Americana.
“Wakristo walikataa . . . kutolea dhabihu roho ya kimungu ya maliki [Mroma]—karibu na vile leo kukataa kusalimu bendera au kurudia kiapo cha uaminifu wa kiraia.”—Those About to Die (1958), cha Daniel P. Mannix, ukurasa 135.
Vijana Waebrania watatu walikataa kuinamia sanamu iliyojengwa na mfalme Mbabiloni Nebukadreza
Tena, Mashahidi wa Yehova hawana nia ya kutostahi serikali yoyote wala watawala wayo kwa kukataa kusalimu bendera. Ni kwamba tu, hawatainamia wala kusalimu sanamu inayowakilisha Serikali katika tendo lolote la ibada. Wanaona hilo kuwa sawa na msimamo uliochukuliwa katika nyakati za Biblia na vijana Waebrania watatu waliokataa kuinamia ile sanamu iliyojengwa katika uwanda wa Dura na mfalme Mbabiloni Nebukadreza. (Danieli, sura ya 3) Kwa hiyo basi, ingawa wengine husalimu na kuapa uaminifu wa kiraia, watoto wa Mashahidi wa Yehova wanafundishwa kufuata dhamiri zao zilizozoezwa na Biblia. Hivyo, kwa ukimya na kwa staha wao huepuka kushiriki. Kwa sababu zizo hizo, watoto Mashahidi huchagua kutoshiriki wakati nyimbo za kitaifa zinapoimbwa au kupigwa.
-